Waokoaji wametumia siku ya Jumanne kutoa mifuko ya miili
na manusura kutoka ndani ya mgodi wa Afrika Kusini ambapo wachimba migodi
haramu bado wanafikiriwa kuwa angalau kilomita 2 (maili 1.2) chini ya ardhi.
Watu 82
wamejitokeza wakiwa hai kutoka ndani ya mgodi huko Stilfontein tangu shughuli
ya uokoaji ilipoanza Jumatatu, polisi wanasema, huku maiti 36 zikitolewa.
Siku ya
Jumanne, BBC ilishuhudia wachimba migodi waliodhoofika wakitoka ndani ya mgodi –
wakiwa wamevalia nguo chakavu na bila viatu au soksi - walisindikizwa hadi
kwenye hema la matibabu.
Baadhi ya mifuko ya miili ilionekana kuwa miepesi kiasi
kwamba ilibebwa na mtu mmoja tu.
Wanaume hao wamekuwa chini ya ardhi tangu operesheni za
polisi zinazolenga uchimbaji madini haramu kuanza mwaka jana kote nchini humo.
Zaidi ya
wachimba migodi 100 haramu, wanaojulikana na wenyeji kama "zama
zamas", wameripotiwa kufa chini ya ardhi tangu msako mkali wa shughuli zao
ulipoanza katika mgodi huo ulioko kilomita 145 (maili 90) kusini-magharibi mwa
Johannesburg mwaka jana.
Mamlaka hata
hivyo, hazijathibitisha takwimu hii kwa kuwa bado "haijathibitishwa na
chanzo rasmi", msemaji aliiambia BBC.
Ndugu, jamaa
na wanajamii wamekuwa wakiandama kwenye eneo la uchimbaji huku wakiwa na
mabango ya kuitaka mamlaka kuwaokoa wachimbaji hao.
Wanaonekana
kuchoka na kuambia BBC Jumanne kwamba wamechoka kuzungumza na vyombo vya
habari.
Zinzi Tom alieleza kuwa kaka yake mwenye umri wa miaka 29, Ayanda, alishuka mgodini mwezi Juni kwa sababu hakuwa na kazi na alitaka kujikimu kimaisha.
"Tuliuliza kama anapaswa kufanya hivyo, lakini umri wake ni mkubwa, anaweza kufanya chochote anachotaka. Lakini hilo sio la msingi kwa sasa. Kipaumbele ni kwamba tunataka kumuokoa. Tunataka atoke," alisema.
Baadhi ya wachimba migodi waliofanikiwa kutoroka wamemwambia Bi Tom kwamba kakake hayuko sawa. Anatumai atakuwa mmoja wa wale waliookolewa hivi karibuni.
Bi Tom anamuelezea kaka yake kuwa mtulivu na msiri, akiongeza: "Ninahitaji kuwa na nguvu kwa ajili yake, kwa sababu siwezi kuwa dhaifu kipindi hiki. Ananihitaji zaidi kuliko hapo awali."
Hali ya sintofahamu miongoni mwa ndugu waliokuwa nje ya mgodi huo ilizidi kuwa mbaya wakati msafara uliokuwa umembeba waziri wa rasilimali madini Gwede Mantashe na waziri wa polisi ulipofika eneo hilo.
Serikali imekosolewa kwa kuchukua msimamo mkali dhidi ya wachimbaji haramu kwa kuzuia wasipewe chakula wala maji. Pia walifunga njia zote za kutoka mgodini isipokuwa moja.
Wiki iliyopita mahakama iliamuru serikali kuwezesha shughuli ya uokoaji ambayo ilikuwa imechelewa kwa muda mrefu.
Mamlaka imetetea madai ya kujikokota katika kushughulikia suala hili na katika mkutano na waandishi wa habari nje ya mgodi Mantashe alisema "vita dhidi ya uchimbaji haramu" inapaswa kuongezwa.
"Ni uhalifu dhidi ya uchumi, ni shambulio kwa uchumi," alisema.