Raia wa Venezuela wakabiliana na polisi baada ya matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na utata

Vikosi vya usalama vilifyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira dhidi ya raia huku maelfu ya watu wakikusanyika mjini Caracas.

Muhtasari

  • Israel imethibitisha kufanya shambulizi la kulipiza kisasi nchini Lebanon
  • Rais Ruto amteua Dorcas Oduor kuwa Mwanasheria mkuu wa Kenya
  • Waandamanaji wa Israel wavamia kambi ya jeshi baada ya wanajeshi kuzuiliwa kwa unyanyasaji wa wafungwa wa Gaza
  • Ukraine yaelezea wasiwasi kuhusu manowari za Urusi katika Bahari Nyeusi
  • Saudi Arabia yawasilisha rasmi nia ya kugombea kuandaa Kombe la Dunia la Soka la 2034
  • Macron anatoa wito kwa rais mpya wa Iran kuacha kuiunga mkono Urusi
  • Mfanyabiashara aliyejaribu kumkabili mshambuliaji alichomwa kisu mguuni
  • Sitini na tatu wafariki, makumi kadhaa wanaswa katika maporomoko ya ardhi India
  • Kamanda wa kundi la mamluki la Urusi auawa katika shambulio Mali
  • Shambulizi la kisu laua watoto wawili na tisa kujeruhiwa katika warsha yao ya kucheza densi
  • Wanajeshi wa Israeli watuhumiwa kumdhulumu mfungwa wa Kipalestina
  • Raia wa Venezuela wakabiliana na polisi baada ya matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na utata

Moja kwa moja

Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Tunakushukuru kwa kuwa nasi kwa matangazo haya ya mubashara ya leo, usikose tena kuwa nasi hapo kesho, alamsiki.

  2. Tazama video ya shambulio la Israel nchini Lebanon

    Maelezo ya video, Moshi unafuka kutoka mjini Beirut baada ya Israel kuthibitisha kutekeleza shambulio hilo
  3. Habari za hivi punde, 'Hezbollah ilivuka mstari mwekundu' - waziri wa ulinzi wa Israel

    .

    Chanzo cha picha, AMIR COHEN

    Maelezo ya picha, Yoav Gallant waziri wa ulinzi nchini Israel

    Yoav Gallant, waziri wa ulinzi, hakusema lolote lingine katika chapisho lake fupi la mtandao wa kijamii.

    Mlipuko huu wa leo huko Beirut unajiri baada ya Israel kuilaumu Hezbollah (iliyoko Lebanon) kwa kuua watoto na vijana kumi na mbili katika shambulio kwenye Milima ya Golan inayokaliwa na Israel mwishoni mwa juma.

    Hizbullah imekanusha vikali kuhusika na hili.

  4. Habari za hivi punde, Israel imethibitisha kufanya shambulizi la kulipiza kisasi nchini Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Eneo la kusini mwa Beirut lililoshambuliwa na Israel

    Jeshi la Israel linasema kuwa limefanya shambulizi mjini Beirut, likimlenga kamanda wa Hezbollah ambayeolinasema alihusika na shambulio hilo kwenye milima ya Golan.

    Takriban watoto 12 na vijana waliuawa katika shambulizi la roketi walipokuwa wakicheza kandanda kwenye milima ya Golan inayokaliwa na Israel siku ya Jumamosi.

    Mlipuko mmoja umedaiwa kupiga kitongoji cha kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, ambao ni ngome ya kundi la Lebanon linaloungwa mkono na Iran Hezbollah.

    Jeshi la anga la nchi hiyo limelaumu kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran Hezbollah kwa shambulio la Jumamosi kwenye mji wa Druze wa Majdal Shams, lakini Hezbollah imekanusha vikali kuhusika kwa vyovyote vile.

  5. Afueni huku wagonjwa huku Wapalestina wakiondoka Gaza

    g
    Maelezo ya picha, Vita huko Gaza vimesababisha ugumu wa kuwaondoa raia wagonjwa na waliojeruhiwa

    Wapalestina waliojeruhiwa na wagonjwa mahututi wako njiani kutoka Gaza kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu kwa matibabu, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema.

    WHO linasema tukio kubwa zaidi la kuhamishwa kwa wagonjwa kwa ajili ya matibabu kuwahi kushuhudiwa tangu vita vianze kufuatia shambulio la kikatili la Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba.

    Vyanzo vya hospitali vya Gaza vilisema wagonjwa 150 walipandamabasi matano, lakini WHO bado haijathibitisha idadi kamili.

    Operesheni kubwa za kijeshi za Israeli zimeharibu mfumo wa afya wa Gaza.

    WHO inasema hadi sasa takriban raia 5,000 wa Gaza wamepokea matibabu nje ya eneo hilo, lakini wengine 10,000 bado wanahitaji kuondoka.

  6. Afrika Kusini: Msichana anayewania taji la urembo huku akikabiliwa na chuki dhidi ya asili yake

    h

    Chanzo cha picha, Chidimma Adetshina/IG

    Mmoja wa washiriki wa shindano la urembomwaka 2024 'Miss South Africa 2024' anazungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii barani Afrika kutokana na taarifa zake zinazosambaa nchini Afrika Kusini kutokana na asili ya wazazi wake.

    Chidimma Vanessa Adetshina ni miongoni mwa wasichana 16 wanaowania taji lakuwa Mlimbwende wa Africa Kusinimwaka 2024 katika hafla itakayofanyika tarehe 10 mwezi wa Agosti.

    Lakini zaidi ya watu 6,000 tayari wametia saini ombi la kutaka aondolewe kwenye shindano hilo wakisema kwamba "ingawa alizaliwa Afrika Kusini" ana asili ya Nigeria na Msumbiji kwa kwamba hilo "linaiweka fahari ya Afrika Kusini hatarini".

    Waandaji wa shindano hilo waliliambia gazeti la The South Africa kwamba walimkubali Chidimma Vanessa kwa sababu "alikidhi mahitaji yote" ya shindano hilo, ikiwa ni pamoja na kuwa Mwafrika Kusini mwenye kitambulisho au hati ya kusafiria.

  7. Rais Ruto amteua Dorcas Oduor kuwa Mwanasheria mkuu wa Kenya

    k

    Chanzo cha picha, www.odpp.go.ke

    Maelezo ya picha, Iwapo ataidhinishwa na bunge Dorcas Agik Oduor atakuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kenya

    Oduor, ambaye kwa sasa anahudumu kama Katibu wa Mashtaka ya Umma katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), ni wakili wa Mahakama ya Juu mwenye Shahada ya Uzamili ya Kudhibiti Migogoro ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Shahada ya sheria kutoka chuo hicho.

    Kabla ya uteuzi wake, Oduor alishikilia nyadhifa mbali mbali katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya ODPP ikiwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi, Mkuu wa Idara ya uhalifu wa kiuchumi, kimataifa, Naibu mwanasheria mkuu wa serikali, na Wakili wa serikali katika ofisi ya mwanasheria mkuu.

    "Wakili Mkuu Oduor amedhihirisha uadilifu , umahiri wa kitaalamu na kujitolea kwa uthabiti kwa utawala wa sheria. Iwapo ataidhinishwa na Bunge la taifa, Dorcas Agik Oduor atakuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke katika taifa letu," taarifa ya Ruto kwa Baraza la Mawaziri, iliyoandikwa na Mkuu wa Wafanyakazi katika ofisi ya rais, Felix Koskei imeeleza.

    Uteuzi wake ni sehemu ya mabadiliko ya viongozi wa juu wa serikali yanayofanywa na Rais Ruto na baada ya kuwateua baadhi ya mawaziri kufuatia maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali yaliyosababishwa kufutwa kwa baraza la mawaziri.

  8. Waandamanaji wa Israel wavamia kambi ya jeshi baada ya wanajeshi kuzuiliwa kwa unyanyasaji wa wafungwa wa Gaza

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waandamanaji wakiwemo wabunge wa muungano unaoongoza Israel walikusanyika katika kambi ya Sde Teiman

    Tahadhari: Taarifa hii ina maelezo kuhusu unyanyasaji wa kingono

    Waandamanaji wa Israel wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia walivamia kambi ya jeshi wakionyesha uungaji mkono kwa wanajeshi wanaotuhumiwa kumdhulumu vikali mfungwa wa Kipalestina.

    Umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya jengo la Sde Teiman baada ya polisi wa Israel kuingia humo kuwazuilia askari wa akiba, ambao sasa wapo chini ya uchunguzi rasmi.

    Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa taarifa akilaani vikali tukio hilo na kutoa wito wa "kutulizwa kwa hasira mara moja".

    Waandamanaji pia walivunja kambi ya pili ya kijeshi, ambapo askari wa akiba walipelekwa kuhojiwa, lakini msemaji wa polisi alisema maafisa waliweza kutuliza hali

    Kambi ya Sde Teiman, iliyopo karibu na Beersheba kusini mwa Israel, kwa miezi kadhaa kumekuwa na ripoti za unyanyasaji mkubwa dhidi ya wafungwa wa Gaza.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya ndani, takriban wanajeshi tisa wa Israel katika kambi hiyo wanatuhumiwa kumtusi mfungwa huyo wa Kipalestina, anayeshukiwa kuwa mpiganaji wa Hamas ambaye alitekwa Gaza.

    Inasemekana amelazwa hospitalini baada ya kile ripoti za vyombo vya habari vya Israel kueleza kuwa ni unyanyasaji mkubwa wa kingono na majeraha kwenye sehemu yake ya haja kubwa na kusababisha kushindwa kutembea.

    Jeshi la Israel lilisema wakili wake mkuu aliamuru uchunguzi "kufuatia unyanyasaji mkubwa wa mfungwa".

    Tume ya Masuala ya Wafungwa ya Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi (PA) ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kwa haraka kwa kufanya uchunguzi ulioamriwa na Umoja wa Mataifa.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Ukraine yaelezea wasiwasi kuhusu nyambizi za Urusi katika Bahari Nyeusi

    f

    Chanzo cha picha, PLANET LABS PBC

    Maelezo ya picha, Manowari tatu za Urusi ziko katika Bahari Nyeusi

    Nyambizi tatu za Urusi ziko katika Bahari Nyeusi, vikosi vya ulinzi vya Ukraine vinaendelea kufuatilia hali ilivyo, msemaji wa Jeshi la Wanamaji la Ukraine Dmitry Pletenchuk amesema.

    "Hali bado haijabadilika - kuna nyambizi tatu huko sasa. Haya ni kama mafunzo ya kijeshi, lakini hata hivyo, mazoezi huishia mara kwa mara kwa ufyatuaji wa risasi.

    Kwa hivyo, kila wakati mtu anapaswa kutarajia hatari kutokana na vitengo hivi na tunatarajia hilo," Pletenchuk alinukuliwa akisema na shirika la habari la Ukraine -Ukrayinska Pravda.

    Hapo awali, Pletenchuk aliripoti kwamba jeshi la wanamaji la Urusi liliweka manowari tatu, ambazo hutumika kusafirisha makombora ya cruise, ndani ya bahari , na alizungumzia kuhusu mabadiliko ya mbinu za Urusi katika Bahari Nyeusi na Azov.

    Urusi haijatoa taarifa zozote kuhusu ripoti za nyambizi zake katika Bahari Nyeusi.

    Tangu 2022, jeshi la Ukraine limeshambulia zaidi ya meli 20 za Urusi na meli za msaada. Kati ya meli hizo angalau saba ziliharibiwa.

  10. Saudi Arabia yawasilisha rasmi ombi la kuwania kuandaa Kombe la Dunia la 2034

    h

    Chanzo cha picha, Saudi Olympic - X Platform

    Maelezo ya picha, Ujumbe huo uliongozwa na Prince Abdulaziz bin Turki bin Faisal, Waziri wa Michezo, Rais wa Kamati ya Olimpiki na Paralimpiki, Rais wa Shirikisho la Soka la Saudi, Yasser Al-Meshal, na watoto wawili kutoka vituo vya mafunzo vya kikanda vya Chama cha Soka cha Saudia

    Siku ya Jumatatu, Saudi Arabia iliwasilisha rasmi stakabadhi zake kuhusu nia yake ya kugombea kuandaa Kombe la Dunia la 2034 katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, katika hafla iliyofanywa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

    Stakabadhi hizo zilikabidhiwa na ujumbe rasmi ulioongozwa na Mwanamfalme Abdulaziz bin Turki bin Faisal, Waziri wa Michezo, Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki na Walemavu ya Saudia, na Rais wa Shirikisho la Soka la Saudia, Yasser Al-Meshal, pamoja na watoto wawili kutoka vituo vya mafunzo vya kikanda vya Chama cha Soka cha Saudi Arabia.

    Waziri wa Michezo wa Saudia alisema: "Stakabadhi za Ufalme za kugombea kuandaa Kombe la Dunia la 2034 zinanajumuisha maono ya kina na ya wazi ya taifa hili kuu kuelekea mustakabali mzuri - Mungu akipenda."

    Aliongeza: "Ufalme una nia ya kuandaa tukio muhimu zaidi katika ulimwengu wa soka, na hivyo kuthibitisha nafasi yake kubwa, yenye ushawishi na chanya kwenye ramani ya dunia nzima, katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na michezo."

  11. Macron atoa wito kwa rais mpya wa Iran kuacha kuiunga mkono Urusi

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Emmanuel Macron alimpigia simu Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, na kumtaka aache kuiunga mkono Urusi katika vita dhidi ya Ukraine, ofisi ya kiongozi huyo wa Ufaransa imesema.

    Haya yalikuwa mazungumzo ya kwanza ya simu ya kimataifa kati ya marais hao wawili tangu Pezeshkian kushinda uchaguzi na kuchukua madaraka.

    Rais wa Ufaransa pia alitoa wito wa "kila linalowezekana kufanywa ili kuepusha kuongezeka kwa harakati za kijeshi" katika mzozo kati ya Israeli na Lebanon kufuatia shambulio la hivi karibuni la roketi kwenye Milima ya Golan (ambalo lilidaiwa kutekelezwa na kundi la Hezbollahl inayoungwa mkono na Tehran).

    Baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuanza, Iran iliunga mkono hatua za Kremlin na, kwa mujibu wa Kyiv na washirika wake wa Magharibi, Iran iliitumia Urusi silaha zake, zikiwemo ndege zisizo na rubani aina ya Shahed.

    Shambulio lolote linaloweza kufanywa na Israel dhidi ya Lebanon "litakuwa na madhara makubwa kwa Israel", Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron, vinaripoti vyombo vya habari vya Iran.

    Rais mpya wa Iran ametangaza nia yake ya kurejesha uhusiano na nchi za Magharibi.

    Pezeshkian anachukuliwa kuwa mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani akilinganishwa na Ibrahim Raisi, aliyefariki katika ajali ya ndege.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Mfanyabiashara adungwa kisu mguuni baada ya kujaribu kumpokonya silaha mshambuliaji

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Mfanyabiashara wa eneo ambalo kumetokea shambulio la kisu alichomwa kisu mguuni alipokuwa akijaribu kujiweka kati ya watoto, gazeti la Telegraph linaripoti.

    Jonathan Hayes, 63, alikimbilia kwenye studio ya kucheza densi kutoka ofisi yake iliyo jirani baada ya kusikia mayowe, mke wake anasema.

    Anatakiwa kufanyiwa upasuaji baadaye.

    "Alisikia kelele na akatoka nje, akamuona mshambuliaji, tayari alikuwa ameumiza mtoto na akajaribu kumpokonya kisu na kuchomwa mguuni," mkewe, Helen, anasema.

    "Amesikitishwa sana kwamba hakuweza kuwa msaada zaidi. Kimwili atakuwa sawa, lakini kiakili sijui."

    Soma zaidi:

  13. Sitini na tatu wafariki, makumi kadhaa wanaswa katika maporomoko ya ardhi India

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waokoaji wanasaidia wakaazi kuhamia mahali salama

    Takriban watu 63 wameuawa na wengine kadhaa wanahofiwa kukwama baada ya mvua kubwa kusababisha maporomoko makubwa ya ardhi katika jimbo la Kerala kusini mwa India.

    Maporomoko ya ardhi yamekumba maeneo ya vilima katika wilaya ya Wayanad alfajiri ya Jumanne.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea, lakini zinatatizwa na mvua kubwa na kuporomoka kwa daraja muhimu.

    "Tutaweza kutathmini ukubwa wa uharibifu baada ya saa chache," waziri wa serikali AK Saseendran aliambia kituo cha BBC Hindi.

    Bw Saseendran alisema hospitali za eneo hilo zilikuwa zikiwahudumia takriban watu 66 waliojeruhiwa, akiongeza kuwa wafanyikazi wa hospitali hiyo ni miongoni mwa waliotoweka kwenye maporomoko hayo.

    Wayanad, wilaya yenye vilima ambayo ni sehemu ya safu ya milima ya Western Ghats, inakabiliwa na maporomoko ya ardhi wakati wa msimu wa monsuni.

    Timu za serikali na za kitaifa zinaendesha shughuli za uokoaji. Wenyeji kadhaa pia wamekuwa wakisaidia.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Kamanda wa kundi la mamluki la Urusi auawa katika shambulio Mali

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Kamanda wa kundi la mamluki la Urusi ameuawa nchini Mali kufuatia shambulio la wapiganaji wa waasi wakati wa dhoruba ya mchanga, kundi hilo lilisema.

    Utawala wa kijeshi katika jimbo hilo la Afrika Magharibi uligeukia kundi la Wagner mwaka 2021, kutafuta uungwaji mkono katika kupambana na vikosi vya jihadi na wanaotaka kujitenga.

    Siku ya Jumatatu kundi la Urusi - ambalo sasa limejigeuza kuwa kundi linaloitwa Africa Corps yaani Kikosi cha Afrika - lilisema limejiunga na jeshi la Mali katika "vita vikali" dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga na wanamgambo wa jihadi wiki iliyopita.

    Hata hivyo, watu wanaotaka kujitenga walifanya shambulizi kubwa, na kuua takriban mamluki 20 hadi 50, vyanzo vya karibu na Africa Corps viliiambia BBC.

    Vile vile, wanablogu kadhaa wa kijeshi wa Urusi waliripoti kwamba takriban watu 20 waliuawa katika shambulio la kuvizia karibu na mji wa kaskazini-mashariki wa Tinzaouaten.

    Katika taarifa rasmi iliyotumwa kwa Telegram, kundi la mamluki la Urusi halikubainisha ni wanajeshi wangapi waliofariki, lakini walithibitisha kupata "hasara". Hii ni pamoja na kamanda, Sergei Shevchenko, ambaye aliuawa wakati wa makabiliano.

    Hapo awali mamluki hao "waliwaangamiza Waislamu wengi na kuwafanya wengine kukimbia", ilisema taarifa hiyo.

    Soma zaidi:

  15. Shambulizi la kisu laua watoto wawili na tisa kujeruhiwa katika warsha yao ya kucheza densi

    .

    Chanzo cha picha, James Speakman/PA Media

    Watoto wawili wameuawa na tisa kujeruhiwa vibaya huku sita wakiwa hali mahututi katika shambulio la kisu kwenye warsha ya watoto kucheza densi.

    Watu wazima wawili pia wako katika hali mahututi baada ya kudungwa visu walipokuwa wakijaribu kuwalinda watoto katika hafla iliyokuwa imepewa jina Taylor Swift kwenye Mtaa wa Hart huko Southport, Polisi wa Merseyside walisema.

    Mvulana mwenye umri wa miaka 17, kutoka Banks huko Lancashire, amekamatwa kwa tuhuma za mauaji na jaribio la kuua.

    Polisi walisema sababu ya shambulio hilo "haikuwa wazi" lakini haikuchukuliwa kama yenye kuhusishwa na ugaidi.

    Shahidi mmoja alielezea tukio hilo kama "la kutisha" na akasema "hawajawahi kuona kitu kama hicho".

    Mfalme na waziri mkuu wameongoza kwa salamu za rambirambi kwa wale walioathiriwa.

    Polisi wa Merseyside walitangaza kutokea kwa tukio kubwa baada ya kupokea simu za dharura saa 11.47 saa za eneo, wiki ya kwanza ya likizo za shule wakati wa majira ya joto kwa watoto wengi nchini Uingereza.

    Magari ya kujihami, ya kubeba wagonjwa 13 na zima moto walikimbilia eneo la tukio ambapo tamasha la watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 10 lilikuwa likifanyika.

  16. Raia wa Venezuela wakabiliana na polisi baada ya matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na utata

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vikosi vya usalama nchini Venezuela vimerusha mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya raia waliokuwa wameandamana kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi wa Jumapili yenye utata.

    Maelfu ya watu walikusanyika katikati mwa Caracas Jumatatu jioni, wengine wakitembea umbali wa maili kutoka makazi ya vijijini kwenye milima inayozunguka jiji hilo, kuelekea ikulu ya rais.

    Maandamano yalizuka katika mji mkuu wa Venezuela siku moja baada ya Rais Nicolas Maduro kudai kuwa ameshinda.

    Upinzani umepinga ushindi wa Bw Maduro na kuuchukulia kama ulaghai, ukisema mgombea wake Edmundo González alishinda kwa kishindo kwa kupata asilimia 73.2 ya kura.

    Kura za maoni kabla ya uchaguzi huo zilipendekeza ushindi wa moja kwa moja kwa mpinzani.

    Vyama vya upinzani viliungana nyuma ya Bw González katika jaribio la kumng'oa Rais Maduro baada ya kukaa madarakani kwa miaka 11, huku kukiwa na hali ya kutoridhika iliyoenea kutokana na kudorora kwa uchumi nchini humo.

    Nchi kadhaa za Magharibi na Amerika Kusini, pamoja na mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na UN, wametoa wito kwa mamlaka ya Venezuela kutoa rekodi za kupiga kura kutoka vituo vya kupigia kura.

    Kundi kubwa la wanajeshi na polisi, ikiwemo mabomu ya kutoa machozi, walionekana kwenye mitaa ya Caracas kwa lengo la kujaribu kuwatawanya waandamanaji na kuwazuia kukaribia ikulu ya rais.

    Umati wa watu uliimba “Uhuru, uhuru!” na kuitaka serikali kuang’atuka madarakani.

    Soma zaidi:

  17. Bila shaka uko salama msomaji wetu, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 30/07/2024