Mapigano yanatarajiwa kusitishwa kwa wiki sita na mateka kuachiwa
Mkataba wa kusitisha mapigano utatekelezwa kwa awamu kadhaa kwa mujibu wa maelezo yaliyokuwa yamevujishwa hapo awali.
Awamu ya kwanza ni usitishaji mapigano wa wiki sita. Katika kipindi hicho Hamas itawaachilia mateka 33 ambao iliwachukuwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 2024.
Haijabainika ni wangapi kati ya hao 33 ambao bado wako hai.
Kwa kila mateka atakayeachiwa huru, Israel itawaachilia makumi ya wafungwa wa Kipalestina.
Israel itawaondoa wanajeshi wake katika maeneo yenye watu wengi zaidi ya Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika eneo la salama upande wa mashariki.
Misaada zaidi na mafuta yataruhusiwa kusafirishwa mara moja - na kutakuwa na udhibiti wa kurudi kwa watu milioni mbili wa Gaza waliokimbia makazi yao.
Bado kuna kundi la mateka wa Israel ambao sio sehemu ya wale kuachiliwa awamu ya kwanza.
Hatima yao itaamuliwa katika duru nyingine ya mazungumzo ambayo yanatarajiwa kuanza siku 16 baada ya kusitishwa kwa mapigano.
Wapalestina washerehekea makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza
Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanasherehekea kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hizi ni baadhi ya picha ambazo tumepokea kutoka Deir Al-Balah katikati mwa Gaza:
Chanzo cha picha, Reuters
Chanzo cha picha, Reuters
Hamas imeidhinisha mpango wa usitishaji mapigano Gaza, afisa aiambia BBC
Chanzo cha picha, Reuters
Afisa wa Hamas ameiambia BBC kuwa kundi hilo la Palestina limewaambia wapatanishi wa Qatar na Misri kwamba limeidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.
Afisa huyo alizungumza na BBC huku vyombo vya habari vya Israel vikiripoti kuwa Hamas wamewasilisha matakwa ya dakika za mwisho katika makubaliano ya kusitisha mapigano - muda mfupi kabla ya Qatar kufanya mkutano na wanahabari kuhusu hali ya mazungumzo hayo.
Kulingana na chanzo hicho hatua hiyo ilifikiwa kufuatia mkutano kati ya Waziri Mkuu wa Qatar na wawakililishi wa Hamas na wawakilishi tofauti wa Israel katika ofisi yake.
Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinasema kuwa imetoa matakwa mapya kuhusu Ukanda wa Philadelphi - sehemu muhimu ya kimkakati ya ardhi kwenye mpaka wa kusini wa Gaza na Misri.
Mara baada ya taarifa hizo Rais Mteule wa Marekani Donald Trum aliandika ujumbe kwenye mtandao wake wa Kijamii wa Truth Social akisema: "TUMEFIKIA MAKUBALIANO MASHARIKI YA KATI. MATEKA WATAACHIWA MUDA MFUPI UJAO. ASANTENI!"
Mlipuko wa Marburg: Kenya yachukua hatua ya tahadhari
Chanzo cha picha, GET
Mkurugenzi wa Mkuu wa Afya wa
Kenya Dkt Patrick Amoth amesema taifa fa hilo liko katika hali ya tahadhari baada
ya ugonjwa unaoshukiwa kuwa wa Marburg kugunduliwa katika tiafa jirani la Tanzania.
Mlipuko wa virusi hivyo
umeripotiwa katika eneo la Kagera kaskazini magharibi mwa Tanzania ambapo watu wanane wameripotiwa kufariki
baada ya kuambukizwa virusi hivyo.
Amoth amesema kutokana na ukaribu
wa Kagera na mji wa Migori magharibi mwaKenya serikali imechukua hatua za
dharura kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo
‘‘Leo tumepokea mawasiliano kutoka kwa
shirika la WHO kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Marburg katika taifa
la Tanzania na kutokana na ukaribu wa maeneo yetu sisi pia
tuko hatarini,’’ Amoth alisema.
Aidha aliongeza kuwa Kenya imeweka
mikakati ya kukabiliana na virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha juhudi za
uangalizi ili kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Israel na Hamas wafanya juhudi za mwisho za kusitisha mapigano Gaza
Chanzo cha picha, Getty Images
Wapatanishi wa Israel na Hamas wanafanya juhudi za mwisho kufikia mkataba wa usitishaji vita vya Gaza mjini Doha, Qatar huku pande zote zikiashiria majadiliano yamekamilika.
Ripoti ziliibuka kuwa pende hizo mbili ziko zinaelekea kufikia makubaliano ya kusitisha mzozo kati yao, huku maafisa wa Israel ambao majina yao hayakutajwa wakidai kuwa Hamas imekubaliana na rasimu ya hivi punde iliyowasilishwa na wapatanishi wa Qatar, Marekani na Misri.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hata hivyo imekanusha madai hayo.
Kundi la Hamas halijatoa tamko lolote kuhusiana na hilo.
Usiku wa Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema majadiliano "yako ukingoni" na wanasubiri "kauli ya mwisho kutoka kwa Hamas".
Afisa mkuu wa Hamas baadaye aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa halijatoa jibu lake rasmi kuhus rasimu hiyo kwa sababu Israel ilikuwa bado haijawasilisha ramani zinazoonyesha jinsi wanajeshi wake wangeondoka katika maeneo ya Gaza.
Roketi ya SpaceX yafanya ziara ya kibinafsi mwezini
Chanzo cha picha, Nasa/SpaceX
Chombo cha anga za juu kilichundwa na kampuni ya kibinafsi nchini Marekani na Japan kimeanza safari kuelekea mwezini kwa kutumia roketi ya SpaceX.
Roketi hiyo aina ya Falcon 9 ilipaa kutoka Kituo cha Anga za Juu cha Kennedy huko Florida saa saba (06:09 GMT) leo Jumatano, ikiwa na wanaanga wa shirika la anga la Marekani la Firefly Aerospace na wenzao wa Japan.
Chombo hicho kitatengana na roketi ya SpaceX kitakapofika kwenye mzunguko wa Mwezi na kufanya uchunguzi huru.
Hii ni safari ya hivi punde ya kibiashara inayoongezeka kuelekea mwezini.
Blue Ghost, inatarajiwa kuchukua takriban siku 45 kufika Mwezini, mara itakapojitenga na roketi ya SpaceX.
Kisha itatoboa, kukusanya sampuli na pia kuchukua picha za X-ray ili "kuendeleza utafiti kwa ajili ya safari ya siku zijazo ya binadamu mwezini na kutoa mwelekeo kuhusu jinsi hali ya anga inavyoathiri sayari", kulingana na SpaceX.
Daniel Chapo aapishwa kuwa Rais wa Msumbiji
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Daniel Chapo, 47, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuliunganisha taifa
Rais mpya wa Msumbiji Daniel Chapo, wa chama tawala cha FRELIMO, ameapishwa rasmi kuwa rais wa Msumbiji katika hafla ya faragha iliyofanywa chini ya ulinzi mkali mjini Maputo.
Kuapishwa kwake kunafuatia miezi kadhaa ya machafuko yaliyosababisa vifo vya watu 300, kulingana na kundi la waangalizi wa uchaguzi la Plataforma Decide.
Katika hotuba yake, Bw. Chapo ameahidi kuzingatia umoja na kuongoza juhudi za maendeleo kote nchini.
Biashara nyingi mjini Maputo zilifungwa baada ya mgombea urais aliyeshindwa Venâncio Mondlane kuitisha mgomo wa kitaifa kupinga kuapishwa kwa Chapo. C
hapo alishinda uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana kwa asilimia 65 ya kura, na kuendeleza utawala wa miaka 49 wa chama cha Frelimo.
Mondlane - ambaye aliwania urais katika uchaguzi huo kama mgombea huru - alishika nafasi ya pili kwa 24% ya kura. Alipinga matokeo hayo akisema yamechakachuliwa.
Vyama vyote viwili vya upinzani nchini Msumbiji - Renamo na MDM - vilisusia sherehe ya kuapishwa kwa Chapo vikidai kuwa ushindi sio halali.
CAR: Uteuzi wa Rigobert Song kama kocha wa timu ya taifa wapingwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rigobert Song aliichezea Cameroon zaidi ya mara 130
Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Afrika ya Kati limepinga kuteuliwa kwa Rigobert Song kama Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya CAR.
CAR FA inasema ilishangaa kwamba waziri wa michezo alimchagua Bw. Song badala ya nahodha wa zamani wa timu ya taifa Eloge Enza Yamissi aliyeteuliwa kuwa naibu wa Bw Song.
Shirikisho hilo limepinga uteuzi huo katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa Jumanne.
Hali kama hiyo ilizuka nchini Cameroon kufuatia kuteuliwa kwa Marc Brys kama kocha wa timu ya taifa ya Cameroon mwaka jana.
Song mwenye umri wa miaka 48 anachukua nafasi ya Mswizi Raoul Savoy, ambaye alitimuliwa Oktoba kuelekea mwisho wa kampeni ya CAR ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 (Afcon) 2025.
Song, ambaye aliichezea Cameroon mara 137 katika kipindi cha miaka 17 ya soka lake la kimataifa aliwahi kuongoza timu ya soka ya nchi yake kwa miaka miwili.
Beki huyo wa zamani wa Liverpool na West Ham aliiongoza Indomitable Lions kwenye michuano ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar na Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana, ambapo timu hiyo ilitolewa katika hatua ya 16 bora.
Raia wa China wahukumiwa kifungo jela kwa uchimbaji haramu wa madini DR Congo
Chanzo cha picha, Reuters
Raia watatu wa China walihukumiwa kifungo cha miaka 7
jela hapo jana Jumanne na kuamriwa kulipa faini ya dola 600,000 kwa kuchimba
madini nchini Kongo kinyume cha sheria, kulingana na kesi zilizowasilishwa
mahakamani.
Washtakiwa hao pia walipatikana na hatia ya ulaghai,
utakatishaji fedha na uporaji. Haijabainika iwapo watasalia katika mji wa
mashariki wa Bukavu, ambako wanazuiliwa, au iwapo watahamishiwa kwingine.
Raia hao walikamatwa Januari 4, wakiwa na dola 400,000 pesa
taslim na vipande 10 vya dhahabu.
Mahakama ya Bukavu pia ilijumuisha kifungo cha miezi
mitatu jela kwa kukaa nchini humo kinyume cha sheria.
Mkoa wa Kivu Kusini una utajiri mkubwa wa dhahabu, eneo
ambalo kwa kiasi kikubwa limetawaliwa na
uchimbaji wa madini, huku baadhi ya migodi ikidhibitiwa na makundi ya waasi yenye
kushirikiana na wafanyabiashara wasio na leseni.
Makampuni mengi ya China yanachimba dhahabu na madini
mengine huko Kivu Kusini, mojawapo ya majimbo ya mashariki mwa DRC ambayo
yamekumbwa na ghasia kutoka kwa makundi yenye silaha kwa takriban miongo
mitatu.
Mnamo 2021, serikali ya Kongo ilisimamisha kampuni sita
za uchimbaji madini za Kichina huko Kivu Kusini kwa kufanya kazi bila idhini
sahihi.
Ukraine yafanya shambulizi kubwa zaidi Urusi - Kyiv
Chanzo cha picha, White Sands Missile Range Public Affairs
Ukraine imeshambulia maeneo kadhaa ya Urusi siku ya
Jumanne katika kile inachosema ni shambulio lake "kubwa zaidi" hadi
sasa.
Maghala ya
kuhifadhia risasi na viwanda vya kemikali vilishambuliwa katika mikoa
kadhaa, baadhi yao ikiwa mamia ya kilomita kutoka mpakani, kulingana na Mkuu wa
Wafanyakazi wa Kikosi cha Wanajeshi cha Ukraine.
Vyanzo vya
shirika la ujasusi la Ukraine SBU viliiambia BBC kwamba shambulio hilo la usiku
lilikuwa "pigo kubwa" kwa uwezo wa Urusi katika vita.
Urusi
ilisema kuwa imedungua makombora ya Atacms yanayotolewa na Marekani pamoja
na makombora ya Uingereza ya Storm Shadow, na kuapa kujibu mashambulizi hayo.
Angalau
viwanja tisa vya ndege katikati na magharibi mwa Urusi vilisimamisha shughuli
zake kwa muda, huku mashambulizi hayo yakisababisha shule za kusini magharibi
mwa mkoa wa Saratov kufungwa.
Mashambulizi
katika eneo la mpakani la Bryansk yalisababisha milipuko katika kiwanda cha
kusafisha mafuta, maghala ya risasi na kiwanda cha kemikali kinachosemekana
kutengeneza baruti na vilipuzi, chanzo cha usalama cha Ukraine kiliiambia BBC.
Maafisa
katika eneo la magharibi la Tula pia waliripoti shambulio la usiku mmoja,
ambapo gavana wa eneo hilo Dmitry Milyaev alisema ulinzi wa anga umedungua
ndege 16 zisizo na rubani.
Hakukuwa na
majeruhi, alisema, ingawa vifusi vinavyoanguka vimeharibu baadhi ya magari na
majengo.
Ukraine
ilisema Urusi pia ilianzisha mashambulizi ya makumi ya ndege zisizo na rubani
kote Ukraine usiku kucha, huku ving’ora vingi vya kutoa onyo vikisikika ndani
na karibu na Kyiv.
Msumbiji: Rais mpya kuapishwa leo huku maandamano yakitarajiwa
Chanzo cha picha, EPA
Rais mteule wa Msumbiji anaapishwa leo Jumatano huku
kukiwa na hofu ya kufanyika kwa "maandamano kote nchini humo", zaidi
ya miezi mitatu tangu kufanyika kwa uchaguzi uliozozaniwa.
Daniel Chapo, mwenye umri wa miaka 48, alipata asilimia
65 ya kura ambayo viongozi wa upinzani, waangalizi wa uchaguzi na wananchi
kwa ujumla walisema kuwa alikuwa na dosari.
Matokeo hayo
yalizua wimbi la maandamano - mengine ya amani lakini mengine ya vurugu - na
kusababisha machafuko, ikiwa ni pamoja na mauaji na uharibifu.
Mpinzani
mkubwa wa Chapo ni Venâncio Mondlane. Wiki iliyopita, alirejea kutoka
uhamishoni alikoenda mwenyewe. Alitumia muda mwingi kuwa nchini Afrika Kusini
ambako anasema alinusurika katika jaribio la mauaji.
Sasa anatoa
wito kwa raia wa Msumbiji kuingia mitaani, kwa mara nyingine tena, siku ya kuapishwa
kwa rais mpya "dhidi ya wezi wa watu".
Afrika Kusini: Jamaa wanasubiri habari za wapendwa wao huku mifuko ya miili ikitolewa kutoka mgodini
Chanzo cha picha, AFP
Waokoaji wametumia siku ya Jumanne kutoa mifuko ya miili
na manusura kutoka ndani ya mgodi wa Afrika Kusini ambapo wachimba migodi
haramu bado wanafikiriwa kuwa angalau kilomita 2 (maili 1.2) chini ya ardhi.
Watu 82
wamejitokeza wakiwa hai kutoka ndani ya mgodi huko Stilfontein tangu shughuli
ya uokoaji ilipoanza Jumatatu, polisi wanasema, huku maiti 36 zikitolewa.
Siku ya
Jumanne, BBC ilishuhudia wachimba migodi waliodhoofika wakitoka ndani ya mgodi –
wakiwa wamevalia nguo chakavu na bila viatu au soksi - walisindikizwa hadi
kwenye hema la matibabu.
Baadhi ya mifuko ya miili ilionekana kuwa miepesi kiasi
kwamba ilibebwa na mtu mmoja tu.
Wanaume hao wamekuwa chini ya ardhi tangu operesheni za
polisi zinazolenga uchimbaji madini haramu kuanza mwaka jana kote nchini humo.
Zaidi ya
wachimba migodi 100 haramu, wanaojulikana na wenyeji kama "zama
zamas", wameripotiwa kufa chini ya ardhi tangu msako mkali wa shughuli zao
ulipoanza katika mgodi huo ulioko kilomita 145 (maili 90) kusini-magharibi mwa
Johannesburg mwaka jana.
Mamlaka hata
hivyo, hazijathibitisha takwimu hii kwa kuwa bado "haijathibitishwa na
chanzo rasmi", msemaji aliiambia BBC.
Ndugu, jamaa
na wanajamii wamekuwa wakiandama kwenye eneo la uchimbaji huku wakiwa na
mabango ya kuitaka mamlaka kuwaokoa wachimbaji hao.
Wanaonekana
kuchoka na kuambia BBC Jumanne kwamba wamechoka kuzungumza na vyombo vya
habari.
Zinzi Tom alieleza kuwa kaka yake mwenye umri wa miaka 29, Ayanda, alishuka mgodini mwezi Juni kwa sababu hakuwa na kazi na alitaka kujikimu kimaisha.
"Tuliuliza kama anapaswa kufanya hivyo, lakini umri wake ni mkubwa, anaweza kufanya chochote anachotaka. Lakini hilo sio la msingi kwa sasa. Kipaumbele ni kwamba tunataka kumuokoa. Tunataka atoke," alisema.
Baadhi ya wachimba migodi waliofanikiwa kutoroka wamemwambia Bi Tom kwamba kakake hayuko sawa. Anatumai atakuwa mmoja wa wale waliookolewa hivi karibuni.
Bi Tom anamuelezea kaka yake kuwa mtulivu na msiri, akiongeza: "Ninahitaji kuwa na nguvu kwa ajili yake, kwa sababu siwezi kuwa dhaifu kipindi hiki. Ananihitaji zaidi kuliko hapo awali."
Hali ya sintofahamu miongoni mwa ndugu waliokuwa nje ya mgodi huo ilizidi kuwa mbaya wakati msafara uliokuwa umembeba waziri wa rasilimali madini Gwede Mantashe na waziri wa polisi ulipofika eneo hilo.
Serikali imekosolewa kwa kuchukua msimamo mkali dhidi ya wachimbaji haramu kwa kuzuia wasipewe chakula wala maji. Pia walifunga njia zote za kutoka mgodini isipokuwa moja.
Wiki iliyopita mahakama iliamuru serikali kuwezesha shughuli ya uokoaji ambayo ilikuwa imechelewa kwa muda mrefu.
Mamlaka imetetea madai ya kujikokota katika kushughulikia suala hili na katika mkutano na waandishi wa habari nje ya mgodi Mantashe alisema "vita dhidi ya uchimbaji haramu" inapaswa kuongezwa.
"Ni uhalifu dhidi ya uchumi, ni shambulio kwa uchumi," alisema.
Tazama: Wachunguzi wakiondoka kwenye makazi ya rais kufuatia kukamatwa kwa Yoon Suk Yeol
Baada ya kukamatwa
kwa Rais wa Korea Kusini aliyeachishwa kazi, wachunguzi waliondoka katika makazi
ya rais.
Kumekuwa na polisi wengi katika makazi hayo tangu
asubuhi. Hapo awali polisi walisema kulikuwa na takriban maafisa 1,000.
Maelezo ya video, Tazama: Wachunguzi wanaonekana wakiondoka kwenye makao ya rais kufuatia kukamatwa kwa Yoon Suk Yeol
Yoon: 'Huu ni uchunguzi usio halali lakini nitatii'
Chanzo cha picha, Yoon Suk Yeol
Katika taarifa ya video, rais wa Korea Kusini aliyekamatwa
Yoon Suk Yeol anasema amekubali kufika mbele ya Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi,
ambayo inaongoza kesi dhidi yake.
"Niliamua kufika mbele ya CIO, ingawa ni uchunguzi
usio halali, ili kuzuia umwagaji wa damu mbaya," amesema.
"Hata
hivyo, hii haimaanishi kwamba ninaidhinisha uchunguzi wao."
Katika video
hiyo fupi - iliyo chini ya dakika 3 tu - alisema kuwa utawala wa sheria nchini
umevunjwa, na kwamba sio vyombo vinavyomchunguza, wala mahakama zinazowapa hati
ya kukamatwa, walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Alimalizia kwa kusema “japo hizi ni siku za giza...
mustakabali wa nchi hii una matumaini”.
"Kwa wananchi wenzangu nawatakia kila la kheri na
muwe imara. Asanteni."
Yoon akiingia
katika ofisi ya wachunguzi
Dakika
chache baada ya msafara kuondoka katika makao ya rais, Yoon aliwasili katika
Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.
Wachunguzi
walithibitisha kwamba walitekeleza agizo la kukamatwa kwa Yoon.
Wakili wake
Seok Dong-hyun alisema katika ujumbe kwenye Facebook kwamba rais amekubali
kuondoka katika makazi yake na kukutana na wachunguzi ili kuzuia "tukio baya".
Habari za hivi punde, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol aliyefutwa kazi akamatwa - Mamlaka
Chanzo cha picha, Maafisa wa polisi wakiingia katika boma la makazi ya rais ya Rais wa Korea Kusini, Januari 15, 2025.
Rais wa
Korea Kusini aliyeachishwa kazi Yoon Suk Yeol amekamatwa, kulingana na mamlaka,
na kuweka kihistoria nchini humo.
Yoon - ambaye anachunguzwa kwa uasi - ndiye rais wa
kwanza aliye madarakani nchini humo kukamatwa.
Baadhi ya wachunguzi waliingia katika makazi ya Yoon kwa
kutumia ngazi
Wachunguzi waliingia katika makazi ya rais kwa kutumia
ngazi, Yonhap inaripoti.
Walizuiliwa mapema na wabunge wa chama tawala na mawakili
wa Yoon kwenye lango la kuingilia, pamoja na kizuizi cha magari kilichowekwa.
Lakini baadhi ya wachunguzi waliripotiwa kufanikiwa
kufikia eneo hilo kupitia njia iliyo karibu ya kupanda mlima.
Na hivyo ndivyo wachunguzi hao walivyofanikiwa kuingia nyumbani
kwa rais, mamlaka imethibitisha.
Waandamanaji wamekuwa wakionekana mara kwa mara wakikita
kambi katika makazi yake katika kipindi cha wiki chache zilizopita na asubuhi
hii umati mkubwa wa watu ulijitokeza tena - wakitazama jinsi wachunguzi
wanavyoendelea katika jaribio lao la pili la kumkamata Yoon.