Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ruto atoa wito wa kuangaliwa upya kwa nyongeza ya mishahara ya maafisa wa serikali

Rais wa Kenya William Ruto ametaka kuangaliwa upya mara moja kwa mapendekezo ya nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali akitaja haja ya hatua za kubana matumizi, Citizen imeripoti.

Muhtasari

  • Man United kuwafuta kazi wafanyakazi 250
  • Ruto atoa wito wa kuangaliwa upya kwa nyongeza ya mishahara ya maafisa wa serikali
  • China yakamata boti ya Taiwan kwa shutuma za uvuvi haramu
  • Huzuni, hasira baada ya watu 121 kupoteza maisha kutokana na mkanyagano India
  • Mtoto ahofiwa kuliwa na mamba nchini Australia
  • Polisi Kenya wachapisha picha za wanaosakwa kwa uhalifu wakati wa maandamano
  • Maafisa wa zamani wasema sera ya Gaza imeweka Marekani katika hatari
  • 'Mimi si mfuasi wa kanisa': F Kennedy Jr ajibu madai ya unyanyasaji wa ngono
  • Euro 2024: Uturuki na Uholanzi zaingia robo fainali ya Euro
  • Rais wa zamu wa EU ataka kusitishwa kwa mapigano ya Ukraine na Urusi
  • Marufuku ya wanasiasa wa Wales kusema uwongo kupitishwa kabla ya 2026
  • Biden alaumu uchovu wa safari ya ndege kwa matokeo duni katika mdahalo na Trump
  • Marufuku ya ndoa za utotoni yapokelewa vyema Sierra Leone

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Man United kuwafuta kazi wafanyakazi 250

    Manchester United itapunguza kazi 250 kama sehemu ya kupunguza gharama na kufutilia mbli baadhi ya shughuli "zisizo muhimu".

    Mkurugenzi wa United Sir Dave Brailsford ameongoza mapitio makubwa ya uendeshaji wa klabu tangu umiliki wa Inoes wa klabu hiyo kuthibitishwa mwezi Desemba.

    Sir Jim Ratcliffe alikuwa tayari amewaambia wafanyikazi juu ya hamu yake ya wao kurudi kufanya kazi katika maeneo ya uwanja wa klabu.

    Hata hivyo, vyanzo vya klabu sasa vinasema mabadiliko makubwa ya kifedha yanahitajika ili kukomesha kupanda kwa gharama za mwaka hadi mwaka.

    Tathmini hiyo imehitimishwa, kulingana na muundo, ukubwa na kwamba sura ya klabu haionyeshi uchezaji wa sasa na wana wafanyakazi wengi kuliko wanaohitaji.

    Vyanzo vinasema uokoaji wa gharama umetambuliwa karibu na shughuli "zisizo muhimu", ambazo zitakoma.

    Bado haijafafanuliwa ni shughuli gani hizi, lakini lengo ni kupunguza idadi ya watu na gharama za wafanyikazi. United ina wafanyikazi wa kudumu 1,150.

    Mtendaji mkuu wa muda Jean-Claude Blanc aliwasilisha habari za kupunguzwa kwa wafanyikazi katika mkutano wa wafanyikazi na karibu watu 800 waliohudhuria.

    Hatua hiyo inaelekea kupokewa vibaya, huku wengi wakitaja usajili duni kwenye kikosi cha kwanza kwamba umepoteza pesa nyingi zaidi kuliko zitakazookolewa kwa kupunguza wafanyikazi .

    Man Utd imemthibitisha Ashworth kama mkurugenzi wa michezo

  2. Ruto atoa wito wa kuangaliwa upya kwa nyongeza ya mishahara ya maafisa wa serikali

    Rais wa Kenya William Ruto ametaka kuangaliwa upya mara moja kwa mapendekezo ya nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali akitaja haja ya hatua za kubana matumizi, Citizen imeripoti.

    Hatua hii ni baada ya notisi ya gazeti la serikali ya Agosti 9, 2023, ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kutangaza mapitio ya nyongeza ya mishahara ya Watendaji na Wabunge kuanzia Julai 1, 2024.

    Mabadiliko hayo yamezua taharuki kwa umma huku kukiwa na kilio cha kupunguza matumizi ya umma.

    Ruto, kupitia kwa msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, aliagiza Hazina ya Kitaifa kukagua notisi ya gazeti la serikali kwa kuzingatia Muswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa sasa na vikwazo vya kifedha vinavyotarajiwa katika mwaka wa kifedha wa 2024/25.

    "Rais amesisitiza kuwa huu ni wakati, zaidi ya hapo awali, kwa Watendaji na vyombo vyote vya serikali kuishi kulingana na uwezo wao," alisema Mohamed kwenye X.

    Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria pia ameeleza kuwa licha ya SRC kupewa jukumu la kukagua mishahara mara kwa mara kwa maafisa wote wa serikali, inapaswa kudumisha hatua za kubana matumizi.

    Unaweza kusoma;

  3. China yakamata boti ya Taiwan kwa shutuma za uvuvi haramu

    China imesema imekamata meli ya Taiwan, iliyokuwa na wafanyakazi watano ndani yake, kwa kuvua samaki kinyume cha sheria katika maji yake Jumanne usiku.

    Taiwan imeitaka China kuachilia meli hiyo na watu hao, wawili wa Taiwan na watatu wa Indonesia, ambayo inashikiliwa huko Weitou, bandari ya kusini-mashariki.

    Maafisa wa Taiwan wameithibitishia BBC kwamba meli hiyo ilinaswa ndani ya eneo la maji ya China, takribani maili 2.8 (5.1km) kutoka pwani yake.

    Ilikuwa pia ikifanya kazi wakati wa marufuku ya uvuvi ya kila mwaka ya China katika majira ya joto kutoka Mei hadi Agosti.

    "Meli ya wavuvi ilikiuka kanuni za kusitisha uvuvi na ilitembea kinyume cha sheria ndani ya eneo lililopigwa marufuku," Liu Dejun, msemaji wa Walinzi wa Pwani ya China, alisema.

    Pia aliishutumu kwa kutumia zana zisizo sahihi za uvuvi na "kuharibu rasilimali za uvuvi wa baharini". Taiwan bado haijajibu lolote kuhusu madai haya.

    Mivutano imekuwa ya kawaida katika eneo linalogombaniwa la maili 110 linalotenganisha China na Taiwan.

    China inadai Taiwan inayojitawala kama yake na bahari kama eneo lake la kipekee la kiuchumi, ingawa nchi nyingine zinazopitia maji haya, kama vile Japan na Marekani hazitambui hili.

    Na jeshi la China limeongeza shinikizo kwa Taiwan katika miaka ya hivi karibuni.

    Mamlaka za China zimekamata meli 17 zilizosajiliwa Taiwan tangu 2003 kwa ajili ya uvuvi wakati wa marufuku ya majira ya joto, data ya Taipei inaonesha. Taiwan pia imezuia boti tano kama hizo kutoka China mwaka huu pekee.

  4. Huzuni, hasira baada ya watu 121 kupoteza maisha kutokana na mkanyagano India

    Siku moja baada ya watu 121 kukanyagana hadi hadi kufa katika hafla ya kidini katika jimbo la kaskazini mwa India la Uttar Pradesh, familia za baadhi ya waathiriwa bado zinawatafuta wapendwa wao.

    Tukio hilo lilitokea wakati wa satsang (tamasha ya kidini ya Kihindu) iliyoandaliwa na mhubiri anayejiita Bhole Baba.

    Polisi walisema kuwa msongamano mkubwa wa watu katika ukumbi huo katika wilaya ya Hathras ulisababisha watu wengi kukumbwa natukio hilo siku ya Jumanne , wamefungua kesi dhidi ya waandaji wakuu wa hafla hiyo.

    Ni mojawapo ya majanga ambayo yamekuwa yakitokea kwa miaka mingi nchini India, ambapo ajali zinazohusisha umati mkubwa mara nyingi hulaumiwa kwa hatua za usalama na usimamizi.

    Siku ya Jumatano, idadi kubwa ya polisi walikuwepo wanasiasa walipotembelea eneo hilo ili kujua jinsi mkasa huo ulivyotokea.

    Makumi ya wafanyakazi walikuwa na shughuli nyingi wakiondoa hema iliyokuwa imetanda kutoka kwa eneo la tukio, karibu mita 500 kutoka barabara kuu.

  5. Mtoto ahofiwa kuliwa na mamba nchini Australia

    Msako mkali unaendelea kaskazini mwa Australia kumtafuta mtoto anayehofiwa kuchukuliwa na mamba.

    Mtoto mwenye umri wa miaka 12 alionekana mara ya mwisho jioni ya Jumanne, akiogelea karibu na mji wa mbali wa Nganmarriyanga umbali wa takribani saa 7 kwa gari kuelekea kusini magharibi mwa Darwin.

    Polisi wanasema timu ya wataalamu wa utafutaji na uokoaji imetumwa baada ya "ripoti za awali kusema mtoto huyo alishambuliwa na mamba".

    Eneo hilo ina makadirio ya mamba 100,000 wa maji ya chumvi, zaidi ya mahali pengine popote duniani, lakini mashambulizi si ya kawaida.

    Wanajamii huko Nganmarriyanga, hapo awali ilijulikana kama Palumpa na makazi ya watu 364 pekee na polisi wa eneo hilo walianza kumtafuta mtoto huyo mara baada ya kutoweka mwendo wa 17:30 saa za ndani (08:00 GMT).

    Sasa wameunganishwa na maafisa wa ziada na timu ya utaftaji na uokoaji wa kitaalamu ambao wanatafuta nchi kavu na majini.

    Utafutaji wa angani unaweza pia kuanza, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

  6. Polisi Kenya wachapisha picha za wanaosakwa kwa uhalifu wakati wa maandamano,

    Huduma ya Polisi ya Kenya imetoa picha za waandamanaji wanaosakwa kutokana na vitendo vyao visivyo halali wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

    ‘’...tunawashauri kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu kwa hatua zaidi...,’’ Huduma ya polisi imesema.

    Hii inawadia huku Wizara ya Usalama nchini humo ikitoa taarifa kusema kuwa kuna watu wanaotumia fursa ya kidemokrasia ya kufanya maandamanamo kutekeleza machafuko, ghasia na uporaji.

    ‘’Licha ya kusitishwa kwa Mswada huo, makundi ya magenge ya wahalifu waporaji yanaendelea kuwa hatari kubwa kwa umma, yakitumia vibaya mipango iliyotangazwa ya maandamano ya amani kuvuruga utulivu wa umma, kuchoma moto, kuzuia usafiri wa umma na kutisha watu wa Kenya kwa kufanya ghasia,’’ Taarifa ya wizara ya usalama ilisema.

    Waziri wa Usalama kithure kindiki alisema kuwa maovu yote hayo yanapaswa kusitishwa kwa namna yeyote ile.

    Maandamano ya Jumanne, 03 Julai, yalishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya miji nchini Kenya huku shughuli za kila siku zikilemazwa.

    Soma zaidi:

  7. Maafisa wa zamani wasema sera ya Gaza imeweka Marekani katika hatari

    Maafisa 12 wa zamani wa utawala wa Biden waliojiuzulu kutokana na sera kuhusu Israel na vita vya Gaza wanasema hatua za serikali zimehatarisha usalama wa taifa la Marekani.

    Sera hizo zimevuruga zaidi eneo hilo na "kurejesha malengo ya Marekani nyuma", wanasema katika taarifa ya pamoja.

    Mmoja wa wale 12 alijiuzulu Jumanne kutoka Idara ya Mambo ya Ndani ya Marekani

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hapo awali ilikanusha madai hayo, ikiashiria ukosoaji wake wa kujeruhi raia huko Gaza na juhudi zake za kuimarisha misaada ya kibinadamu.

    Taarifa ya pamoja ya maafisa hao wa zamani inasema: "Njia ya kidiplomasia ya Marekani na kuendelea kuipa silaha Israel kumehakikisha ushiriki wetu usiopingika katika mauaji na usababishaji wa baa la njaa kwa wakazi wa Palestina waliozingirwa huko Gaza."

    Hii si kauli ya kwanza kama hiyo kutoka kwa maafisa wa zamani lakini inakuja sambamba na kujiuzulu kwa hivi punde kutoka kwa utawala wa Maryam Hassanein, msaidizi maalum katika Idara ya Mambo ya Ndani ya Marekani. Pia alitia saini taarifa hiyo.

    Maafisa hao wa zamani wanaishutumu serikali ya Marekani kwa kung'ang'ania "sera iliyofeli" ambayo sio tu imekuwa mbaya kwa watu wa Palestina lakini imehatarisha Waisrael, kukandamiza uhuru wa kujieleza na kudhoofisha uaminifu wa Marekani juu ya kujitolea kwake kwa utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria.

    Soma zaidi:

  8. 'Mimi si mfuasi wa kanisa': Robert F Kennedy Jr ajibu madai ya unyanyasaji wa ngono

    Mgombea huru wa urais wa Marekani Robert F Kennedy Jr ameelezea simulizi ya Vanity Fair kama "takataka chungu nzima", akijibu madai kadhaa ikiwa ni pamoja na kwamba alimnyanyasa kingono aliyekuwa mlezi wa familia.

    Vanity Fair iliripoti kwamba mwishoni mwa miaka ya 1990, Bw Kennedy alikuwa amempapasa Eliza Cooney, mhitimu wa chuo kikuu hivi majuzi aliyeajiriwa kama mlezi wa watoto wake wa muda na kumsaidia katika kazi yake ya sheria ya mazingira. Alikuwa na umri wa miaka 23 wakati huo.

    Alipoulizwa haswa kuhusu madai haya na mengine kwenye podcast ya Breaking Points , Bw Kennedy alisema, "Mimi si mfuasi wa kanisa."

    "Nilikuwa kijana mbaya sana," alisema. "Nilisema katika hotuba yangu ya tangazo kwamba nina mengi mabaya ambayo yapo kama siri na ikiwa yote wanaweza kupiga kura, ningeweza kugombea mfalme wa ulimwengu wote."

    Alipobanwa na mtangazaji wa podikasti Saagar Enjeti zaidi kuhusu madai ya unyanyasaji wa kijinsia, Bw Kennedy alisema hakuwa na maoni yoyote.

    Jarida hilo pia liliripoti kwamba alikuwa na mahusiano kadhaa ya nje ya ndoa na alimtetea kwa nguvu binamu yake, Michael Skakel, ambaye alipatikana na hatia ya mauaji ya msichana wa miaka 15 huko Greenwich, Connecticut.

    Kampeni ya Bw Kennedy ilielekeza wanahabari kwenye ujumbe wa mtandao wa X ambapo alishutumu jarida hilo kwa kushirikiana na uongozi wa Chama cha Democratic.

    Walipokuwa wakijadili makala kuhusu podikasti hiyo, Bw Kennedy aliangazia madai tofauti katika simulizi hiyo - kwamba alipiga picha na mbwa aliyechomwa alipokuwa safarini kuelekea Korea, baadaye akatania kuhusu hilo katika ujumbe kwa rafiki yake.

    Bw Kennedy alisema picha hiyo haikupigwa nchini Korea bali katika eneo la Patagonia Amerika Kusini, na kwamba mnyama aliyeonyeshwa alikuwa mbuzi.

    Ripota wa Vanity Fair Joe Hagen, ambaye hapo awali aliandika wasifu wa Bw Kennedy kwa jarida hilo, na kusema picha hiyo ilikuwa ushahidi wa Bw Kennedy "wakati huo huo akidhihaki utamaduni wa Wakorea, akifurahia ukatili wa wanyama, na kuhatarisha sifa yake na ya familia yake bila sababu".

    Simulizi hiyo pia ilielezea madai ya mahusiano ya Bw Kennedy na ilijumuisha maelezo ya uraibu wa dawa za kulevya katika ujana wake, ambayo mgombea huyo amekuwa wazi.

    Katika podikasti hiyo hiyo, Bw Kennedy - mtoto wa Robert F Kennedy na mpwa wa Rais John F Kennedy - alisema kwamba ingawa alikuwa amejitolea kugombea urais kama mgombea huru, "njia bora kwangu ya Ikulu ya White House ni kupitia chama cha Democratic”.

    Soma zaidi:

  9. Euro 2024: Uturuki na Uholanzi zaingia robo fainali ya Euro

    Merih Demiral alifunga mara mbili - ikiwa ni pamoja na bao la haraka zaidi la hatua ya mtoano katika historia ya Uropa - huku Uturuki ikiishangaza Austria kwa ushindi wa mabao 2 -1 na kutinga robo fainali na Uholanzi.

    Kwingineko mchezaji wa akiba Donyell Malen alifunga mara mbili naye Cody Gakpo akafunga bao lake la tatu la Euro 2024 na kusaidia Uholanzi kuishinda Romania mabaoa 3-0 na kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.

    Mshambulizi wa Liverpool Gakpo alifunga bao la kwanza kwa kumalizia vyema katikati ya kipindi cha kwanza.

    Unaweza pia kusoma

  10. Rais wa zamu wa EU ataka kusitishwa kwa mapigano ya Ukraine na Urusi

    Viktor Orban aliwasili Ukraine siku ya Jumanne kwa ziara ambayo haijatangazwa baada tu ya kuchukua nafasi ya rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya.

    Akiwa mjini Kyiv, waziri mkuu wa Hungary alisema kusitishwa kwa mapigano kati ya Urusi na Ukraine kunaweza kuharakisha mazungumzo ya kumaliza vita vilivyofuatia uvamizi wa Urusi mwaka 2022.

    Bw Orban amekuwa mkosoaji wa uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine na anaonekana kuwa kiongozi wa Ulaya aliye karibu zaidi na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Hii ilikuwa ziara yake ya kwanza nchini Ukraine katika kipindi cha miaka 12, ingawa amekutana na Bw Putin mara kwa mara wakati huo.

    Wakati wa kuonekana kwake pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hakukuonekana kuwa na wasiwasi wowote kati yao lakini pia hakujibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari baada ya kutoa taarifa zao.

    Hapo awali Bw Orban alipunguza kasi ya makubaliano ya mfuko wa msaada wa Euro bilioni 50 ($54bn; £42bn) uliotengwa kusaidia Ukraine katika utetezi wake dhidi ya Urusi.

    Lakini kwa muda wa miezi sita ijayo nafasi yake kama mkuu wa Baraza la Ulaya ina maana kwamba ana jukumu kubwa kama kiongozi wa Ulaya. Alikuja Ukraine katika siku yake ya pili katika jukumu hilo kwa majadiliano, akisema kuna haja ya kusuluhisha kutoelewana kwa hapo awali na kuzingatia siku zijazo.

    Katika taarifa yake kufuatia mkutano wao, Bw Zelensky alisema ni "muhimu sana Ukraine kuungwa mkono na Ulaya kuendelea kudumishwa kwa kiwango cha kutosha... ni muhimu kwa ushirikiano kati ya majirani wote barani Ulaya kuwa wa maana zaidi na wa kunufaishana".

    Katika taarifa yake mwenyewe, Bw Orban alisisitiza haja ya kufanya kazi pamoja lakini pia alisema ameibua wazo la kusitisha mapigano ili kuharakisha mazungumzo na Urusi.

    Soma zaidi:

  11. Marufuku ya wanasiasa wa Wales kusema uwongo kupitishwa kabla ya 2026

    Marufuku ya wanasiasa wanaosema uwongo italetwa kabla ya uchaguzi wa Senedd wa 2026, serikali ya Wales imeahidi.

    Wakili Mkuu Mick Antoniw aliapa kutunga sheria siku ya Jumanne katika hatua iliyoepusha serikali kushindwa katika Bunge la Wales.

    Labor ilikabiliwa na kupoteza kura ilipojaribu kusitisha jaribio la Plaid Cymru kupitisha toleo lake la kupiga marufuku kusema uwongo.

    Bw Antoniw aliahidi kwamba sheria hiyo itawanyima haki wanasiasa wa Senedd na wagombeaji watakaopatikana na hatia ya udanganyifu wa kimakusudi kuwa Mbunge wa Senedd.

    BBC Wales iliambiwa kwamba mawaziri walifikia makubaliano na Plaid Cymru na waziri wa zamani wa Leba Lee Waters saa chache kabla ya upigaji kura kufanyika.

    Mwishowe, serikali ilishinda kwa kura 26, 13 za kupinga na 13 hawakupiga kura.

    Kiongozi wa zamani wa Plaid Cymru Adam Price alisema kilichotangazwa ni cha "kihistoria kweli".

    Majadiliano yalikuwa yamefanyika na vyama vya upinzani siku nzima, huku Bw Antoniw akichukua hatua isiyo ya kawaida ya kwenda kwenye mkutano wa kundi la Conservative Party Jumanne asubuhi.

    Mnamo mwezi Mei, Bw Waters alimsaidia kiongozi huyo wa zamani wa Plaid kurekebisha sheria kuhusu uendeshaji wa uchaguzi, ambayo kwa sasa inazingatiwa na bunge, kuanzisha kosa jipya la udanganyifu katika siasa.

    Sheria hiyo, kama ingepitishwa, ingewapa wanasiasa na wagombea siku 14 kufuta taarifa ya uwongo.

    Ikiwa wangefunguliwa mashtaka kupitia mahakama wangepigwa marufuku kuwa wabunge kwa miaka minne.

    Bado haijabainika ikiwa sheria inayopendekezwa itafanya kusema uwongo kuwa kosa la jinai au adhabu ya raia.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Biden alaumu uchovu wa safari ya ndege kwa matokeo duni katika mdahalo na Trump

    Rais Joe Biden amelaumu utendaji wake duni wa mijadala wiki iliyopita kutokana na uchovu wa safari ya ndege, akiwaambia waandishi wa habari kwamba "hakuwa mwerevu sana" kwa "kuzunguka ulimwengu mara kadhaa" kabla ya mjadala.

    "Sikuwasikiliza wafanyakazi wangu... na kisha nikakaribia kulala jukwaani," alisema.

    Bw Biden, 81, alirejea mara ya mwisho kutoka safarini tarehe 15 Juni, karibu wiki mbili kabla ya mjadala wa tarehe 27 Juni.

    Matamshi ya Bw Biden yanakuja huku kukiwa na hofu ya ndani ya chama kabla ya uchaguzi wa Novemba kuhusu utimamu wake wa kiakili, na baada ya mbunge kutoka Texas kuwa mbunge wa kwanza wa chama cha Democratic kumtaka ajiondoe kinyang’anyironi kufuatia mjadala wake.

    "Nina matumaini kwamba atafanya maamuzi magumu ya kujiondoa," Mwakilishi Lloyd Doggett alisema katika taarifa Jumanne.

    Rais Biden alionekana kutatizika kupitia baadhi ya majibu wakati wa mjadala na Rais wa zamani Donald Trump Alhamisi iliyopita.

    "Sio kisingizio bali ni maelezo," alisema katika harambee ya kibinafsi huko Virginia Jumanne jioni, akimaanisha safari yake.

    Pia aliomba radhi kwa utendaji wake na kusema ni "muhimu" kwamba ashinde uchaguzi tena, kulingana na ABC News.

    Bwana Biden alifanya safari mbili tofauti kwenda Ulaya katika muda wa wiki mbili mwezi uliopita.

    Tarehe 15 Juni, alionekana kwenye harambee ya kuchangisha pesa pamoja na Rais wa zamani Barack Obama baada ya safari ya usiku kucha kutoka Italia. Alirudi Washington DC siku iliyofuata.

    Maafisa wa Ikulu ya White House hapo awali walisema Bw Biden alikuwa akipambana na mafua siku ya mjadala.

    Rais hakutaja ugonjwa wowote katika matamshi yake siku ya Jumanne. Msemaji wa Ikulu ya White House alisema mapema siku hiyo kwamba hakuwa akinywa dawa yoyote ya mafua wakati wa mjadala.

    Soma zaidi:

  13. Marufuku ya ndoa za utotoni yapokelewa vyema Sierra Leone

    Sierra Leone imeanzisha sheria mpya ya kupiga marufuku ndoa za utotoni kwa mbwembwe nyingi katika sherehe iliyoandaliwa na mke wa Rais Fatima Bio katika mji mkuu, Freetown.

    Wageni waalikwa, wakiwemo wake wa marais kutoka Cape Verde na Namibia, walitazama jinsi mumewe Rais Julius Maada Bio akitia saini mswada wa Marufuku ya Ndoa za Utotoni kuwa sheria.

    Mtu yeyote ambaye sasa atahusika katika ndoa ya msichana aliye na umri wa chini ya miaka 18 atafungwa jela kwa takriban miaka 15 au kutozwa faini ya karibu $4,000 (£3,200), au zote mbili.

    Mwanafunzi wa chuo kikuu Khadijatu Barrie, ambaye dadake aliolewa akiwa na umri wa miaka 14, aliambia BBC kuwa alifurahishwa na marufuku hiyo lakini akatamani ilianza mapema ili kumwokoa mdogo wake.

    “Natamani sana ingeanza mapema. Angalau ningeweza kumuokoa dada yangu na marafiki zangu na majirani wengine,” mhitimu huyo wa masomo ya jinsia mwenye umri wa miaka 26 alisema.

    Sierra Leone ni jamii ya mfumo dume na ni kawaida kwa baba kumtoa bintiye kwa ndoa ya lazima.

    Bi Barrie alikabiliana na hali hiyo akiwa na umri wa miaka 10. Alikataa na kutoroka nyumbani baada ya babake kumkataa.

    Alipata bahati ya kupata walimu waliomlipia karo ya shule na mfanyakazi mwenye huruma kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ambaye alimsaidia kwa kumpa mahali pa kuishi.

    Lakini anasema ni vigumu kwa wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini kupinga mila hiyo na kila jamii itahitaji kufahamishwa kuhusu sheria hiyo mpya ili kuanza kutekelezwa kwa ufanisi.

    "Ikiwa kila mtu ataelewa kile kinachokungoja utakapofanya hivyo, nina uhakika nchi hii itakuwa bora," Bi Barrie alisema.

    Wizaŕa ya afya inakadiria kuwa thuluthi moja ya wasichana wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18, na hivyo kusababisha idadi kubwa ya vifo vya uzazi nchini humo – miongoni mwa vifo vya juu zaidi duniani.

    Wale wanaokabiliwa na adhabu chini ya sheria hizo mpya ni pamoja na bwana harusi, wazazi au walezi wa mtoto harusi, na hata wale wanaohudhuria harusi.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 03/07/2024