Wizara ya Sheria ya Marekani imemkamata mtu anayedaiwa
kupanga shambulizi siku ya Uchaguzi na anahusishwa na kundi la Islamic State.
Mshukiwa, Nasir Ahmad Tawhedi, 27, ni raia wa Afghanistan
anayeishi katika mji wa Oklahoma, kulingana na waendesha mashtaka.
Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray alisema katika taarifa
ya Jumanne kwamba: "Mshtakiwa huyu, akichochewa na ISIS, alikula njama ya
kufanya shambulio la kikatili, Siku ya Uchaguzi, hapa nchini kwetu."
FBI ilisema alikuwa akijaribu kuhifadhi silaha, na
alikuwa amechukua hatua kuuza mali za familia yake na kuwahamisha wanafamilia
wake nje ya nchi.
Bw Tawhedi anashtakiwa kwa kutoa, kujaribu kutoa, na kula
njama ya kusaidia au kutoa rasilimali kwa shirika la kigeni la kigaidi; na kwa
kujaribu kununua bunduki na risasi za kutumia kufanya uhalifu au kitendo cha
kigaidi.
FBI ilisema Bw Tawhedi alifanya kazi na mwenzake ambaye
jina lake halikutajwa, jamaa wake mwenye umri mdogo na pia ni raia wa
Afghanistan.
Inamtuhumu kwa kutumia propaganda za Islamic State
kupitia mtandao, kulingana na rekodi za Google zilizopatikana na vyombo vya
sheria, na kutoa michango kwa shirika la kutoa msaada linalotumika na IS.
"Tutaendelea kupambana na tishio linaloendelea
ambalo ISIS na wafuasi wake wanaleta kwa usalama wa taifa wa Marekani, na
tutawatambua, kuwachunguza na kuwafungulia mashtaka watu wanaotaka kuwatisha
watu wa Marekani,'' alisema Mwanasheria Mkuu Merrick Garland.
Bw Tawhedi alitafuta bunduki aina ya AK-47 ili kutumia
katika shambulio hilo, mamlaka zinadai.
Mnamo tarehe 7 Oktoba, yeye na mwanzilishi mwenza
walikutana na watu ambao kwa kweli walifanya kazi kwa siri kwa FBI kununua
silaha na risasi.
Baada ya ununuzi huo, Bw Tawhedi na mshiriki mwenzake
walikamatwa.
Bw Tawhedi aliwasili Marekani mnamo Septemba 2021 kwa
visa maalum ya wahamiaji pamoja na mkewe na mtoto wake mdogo.
Alikuwa anaishi katika mji wa Oklahoma wakati wa
kukamatwa kwake.
Haijabainika mara moja ikiwa ana uwakilishi wa kisheria.