Marekani yaituhumu Rwanda kukiuka mkataba wa amani Mashariki mwa DRC

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa hatua za Rwanda katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya demokrasia ya Congo (DRC) zinakiuka makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump.

Muhtasari

  • Marekani yaituhumu Rwanda kukiuka mkataba wa amani Mashariki mwa DRC
  • Mashabiki wenye hasira wazua taharuki, wamrushia chupa Messi
  • Mfalme Charles apongezwa kwa ujumbe unaohamasisha kupima saratani mapema
  • Mapigano ya Thailand na Cambodia yaendelea licha ya Trump kusema wamekubali kusitisha mapigano
  • Witkoff kukutana na Zelensky kwa mazungumzo ya kukomesha vita Ukraine
  • Rais Kagame asema Rwanda haihusiki na ukiukwaji wa makubaliano na DRC
  • EU yaunga mkono kuzuia fedha za Urusi bila kikomo kabla ya mpango wa mkopo kwa Ukraine

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Marekani yaituhumu Rwanda kukiuka mkataba wa amani Mashariki mwa DRC

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa hatua za Rwanda katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya demokrasia ya Congo (DRC) zinakiuka makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump.

    Amesema hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa ahadi zilizotolewa chini ya makubaliano hayo zinaheshimiwa.

    Kwa upande wake, Rwanda imeituhumu DRC kwa kupuuza usitishaji mapigano na kuendeleza mashambulizi yake ya kurejesha maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23.

    Waziri wa Mambo ya kigeni wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, ameonyesha kushangazwa na madai yakuishutumu Rwanda kwa mapigano mapya, akisema kuwa waasi wa M23 walikuwa wakijibu mashambulizi kutoka kwa majeshi ya Congo.

    Kauli yake inajiri baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kuituhumu Rwanda kwa kuchochea eneo la Maziwa Makuu kuelekea vitani.

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameudhibiti mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Kivu Kusini, karibu na mpaka wa Burundi.

    Umoja wa Mataifa unasema kuwa ghasia za hivi karibuni zimesababisha zaidi ya watu laki mbili kuhama makazi yao.

    Soma zaidi:

  2. Mashabiki wenye hasira wazua taharuki, wamrushia chupa Messi

    xcv

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kwa msaada wa maafisa usalama Messi aliondolewa uwanjani, vyombo vya habari nchini India vinasema hali ilibadilika kuwa mbaya.

    Mashabiki wenye hasira waliohudhuria ziara ya Lionel Messi nchini India walirarua viti na kurusha vitu kuelekea uwanjani baada ya kuonekana katika Uwanja wa Salt Lake mjini Colkata.

    Maelfu ya mashabiki wanaomuhusudu walilipia hadi rupia 12,000 (£100; $133) ili kumwona nyota huyo wa mpira wa miguu, lakini alipojitokeza kutembea uwanjani, na akafichwa na kundi kubwa la maafisa na watu mashuhuri.

    Mshambuliaji huyo wa Argentina na Inter Miami alipoondolewa mapema na maafisa usalama baada ya takriban dakika 20, baadhi ya watu katika umati walipata ghadhabu.

    Waziri mkuu wa West Bengal, Mamata Banerjee, alisema "alifadhaishwa sana na kushtushwa" na matukio hayo.

    Messi anafanya ziara ya “GOAT (Greatest of All Time)” nchini India, ikiwa ni mfululizo wa matukio ya matangazo yanayofanyika Kolkata, Hyderabad, Mumbai na Delhi.

    Ziara yake ilianza kwa uzinduzi wa sanamu yake yenye urefu wa futi 70 (mita 21) huko Kolkata, ambayo ilijengwa kwa kipindi cha siku 27 na jopo ya watu 45.

    Messi alitumia njia ya mtandao kuonana na mashabiki kutokana na sababu za kiusalama.

    Maelfu ya mashabiki walisafiri hadi uwanja wa jiji hilo kwa matumaini ya kupata nafasi ya kumuona mchezaji huyo wa soka ana kwa ana.

    Soma zaidi:

  3. Mfalme Charles apongezwa kwa ujumbe unaohamasisha kupima saratani mapema

    cvx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mfalme Charles

    Mfalme Charles amepongezwa kwa uwazi wake katika kuzungumzia matibabu yake ya saratani ambapo alisisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kiafya mapema.

    Katika ujumbe wa video uliorekodiwa, uliotangazwa kwenye Channel 4 ukilenga kampeni ya Stand Up To Cancer, Mfalme alisema matibabu yake yanapungua na aliwasihi watu kukubali fursa za bure za kufanyiwa uchunguzi wa saratani, akisema "uchunguzi wa mapema unaokoa maisha kwa urahisi."

    Hata hivyo bado haijawekwa wazi aina ya saratani anayotibiwa Mfalme huyo, mwenye umri wa miaka 77, ataendelea kupokea matibabu na ufuatiliaji.

    Clare Garnsey, mkurugenzi mshiriki wa matibabu wa Greater Manchester Cancer Alliance, alisema ujumbe wake ulikuwa "mwenye nguvu sana".

    Mfalme huyo, ambaye alifichua ugonjwa wake Februari mwaka jana, hajaelezewa kuwa yuko katika hali ya kupona kabisa au “amepona”, lakini utaratibu wa matibabu yake utapunguzwa kwa kiasi kikubwa katika mwaka ujao.

    Katika ujumbe wake wa video, uliorekodiwa Clarence House wiki mbili zilizopita, alisema kuwa alihuzunika kujua kuwa watu milioni tisa kote Uingereza hawajafanya uchunguzi wa saratani.

    Soma zaidi:

  4. Mapigano ya Thailand na Cambodia yaendelea licha ya Trump kusema wamekubali kusitisha mapigano

    xcv

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Mapigano kati ya vikosi vya Thailand na Cambodia yaliendelea mapema Jumamosi saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema nchi hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano.

    Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul alisema alimwambia Trump kwamba kusitisha mapigano kutawezekana tu baada ya Cambodia kuondoa vikosi vyake vyote na kuondoa mabomu ya ardhini.

    Aliandika kwenye mitandao ya kijamii: "Thailand itaendelea na oparesheni ya kijeshi hadi tutakapohisi hakuna madhara na vitisho tena kwa ardhi yetu na watu wetu.

    Nataka kuweka wazi. Vitendo vyetu asubuhi ya leo tayari vimezungumza."

    Pande zote mbili ziliripoti kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu na kubadilishana mizinga kuvuka mpaka Jumamosi.

    Soma zaidi:

  5. Witkoff kukutana na Zelensky kwa mazungumzo ya kukomesha vita Ukraine

    xcv

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff atafanya mazungumzo na viongozi wa Ulaya mjini Berlin mwishoni mwa wiki

    Mjumbe wa masuala ya kigeni wa Rais wa Marekani Donald Trump atasafiri kwenda Ujerumani wikendi hii kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi wa Ulaya kwa ajili ya mazungumzo ya hivi karibuni ya ngazi ya juu kuhusu kukomesha vita.

    Steve Witkoff, ambaye amekuwa akiongoza majaribio ya Ikulu ya White House ya upatanishi kati ya Ukraine na Urusi, atajadili katika duru nyingine ya makubaliano ya amani yaliyopendekezwa huko Berlin.

    Utawala wa Trump unashinikiza makubaliano yafanyike ifikapo krismasi na amekuwa na mazungumzo kadhaa na wawakilishi wa Ukraine na Urusi katika wiki za hivi karibuni, ingawa kumekuwa na matumaini kidogo ya mafanikio kufikiwa.

    Bado haijathibitishwa ni viongozi gani wa Ulaya watahudhuria mazungumzo ya Berlin.Bottom of Form

    Gazeti la The Wall Street Journal, ambalo liliripoti kwa mara ya kwanza maelezo ya mkutano huo, lilisema kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wote watashiriki.

    Soma zaidi:

  6. Rais Kagame asema Rwanda haihusiki na ukiukwaji wa makubaliano na DRC

    Tshisekedi na Kagame

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema nchi yake haihusiki na ukiukwaji wa makubaliano yaliyosainiwa baina yake,Marekani na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo wiki iliyopita mjini Washington.

    Akizungumza mjini Kigali Rais Kagame amesisitiza kwamba mapigano mashariki mwa Congo yamekuwa yakiendelea hata kabla ya mapatono hayo kutiwa saini.

    Congo na nchi za magaharibi wamekuwa wakiishtumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23 waliouteka mji wa Uvira katika Kivu ya kusini mapema wiki hii mara tu baada ya makubaliano hayo kusainiwa.

    Akizungumza katika khafla ya kuapisha baadhi ya viongozi walioteluliwa serikalini,Rais Paul Kagame amesema yeye binafsi amekuwa chini ya shinikizo kubwa hasa na tuhuma zinazoihusisha Rwanda katika vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

    Alisema kuwa mkataba kati ya Rwanda,DRC na Marekani ulitiwa saini mjini Washington mnamo tarehe 4 mwezi huu nchi yake ilishiriki kwa hiari na kwa nia ya amani huku akisema Rwanda imeukubali na itatii matakwa yake ili makubaliano hayo yaweze kuongoza nchi mbili kwa amani.

    “Rwanda ilisaini makubaliano kwa hiari na iko tayari kutii kile inachotakiwa kufanya ili makubaliano kama yatatekelezwa ipasavyo na kila upande kutii majukumu yaje ,yaweze kuzifikisha nchi mbili kwa amani.ni kweli siyo rahisi na mara nyingi inakuwa ngumu,wapo wasiosema ukweli au kukosa kile wanachokitaka kwenye makubaliano, "Katika mkataba, haupati kila kitu unachotaka, lakini unapata kile unachohitaji na mtu mwingine anapata kile ambacho ni muhimu kwake."

    Unaweza kusoma;

  7. EU yaunga mkono kuzuia fedha za Urusi bila kikomo kabla ya mpango wa mkopo kwa Ukraine

    Rais wa Ukraine asema ni sawa kwa mali zilizozuiliwa za Urusi kutumika kujenga upya nchi yake

    Chanzo cha picha, Thierry Monasse/Getty Images

    Serikali za Umoja wa Ulaya zimekubali kuzuia mali za Urusi kwa muda usiojulikana za hadi €210bn (£185bn) ambazo zimezuiliwa katika EU tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi dhidi ya Ukraine.

    Fedha nyingi za Moscow zimehifadhiwa katika benki ya Ubelgiji ya Euroclear, na viongozi wa Ulaya wanatumai kukubaliana katika mkutano mkuu wa EU wa wiki ijayo ambao utatumia pesa hizo kwa mkopo kusaidia Kyiv kufadhili jeshi lake na uchumi.

    Baada ya karibu miaka minne ya vita vya Urusi, Ukraine inaishiwa na pesa taslimu, na inahitaji takriban €135.7bn (£119bn; $159bn) katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

    Ulaya inalenga kutoa theluthi mbili ya pesa hizo, lakini maafisa wa Urusi wanaishutumu EU kwa wizi.

    Benki Kuu ya Urusi ilisema Ijumaa kuwa inaishtaki benki ya Ubelgiji Euroclear katika mahakama ya Moscow, kujibu mpango wa mkopo wa EU.

    Mali za Urusi katika EU zilizuiliwa ndani ya siku chache baada ya uvamizi wa Ukraine mnamo Februari 2022, na euro bilioni 185 kati ya hizo zinashikiliwa na Euroclear.

    EU na Ukraine zinasema kwamba pesa zinapaswa kutumika kujenga upya kile ambacho Urusi imeharibu: Brussels inakiita "mkopo wa fidia" na imekuja na mpango wa kuunga mkono uchumi wa Ukraine hadi kufikia euro bilioni 90.

    Unaweza kusoma;

  8. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu