Kama tulivyoripoti hapo awali ni vigumu kufuatilia mawasiliano ya pager ukilinganisha na simu za rununu.
Vyanzo vya habari viliiambia shirika la habari la Reuters kwamba Hezbollah, mapema mwaka jana, ilianza kushuku kuwa Israel ilikuwa ikifuatilia simu zao. Hivyo kufikia Februari mwaka huu, kundi hilo lilipiga marufuku matumizi ya simu zao za mkononi walipokuwa wakiendesha operesheni.
Wanasiasa wakuu wa Hezbollah pia walikwepa kuleta simu kwenye mikutano, na kiongozi wa kundi hilo alionya kuwa simu ni hatari zaidi kuliko majasusi wa Israeli.
Katika hotuba ya televisheni, Hassan Nasrallah aliwaambia wafuasi kuvunja, kuzika au kufunga simu zao kwenye sanduku la chuma. Badala yake waliamua kutumia pager.
Lakini mchambuzi mmoja anasema onyo la Hezbollah kuhusu matumizi ya simu ya mkononi lilikuwa hadharani sana.
"Hezbollah kimsingi ilitangaza kwa ulimwengu kwamba walikuwa wakipunguza kiwango cha matumizi ya simu za rununu hadi wapeja," Joseph Steinberg, mwandishi wa Cybersecurity for Dummies, aliiambia Reuters.
"Kimsingi unamwambia adui na wapinzani wengine wowote- na( Hezbollah ina wengi tu) ni aina gani ya teknolojia unataka kutumia."
Hadi tukio la jana, pager zilikuwa teknolojia ya mawasiliano iliyosahaulika.
Zilikuwa zikionekana mara kwa mara katika hospitali na huduma za dharura lakini sasa hazizungumziwi sana, baada ya nafasi yake kunyakuliwa miaka ya 2000 na simu za rununu.
Pager ni kifaa chenye ukubwa wa pakiti ya sigara kawaida huunganishwa kwenye vifungo vya mikanda kwa kumbukumbu ya haraka.
Zinafanya kazi kwa kusawazisha na visambaza sauti vinavyotumia nguvu nyingi - huhitaji nyingi kati ya hizo ili kufikia eneo kubwa, tofauti na milingoti ya simu za mkononi.
Watumiaji wa pager kila wakati wanapokea ujumbe mpya unaotumwa mara kwa mara na zinaweza kupokea taarifa za pekee - kwani hazitoi mawimbi ya mawasiliano.
Hii ndio sababu Hezbollah iliripotiwa kuzipendelea zaidi ya simu za rununu, kwani watumiaji wa pager hawawezi kupatikana kupitia GPS au njia zingine.
Peja inapopokea ujumbe, hutoa mlio fulani na maandishi mafupi huonyeshwa - kwa kawaida humwomba mpokeaji ampigie simu mtu huyo au aende mahali alipo.