Ukraine na Urusi zabadilishana mamia ya wafungwa

Pande zote mbili zilikubaliana kubadilishana wafungwa 1,000 na kuthibitisha kutakuwa na mabadilishano zaidi katika siku zijazo.

Muhtasari

  • Mwanaharakati Agather wa Uganda naye akiri kuteswa kizuizini Tanzania
  • Ukraine na Urusi zabadilishana mamia ya wafungwa wa vita
  • Kangaruu ajaribu kumzamisha mtu katika mafuriko huko Australia
  • Kabila la Amazon lalishitaki gazeti la Marekani juu ya ripoti kuhusu uraibu wa picha za ngono
  • Binti Mfalme wa Ubelgiji ni miongoni mwa wanafunzi waliopigwa marufuku kusoma Harvard
  • Seneta ashitakiwa kwa kuwatuhumu wanasiasa wenzaka kuwa wanataka kumuua
  • Marekani na Iran zarejea katika mazungumzo ya nyuklia
  • Mwanaharakati Agather apatikana katika mpaka wa Tanzania na Uganda
  • Trump apotosha kwa kutumia picha ya Congo na kudai ni ya mauaji ya kimbari ya Wazungu wa Afrika Kusini
  • Trump akizuia Chuo Kikuu cha Harvard kusajili wanafunzi wa kimataifa
  • Kiongozi wa upinzani akamatwa Tanzania
  • Usalama ni mdogo wakati wa utoaji wa misaada huko Gaza
  • Mwanamume amka na kupata meli kubwa kwenye bustani yake
  • Kundi la watu lamuua Chuimilia nchini India
  • Mwanaharakati Agather Atuhaire, aliyekuwa akishikiliwa Tanzania aachiwa
  • Marekani yasema Sudan ilitumia silaha za kemikali katika vita huku ikiweka vikwazo vipya
  • Netanyahu amshutumu Starmer kwa kuwa upande wa Hamas
  • Bunge la Seneti DRC laondoa kinga ya kutoshtakiwa ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho.

  2. Mwanaharakati Agather wa Uganda naye akiri kuteswa kizuizini Tanzania

    Agatha

    Chanzo cha picha, x

    Mwanaharakati maarufu wa Uganda, Agather Atuhaire, amerejea nyumbani Uganda lakini amefichua kuwa aliteswa na kulazimishwa kuvuliwa nguo akiwa kizuizini nchini Tanzania.

    Akizungumza kwa uchungu, Agather ameahidi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale waliomtesa. Haya yanajiri siku moja baada ya mwanaharakati mwingine wa Kenya, Boniface Mwangi, ambaye alikamatwa pamoja na Agather kuachiliwa na kudai pia aliteswa.

    Akisimulia mkasa wake, Agather alisema alifika nchini usiku wa manane siku moja kabla ya kesi ya Tundu Lissu, kiongozi wa upinzani Tanzania anayeshitakiwa kwa uhaini. Asubuhi yake, alishtushwa kuona simu nyingi kutoka kwa Boniface Mwangi na mkewe, ambaye alimuuliza kama yuko salama. Ujumbe kutoka kwa Mwangi ulimjulisha kuwa amekuja kukamatwa hotelini. Tukio hili lilimshtua sana.

    Akielezea namna alivyokamatwa, Agather alisema baada ya kumaliza kufuatilia kesi ya Tundu Lissu, Mei 19, 2025 katika Mahatma ya Kisutu, Dar es Salaam alirejea hotelini alikofikia.

    Polisi walifika, na baada ya kuangalia kamera za CCTV na kumwona akichukua begi la Boniface Mwangi, walimkuta akila na kumuomba kuzungumza naye.

    Anasema walikuwa kama watano na walikuwa na ghadhabu, ingawa yeye aliwapa ushirikiano kamili akiamini ni jambo dogo, akiwa na Mwangi.

    a

    Chanzo cha picha, Martha Karua

    Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa Kenya Mwangi (kushoto) akiwa na wakili Martha Karua aliyekwenda kumtembelea hospitali, muda mfupi baada ya kuachiliwa Tanzania

    "Waliniuliza nimekuja kufanya nini Tanzania, na nilijibu kuwa kuja Tanzania si kosa la jinai. Niliwauliza kama walikuwa wametoa tangazo kuzuia wageni kuingia, na kama ndiyo, basi maafisa wa uhamiaji uwanja wa ndege walikuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao," Agather alieleza.

    Aliongeza kuwa walionekana kukasirika zaidi kwa kuwa alikuwa akiwajibu kwa kujiamini, na walimwambia mawakili waliokuwa nao waondoke na warudi kesho.

    Anasema walimwambia Boniface Mwangi watamtahiri kwa mara ya pili. Kuhusu yeye mwenyewe, walimwambia watamfundisha adabu. "Waliniuliza nina watoto wangapi, nikawaambia wawili, wakanijibu 'unataka mtoto wa tatu? Utapata watatu'," Agather alisimulia kwa uchungu.

    Katika kile kinachotajwa kuwa mateso makali, Agather alifichua kuwa: "Walinivua nguo, walinitupa chini, walinifunga pingu, walinifunga miguu na mikono wakapitisha mbao kati ya miguu yangu na mikono, na kunining'iniza. Wakaanza kunipiga kichwani, na kunifanyia vitendo vibaya."

    Maelelzo haya Agather yanakuja baada ya taarifa za kuachiliwa kwa Boniface Mwangi, ambaye pia alidai kuteswa wakati akiwa kizuizini. Wawili hao walikamatwa wakiwa pamoja, na sasa wote wawili wanajitokeza na madai mazito ya kuteswa, wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliowatesa.

    Wanaharakati hao walikuja kuhudhuria kesi ya tundu Lissu ambayo imehairishwa mpaka Juni 2, mwaka huu, huku wanaharakati wengine kutoka Kenya akiwemo wakili Martha Karua, kuzuiwa kuingia Tanzania wakirudishwa kwao kenya.

    Mpaka sasa Polisi nchini Tanzania haijatoa tamko lolote kuhusiana na tariff hizi za kuteswa kwa wanaharakati hawa, ingawa awali Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa “shamba la bibi” ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.

    Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024) wiki hii, Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.

    “Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku,” alisema Rais Samia.

    Alitoa kauli hiyo siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wanaharakati wengine wawili, kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.

    Walikuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ambayo imeendelea leo katika Mahakama ya Kisutu.

  3. Ukraine na Urusi zabadilishana mamia ya wafungwa wa vita

    FC

    Chanzo cha picha, X

    Maelezo ya picha, Baadhi ya raia wa Ukraine walioachiliwa walipigwa picha muda mfupi baada ya kuachiliwa na Urusi

    Urusi na Ukraine kila moja imekabidhi wanajeshi na raia 390 katika mbadilishano mkubwa wa wafungwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mnamo 2022.

    Nchi zote mbili zimerejesha wanajeshi 270 na raia 120 kwenye mpaka wa Ukraine na Belarus, kama sehemu ya makubaliano yaliyokubaliwa katika mazungumzo ya moja kwa moja huko Istanbul wiki moja iliyopita.

    Pande zote mbili zilikubaliana kubadilishana wafungwa 1,000 na kuthibitisha kutakuwa na mabadilishano zaidi katika siku zijazo.

  4. Kangaruu ajaribu kumzamisha mtu katika mafuriko huko Australia

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kangaroo "mwenye misuli" alijaribu kumzamisha" mwanaume mmoja huko Australia, baada ya wawili hao kupigana ngumi.

    Mwanaume huyo Don James inasemekana alijikuta akipigania maisha yake huku mnyama huyo akimshikilia kwenye maji ya mafuriko ambayo yalikuwa yamejikusanya kando ya barabara karibu na mji wa Port Macquarie – kangaroo huyo alitoroka baada ya kukimbizwa.

    Kristy Lees, ambaye alitazama vita hivyo kupitia kioo chake cha ndani cha gari, aliiambia BBC:

    "Kangaroo alijaribu kumzamisha mtu huyo," alisema. "Niliona kilichokuwa kikitokea na kumwambia mume wangu atoke kwenye gari na kwenda kumsaidia mtu huyo."

  5. Kabila la Amazon lalishitaki gazeti la Marekani juu ya ripoti kuhusu uraibu wa picha za ngono

    vc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kabila moja katika msitu wa Amazonia limelishtaki gazeti la New York Times (NYT) la Marekani kutokana na ripoti kuhusu kabila hilo kupata huduma ya intaneti na kudai huduma hiyo imesababisha watu wa kabila hilo kuwa waraibu wa picha za ngono.

    Kesi ya kashfa imefunguliwa na kabila la Marubo, pia kesi hiyo imetaja mtandao wa TMZ na Yahoo kama washtakiwa, na kusema habari zao "zilidhihaki vijana wa kabila hilo" na "kupotosha mila zao."

    NYT imesema ripoti yake haikusema kuwa watu wa kabila hilo wana uraibu na picha za ngono. TMZ na Yahoo hazijatoa kauli yoyote.

    Marub oni jamii ya watu 2,000, inatafuta fidia ya dola za kimarekani milioni 180m (£133m).

    Ripoti ya NYT, iliyoandikwa miezi tisa baada ya Marubo kupata huduma ya Starlink, huduma ya mtandao wa intaneti ya satelaiti kutoka SpaceX ya Elon Musk, ilisema kabila hilo "linapambana na changamoto zilezile ambazo zimezikumba kaya za Marekani kwa miaka mingi."

    Changamoto hizo zikijumuisha "vijana kukaa muda mrefu na simu," "michezo ya video yenye vurugu" na "watoto kutazama picha za ngono," ilisema ripoti hiyo.

    Ripoti hiyo pia ilibainisha manufaa ya inteneti hiyo kwa kabila hilo, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu masuala ya afya na uharibifu wa mazingira na kuwasiliana na familia za mbali.

  6. Binti Mfalme wa Ubelgiji ni miongoni mwa wanafunzi waliopigwa marufuku kusoma Harvard

    ik

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Princess Elisabeth wa Ubelgiji katika sherehe ya miaka 18 ya kuzaliwa kwa Prince Christian katika Kasri la Christiansborg huko Copenhagen, Denmaki tarehe 15 Oktoba 2023.

    Binti Mfalme Elisabeth, malkia wa baadaye wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 23, amemaliza mwaka wake wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Harvard lakini marufuku iliyowekwa na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa wanafunzi wa kigeni wanaosoma chuo hicho inaweza kuathiri masomo yake.

    Utawala wa Trump uliondoa uwezo wa Chuo Kikuu cha Harvard kusajili wanafunzi wa kimataifa siku ya Alhamisi, na kulazimisha wanafunzi wa sasa wa kigeni kuhamia vyuo vingine au kupoteza haki yao ya kuishi Marekani.

    lisabeth anasomea Sera ya Umma huko Harvard, programu ya miaka miwili ya shahada ya uzamili ambayo inawaandaa wanafunzi kwa ajili ya utumishi wa umma.

    Binti mfalme ndiye mrithi wa kiti cha enzi cha Ubelgiji, kama mtoto mkubwa kati ya watoto wanne waliozaliwa na Mfalme Philippe na Malkia Mathilde. Kabla ya kujiunga na Harvard, alipata digrii ya historia na siasa kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza.

    Harvard imesema siku ya Alhamisi hatua ya utawala wa Trump - ambayo inaathiri maelfu ya wanafunzi - sio halali na ni ya kulipiza kisasi.

    Kufuatia marufuku hiyo, chuo hicho kimeushitaki utawala wa Trump siku ya Ijumaa. Katika malalamiko yaliyowasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya Boston, Harvard imeitaja marufuku hiyo kuwa ni "ukiukaji wa wazi" wa Katiba ya Marekani na sheria nyingine za shirikisho, na kuathiri chuo kikuu na zaidi ya wenye viza 7,000.

  7. Seneta ashitakiwa kwa kuwatuhumu wanasiasa wenzake kuwa wanataka kumuua

    DC
    Maelezo ya picha, Natasha Akpoti-Uduaghan alisimamishwa kazi kutoka katika Seneti baada ya kutoa madai ya unyanyasaji wa kijinsia.

    Serikali ya Nigeria imemfungulia mashtaka seneta mmoja ambaye alimtuhumu mmoja wa wanasiasa wakuu wa nchi hiyo kwa anapanga njama ya kumuua.

    Mwezi Aprili, Natasha Akpoti-Uduaghan alidai kuwa Godswill Akpabio, rais wa Seneti, na Yahaya Bello, gavana wa zamani wa jimbo hilo, wanataka "kummaliza." Wote wawili wamekanusha shtaka hilo.

    Wiki kadhaa kabla, Akpoti-Uduaghan alimshutumu rais wa Seneti kwa kumnyanyasa kingono - madai ambayo pia ameyakanusha.

    Serikali imewasilisha mashtaka katika Mahakama Kuu, ikisema madai ya njama za mauaji ya Akpoti-Uduaghan yamemkashifu Akpabio na Bello.

    Katika karatasi ya mashtaka, iliyoonekana na BBC, mwanasheria mkuu wa Nigeria alirejelea mahojiano ya Channels TV ya Nigeria mwezi uliopita.

    Katika mahojiano hayo, Akpoti-Uduaghan alizungumzia "majadiliano ya Akpabio na Yahaya Bello ya kumuua yeye.

    Mwanasheria mkuu alisema kauli hiyo, na nyingine zilizotolewa katika mahojiano hayo, zinaweza kuharibu sifa za Bello na Akpabio.

    Akpoti-Uduaghan hajasema chochote juu ya mashitaka dhidi yake na hakuna tarehe iliyopangwa ya kufika mahakamani.

    Akpoti-Uduaghan ni mmoja wa wanawake wanne kati ya maseneta 109.

    Baada ya kumshutumu Akabio kwa unyanyasaji wa kijinsia mnamo Februari, alisimamishwa kazi kutoka katika Seneti kwa miezi sita bila malipo.

    Kamati ya maadili ya Seneti ilisema kusimamishwa kwake ni kwa tabia yake ya "ukaidi na usumbufu" wakati Seneti ilikuwa ikijadili madai yake.

    Hata hivyo, Akpoti-Uduaghan na wafuasi wake waliteta kuwa kamati hiyo ilimlenga kwa sababu ya madai aliyotoa dhidi ya rais wa seneti.

    Machi, aliiambia BBC kuwa anahisi Seneti "inafanya kazi kama kikundi tu cha watu. Pia alisema kwa sababu ulinzi wake kuondoshwa, anahofia usalama wa mtoto wake wa miaka miwili.

  8. Marekani na Iran zarejea katika mazungumzo ya nyuklia

    cx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wapatanishi wa Iran na Marekani wameaanza tena mazungumzo siku ya Ijumaa mjini Roma ili kutatua mzozo wa miongo kadhaa juu ya malengo ya nyuklia ya Iran, vimeripoti vyombo vya habari vya Iran.

    Rais Donald Trump anataka kuondoa uwezo wa Tehran wa kuweza kutengeneza silaha za nyuklia, huku Jamhuri ya Kiislamu kwa upande wake inataka kuondolewa vikwazo dhidi ya uchumi wake unaotegemea mafuta.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi na mjumbe wa Trump katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff wanatarajiwa kuongoza duru ya tano ya mazungumzo hayo, kupitia wapatanishi wa Oman.

    Washington imechukua msimamo mkali juu ya mpango huo wa Iran wa kurutubisha madini ya uranium, ingawa Tehran inasema haina malengo ya kuunda silaha za nyuklia, na ni kwa madhumuni ya matumizi ya kiraia tu.

    Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kwamba Trump anaamini mazungumzo na Iran "yanakwenda katika mwelekeo sahihi".

    Tehran na Washington wote wamesema wanapendelea diplomasia kusuluhisha mgogoro huo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema Jumanne kwamba Washington inajitahidi kufikia makubaliano ambayo yataruhusu Iran kuwa na mpango wa nishati ya nyuklia wa kiraia lakini sio kurutubisha uranium, huku akikiri kwamba kufikia makubaliano hayo "hakutakuwa rahisi".

    Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, ambaye ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu masuala ya serikali ya Iran, alikataa matakwa ya Washington ya kwamba Tehran ikome kabisa kurutubisha uranium, akionya kwamba mazungumzo hayo hayawezi kuleta matokeo.

    Miongoni mwa vikwazo vilivyosalia ni kukataa kwa Tehran kusafirisha nje ya nchi hifadhi yake yote ya uranium na kushiriki katika majadiliano juu ya mpango wake wa makombora ya balestiki.

    Iran inasema iko tayari kukubali ukomo wa urutubishaji wa uranium, lakini inahitaji uhakikisho kwamba Washington haitakataa makubaliano ya baadaye ya nyuklia.

  9. Mwanaharakati Agather apatikana katika mpaka wa Tanzania na Uganda

    d

    Chanzo cha picha, Twitter

    Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa Uganda na wakili wa haki za binadamu Agather Atuhaire

    Mwanaharakati wa Uganda na wakili wa haki za binadamu Agather Atuhaire, ambaye alizuiliwa nchini Tanzania amepatikana akiwa salama.

    Kwa mujibu wa Mwanaharakati wa Kenya, Hussein Khalid, anasema Aghather aliyekamatwa Tanzania mapema wiki hii - amepatika kwenye mpaka wa Mutukula kati ya Uganda na Tanzania.

    Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa VOCAL Africa, alithibitisha kuachiliwa kwa Agather, akieleza hali yake si nzuri na kutaka haki itendeke kwa mwanaharakati huyo.

    Agather walikamatwa jijini Dar es Salaam Mei 19 wakihudhuria kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lissu.

    Familia ya Agather imethibitisha kwamba amepatikana akiwa ametelekezwa karibu na mpaka wa Mutukula usiku.

    Mazingira yanayozunguka kuachiliwa kwake bado hayajulikani, na bado hajatoa taarifa kwa umma.

  10. Mwanaume amka na kukuta meli kubwa kwenye bustani yake

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mwanaume mmoja huko Norway aliamka na kukuta meli kubwa ya kubebea mizigo ikiwa imetia nanga kwenye bustani yake.

    Meli hiyo yenye urefu wa mita 135 (443ft) nusra igonge nyumba ya Johan Helberg siku ya Alhamisi.

    Bw Helberg alifahamishwa kuhusu tukio hilo na jirani yake aliyejawa na hofu ambaye alikuwa ameona meli hiyo ilipokuwa ikielekea moja kwa moja ufukweni upande wa nyumba yake, huko Byneset, karibu na Trondheim.

    "Kengele ya mlango ililia wakati wa mchana ambapo sipendi kufungua," Bw Helberg aliambia kituo cha televisheni cha TV2.

    "Nilienda dirishani na nikashangaa sana kuona meli kubwa," alisema katika mahojiano na Guardian.

    "Ilinibidi niinamishe shingo yangu ili kuona sehemu ya juu. Sikuamini."

    "Mita tano zaidi upande wa kusini ingeingia chumbani," aliongeza wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Norway. "Sikusikia chochote."

    Jirani Jostein Jorgensen alisema aliamshwa na mlio wa meli hiyo ilipokuwa ikielekea nchi kavu kwa kasi, na kukimbilia nyumbani kwa Bw Helberg.

    "Nilikuwa na uhakika kwamba tayari alikuwa ameshatoka kwa sababu hakukuwa na dalili ya mtu kuwa ndani. Niligonga kengele ya mlango mara nyingi bila kusikia chochote," alisema Bw Jorgensen.

    “Na hapo ndipo nilipompigia simu na kuwasiliana naye,” aliiambia TV2.

    Hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

    Haijulikani ni nini kilisababisha ajali hiyo na polisi wa Norway wanasemekana wanafanya uchunguzi.

  11. Trump apotosha kwa kutumia picha ya Congo na kudai ni ya mauaji ya kimbari ya Wazungu wa Afrika Kusini

    fvc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump alionyesha picha iliyochukuliwa katika video ya shirika la habari la Reuters katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuiwasilisha kama ushahidi wa mauaji ya halaiki ya Wazungu wa Afrika Kusini.

    "Hawa wote ni wakulima wa kizungu ambao wanazikwa," Trump alisema siku ya Jumatano, akionesha picha hiyo wakati wa mkutano katika Ikulu ya Marekani na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

    Picha hiyo ilitokana na video iliyochapishwa na Reuters Februari 3, 2025, inaonyesha wafanyakazi wa kibinadamu wakinyanyua mifuko yenye miili katika mji wa Goma nchini Congo.

    Picha hiyo ilitolewa kutoka katika video ya Reuters iliyopigwa kufuatia mapigano makali na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

    Picha hiyo iliyooneshwa na Trump lilichapishwa na American Thinker, jarida la kihafidhina la mtandaoni – likionesha migogoro na mivutano ya kirangi Afrika Kusini na Congo.

    Ikulu ya White House haikujibu maswali ya Reuters kuhusu picha hiyo.

    Andrea Widburg, mhariri mkuu wa American Thinker na mwandishi wa picha husika, aliandika akijibu swali la Reuters kwamba Trump "ameielewa vibaya picha hiyo."

  12. Trump akizuia Chuo Kikuu cha Harvard kusajili wanafunzi wa kimataifa

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump umeamua kukizuia Chuo Kikuu kikongwe zaidi Marekani cha Harvard kusajili wanafunzi wa kimataifa.

    Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem amesema utawala wa Trump umezuia "ruhusa ya kupokea wanafunzi wa kigeni kutokana na Harvard kushindwa kutii sheria."

    "Hili liwe onyo kwa vyuo vikuu vyote na taasisi za elimu kote nchini," aliandika kwenye X siku ya Alhamisi.

    Harvard umesema agizo hilo "ni kinyume cha sheria," na kusema, "tumejitolea kikamilifu kukaribisha wanafunzi na wasomi wa kimataifa, ambao wanatoka zaidi ya nchi 140."

    Maamuzi ya utawala wa Trump yanaweza kuathiri maelfu ya wanafunzi wa kimataifa wanaosoma katika chuo kikuu hicho.

    Zaidi ya wanafunzi 6,700 wa kimataifa waliandikishwa katika taasisi hiyo mwaka jana, takwimu za Harvard zinaonyesha, wanafunzi wa kigeni ni asilimia 27 ya wanafunzi wote.

  13. Usalama ni mdogo wakati wa utoaji wa misaada huko Gaza

    Mfanyakazi wa Kipalestina akibeba gunia la unga wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) huko Deir Al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza, tarehe 22 Me

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani malori 130 yamevuka mpaka na kuingia Gaza ndani ya siku tatu zilizopita.

    Wengi wao bado wanasubiri katika maghala ya mashirika ya misaada ya kimataifa.

    Asubuhi ya leo, waokaji walitoa taarifa kwamba hawawezi kuzalisha chakula tena kwa sababu hakuna usalama wa kutosha wa kuwalinda.

    Siku ya Alhamisi, unga na mafuta vilipokuwa vikiwasilishwa kwa waokaji katika kambi za wakimbizi, hali ilikuwa ya vurugu huku umati wa watu wenye njaa wakijaribu kuchukua bidhaa hizo.

    Msafara wa malori yapatayo 20 ulipitia, yakiwa yamebeba unga na moja iliyobeba dawa, mamlaka za eneo hilo zilisema.

    Wakati msafara huo ulipokuwa unakaribia katikati ya Ukanda wa Gaza, ulishambuliwa na kile wanahabari wa eneo hilo wanachokielezea kama "magenge" yanayojaribu kuwapora.

    Kulikuwa na ufyatulianaji wa risasi katika malori mawili, na kitengo kidogo cha polisi cha Hamas kilirushiana risasi na waporaji.

    Baada ya hapo, kulikuwa na mashambulizi matatu ya anga ya Israel katika eneo hilo, na kuua wapiganaji 6 wa Hamas.

    Hii inaonesha tu jinsi hali ya usalama ilivyo ngumu na dhaifu.

    Baada ya wiki 11 za msaada kutoruhusiwa na Israel, njaa inakaribia.

    Hakuna mafuta au gesi ya kupika huko Gaza, kwa hivyo malori 100 ni kidogo sana. Watu wanaamini wanahitaji angalau malori 500 kila siku kwa miezi miwili ili kubadilisha hali hiyo.

  14. Kiongozi wa upinzani akamatwa Tanzania

    c

    Chanzo cha picha, Mwananchi

    Maelezo ya picha, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita

    Makamu Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, Isihaka Mchinjita amekamatwa na Jeshi la Polisi nchini humo baada ya kutembelea mradi wa mwendokasi ili kuangalia kero za mradi huo.

    Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, taarifa ya kukamatwa kwa kiongozi huyo imetolewa Abdallah Khamis ambaye ni ofisa habari wa chama hicho leo Mei 23,2025.

    "Alikuwa akifanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Stendi ya Mwendokasi Kimara Mwisho, lengo ni kushuhudia namna ambavyo wananchi wanapitia changamoto katika usafiri huo wa umma," amesema.

    Abdalah amesema baadhi ya viongozi waliojitambulisha ni wafanyakazi wa mradi wa mwendo kasi, walimfanyia fujo kiongozi huyo wakitaka asipokee malalamiko ya wananchi katika kituo cha Kimara.

    "Kwa sasa Mchinjita anashikiliwa na polisi, katika kituo cha polisi cha mwendokasi," amesema.

    Mrandi wa mabasi ya mwendo kasi katika jiji la Dar es Salaam ambao ulianza tangu mwaka 2016, umekuwa ukikumbwa na changamoto za mara kwa mara za uwepo wa abiria wengi katika vituo huku kukioneka kuwepo kwa uhaba wa mabasi.

    Jeshi la Polisi Tanzania bado halijatoa taarifa rasmi ya sababu za kukamatwa kwa kiongozi huyo.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Kundi la watu lamuua Chuimilia nchini India

    Chui milia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chuimilia wa Bengal ameuawa na kukatwakatwa na kundi la watu katika jimbo la Assam kaskazini mashariki mwa India, afisa wa misitu amesema.

    Wakazi wenye hasira kutoka kijiji kimoja katika wilaya ya Golaghat wanaripotiwa kuchukua hatua hiyo kwa sababu simbamarara huyo alikuwa ameua mifugo katika eneo hilo na kuwa tishio kwa maisha yao.

    Idara ya misitu ya serikali imefungua kesi.

    Matukio ya mzozo kati ya binadamu na wanyama si mapya kwa Assam.

    Haya ni mauaji ya tatu ya chui milia ambayo yameripotiwa mwaka huu. Afisa mkuu wa misitu Gunadeep Das aliliambia gazeti la Times of India kwamba chui milia huyo alikufa kutokana na majeraha makubwa na wala sio risasi.

    Mzoga huo ulipatikana baadaye mbele ya hakimu, ripoti zinasema. Bw Das aliliambia gazeti moja la ndani kuwa "takribani watu elfu moja walikuwa wamekusanyika kumuua chui milia" na kwamba baadhi yao walimshambulia kwa mapanga.

    Aliongeza kuwa mzoga wa simbamarara ulipelekwa kufanyiwa uchunguzi.

    Takwimu za hivi punde za idara ya misitu ya Assam zinaonyesha idadi ya chui milia katika jimbo hilo imeongezeka kutoka 70 tu mnamo 2006 hadi 190 mnamo 2019 kwa sababu ya juhudi mbali mbali za uhifadhi.

    Hata hivyo, matukio ya chuimilia kuuawa kutokana na migogoro na wanakijiji mara nyingi yameripotiwa kwenye vyombo vya habari

    Chui ni wanyama wanaolindwa chini ya Sheria ya Ulinzi ya Wanyamapori ya India (1972), ambayo inakataza ujangili, uwindaji na biashara ya sehemu za mwili za chuimilia.

  16. Mwanaharakati Agather Atuhaire, aliyekuwa akishikiliwa Tanzania aachiwa

    Agather Atuhaire

    Chanzo cha picha, Agather Atuhaire

    Mwanaharakati Agather Atuhaire, ambaye alikuwa akishikiliwa nchini Tanzania, amepatikana akiwa ametupwa karibu na mpaka wa Mutukula wa Uganda usiku, familia yake na marafiki zake wamethibitisha. NTV imeripoti.

    Mwanaharakati Agather Atuhaire wa Uganda alizuiliwa nchini Tanzania pamoja na mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi mapema wiki hii.

    Wanaharakati hao walikuwa wameenda kuhudhuria kesi ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wiki hii alitoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa "shamba la bibi" ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.

    Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.

    "Tusiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku," alisema Rais Samia.

    Kauli hiyo aliitoa siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.

    Unaweza kusoma;

  17. Marekani yasema Sudan ilitumia silaha za kemikali katika vita huku ikiweka vikwazo vipya

    Mwanaume mmoja raia wa Sudan akionyesha sanduku la risasi ambazo hazijalipuka zilizopatikana katika shule moja mjini Khartoum, mji mkuu wa nchi hiyo.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani itaiwekea Sudan vikwazo vipya baada ya kubaini kuwa ilitumia silaha za kemikali mwaka jana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea dhidi ya Wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF), Wizara ya mambo ya nje imesema.

    Usafirishaji wa bidhaa za Marekani kwa nchi hiyo utawekewa vikwazo na vikomo vya kukopa fedha kuwekwa kuanzia tarehe 6 Juni, taarifa kutoka kwa msemaji Tammy Bruce ilieleza.

    Wanajeshi wa Sudan na kundi la wanamgambo la RSF hapo awali walishutumiwa kwa uhalifu wa kivita wakati wa vita.

    BBC imewasiliana na Sudan ili kujibu hatua za hivi punde za Marekani. Maafisa wa Sudan wanasema bado hawana taarifa.

    Zaidi ya watu 150,000 wameuawa wakati wa mzozo huo, ambao ulianza miaka miwili iliyopita wakati jeshi la Sudan na RSF walipoanza mapambano makali ya kuwania madaraka.

    Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Sudan limeuteka tena mji mkuu wa Khartoum, lakini mapigano yanaendelea kwingineko.

    Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu silaha za kemikali ambazo Marekani ilisema ilizipata, lakini gazeti la New York Times liliripoti mwezi Januari kwamba Sudan ilitumia gesi ya klorini mara mbili, ambayo husababisha aina mbalimbali za madhara na hata vifo.

    "Marekani inaitaka serikali ya Sudan kusitisha matumizi yote ya silaha za kemikali na kutekeleza wajibu wake chini ya CWC," taarifa hiyo ilisomeka, ikirejelea Mkataba wa Silaha za Kemikali ambapo watia saini wamejitolea kuharibu hifadhi zao za silaha.

    karibu katika kila nchi duniani, ikiwa ni pamoja na Sudan zimeukubali mkataba wa CWC, mbali na Misri, Korea Kaskazini na Sudan Kusini kulingana na Chama cha Kudhibiti Silaha, shiŕika la wanachama lisiloegemea upande wowote lenye makao yake makuu nchini Marekani.

    "Marekani inasalia kujitolea kikamilifu kuwawajibisha wale wanaohusika na kuchangia kuenea kwa silaha za kemikali," Bruce aliongeza.

    Unaweza kusoma;

  18. Netanyahu amshutumu Starmer kwa kuwa upande wa Hamas

    Netanyahu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Sir Keir Starmer na viongozi wengine "wamesema wanataka Hamas ibaki madarakani".

    Pia aliwashutumu viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Canada kwa kushirikiana na "wauaji wengi, wabakaji, wauaji wa watoto na watekaji nyara".

    Katika video iliyowekwa kwenye X , akizungumzia shambulio la Alhamisi dhidi ya wafanyakazi wa ubalozi wa Israel huko Washington DC, Netanyahu alisema Sir Keir, Emmanuel Macron na Mark Carney walitaka Israel "kukubali kwamba jeshi la Hamas la wauaji wa umati litanusurika".

    Downing Street imekataa kutoa maoni moja kwa moja juu ya matamshi ya Netanyahu, lakini ilionesha chapisho la Sir Keir la kulaani shambulio la Washington kwenye mtandao wa X.

  19. Bunge la Seneti DRC laondoa kinga ya kutoshtakiwa ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila

    Kabila

    Chanzo cha picha, Reuters

    Bunge la Seneti la DRC limeondoa kinga ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, na kumtengenezea njia ya kufunguliwa mashitaka.

    Kabila ambaye pia ni seneta wa maisha, anatuhumiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, na kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo liliteka miji mikubwa Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.

    Kwa jumla, Maseneta 88 walipiga kura ya kuunga mkono kushitakiwa kwake, ni watano pekee waliopiga kura dhidi yake, huku kura nyingine tatu zikibatilishwa. Joseph Kabila ambaye aliondoka nchini 2023 hakufika mbele ya seneti kujitetea kabla ya kura ya leo.

    Anakuwa Mkuu wa kwanza wa zamani wa Nchi kushtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita na mashtaka yanayohusiana nayo.

    Unaweza kusoma;

  20. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu