Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Maelfu ya wanajeshi wa Congo kushtakiwa kwa kuwakimbia waasi wa M23

Umoja wa Mataifa imeripoti ukiukwaji mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji wa genge na utumwa wa kingono kufuatia kuingia kwa waasi wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari na hatimaye kuuteka mji mkuu wa Goma.

Moja kwa moja

Na Asha Juma na Mariam Mjahid

  1. Shukran za dhati wasomaji wetu kwa kufuatilia matangazo haya ya moja kwa moja kuanzia asubuhi hadi sasa. Huu ndio mwisho wa matangazo yetu siku ya leo.Nawatakia usiku mwema,kila la kheir.

  2. Rais wa Romania Klaus Lohannis ajiuzulu kabla ya duru ya pili ya uchaguzi

    Rais wa Romania, Klaus Iohannis, amejiuzulu kufuatia shinikizo la kumtaka aachie madaraka kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais mpya baada ya uchaguzi wa mwaka jana kutenguliwa kwa utata.

    Uchaguzi wa mwezi Disemba ulifutwa na mahakama kuu ya Romania baada ya tuhuma za kuingiliwa na serikali ya Urusi.

    Rais anayeondoka Iohannis, ambaye ni mliberali anayeunga mkono Umoja wa Ulaya, alieleza kuwa atabaki madarakani hadi rais mwingine atakapochaguliwa mwezi Mei.

    Hata hivyo, jambo hili lilikosolewa vikali na wanasiasa wa mrengo wa kulia na wafuasi wao, ambao walifanya vizuri katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Disemba.

    Ukosoaji wao uliwahamasisha maelfu ya Waromania kuandamana mwezi jana kupinga kufutwa kwa uchaguzi.

    Wabunge wa upinzani walileta pendekezo tena bungeni Jumatatu kutaka rais asimamishwe.

    Akionekana kuwajibu, Iohannis alisema angejiuzulu ili kupunguza kile alichokiita “kura ya maoni inayoweza kuwa na madhara” na inayoweza kugawanya nchi.

    “Kwa ajili ya kuiepusha Romania na wananchi wa Romania katika mgogoro… najiuzulu kutoka nafasi ya rais wa Romania,” alisema.

    Rais huyo wa Romania alisema atajiuzulu rasmi Jumatano.

  3. Ugiriki: Santorini na visiwa vilivyo karibu vyaendelea kukumbwa na matetemeko ya ardhi

    Matetemeko mengine matatu ya ardhi yametokea karibu na kisiwa cha Ugiriki cha Santorini, na kuzua wasiwasi unaoendelea kukumba eneo hilo ambalo ni kivutio cha watalii.

    Wakazi wa nchi jirani ya Amorgos wamesalia katika hali ya tahadhari baada ya tetemeko la Jumatatu, ambalo lilifuatia tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa wastani wa 5.0 kati ya visiwa hivyo Jumapili jioni.

    Eneo hilo limekumbwa na matetemeko ya ardhi kwa muda wa wiki mbili zilizopita, na wataalam wanakisia huenda kutokea tetemeko kubwa la ardhi.

    Hali ya dharura itaendelea kudumishwa katika kisiwa cha Santorini hadi angalau 3 Machi.

  4. Ushuru wa China dhidi ya Marekani waanza rasmi

    China imeanza kutoza ushuru bidhaa za Marekani zinazongia nchini humu hii leo, huku mzozo wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili ukichacha.

    Rais Donald Trump ametishia kutoza ushuru zaidi mataifa mengine.

    Beijing ilitangaza msimamo wake tarehe 4 Februari muda mfupi baada ya Marekani kutoza ushuru wa 10% kwa bidhaa zote kutoka China kuanza kutekelezwa.

    Siku ya Jumapili, Trump alidokeza kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za alumini na chuma zinazoingia nchini humo.

    Akizungumza na wanahabari alipokuwa akielekea katika shindano la Super Bowl, alisema alikuwa anapanga kutoza ushuru kwa mataifa mengine lakini hakufichua ni nchi kama zipi.

    Ushuru wa hivi punde zaidi wa China kwa bidhaa za Marekani ni pamoja na ushuru wa mpaka wa asilimia 15% kwa uagizaji wa makaa ya mawe ya Marekani na bidhaa za gesi asilia iliyoyeyushwa.

    Pia kuna ushuru wa asilimia 10% kwa mafuta yasiyosafishwa ya Amerika, mashine za kilimo na magari ya injini kubwa.

    Trump amelalamika mara kwa mara kwamba ushuru wa Umoja wa Ulaya kwa uagizaji wa magari ya Marekani ni kubwa zaidi kuliko ushuru wa Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Marekani imejitolea 'kuinunua na kuimiliki' Gaza -Trump

    Rais wa Marekani Donlad Trump ametangaza kuwa Marekani imedhamiria kununua na kumiliki Ukanda wa Gaza na kuhamisha Wapalestina milioni mbili wanaoishi huko, licha ya pendekezo hilo kupingwa vikali duniani.

    Trump amewaambia wanahabari kuwa huenda akaruhusu mataifa ya kiarabu kuhusika katika kukarabati upya sehemu mbalimbali na kuwa atahakikisha raia wa Palestina wataishi maisha mazuri.

    Mamlaka ya Palestina na kikundi kilicho na silaha cha Hamas ambao wamekuwa vitani kwa miezi 16 na Israel na kusababisha maafa Gaza, wamemjibu wakisema ardhi ya Palestina sio ya kuuzwa''.

    Lakini waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameipigia upatu pendekezo hilo la Trump akilitaja ni ''mwamko mpya na bunifu''.

    Haya yanajiri wiki tatu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza kuanza, Huku Hamas ikiachilia huru baadhi ya mateka wa Israel inayowazuia ili kubadilishana na Wafungwa wa Palestina walioko katika magereza ya Israel.

    Wanajeshi wa Israel walianzisha kampeini ya kuvamia na kuharibu Gaza wakijibu shambulizi la kushtukizia la mwezi Oktoba tarehe 7 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na 251 wakatekwa nyara.

    Zaidi ya watu 48,180 wameuliwa Gaza tangu mapigano hayo yaanze , hii ni kwa mujibu wa wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Trump aagiza hazina ya Marekani kukomesha utengezaji wa senti moja

    Rais wa Marekani Donald Trump amemuagiza waziri fedha wa nchi hiyo, Scott Bessent kukomesha utengenezaji wa senti moja, au mapenikatika tangazo alilotoa kwenye akaunti yake ya mitandao ya kijamii ya Truth Social.

    “Tuchukue hatua ya kukomesha matumizi yasiyo ya lazima kutoka kwenye bajeti yetu ya taifa, hata kama ni senti moja kwa wakati mmoja,” ilisema taarifa hiyo ya Trump, ikiielezea hatua hiyo kama jitihada ya kupunguza gharama.

    Haya yanajiri baada ya Idara isiyo rasmi ya Ufanisi wa Serikali (Doge) ya Elon Musk kuvutia umakini kuhusu gharama ya kutengeneza senti moja katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa X mwezi uliopita.

    Mjadala kuhusu gharama na manufaa ya senti moja umekuwa wa muda mrefu nchini Marekani.

    “Haya ni matumizi mabaya ya rasilimali,” ilisema taarifa hiyo ya Trump kwenye Truth Social.

    “Nimemuaru Waziri wangu wa Fedha ya Marekani aache kutengeneza senti mpya.”

    Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya Mint ya Marekani ya 2024, kutengeneza na kusambaza sarafu ya senti moja inagharimu senti 3.69.

    Maafisa wa serikali ya Marekani na wabunge wamewahi kupendekeza utengenezaji wa senti kukomeshwa lakini pendekezo hilo liligonga mwamba.

    Wale wanaopinga wanasema kwamba sarafu ya shaba na zinki ni matumizi mabaya ya fedha na rasilimali, huku wafuasi wake wakiisema kuwa sarafu hii inasaidia kupunguza bei na kuongeza michango kwa mashirika ya hisani.

    Nchi zingine zimeacha kutengeneza sarafu kama hizi.

    Canada iliacha kutengeneza sarafu ya senti moja mwaka 2012 ikieleza gharama ya kutengeneza sarafu hiyo na kupungua kwa nguvu yake ya ununuzi kutokana na kupanda kwa bei.

    Kupungua kwa matumizi ya fedha taslimu kumefanya Uingereza kutotengeneza sarafu mpya mwaka 2024, baada ya maafisa kuamua kuwa tayari kuna sarafu za kutosha katika mzunguko.

    Hazina ya Uingereza imesema kuwa sarafu za peni moja au peni 2 hazitafutwi, lakini kwa kuwa zaidi ya watu wanaishi maisha yasiyo na fedha taslimu, kumekuwa na miaka kadhaa ambapo sarafu za peni mbili hazikutengenezwa.

    Sarafu za peni 20 pia zimepitia vipindi mbalimbali bila kutengenezwa mpya.

    Pia unaweza kusoma:

  7. RSF wahimizwa kuondoa vizuizi vya kusambaza misaada ya chakula Darfur

    Shirika la Umoja wa Mataifa linawahimiza Vikosi vya waasi wa RSF nchini Sudan kuondoa vikwazo vya msaada katika eneo la Darfur, ambako vita vimeharibu kila kitu.

    Mratibu wa misaada anasema kuwa vikwazo na vizingiti vya kusambaza msaada vilivyowekwa na RSF vimezuia sana juhudi za kufikia jamii zilizohama zinazokumbwa na njaa kali.

    Mratibu mkazi, Clementine Nkweta-Salami, anatahadharisha kuhusu janga la kibinadamu iwapo RSF itaendelea kuzuia misaada kuingia Darfur, ambapo wamekuwa wakipigana na jeshi kwa miaka miwili.

    Anasema kuingilia katika juhudi za msaada hakukubaliki.

    Wafanyakazi wa misaada wameripoti uhalifu, kuzuia misaada, na vitisho kutoka kwa RSF na jeshi la Sudan.

    Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 25 wanakutana na upungufu mkubwa wa chakula, huku njaa ikishuhudiwa katika maeneo matatu ya Kaskazini mwa Darfur.

    Vita vimeua maelfu ya watu na kuwahamisha milioni kadhaa wakitoroka kutafuta chakula.

    Soma pia:

  8. DRC yajibu mkutano wa pamoja wa EAC-SADC

    Serikali ya DRC imetoa shukrani zake kwa mkutano wa pamoja wa EAC-SADC ambao ulitoa taarifa ya pamoja kuwataka viongozi wanaoshiriki miungano hiyo kuheshimu uhuru wa DRC na kuendeleza mpango wa kuondoa vikosi kutoka nchi za kigeni ambavyo havijaidhinishwa kutoka eneo lake.

    Hii lilikusudiwa kulenga vikosi vya Rwanda na washirika wao wanaoendsha shughuli zao ndani ya mipaka ya Congo.

    ‘’Kujitolea kumaliza uwepo wowote wa kijeshi ambao haujaalikwa ni hatua muhimu katika juhudi za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,’’ serikali ya DRC ilisema.

    Kwa kuzingatia hali mbaya za usalama na matatizo ya kibinadamu, hatua za haraka zilipitishwa wakati wa mkutano huo. Hii ni pamoja na:

    1. Kukomesha vita na uhasama bila masharti.

    2. Uwasilishaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu, pamoja na kurudishwa kwa watu waliofariki na kuhamishwa kwa waliojeruhiwa.

    3. Kuhakikisha usalama katika njia muhimu za usambazaji bidhaa kama barabara na maziwa.

    4. Kufungua tena uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma.

    5. Kuhakikisha usalama katika mji wa Goma na maeneo yaliyo karibu

    Serikali ya DRC ilisisitiza umuhimu wa kuanza tena michakato ya Luanda na Nairobi kama njia kuu za utatuzi wa migogoro.

    Mchakato wa Luanda unazingatia kugeuza vikundi vyenye silaha kama Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) na kuhakikisha kuwa vikosi vya Rwanda vinaondoka Congo.

    Wakati huo huo, mashauriano chini ya mchakato wa Nairobi yamekusudiwa kuwashirikisha watendaji wasio wa serikali katika majadiliano ya kuleta amani.

    Taarifa iliyotolea na DRC pia ilisisitiza ahadi yake ya kufuatilia maendeleo ya makubaliano kutoa wito kwa wadau wote wanaohusika - wa ndani na wa kimataifa – kutimiza wajibu wao, kujizuia, na kutekeleza kwa uaminifu hatua zilizokubaliwa.

    Soma zaidi:

  9. Jeshi la Sudan linapanga serikali mpya baada ya kutwaa tena mji mkuu

    Jeshi la Sudan limetaka uungwaji mkono wa kidiplomasia kwa serikali mpya ambayo inasema inataka kuunda baada ya kutwaa tena mji mkuu, Khartoum, kutoka kwa vikosi vinavyohasimiana.

    Jeshi hilo limekuwa likidhibiti tena maeneo ya mji huo yaliyokuwa yakishikiliwa na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) katika wiki za hivi karibuni.

    Kiongozi wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan aliambia mkutano wa wanasiasa wanaounga mkono jeshi mwishoni mwa juma kwamba ataunda serikali yenye kuzingatia "taaluma na ustadi" wakati huu wa vita na waziri mkuu.

    Alisisitiza hakutakuwa na mazungumzo na RSF.

    Pande hizo mbili zimekuwa zikipigana kwa takriban miaka miwili - mzozo ambao umewalazimu watu milioni 12 kutoroka makwao na kuwaacha wengi wakihangaika kwa njaa.

    Jenerali Burhan pia alisema kutakuwa na katiba mpya kabla ya kuunda serikali ya mpito.

    "Tunaweza kuiita serikali ya muda, serikali ya wakati wa vita, lakini ni serikali ambayo itatusaidia kukamilisha kilichosalia katika malengo yetu ya kijeshi, ambayo ni kuweka huru Sudan kutokana na waasi hawa," alisema Jumamosi.

    Taarifa ya wizara ya mambo ya nje siku ya Jumapili ilitoa wito kwa "jumuiya ya kimataifa, haswa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kuunga mkono mpangokazi uliowasilishwa na serikali kama makubaliano ya kitaifa ya kurejesha amani na utulivu na kukamilisha majukumu ya mpito".

    Jeshi na RSF, ambazo ziliwahi kufanya kazi pamoja, wamekuwa wakikabiliana katika vita vikali vya kuwania madaraka.

    Soma zaidi:

  10. Maelfu ya wanajeshi wa Congo kushtakiwa kwa kuwakimbia waasi wa M23

    Mamlaka ya Congo itawahukumu wanajeshi wasiopungua 75 siku ya Jumatatu kwa kuwakimbia waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika eneo la Kivu Kusini kwa kusababisha vurugu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji na uporaji, ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi ilisema Jumapili.

    Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukwaji mkubwa ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji wa genge na utumwa wa kingono kufuatia kuingia kwa waasi wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari na hatimaye kuuteka mji mkuu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Wapiganaji wa M23, wanajeshi wa Congo na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wote walihusishwa, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za kibinadamu iligundua.

    Congo haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti zinazohusu wanajeshi wake, lakini ilitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukaji unaoulaumu waasi wa M23 na Rwanda.

    Rwanda, ambayo inakanusha kuunga mkono kundi hilo, imekataa kuwajibika kwa lolote.

    Waasi wa M23 hawajajibu ombi la kutoa maoni yao.

    Licha ya kutangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja, waasi hao wameendelea kusonga mbele kuelekea kusini katika mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu.

    Soma zaidi:

  11. Trump asema atatangaza viwango vipya vya ushuru wa biashara

    Rais Donald Trump amesema kuwa atatangaza ushuru wa 25% kwa chuma na aluminium zote zinazoingia Marekani, hatua ambayo itakuwa na athari kubwa zaidi nchini Canada.

    Trump pia alisema kutakuwa na tangazo baadaye wiki hii kuhusu ushuru sawa na nchi zote zinazotoza ushuru bidhaa kutoka Marekani lakini hakufafanua ni mataifa gani yangelengwa, au ikiwa kutakuwa na misamaha yoyote.

    "Ikiwa wanatutoza, pia sisi tutawatoza," Trump alisema.

    Aliwaambia waandishi wa habari kuhusu mipango yake alipokuwa akisafiri kutoka eneo la mapumziko la Mar-a-Lago huko Florida hadi New Orleans kulikokuwa na michezo aa Super Bowl siku ya Jumapili.

    Canada na Mexico ni washirika wawili wakubwa wa biashara ya chuma nchini Marekani, na Canada ndiyo msambazaji mkubwa wa madini ya alumini nchini Marekani.

    Wakati wa muhula wake wa kwanza, Trump aliweka ushuru wa 25% kwa uagizaji wa chuma na 10% kwa uagizaji wa alumini kutoka Canada, Mexico na Umoja wa Ulaya.

    Lakini Marekani ilifikia makubaliano mwaka mmoja baadaye na Canada na Mexico kumaliza ushuru huo, ingawa ushuru wa uagizaji wa EU ulibakia hadi 2021.

    Akizungumza akiwa kwenye ndege ya Air Force One, Trump alisema Jumatatu atatangaza ushuru kwa "kila mtu" kwa chuma na alumini.

    "Chuma chochote kinachoingia Marekani kitakuwa na ushuru wa 25%," alisema.

    Soma zaidi:

  12. Miili ya wahamiaji yapatikana katika kaburi la halaiki huko Libya - mamlaka

    Miili ya wahamiaji wasiopungua 28 imetolewa kutoka kwenye kaburi la halaiki katika jangwa la kusini-mashariki mwa Libya, mwanasheria mkuu wa nchi hiyo alisema.

    Kaburi hilo liligunduliwa kaskazini mwa Kufra, siku chache tu baada ya kaburi lingine la pamoja lililokuwa na miili 19 kupatikana kwenye shamba katika mji huo huo.

    Maafisa walipata kaburi la hivi karibuni kufuatia uvamizi kwenye tovuti ya usafirishaji binadamu kwa njia haramu, ambapo mamlaka iliwaachilia wahamiaji 76 waliokuwa wamezuiliwa na kuteswa, ofisi ya mwanasheria mkuu ilichapisha kwenye Facebook.

    Raia mmoja wa Libya na wageni wawili wamekamatwa, iliongeza.

    “Kulikuwa na genge ambalo wanachama wake kwa makusudi waliwanyima uhuru wahamiaji haramu, liliwatesa na kuwatendea ukatili, udhalilishaji na unyama,” ilisema taarifa hiyo.

    Picha zilizoshirikishwa mtandaoni - ambazo BBC haijathibitisha kwa kujitegemea - zinaonyesha polisi na watu waliojitolea wakichimba mchanga kabla ya kuweka maiti kwenye mifuko nyeusi.

    Msako unaendelea huko Kufra - zaidi ya kilomita 1,700 (maili 1,056) kutoka mji mkuu wa Libya Tripoli -

    Mwanasheria mkuu anasema miili iliyopatikana imechukuliwa kwa uchunguzi, huku wachunguzi wakishuku kuwa na uhusiano na mitandao ya usafirishaji binadamu kwa njia haramu.

    Mamlaka zinarekodi ushuhuda wa walionusurika.

    Soma zaidi:

  13. Tumbili alaumiwa na waziri kwa kukatika kwa umeme kote Sri Lanka

    Waziri wa nishati Kumara Jayakody nchini Sri Lanka amelaumu tumbili kwa kukatika kwa umeme kote nchini humo akidaiwa kuingia kwenye kituo cha uzalishaji umeme kusini mwa Colombo.

    Umeme unarejeshwa taratibu katika taifa hilo lenye watu milioni 22, huku vituo vya matibabu na mitambo ya kusafisha maji vikipewa kipaumbele.

    "Tumbili aligusa transfoma ya gridi yetu, na kusababisha kukosekana kwa usawa katika mfumo wa umeme," Waziri wa Nishati Kumara Jayakody aliwaambia waandishi wa habari.

    Ukosefu wa umeme ulianza karibu 11:00 saa za eneo Jumapili, na kuwalazimu wengi kutegemea jenereta. Maafisa wanasema inaweza kuchukua saa chache zijazo kurejesha huduma hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Raia wa Israel aliyeachiwa huru hakujua kuwa mke na binti yake waliuawa - familia ya Uingereza

    Mateka wa Israeli hakujua mke na binti zake waliuawa katika shambulio la Oktoba 7 hadi baada ya kuachiliwa huru kutoka Gaza Jumamosi, familia yake ya Uingereza ilisema.

    Eli Sharabi alichukuliwa na Hamas miezi 16 iliyopita na kuachiliwa Jumamosi huko Deir al-Balah, huko Gaza.

    Mkewe Lianne Sharabi, ambaye alikuwa akitoka Uingereza, na binti zake Noiya na Yahel walipatikana wameuawa katika nyumba yao wakiwa "wameshikana pamoja" mnamo mwaka 2023.

    Wazazi wa Lianne Gill na Pete Brisley waliiambia BBC Jumapili kwamba wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi cha Israeli (IDF) walimwambia Bwana Sharabi kilichotokea kwa familia yake.

    Jamaa zake hawakuwa na uhakika kama Bwana Sharabi alijua kuwa Lianne, Noiya na Yahel – binti na wajukuu zake - waliuawa katika shambulio la Oktoba 7.

    Alikuwa mmoja wa mateka watatu waliokabidhiwa Msalaba Mwekundu na Hamas katika picha zilizotolewa Jumamosi kama sehemu ya mpango wa kusitishwa kwa mapigano ya kimataifa.

    Akiongea kwenye jukwaa wakati wa kuachiliwa kwake, Bwana Sharabi alisema "ninafuraha sana leo kurudi nyumbani ... kwa mke na binti yangu", na kuongeza wasiwasi kwamba hakujua kile kilichowatokea.

    "Kitu pekee kinachotufanya tuendelee kusonga mbele ni kwamba Eli amerejea. Angalau kuna mtu mmoja wa familia yetu wa karibu ambaye bado yuko hai," Bi Brisley alisema.

    "[Tuna] shukrani kwake kwa wajukuu wetu wawili wa kike warembo, anao hakuwa nao kwa muda mrefu sana. Cha kuzingatia sasa ni nyakati zote za furaha.

    Bw Brisley alisema: "Tunatumai kuwa sehemu ya kumrudisha hadi kuwa katika hali ya kawaida."

    Soma zaidi:

  15. Vikosi vya Israeli vyajiondoa kutoka ukanda unaogawanya Gaza

    Wanajeshi wa Israeli wamejiondoa kutoka ukanda wa Netzarim - eneo la jeshi la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kutoka kusini.

    Mamia ya Wapalestina walionekana kwenye magari na mikokoteni iliyojaa magodoro na bidhaa zingine wakiwa wanarudi Kaskazini mwa Gaza kufuatia kujiondoa kwa vikosi vya Israeli – hasa katika maeneo yaliyoharibiwa zaidi.

    Uondoaji wa vikosi vya Israeli unaambatana na makubaliano ya kukomesha mapigano ya Israeli-Hamas ya Januari 19 ambapo mateka 16 wa Israeli na wafungwa 566 wa Palestina wameachiliwa.

    Mwisho wa hatua ya kwanza ya kusitisha mapigano katika muda wa wiki tatu, mateka 33 na wafungwa 1,900 wanatarajiwa kuachiliwa.

    Israeli inasema nane kati ya 33 wamefariki dunia.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya leo.