Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Zaidi ya watu 1,700 wauawa katika vita vinavyozidi kupanuka Mashariki ya Kati

Taarifa za serikali na maafisa wa usalama zinaonyesha vifo vingi vimetokea nchini Iran na Lebanon, na kiasi Israel huku mashambulizi pia yakileta athari pia katika nchi za Kuwait, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio nakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Israel yaanzisha 'mashambulizi mapya makubwa' dhidi ya Iran

    Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) linasema limeanzisha "mashambulizi mapya makubwa" dhidi ya maeneo lengwa huko Tehran na sehemu zingine za Iran.

    Mashambulizi haya yanaanza takriban saa moja baada ya IDF kusema kuwa imeshambulia makao makuu ya Jeshi la Anga za Juu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu huko Tehran, pamoja na mahandaki 50 ya risasi, katika mashambulizi ya awali leo.

    Centcom yaishutumu Iran kwa kutumia maeneo 'yenye msongamano' wa raia kuanzisha mashambulizi

    Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) inawasihi Wairani "kusalia nyumbani" huku ikidai kwamba utawala wa Jamhuri ya Kiislamu unafanya operesheni za kijeshi kutoka maeneo yenye raia wengi.

    Iran imetumia "maeneo yenye msongamano wa watu katika miji kama vile Dezful, Isfahan na Shiraz kurusha ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu", Centcom ilisema katika taarifa iliyotolewa kwenye X.

    Iliongeza kuwa tabia hii inaweka maisha ya raia hatarini "kwa kuwa maeneo yanayotumika kwa madhumuni ya kijeshi hupoteza hadhi ya ulinzi" na yanaweza kuwa shabaha halali.

    "Utawala wa kigaidi wa Iran unapuuza waziwazi maisha ya raia kwa kushambulia washirika wa Ghuba huku ukihatarisha usalama wa watu wao wenyewe," anasema kamanda wa Centcom Adm Brad Cooper.

    Soma zaidi:

  3. Zaidi ya watu 1,700 wauawa katika vita vinavyozidi kupanuka Mashariki ya Kati

    Zaidi ya watu 1,700 wameripotiwa kuuawa katika vita vinavyoendelea kati ya Iran, Israel na washirika wao, huku mashambulizi ya anga na makombora yakiripotiwa katika nchi kadhaa za Mashariki ya Kati.

    Taarifa za serikali na maafisa wa usalama zinaonyesha vifo vingi vimetokea nchini Iran na Lebanon, wakati mashambulizi pia yameripotiwa Kuwait, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)

    Kwa mujibu wa balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, zaidi ya raia 1,300 wameuawa tangu mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya maeneo mbalimbali nchini humo kuanza mwishoni mwa Februari.

    Nchini Lebanon, wizara ya afya imesema takribani watu 394 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel, wakiwemo watoto 83 na wanawake 42.

    Kwa upande wa Israel, mamlaka zimeripoti vifo 10 tangu Iran ianze mashambulizi ya makombora dhidi ya nchi hiyo.

    Mashambulizi pia yameripotiwa katika nchi nyingine za Ghuba. Kuwait imesema wanajeshi wawili pamoja na walinzi wawili wa mpaka wameuawa kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kambi ya kijeshi. Aidha, msichana mmoja ameripotiwa kufariki baada ya vipande vya chuma vya kombora kuanguka karibu na makazi ya raia.

    Huko UAE, Wizara ya ulinzi imesema watu wanne wameuawa kutokana na mashambulizi ya makombora yaliyodaiwa kurushwa kutoka Iran.

    Nchini Bahrain, Wizara ya mambo ya ndani imeripoti kuwa mfanyakazi mmoja aliuawa baada ya mabaki ya kombora kuanguka katika eneo la viwanda.

    Pamoja na takwimu , ni vigumu kwa BBC kuzithibitisha zote kutokana na mazingira magumu yaliyopo kwenye maeneo yanayohusisha mashambulizi ya vita hivi vinavyopanuka kila uchwao.

  4. Wanajeshi wawili wa Israel wauawa kusini mwa Lebanon

    Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) linasema wanajeshi wake wawili wameuawa kusini mwa Lebanon.

    Katika taarifa iliyosambazwa kwenye Telegram, IDF imemtaja mmoja wa wanajeshi hao kuwa ni Sajenti Mkuu Maher Khatar, 38, kutoka Majdal Shams.

    Inasema mwanajeshi huyo kutoka Kikosi cha Uhandisi wa Makabiliano aliuawa wakati wa mapigano kusini mwa Lebanon.

    Soma zaidi:

  5. Idara ya hali ya hewa Kenya yatahadharisha mvua kubwa kuendelea kunyesha jijini Nairobi

    Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imesema jiji la Nairobi litaendelea kushuhudia mvua mkubwa, ikiwaonya wakazi kuendelea kuchukua tahadhari huku ngurumo za radi zikiendelea katika eneo hilo.

    Tahadhari hii itaendelea kudumishwa hadi saa 1 jioni Jumatatu, Machi 9, 2026.

    Met alibainisha kuwa ingawa kiwango cha mvua kimepungua kidogo ikilinganishwa na kipindi cha kilele kati ya Machi 4-7, mvua ya wastani hadi kubwa itaendelea, na pia ina uwezekano wa kusababisha mafuriko.

    Idara ya hali ya hewa imewasihi madereva na abiria kuendesha magari kwa tahadhari kwenye barabara zinazoteleza na kuepuka kuvuka sehemu za mito na barabara zilizojaa maji.

    Soma zaidi:

  6. Vitisho vipya vya makombora UAE huku raia wakiagizwa kutahadhari

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya UAE inasema ulinzi wa anga "sasa unakabiliana na tishio la kombora".

    "Tafadhali kaa mahali salama na ufuate maonyo na taarifa mpya kwenye tovuti rasmi," inasema taarifa hiyo.

    Tunayojua kufikia sasa:

    Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Tehran chatoka moshi - haya ndiyo tunayojua kufikia sasa:

    Viongozi wa kidini wa Iran wamefikia makubaliano kuhusu kiongozi mpya mkuu - lakini wanasema bado kuna "changamoto" kadhaa kabla ya kumtaja.

    Israel pia imetishia "kumfuata kila mrithi" wa Ayatollah Ali Khamenei, ambaye aliuawa katika mashambulizi ya pamoja kati ya Marekani na Israel wikendi iliyopita.

    Mashambulizi ya Israel yanayolenga viwanda vya kusafisha mafuta yamesababisha moshi mzito mweusi unaoifunika Tehran - wakazi wanasema "ni kama jua limetoweka kabisa".

    Shambulizi la ndege zisizo na rubani za Iran limeathiri jengo refu la Taasisi ya Umma ya Usalama ya Kuwait, na kusababisha moto mkubwa - mamlaka zinasema moto huo umedhibitiwa.

    Mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon yanaendelea - kulingana na Waziri wa afya nchini humo na watu 394 wameuawa tangu mapigano ya hivi karibuni na Israeli yaanze.

    Soma zaidi:

  7. Wizara ya Afya yasema watu 400 wameuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon

    Idadi ya vifo nchini Lebanon kutokana na mapigano na Israel imeongezeka hadi watu 394, kulingana na waziri wa afya wa serikali.

    Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili, Rakan Nasserdine alisema waliofariki ni pamoja na watoto 83 na wanawake 42 tangu Lebanon ilipoanza kuhusika na vita kati ya Marekani na Israeli na Iran.

    Nasserdeddine aliongeza kuwa wafanyakazi tisa wa uokoaji pia wamefariki.

    Jumla ya vifo nchini Lebanon imeongezeka ikilinganishwa na Jumamosi, wakati waziri wa afya aliposema idadi hiyo ni watu 294.

  8. Vita vya usiku kucha: Picha zaonyesha makombora na moto ukiwaka katika anga la usiku

    Moto mkubwa wateketeza kituo cha mafuta cha Aqdasieh cha Iran mjini Tehran baada ya jeshi la Israel kusema kuwa limeshambulia baadhi ya vituo vya mafuta vya nchi hiyo usiku kucha.

    Wahudumu wa afya wakikagua uharibifu katika Hoteli ya Ramada huko Beirut baada ya Israel kushambulia jengo hilo, na kuua watu wasiopungua wanne. Israel ilisema ilikuwa ikiwalenga makamanda wa Iran katika mji mkuu wa Lebanon.

    Moto uliharibu jengo la serikali ya Kuwait mapema Jumapili kufuatia mashambulizi zaidi ya ndege zisizo na rubani katika jimbo la Ghuba.

    Njia ya roketi kutoka kwa kombora inaangaza katika anga la usiku juu ya Netanya, mji wa pwani na eneo la watalii nchini Israeli, na kusababisha ving'ora vya mashambulizi ya angani.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Israel yatoa amri mpya za kuwahamisha walioko kusini mwa Lebanon

    Jeshi la Israel limetoa amri mpya za kuwahamisha watu wanaoishi kusini mwa Lebanon.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X na msemaji wa IDF wa lugha ya Kiarabu Avichay Adraee, amesema "wakazi wa kusini mwa Lebanon katika vijiji vifuatavyo: Arnoun, Yahmar, Zoutar al-Sharqiya, Zoutar al-Gharbiya".

    "Kwa usalama wenu, lazima muondoke majumbani mwenu mara moja na kuelekea kaskazini mwa Nabatieh," amesema.

    Adraee ameongeza hii ni kwa sababu shughuli za Hezbollah "zinalazimisha Vikosi vya Ulinzi vya Israeli kuchukua hatua kali dhidi yake."

    Soma zaidi:

  10. Habari za hivi punde, Kiongozi mpya mkuu wa Iran achaguliwa

    Ahmad Alamolhoda, mjumbe wa Baraza la Wataalamu la Iran, amesema kwamba uchaguzi wa kiongozi ajaye umefanyika na kiongozi huyo amechaguliwa.

    Amesema kwamba sasa yote yanategemea mkuu wa Sekretarieti ya Baraza la Wataalamu, Hosseini Bushehri, ambaye kwa sasa ana jukumu la kutangaza uamuzi huo hadharani, shirika la habari la Mehr ambalo si rasmi linaripoti.

    Soma zaidi:

  11. Jeshi la Israeli laonya kuwa 'litamsaka kila mrithi' wa Khamenei nchini Iran

    Jeshi la Israel limetoa onyo kwa Iran kwamba litaendelea kumsaka kila mrithi wa kiongozi mkuu wa nchi hiyo aliyefariki, Ayatollah Ali Khamenei.

    Katika chapisho kwenye X, akaunti ya lugha ya Kiajemi ya IDF ilisema: "Bunge la Wataalamu la Iran, ambalo halijakutana kwa miongo kadhaa, litakusanyika hivi karibuni katika jiji la Qom.

    "Tunataka kuwaambia kwamba mkono wa Taifa la Israeli utaendelea kumfuatilia kila mrithi na kila mtu anayetaka kumteua mrithi.

    "Tunawaonya wale wote wanaokusudia kushiriki katika mkutano wa uteuzi wa mrithi kwamba hatutasita kuwalenga nyinyi pia. Hili ni onyo!"

    Soma zaidi:

  12. Idadi ya waliofariki Kenya kwa mafuruko yafikia 28 huku tahadhari ya hatari za kiafya ikitolewa

    Idadi ya waliofariki dunia imeonezeka hadi 28 kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kote nchini huku wizara ya afya Kenya ikitoa tahadhari kuhusu hatari zinazoweza kutokea kiafya.

    Timu za uokozi bado zinatafuta manusura, polisi imesema.

    Mkuu wa polisi wa Nairobi George Seda alisema miili mitano zaidi ilipatikana Jumamosi jioni huku kukiwa na hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka wakati shughuli za utafutaji zikiendelea.

    "Timu ziko huko tena kuendelea kutafuta manusura wanaoweza kupatikana lakini tunatarajia kupata miili zaidi," alisema.

    Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Afya nchini Kenya Mary Muthoni amesema kwamba mvua kubwa na mafuriko vinaweza kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji, kuongezeka kwa uzalishaji wa vijidudu vya magonjwa kama vile mbu na kuvuruga mifumo ya usafi.

    Hali hizi, aliongeza, zinaweza kuchangia milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na mengineo kama kipindupindu, homa ya matumbo, na kuhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na unywaji wa maji au chakula kilichochafuliwa.

    Maafisa wa afya walitahadharisha zaidi kwamba hali ya hewa ya baridi na unyevunyevu inaweza kusababisha kuongezeka kwa maambukizi ya njia ya upumuaji, hasa miongoni mwa makundi yaliyo hatarini kama vile watoto, wazee na wenye kinga dhaifu.

    Majeraha yanayohusiana na mafuriko pia yaliorodheshwa miongoni mwa hatari zinazowezekana wakati wa msimu wa mvua.

    Wizara pia imetaka raia kuwa na tahadhari juu ya kuzama maji pamoja na kuumwa na nyoka kipindi hiki cha mafuriko.

    Soma zaidi:

  13. Trump amtuhumu Starmer kwa kutaka 'kujiunga na vita baada ya sisi kushinda'

    Rais wa Marekani Donald Trump ameiambia Uingereza kuwa haihitaji meli zake za kubeba ndege na kumshutumu Waziri Mkuu Sir Keir Starmer kwa kutaka "kujiunga na vita baada ya sisi kushinda", huku Marekani na Israel zikiendelea kushambulia Iran.

    Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema Uingereza "inafikiria kwa uzito" kutuma meli mbili za kubeba ndege Mashariki ya Kati, kabla ya kusema kwamba Marekani "haihitaji". Uingereza haijajibu.

    Wizara ya Ulinzi ilithibitisha kuwa moja ya meli mbili za kubeba ndege za Uingereza imewekwa katika hali ya utayari.

    Matamshi ya Trump yalikuja baada ya ndege za kivita za Marekani kuonekana zikitua Uingereza huku Marekani ikianza kutumia kambi za Uingereza kwa "shughuli maalum za kujilinda".

    "Uingereza, ambayo hapo awali ilikuwa mshirika wetu mkuu, labda mkubwa kuliko wote, hatimaye inafikiria kwa uzito kutuma meli mbili za kubeba ndege Mashariki ya Kati," Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social Jumamosi. "Hiyo ni sawa, Waziri Mkuu Starmer, hatuzihitaji tena - Lakini hili tutalikumbuka."

    "Hatuhitaji watu wanaojiunga na vita baada ya kushinda!"

    Akizungumza kwenye Air Force One akijibu swali kuhusu matumizi ya kambi za Uingereza katika vita, Trump alirejelea chapisho lake kwenye Truth Social, akisema: "Hatuzihitaji", akionekana kurejelea ndege hizo.

    Aliongeza: "Sio wakati mwafaka. Ingekuwa vizuri kuwa nao wiki mbili zilizopita."

    Serikali ya Uingereza ilisema wazi kwamba haina nia ya kujiunga na operesheni kubwa ya mashambulizi Mashariki ya Kati.

    Soma zaidi:

  14. Mlipuko watokea nje ya ubalozi wa Marekani huko Norway – Polisi

    Polisi nchini Norway wamezingira eneo linalozunguka ubalozi wa Marekani mjini Oslo baada ya mlipuko kuripotiwa katika eneo hilo.

    "Idadi kubwa ya maafisa wa usalama" imetumwa katika eneo hilo takriban saa 1:00 usiku wa manane (GMT), polisi walisema.

    "Polisi wanafanya mazungumzo na ubalozi na hakuna majeraha yaliyoripotiwa," ilisema taarifa hiyo.

    "Kwa sasa hakuna taarifa kuhusu hasa kilichotokea au ni nani anayeweza kuhusika," polisi waliongeza.

    Michael Dellemyr, ambaye anaongoza kundi la polisi waliofika eneo la tukio, aliambia mtangazaji wa Norway NRK kwamba mlipuko huo ulitokea kwenye mlango wa umma wa jengo hilo.

    Ubalozi ulipata uliharibiwa kidogo, ripoti za vyombo vya habari zinasema.

    Ubalozi wa Marekani upo katika wilaya ya Morgedalsvegen ya Oslo, yapata kilomita 7 (maili nne) nje ya katikati mwa jiji.

    Soma zaidi:

  15. Moto mkubwa waunguza mnara wa jiji la Kuwait

    Ni siku nyingine tena tunapokutana, tukiwa tayari kukuletea habari kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati, ambao sasa umeingia wiki yake ya pili.

    Maghala ya mafuta mjini Tehran yameshambuliwa, maafisa wa Lebanon wanasema watu wanne wameuawa katika shambulio la Israel kwenye hoteli moja mjini Beirut, na Israel inasema iliwashambulia "makamanda wakuu" wa Kikosi cha Lebanon cha Wakurdi, ambacho ni tawi la operesheni za nje ya nchi la IRGC.

    Mataifa ya Ghuba pia yamekuwa yakiripoti makombora na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

    Moto mkubwa umeteketeza mnara huko Kuwait, ambapo jeshi linasema limekuwa likikabiliana na "wimbi la ndege zisizo na rubani za adui zilizovamia anga ya nchi hiyo".

    "Baadhi ya vituo vya raia vimeharibika kutokana na vifusi na vipande vya silaha vilivyoanguka wakati wa operesheni ya kuzuia ndege za adui," msemaji rasmi wa Wizara ya Ulinzi amenukuliwa akisema katika chapisho kwenye mtandao wa X, lililoshirikishwa na jeshi la Kuwait.

    Jeshi la anga la nchi hiyo "linaendelea kushambulia maeneo fulani angani ya maadui", msemaji huyo anasema, huku jeshi likiwahimiza raia na wakazi "kufuata maagizo ya usalama na usalama".

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 08/03/2026.