Wachunguzi wa Korea Kusini wamtaka kaimu rais arahisishe kukamatwa kwa Rais Yoon
Wachunguzi wa Korea Kusini wamemtaka tena kaimu rais wa nchi hiyo Jumamosi kuamuru idara ya usalama ya rais kufuata agizo la kukamatwa kwa Rais aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol.
Muhtasari
- Trump alalamika kuwa bendera za Marekani zitakuwa nusu mlingoti siku ya kuapishwa kwake.
- Mtu mkongwe zaidi duniani Tomiko Itooka afariki akiwa na umri wa miaka 116
- Wachunguzi wa Korea Kusini wamtaka kaimu rais arahisishe kukamatwa kwa Yoon
- Msamaha wa familia ya muathirika ndio tumaini la mwisho kwa muuguzi wa India anayesubiri kunyongwa nchini Yemen
- Jeshi la Ukraine: Ndege zisizo na rubani 34 zadunguliwa angani juu ya Ukraine
- Ghana yazindua visa ya bila malipo kwa Waafrika wote
- Apple kulipa dola milioni 95 kutatua kesi ya kusikiliza mawasiliano ya watumiaji bila idhini
- Trump kuhukumiwa kwa kutoa pesa kwa ajili ya kuzuia taarifa, lakini jaji aashiria kuwa hatafungwa jela
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi
Trump alalamika kuwa bendera za Marekani zitakuwa nusu mlingoti siku ya kuapishwa kwake

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais mteule Donald Trump amelalamika kwamba bendera za Marekani bado zitakuwa zimeshushwa nusu mlingoti kwa heshima ya marehemu Rais Jimmy Carter wakati wa kuapishwa kwa Trump Januari 20.
Rais Joe Biden aliamuru bendera zishushwe nusu mlingoti kwa siku 30 kutoka siku ya kifo cha Carter mnamo Desemba 29, kama ilivyo kawaida rais wa Marekani anapofariki.
Trump ametangaza mipango ya kuhudhuria ibada ya kumbukumbu ya Carter huko Washington mnamo Januari 9.
"Wanademocrat wote 'wana hasira' kuhusu Bendera yetu nzuri ya Marekani ambayo inaweza kuwa "nusu mlingoti" wakati wa kuapishwa kwangu,"
"Wanafikiri ni vizuri sana, na wanafurahi sana kuhusu hilo, kwa kweli, hawaipendi nchi yetu, wanajifikiria wao tu," Trump alisema.
Trump alisema kutokana na kifo cha Carter wiki iliyopita bendera ya Marekani "kwa mara ya kwanza kabisa wakati wa kuapishwa kwa rais anayeingia madarakani kutafanika huku bendera ikiwa nusu mlingoti."
"Hakuna anayetaka kuona hili, na hakuna Mmarekani anayeweza kufurahishwa nalo. Hebu tuone jinsi litakavyokuwa," alisema.
Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre alisema Ikulu ya White House haina mpango wa kufikiria upya uamuzi huo.
Mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani Tomiko Itooka afariki akiwa na umri wa miaka 116

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamke wa Kijapani, anayetambuliwa kama mtu mzee zaidi duniani na Guinness World Records, amefariki akiwa na umri wa miaka 116.
Tomiko Itooka alifariki katika makazi ya wazee katika jiji la Ashiya, Mkoa wa Hyogo, kulingana na maafisa.
Alikua mtu mzee zaidi ulimwenguni baada ya Maria Branyas Morera wa Uhispania kufariki mnamo Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 117.
"Bi Itooka alitupa ujasiri na matumaini kupitia maisha yake marefu," meya wa Ashiya mwenye umri wa miaka 27 Ryosuke Takashima alisema katika taarifa.
"Tunamshukuru kwa hilo."
Bi Itooka alizaliwa Mei 1908 - miaka sita kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia na mwaka huo huo gari la Ford Model T lilizinduliwa nchini Marekani.
Alithibitishwa kuwa mtu mzee zaidi duniani mnamo Septemba 2024 na akakabidhiwa cheti rasmi cha GWR katika sikukuu ya kuheshimu wazee, ambayo ni sikukuu ya umma ya Japani inayoadhimishwa kila mwaka ili kuwaenzi wazee wa nchi hiyo.
Bi Itooka, ambaye alikuwa mmoja wa ndugu watatu, aliishi na alishuhudia vita vya dunia na magonjwa ya milipuko pamoja na mafanikio ya kiteknolojia.
Akiwa mwanafunzi, alicheza mpira wa wavu na kupanda Mlima Ontake wa mita 3,067 (futi 10,062) mara mbili.
Katika umri wake, alifurahia ndizi na Calpis, kinywaji baridi cha maziwa maarufu nchini Japani, kulingana na taarifa ya meya.
Aliolewa akiwa na umri wa miaka 20, na alikuwa na binti wawili na wana wawili wa kiume, kulingana na Guinness.
Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu alisimamia ofisi ya kiwanda cha nguo cha mumewe. Aliishi peke yake huko Nara baada ya mumewe kufariki mnamo 1979.
Ameacha mtoto mmoja wa kiume na wa kike mmoja na wajukuu watano. Ibada ya mazishi iliandaliwa na familia na marafiki, kulingana na maafisa.
Kufikia Septemba, Japan ilihesabu zaidi ya watu 95,000 ambao walikuwa umri wa miaka 100 au zaidi na 88% kati yao walikuwa wanawake.
Unaweza pia kusoma:
Wachunguzi wa Korea Kusini wamtaka kaimu rais arahisishe kukamatwa kwa Rais Yoon

Chanzo cha picha, Reuters/Tyrone Siu
Maelezo ya picha, Polisi wakijaribu kuwazuia watu wakati wa maandamano ya kumpinga Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, karibu na makazi yake rasmi huko Seoul, Korea Kusini, 4, Januari 2025. Wachunguzi wa Korea Kusini wamemtaka tena kaimu rais wa nchi hiyo Jumamosi kuamuru idara ya usalama ya rais kufuata agizo la kukamatwa kwa Rais aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol.
Siku ya Ijumaa Idara ya usalama, pamoja na wanajeshi, waliwazuia waendesha mashtaka kumkamata Yoon Suk Yeol katika mzozo uliodumu kwa saa sita ndani ya makazi ya Yoon.
Wachunguzi walipata hati ya kumkamata Yoon kutokana na tamko lake la muda mfupi la sheria ya kijeshi mwezi uliopita.
Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi kwa Maafisa wa Vyeo vya Juu, ambayo inachunguza kesi hiyo, ilisema Jumamosi ilimtaka tena kaimu Rais Choi Sang-mok, waziri wa fedha wa taifa hilo, kuamuru idara ya usalama ya rais kuonyesha ushirikiano na agizo la kibali hicho.
Msemaji wa wizara ya fedha alikataa kutoa maoni yake.

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kimekua kibarua kigumu mkukamata Rais Yoon Suk Yeol Polisi walimtaka mkuu wa huduma ya usalama ya rais, Park Chong-jun, kufika kuhojiwa siku ya Jumanne, shirika la habari la Yonhap News liliripoti.
Tangazo la kijeshi la Yoon la Desemba 3 liliishangaza Korea Kusini na kupelekea kutolewa kwa hati ya kwanza ya kukamatwa kwa rais aliye madarakani.
Unaweza pia kusoma:
Guardiola akubali kubeba lawama lawama za kiwango kibovu cha Man City

Chanzo cha picha, Getty Images
Pep Guardiola alisaini mkataba mpya na Manchester City mwezi Novemba
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola anasema anajilaumu kwa mwenendo mbaya wa klabu hiyo.
City, ambao wameshinda taji la Primia Ligi kwa miaka minne iliyopita na katika sita kati ya miaka saba zilizopita, wako pointi 14 nyuma ya vinara Liverpool.
Ushindi wa 2-0 dhidi ya Leister Jumapili ulikuwa ushindi wao wa pili tu katika mechi 14.
Huu ni utendaji mbaya zaidi wa kazi kuwahi kufanywa na meneja huyo mwenye mafanikio makubwa yaliyoshuhudiwa katika Barcelona na Bayern Munich.
"Kuna mambo mengi, mengi [yaliyohusika na kuwa meneja] na nilikosa kitu - kitu ambacho sifanyi vizuri," Guardiola, ambaye amekuwa katika klabu hiyo kwa misimu tisa alisema.
"Mwishowe, unapopoteza michezo mingi ni jukumu la ajabu kwa meneja kuchukua. Kuna kitu ambacho timu inahitaji na kwa kujiamini na sikuweza kukifanya.
"Wito uko kwangu kwanza, sio wachezaji. Kwa kawaida wanashuka kidogo na hiyo ni kawaida. Ilitokea kidogo msimu uliopita pia."
City imekuwa na mwanzo mwepesi kwa misimu iliyopita - na iliwafuata vinara kwa pointi sita au zaidi katika kila moja ya mashindano nne yaliyopita ya taji - lakini haijawahi kufanya vibaya hivi.
"Najilaumu [mwenyewe]. Sio kusema, 'oh jinsi Pep alivyo mzuri' - ni ukweli. Ninaongoza kundi hilo la wachezaji na sikuweza kuwainua. Huu ndio ukweli."
Unaweza pia kusoma:
Msamaha wa familia ya muathirika: Tumaini pekee kwa muuguzi wa India anayesubiri kunyongwa nchini Yemen

Maelezo ya picha, Kwa sasa Nimisha Priya amewekwa katika jela iliyopo katikati ya mji mkuu wa Yemen Sanaa Wanafamilia wa muuguzi wa Kihindi ambaye anasubiri kunyongwa katika nchi ya Yemen iliyokumbwa na vita wanasema wanaweka matumaini yao katika juhudi za mwisho za kumwokoa.
Nimisha Priya, 34, alihukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanamume wa eneo hilo - mshirika wake wa zamani wa biashara Talal Abdo Mahdi - ambaye mwili wake uliokatwakatwa uligunduliwa kwenye tanki la maji mnamo 2017.
Akiwa katika jela kuu la mji mkuu Sanaa, anatazamiwa kunyongwa hivi karibuni, huku Mahdi al-Mashat, rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la waasi wa Kihouthi, akiidhinisha adhabu yake wiki hii.
Chini ya mfumo wa mahakama ya Kiislamu, unaojulikana kama Sharia, njia pekee ya kukomesha unyongaji sasa ni kupata msamaha kutoka kwa familia ya muathiriwa.
Kwa miezi kadhaa, jamaa na wafuasi wa Nimisha wamekuwa wakijaribu kufanya hivi kwa kuchangisha diyah, au pesa ya damu, ili kulipwa kwa familia ya Mahdi, na mazungumzo yamekuwa yakiendelea.
Lakini baada ya muda kuisha, wafuasi wanasema matumaini yao yanategemea kabisa uamuzi wa familia.
Chini ya sheria za Yemen, familia ya Nimisha haiwezi kuwasiliana moja kwa moja na familia ya muathirika na lazima iajiri wanaofanya mazungumzo.
Subhash Chandran, wakili ambaye ameiwakilisha familia ya Nimisha nchini India siku za nyuma, aliiambia BBC kwamba familia hiyo tayari ilikuwa imefadhilisha $40,000 (£32,268) kwa ajili ya familia ya muathiriwa.
Pesa hizo zimetolewa kwa awamu mbili kwa mawakili walioajiriwa na serikali ya India ili kujadili kesi hiyo (kucheleweshwa kwa kupeleka awamu ya pili kuliathiri mazungumzo, Bw Jerome anasema).
Jeshi la Ukraine: Ndege zisizo na rubani 34 zadunguliwa angani juu ya Ukraine

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Urusi limefanya mashambulizi Ukraine kwa kutumia ndege 81, ulinzi wa anga wa Ukraine ukadungua ndege zisizo na rubani 34, na ndege nyingine 47 zilipotea mashinani, Jeshi la anga la Ukraine limeripoti.
Mikoa iliyoshambuliwa ni Poltava, Sumy, Kharkov, Kiev, Chernigov, Cherkasy, Kirovograd, Dnepropetrovsk, Odessa na Nikolaev, imesema ripoti hiyo
Katika mikoa ya Chernihiv na Sumy, nyumba za watu binafsi ziliharibiwa kutokana na mashambulizi hayo
Ijumaa Jeshi la Ukraine lilitoa tahadhari ya uvamizi wa anga kote nchini Ukraine.
Jeshi la anga la Ukraine liliripoti mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi na tisho la mashambulizi ya makombora.
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Daktari wa ngazi ya juu wa Marekani atoa wito kutolewa kwa onyo la saratani kwenye pombe

Chanzo cha picha, Getty Images
Daktari wa ngazi ya juu wa Marekani ametoa wito wa tahadhari ya hatari kwa vileo, sawa na lebo kwenye sigara, kufuatia utafiti mpya unaohusisha vinywaji hivyo na aina saba za saratani.
Ushauri kutoka kwa daktari huyo wa ngazi ya juu wa upasuaji wa Marekani Vivek Murthy anasema "wengi wa Wamarekani hawajui hatari hii" ambayo husababisha takriban visa 100,000 vya saratani na vifo 20,000 kila mwaka nchini Marekani
Itahitaji kitendo cha Congress kubadilisha lebo zilizopo za onyo ambazo hazijaidhinishwa tangu 1988.
Bw Murthy pia ametoa wito wa kutathmini upya viwango vinavyopendekezwa vya unywaji pombe na kuongeza juhudi za elimu kuhusu vileo na saratani.
Daktari Mkuu wa Upasuaji, ambaye ndiye msemaji mkuu wa maswala ya afya ya umma katika serikali ya shirikisho, alisema kuwa pombe ni sababu ya tatu ya saratani inayoweza kuzuilika baada ya tumbaku na unene wa kupita kiasi.
Unaweza pia kusoma:
Ghana yazindua visa ya bila malipo kwa Waafrika wote

Chanzo cha picha, Getty Images
Wamiliki wote wa pasipoti wa Kiafrika sasa wanaweza kuzuru Ghana bila kuhitaji visa, Rais anayemaliza muda wake Nana Akufo-Addo amesema.
Alitangaza mpango huo mwezi uliopita lakini katika hotuba yake ya mwisho ya hali ya taifa siku ya Ijumaa alisema kuwa sera hiyo ilianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka.
Usafiri bila visa ndani ya bara kwa muda mrefu umekuwa hamu kwa wale wanaokuza maadili ya Uafrika na inaonekana kuwa muhimu kwa ushirikiano wa kiuchumi.
Ghana sasa ni nchi ya tano barani Afrika kutoa hii kwa wasafiri kutoka bara zima.
Nchi nyingine ni Rwanda, Ushelisheli, Gambia na Benin.
"Ninajivunia kuidhinisha safari bila viza kwenda Ghana kwa wamiliki wote wa pasipoti wa Kiafrika, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu," Akufo-Addo aliwaambia wabunge katika hotuba yake ya mwisho bungeni kabla ya kujiuzulu wiki ijayo baada ya miaka minane mamlakani.
Unaweza pia kusoma:
Apple kulipa dola milioni 95 kutatua kesi ya kusikiliza mawasiliano ya watumiaji bila idhini

Chanzo cha picha, Getty Images
Apple imekubali kulipa dola milioni 95 ili kutatua kesi inayodai kuwa baadhi ya vifaa vyake vilikuwa vikisikiliza na kurekodi watumiaji bila ruhusa.
Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia imeshutumiwa kusikiliza mazungumzo ya wateja wake kupitia programu yake ya usaidizi ya Siri.
Walalamikaji pia wanadai kuwa rekodi za sauti zilishirikiwa kwa watangazaji wa bidhaa.
Apple, inakanusha kufanya makosa yoyote.
Katika juhudi za awali za kutatua tatizo hilo, kampuni hiyo ilikanusha makosa yoyote ya "kurekodi, kufichua taarifa za watu, au kushindwa kufuta mazungumzo yaliyorekodiwa " bila idhini ya watumiaji.
Mawakili wa Apple pia wanaahidi kuthibitisha kuwa "wamefuta rekodi za sauti za Siri zilizokusanywa na Apple kabla ya mwezi Oktoba, 2019."
Lakini mashtaka hayo yanasema kampuni hiyo iliwarekodi watu ambao bila kukusudia walianzisha msaidizi wa kawaida bila kutumia neno la siri la "Hey, Siri" linalohitajika kutumia programu.
Trump kuhukumiwa kwa kutoa pesa kuzuia taarifa, lakini jaji aashiria kuwa hatafungwa jela

Chanzo cha picha, Reuters
Jaji ameamuru kwamba Donald Trump atahukumiwa Januari 10 katika kesi yake ya fedha mjini New York - chini ya wiki mbili kabla ya kuapishwa kuwa rais.
Jaji wa New York Juan Merchan aliashiria kuwa hatamhukumu Trump kifungo cha jela, mashtaka au faini, lakini badala yake "atamuachilia bila masharti", na akaandika kwamba rais mteule anaweza kufika mahakamani binafsi au kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kusikilizwa.
Trump alijaribu kutumia ushindi wake wa urais ili kesi dhidi yake ifutwe.
Rais mteule amechapisha kwenye mitandao ya kijamii akitupilia mbali amri ya jaji huyo kama "shambulio la kisiasa lisilo halali" na kuiita kesi hiyo kuwa "hakuna chochote isipokuwa ni wizi wa kura".
Trump alipatikana na hatia mwezi Mei kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara zinazohusiana na malipo ya $130,000 (£105,000) kwa nyota wa filamu za watu wazima Stormy Daniels.
Mashtaka yanayohusiana na majaribio ya kuficha malipo kwa mwanasheria wake wa zamani, Michael Cohen, ambaye katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi wa 2016 alimlipa pesa nyota huyo wa filamu za watu wazima ili kukaa kimya kuhusiana na madai ya kukutana na Trump.
Rais mteule amekana kufanya makosa yote na kusema kuwa hana hatia, akidai kuwa kesi hiyo ilikuwa jaribio la kudhuru kampeni yake ya urais mwaka 2024.
Katika makala yake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth siku ya Jumamosi Trump alisema amri ya jaji "inakwenda kinyume na katiba yetu na, ikiwa itaruhusiwa, itakuwa mwisho wa urais kama tunavyojua".
Msemaji wa Trump Steven Cheung awali aliita amri hiyo kuwa sehemu ya "hila".
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu tena kwa matangazo ya mubashara leo ikiwa ni Jumamosi 04.01.2025
