Mzozo wa DRC: Mawaziri wa SADC na EAC wataka suluhu ya kudumu
Mawaziri hao wamekutana leo mjini Dar Es Salaam, Tanzania katika kikao kinachotangulia mkutano wa marais wa jumuiya hizo utakaofanyika hapo kesho ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Muhtasari
- Mawaziri wa SADC na EAC wataka suluhu ya kudumu DRC
- Marekani yatishia kuiwekea vikwazo Rwanda na Congo
- USAID inaweza kubakisha wafanyakazi chini ya mia tatu pekee
- Mamlaka ya Alaska yatafuta ndege ndogo iliyoripotiwa kutoweka
- Nyoka wenye sumu zaidi ya 100 wagunduliwa nyuma ya nyumba Sydney
- 'Tutahakikisha kwamba wanajeshi wetu wanarejea nyumbani' - Ramaphosa kuhusu wanajeshi nchini DRC
- Mawaziri wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakutana kuhusu mzozo wa DRC
- 'Watumiaji wa tovuti ya kujitoa uhai walimhimiza kijana wetu kunywa sumu'
- Uingereza yamfukuza mwanadiplomasia wa Urusi baada ya mzozo wa kijasusi
- Jaji asitisha mpango wa Trump wa kuwapatia fedha wafanyakazi wa serikali ili wajiuzulu
- Silaha za Ukraine: Marekani, Uingereza na mataifa mengine yanaipatia Ukraine silaha gani?
- Jaji asitisha mpango wa Trump wa kuwapatia fedha wafanyikazi wa serikali ili wajiuzulu
- Trump aiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na kuitaja kuwa ''kinyume cha sheria''
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma
Mzozo wa DRC: Mawaziri wa SADC na EAC wataka suluhu ya kudumu,

Chanzo cha picha, Wizara ya masuala ya kigeni Kenya
Na Peter Mwangangi, BBC Swahili
Mawaziri wa nchi za Jumuiya za maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki (EAC) wanataka suluhu ya kudumu kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mawaziri hao wamekutana leo mjini Dar Es Salaam, Tanzania katika kikao kinachotangulia mkutano wa marais wa jumuiya hizo utakaofanyika hapo kesho ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
“Hali ya usalama nchini DRC bado ni mbaya na inaathiri hali ya kibinadamu na kutishia usalama wa ukanda. Tunakutana sote hapa, tukiwa na mioyo ya kupata suluhu ya kudumu," amesema Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa mambo ya nje, Tanzania.

Chanzo cha picha, Wizara ya masuala ya kigeni ya Kenya
Waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi ambaye ni mwenyekiti-mwenza wa mkutano huo amesema kuwa hii ni fursa mwafaka kwa EAC na SADC kuwasaidia watu wa DRC, akisema kwamba kuna haja ya kutekeleza kwa haraka mapendekezo ya mkutano wa marais.
“Hali hii inahitaji tuchukue hatua za haraka, kwa pamoja, na kwa njia endelevu," amesema Mudavadi.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wameuteka mji wa mashariki wa Goma, wamekuwa wakikabiliana vikali na majeshi ya serikali ya DRC.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibua watu 3,000 wamefariki kufuatia makabiliano baina ya M23 na wanajeshi wa serikali.
Soma zaidi:
Marekani yatishia kuiwekea vikwazo Rwanda na Congo

Marekani imeonya juu ya uwezo wa kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa Rwanda na Congo kabla ya mkutano wa kilele uliokusudiwa kushughulikia mzozo wa Mashariki mwa Congo, kulingana na barua ya kidiplomasia iliyoonekana na Reuters siku ya Ijumaa.
Congo na Rwanda wamekuwa wakilaumiana kwa mzozo ulioanza tena mashariki mwa Congo, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji mkuu wa mkoa Goma na wanaendelea katika maeneo mengine zaidi.
Ujumbe wa kidiplomasia uliotumwa Ijumaa na Marekani kwenda Kenya, ambayo ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na imekuwa mpatanishi katika mzozo huo, ulisema utulivu katika eneo hilo utahitaji jeshi la Rwanda "kuondoa vikosi vyake na silaha" nchini Congo.
"Tunapotoa matakwa haya kwa pande zote mbili, tutazingatia kuweka vikwazo dhidi ya wasio washirika, pamoja na maafisa wa jeshi na serikali katika serikali zote mbili," taarifa hiyo ilisema.
Soma zaidi:
USAID inaweza kubakisha wafanyakazi chini ya mia tatu pekee

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la misaada ya kigeni la Marekani (USAID) linaweza kupunguza wafanyikazi wake kutoka karibu 10,000 hadi chini ya 300 ulimwenguni kote wakati utawala wa Trump unapunguza matumizi ya serikali.
Wafanyikazi karibu wote isipokuwa wachache tu waliopo katika nyadhifa za lazima wanalazimika kuanza likizo usiku wa manane Ijumaa, ikiwa ni pamoja na maelfu walio nje ya nchi.
Ilani mtandaoni inasema mipango inaandaliwa kwa kusafiri kwa kurudi na kusitishwa kwa mikataba isio muhimu.
Chama kimoja kinachowakilisha wafanyikazi - ambacho kimepinga mpango huo kisheria - kiliambia mshirika wa BBC wa Marekani CBS News kwamba ni wafanyakazi 294 pekee ambao wanachukuliwa kuwa muhimu.
Vikwazo vya Trump kwa USAID - vilivyochangiwa na mshauri wake wa suala la kupunguza gharama Elon Musk – vimefanya mabadiliko katika mfumo wa kutoa misaada ya kimataifa, na mamia ya programu tayari zimesitishwa nchi Marekani na duniani kote.
Soma zaidi:
Mamlaka ya Alaska yatafuta ndege ndogo iliyoripotiwa kutoweka

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Marekani inatafuta ndege ndogo iliyobeba watu 10 ambayo imeripotiwa kutoweka katika jimbo la Alaska.
Walinzi wa Pwani wa Marekani katika eneo la Alaska walisema ndege ya Cessna Caravan ilikuwa maili 12 (km 19) nje ya pwani kutoka Unalakleet hadi Nome wakati "ilipopotea kwenye rada".
Wafanyakazi wa uokoaji "wanajitahidi kutafuta mawasiliano ya mwisho" ya ndege hiyo, maafisa wa serikali walisema katika taarifa.
Walisema walikuwa wamearifiwa kuhusu ndege "iliyochelewa" inayoendeshwa na shirika la ndege la Bering Air saa 16:00 kwa saa za eneo siku ya Alhamisi.
Watu 10 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa ni abiria tisa na rubani, taarifa kutoka Idara ya Usalama wa Umma ya Alaska ilisema.
Hakukuwa na taarifa zilizopatikana mara moja kuhusu ni nani aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.
BBC imewasiliana na Bering Air kwa maoni.
Pia unaweza kusoma:
Nyoka wenye sumu zaidi ya 100 wagunduliwa nyuma ya nyumba Sydney

Chanzo cha picha, Reptile Relocation Sydney
Wahudumu wa wanyama wanaotambaa nchini Australia wamepigwa na butwaa walipojikuta wakiwaokoa nyoka 102 wenye sumu kutoka kwenye eneo lililokuwa na rundo la mchanga nyuma ya nyumba huko Sydney.
Cory Kerewaro alisema waliitwa kuokoa "rundo" la wanyama hao watambaao baada ya mmoja kuripotiwa kumng'ata mbwa katika eneo hilo.
Wakati mwenzake alipofika, aligundua nyoka 40 wa rangi nyeusi – wanne waligundulika kuwa wameangua mayai yao wakiwa na nyoka wao wadogo waliowekwa kwenye karatasi.
Nyoka mweusi mwenye tumbo jekundu ni moja ya spishi zenye sumu huko Australia lakini hawajasababisha vifo kwa binadamu kwa yeyote.
Nyoka hao watano waliokomaa na watoto 97 kwa sasa wamewekwa karantini na wataachiliwa katika mbuga ya wanyama pindi hali ya hewa itakapokuwa nzuri.
Bw Kerewaro alisema ilikuwa ni kumbukumbu kubwa kwa washika nyoka hao, ambao kwa kawaida hukamata kati ya wanyama watambaao watano hadi 15 kwa siku.
Soma zaidi:
Mtangazaji nguli wa Kenya Leonard Mambo Mbotela amefariki

Chanzo cha picha, Mtandao wa Kijamii
Tasnia ya habari nchini Kenya inaomboleza kifo cha mwanahabari nguli Leonard Mambo Mbotela aliyefariki akiwa na umri wa miaka 84.
Mbotela amefanya kazi ya uandishi wa habari kwa zaidi ya miongo mitano, lakini tukio lililoandikisha historia katika maisha yake ni jaribio la mapinduzi ya mwaka 1982 ambapo baadhi ya wanajeshi wakati huo walitaka kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa wakati huo Danie Arap Moi.
Wanajeshi hao waasi walimchukua nyumbani kwake na kumpeleka katika kituo cha redio cha Sauti ya Kenya VOK na kumlazimisha atangaze kuwa serikali ya Rais Moi imepinduliwa.
Pia atakumbukwa kwa kipindi chake cha Jee Huu ni Ungwana alichokifanya kwa ucheshi uliowakonga mioyo wasikilizaji wake na ambacho kilopeperushwa hewani kwenye Redio na ba baadaye kwenye Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Kenya KBC.
Kipindi hicho kilianzishwa mnamo 1966 na kilipeperushwa hewani kwa takriban miaka 55.
'Tutahakikisha kwamba wanajeshi wetu wanarejea nyumbani' - Ramaphosa kuhusu wanajeshi nchini DRC

Chanzo cha picha, Cyril Ramaphosa/X
Maelezo ya picha, Rais Ramaphosa alitoa hotuba kwa taifa usiku wa kuamkia leo Akizungumza kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Afrika kusini katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Rais Cyril Ramaphosa, alisema watafanya kazi "ili wanajeshi wetu wanarudi nyumbani".
Katika hotuba yake kwa taifa jana usiku, Ramaphosa - ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa nchini mwake kwa siku kadhaa baada ya wanajeshi 14 wa nchi yake kuuawa katika mapigano katika wiki za hivi karibuni DRC- alisema suluhu la amani lazima lipatikane.
Afrika Kusini imetuma zaidi ya wanajeshi 1,000 katika kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusaidia jeshi la DRC kupambana na waasi wa M23.
Alisema: "Tunatoa wito kwa pande zote kuafiki juhudi za kidiplomasia zinazoendelea za kutafuta suluhu la amani, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mazungumzo ya Luanda."
Amethibitisha kuwa atahudhuria mkutano wa wakuu wa EAC na SADC unaoanza Ijumaa hii na kumalizika kesho Jumamosi, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Kuhusu mkutano wa Dar es Salaam, Ramaphosa alisema: "Tutasisitiza wito wetu wa kusitishwa kwa uhasama na kuanza tena mazungumzo ili kufikia suluhu la kweli na la kudumu, na tutajitahidi kuhakikisha wananajeshi wetu wanarejea nyumbani."
Baadhi ya wabunge wa bunge la Afrika Kusini wiki hii walilaani uamuzi wa nchi hiyo kutuma wanajeshi wake DR Congo, na kwamba Wizara ya Ulinzi bado haijapata miili ya wanajeshi waliouawa huko.
Afrika Kusini, Malawi na Tanzania ni nchi za SADC ambazo zimetuma wanajeshi kuisaidia serikali ya DR Congo. Siku ya Jumatano, Rais wa Malawi alitangaza kwamba jeshi la nchi yake linapaswa kujiandaa kurejea nyumbani.
Soma zaidi:
Mawaziri wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana kuhusu mzozo wa DRC

Chanzo cha picha, SADC
Mawaziri wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC wanakutana leo jijini Dar es Salaam, Tanzania kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) kabla ya kikao cha Marais wa jumuiya hizo kitakachofanyika Jumamosi.
Kongamano hilo linatarajiwa kutafuta suluhu ya mzozo mjini Goma, mashariki mwa DRC.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wameuteka mji wa mashariki wa Goma, wamekuwa wakikabiliana vikali na majeshi ya serikali ya DRC.
Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya miili 2,000, ilipatikana imetapakaa mjini Goma wiki jana kufuatia makabiliano baina ya M23 na wanajeshi wa serikali.
Kongamano la viongozi wa SADC na EAC linafanyika huku kukiwa na changamoto ya kuwaleta wadau wote wa mzozo wa DRC.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi, akiapa kutozungumza na waasi wa M23, huku EAC ikipendekeza majadiliano kati ya wote wanaohusika kwenye mzozo huo.
''Suluhu mojawapo la mzozo huu ni kuwawaleta wanasiasa na wadau wote wa mzozo huu katika meza ya mazungumzo mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Maina Karobia katika mazungumzo na BBC.
''Natumai kwamba kongamano la Dar es salaam la jumuiya za SADC na Afrika Mashariki watavileta vikundi vyote kwenye meza ya mazungumzo, shida zao zitatuliwe vikubaliwe kuwa vitawekwa kwenye serikali na kunyang’anywa silaha’’, alipendekeza Bw Karobia.
Soma zaidi:
'Watumiaji wa tovuti ya kujitoa uhai walimhimiza kijana wetu kunywa sumu'

Chanzo cha picha, Picha ya familia
Maelezo ya picha, Vlad Nikolin-Caisley alifariki tarehe 7 Mei 2024 baada ya kumeza sumu aliyonunua mtandaoni "Nilimwona mwanangu akihangaika kupumua hadi alipokufa," anasema Anna Nikolin-Caisley. "Alifariki kwa uchungu."
Anna anaamini kuwa mtoto wake mdogo, Vlad, 17, "alihimizwa" kumeza sumu na watumiaji wa kikundi cha mtandaoni cha kinachounga mkono kujiua" ambacho bado kinaendelea nchini Uingereza, licha ya kupigwa marufukuy.
Familia ya Vlad imeamua kufichua habari za kuhuzunisha za kifo chake, huko Hampshire mnamo Mei 2024, kama njia ya tahadhari kwa wengine.
Serikali ilisema majukwaa yanapaswa kuondoa maudhui ya maudhui ya kujidhuru wakati sheria mpya zitakapoanza kutumika mwaka huu kama sehemu ya sheria ya usalama mtandaoni .
Uingereza yamfukuza mwanadiplomasia wa Urusi baada ya mzozo wa kijasusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanadiplomasia wa Urusi amefukuzwa nchini Uingereza katika mzozo wa hivi karibuni wa kurushiana maneno baada ya Moscow kumtimua afisa wa Uingereza mwaka jana.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy alisema hatua imechukuliwa "kufuatia hatua ya Urusi ya kumfukuza mwanadiplomasia wa Uingereza" mnamo Novemba.
Urusi ilimshutumu mwanadiplomasia huyo kwa kutoa habari za uongo na ujasusi kama sababu za kumtaka aondoke.
Serikali ilisema Uingereza "haitakubali vitisho kwa wafanyikazi wetu kwa njia hii" na kwamba "hatua yoyote zaidi itakayochukuliwa na Urusi itachukuliwa kama ya uhasama na itajibiwa ipasavyo".
Balozi wa Urusi nchini Uingereza Andrey Kelin, ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu 2019, aliitwa katika Wizara ya mambo ya nje ili kufahamishwa kuwa kibali cha mmoja wa wanadiplomasia wake kimebatilishwa.
"Hatuna msamaha kuhusu kulinda maslahi yetu ya kitaifa," Lammy alisema.
"Ujumbe wangu kwa Urusi uko wazi - ikiwa utachukua hatua dhidi yetu, tutajibu."
Unaweza pia kusoma:
Jaji asitisha mpango wa Trump wa kuwapatia fedha wafanyakazi wa serikali ili wajiuzulu

Chanzo cha picha, Getty Images
Jaji wa Marekani amesitisha kwa muda mpango wa Rais Donald Trump wa kutoa motisha kwa wafanyikazi wa shirikisho kujiuzulu kwa hiari kabla ya makataa ya Alhamisi usiku wa manane.
Jaji wa shirikisho George O'Toole Jr alisema mpango huo utasitishwa hadi kesi itakaposikilizwa siku ya Jumatatu ambapo ataweza kubaini uhalali wa kesi iliyowasilishwa na vyama vya wafanyakazi vya serikali, limeripoti shirika la habari la CBS, mshirika wa BBC wa Marekani.
Mpango wa kuwalipa wafanyakazi wanaojiuzulu kwa hiari ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za utawala wa Trump za kupunguza ukubwa wa serikali ya shirikisho.
Ikulu ya Marekani inasema zaidi ya wafanyakazi 40,000 wamekubali ombi la kujiuzulu ili wapate malipo hadi kufikia tarehe 30 Septemba.
Baadhi ya wafanyikazi wametoa maoni ya mkanganyiko kuhusu masharti ya mpango huo.
Unaweza pia kusoma:
Trump aiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na kuitaja kuwa 'si halali'

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Hapo awali Trump aliwaidhinisha maafisa wa ICC wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani mnamo 2020. Rais Donald Trump ametia saini amri ya utendaji inayoiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, akiituhumu kwa "vitendo vinavyokiuka sheria na visivyo na msingi vinavyoilenga Marekani na mshirika wetu wa karibu Israel".
Hatua hiyo inaiwekea vikwazo vya kifedha na visa kwa watu binafsi na familia zao wanaosaidia katika uchunguzi wa ICC wa raia au washirika wa Marekani.
Trump alitia saini hatua hiyo wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akizuru Washington.
Novemba mwaka jana, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, jambo ambalo Israel inakanusha. ICC pia ilitoa kibali cha kukamatwa kwa kamanda wa Hamas.
Amri ya utendaji ya Trump ilisema hatua za hivi majuzi za ICC "ziliweka historia ya hatari" ambayo inahatarisha Wamarekani kwa kuwaweka kwenye "unyanyasaji na uwezekano wa kukamatwa".
"Tabia hii mbovu nayo inatishia kukiuka uhuru wa Marekani na inadhoofisha kazi muhimu ya usalama wa kitaifa na sera ya kigeni ya serikali ya Marekani na washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Israel," amri hiyo ilisema.
Marekani si mwanachama wa ICC na mara kwa mara imekataa mamlaka yoyote ya chombo hicho juu ya maafisa wa Marekani au raia.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya Ijumaa tarehe 07.02.2025
