Jeshi la Israel lilitangaza kuwa jeshi lake la anga lilizuia makombora mawili yaliyorushwa kutoka Yemen siku ya Alhamisi kabla ya kuingia kwenye anga ya Israel.
Ving'ora vya mashambulizi ya anga vilisikika mjini Jerusalem, Tel Aviv na maeneo mengine ya Israel ya kati kufuatia kurushwa kwa roketi kutoka Yemen.
Milipuko mikubwa ilisikika huko Yerusalemu baada ya ving'ora kulia.
Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha vipande vya roketi vikianguka katika mji wa Adh Dhahiriya, karibu na Hebron, kusini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Shirika la utangazaji la Israel limeripoti kuwa mfumo wa ulinzi wa makombora wa Marekani wa THAAD ulishiriki katika kuzuia makombora yaliyorushwa kutoka Yemen kuelekea Israel.
televisheni ya Israel, channel 12, iliripoti kuwa maagizo yalitolewa kwa ndege iliyopangwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion ili kugeuza safari yake kuelekea Larnaca, Cyprus, sanjari na kuzuiwa kwa kombora.
Kwa upande wao, Wahouthi walisema walilenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion na kambi ya kijeshi katikati mwa Israel kwa makombora mawili.
Televisheni ya Al Masirah yenye uhusiano na Waouthi iliripoti kwamba makombora mawili yaliyotumika ni kombora la balistiki la "Dhu al-Fiqar" na kombora la "Palestine 2" la hypersonic.
Kituo hicho kiliongeza kuwa Wahouthi pia walilenga meli za kivita za "maadui" katika Bahari Nyekundu, ikiwa ni pamoja na meli ya kubeba ndege za Marekani Truman.
Waasi wa Kihouthi wanarusha makombora kuelekea Israel kutoka Yemen, kwa kile wanachodai ni "kuiunga mkono Gaza."
Huku Israel ikirejelea operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza takriban siku 10 zilizopita, kasi ya kurusha roketi kutoka Yemen imeongezeka, huku jeshi la Israel ikiripotiwa kuzuia makombora sita katika kipindi cha wiki iliyopita.