Ukraine yadai kudhibiti kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi

Kiongozi wa Urusi Vladimir Putin ameelezea shambulio la kuvuka mpaka kama "uchokozi mkubwa".

Muhtasari

  • Homa ya Nyani yatangazwa kuwa dharura ya kiafya barani Afrika
  • Iran yakataa wito wa nchi za Magharibi kujizuia kuishambulia Israel
  • Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka Afrika ipewe kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN
  • Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachojua kufikia sasa
  • Urusi lazima ilazimishwe kuleta amani - Zelensky
  • Mahojiano ya Trump na Musk yakumbwa na changamoto za kiufundi
  • Nigeria: Mwanamke ahojiwa kwa kuchana pasipoti ya mumewe
  • Tanzania: Polisi waachia baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema
  • FBI yachunguza madai kuwa Iran ilidukua kambi ya kampeni ya Trump
  • Uingereza yaitaka Iran kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israeli
  • Ukraine yadai kudhibiti kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Habari za hivi punde, Homa ya Nyani yatangazwa kuwa dharura ya kiafya barani Afrika

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Athari za Homa ya Nyani

    Homa ya Nyani, ugonjwa hatari wa kuambukiza ambao ulikuwa ukiitwa Mpox, umetangazwa kuwa dharura ya kiafya ya umma barani Afrika na bodi kuu ya afya ya bara hilo.

    Wanasayansi kutoka Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) wanasema wanasikitishwa na kasi ambayo maambukizi mapya ya mpox yamekuwa yakienea.

    Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya kesi 13,700 na vifo 450 vimerekodiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Virusi hivyo vinavyoweza kusababisha vidonda katika mwili mzima vimesambaa hadi katika mataifa mengine ya Afrika, ikiwemo Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) Kenya na Rwanda.

    Mpox ni nini na inaeneaje?

    Tangazo la dharura ya afya ya umma litasaidia serikali kuratibu majibu yao na uwezekano wa kuongeza usambazaji wa vifaa vya matibabu na misaada katika maeneo yaliyoathirika.

    Wakuu wa afya nje ya Afrika pia watakuwa wakifuatilia hali hiyo ili kutathmini hatari ya mlipuko huo kuenea zaidi.

    Homa ya Nyani huenea kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu na kati ya watu kwa kuwasiliana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa - ikiwa ni pamoja na ngono, kugusana kwa ngozi hadi ngozi na kuzungumza au kupumua karibu na mtu mwingine.

    Inaweza kusababisha dalili kama vile homa, maumivu ya misuli na vidonda kwenye mwili.

    Ikiachwa bila kutibiwa, mpox inaweza kuwa hatari.Kuna aina mbili kuu za virusi vinavyojiulikana kuwepo.

    Hali mbaya zaidi ilisababisha mlipuko wa kimataifa mnamo 2022 ambao uliathiri bara Uropa, Australia, Marekani na nchi zingine nyingi - na ulienezwa haswa kupitia mawasiliano ya ngono.

  2. Iran yakataa wito wa nchi za Magharibi kujizuia kuishambulia Israel

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Iran imetupilia mbali wito wa Uingereza na nchi nyingine za Magharibi kujiepusha na kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran mwezi uliopita.

    Huku kukiwa na msururu wa mazungumzo ya diplomasia ya kimataifa ili kupunguza mvutano, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amemtaka Rais wa Iran Masoud Pezeshkian "kuondoa vitisho vyake vya mashambulizi ya kijeshi" katika mazungumzo ya simu yasio ya kawaida siku ya Jumatatu.

    Lakini Bw Pezeshkian amesema kulipiza kisasi ni "njia ya kukomesha uhalifu" na "haki ya kisheria" ya Iran, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

    Israel, ambayo haikusema ilihusika katika mauaji ya Haniyeh, wakati huo huo imeweka jeshi lake katika hali ya tahadhari.

    Marekani imeonya kwamba inajiandaa kwa "mashambulizi makubwa ya Iran au washirika wake wiki hii, na imejenga uwepo wake wa kijeshi katika Mashariki ya Kati ili kusaidia kuilinda Israel.

    Wapiganaji wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran nchini Lebanon pia wametishia kulipiza kisasi mauaji ya mmoja wa makamanda wake wakuu yaliotekelezwa na Israel katika shambulio la angani huko Beirut.

    Starmer wa Uingereza anaitaka Iran kujiepusha na mashambulizi dhidi ya Israel.

    Siku ya Jumatatu jioni, viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani walitoa taarifa ya pamoja wakiitaka Iran na washirika wake "kujiepusha na mashambulizi ambayo yatazidisha mivutano ya kikanda".

    "Watawajibika kwa vitendo vinavyohatarisha fursa hii ya amani na utulivu," Sir Keir, Rais Emmanuel Macron na Kansela Olaf Scholz walisema.

    Baadaye, waziri mkuu wa Uingereza pia alionyesha wasiwasi wake mkubwa kupitia simu ya moja kwa moja na rais wa Iran - simu ya kwanza kama hiyo tangu Machi 2021.

    Sir Kier alimwambia Bw Pezeshkian kwamba "kulikuwa na hatari kubwa ya kufanya makosa na sasa ulikuwa wakati wa utulivu na uangalifu", Downing Street ilisema.

    "Alitoa wito kwa Iran kujizuia kushambulia Israeli, akiongeza kuwa vita havina maslahi ya mtu yeyote," iliongeza.

    Siku ya Jumanne asubuhi, shirika la habari la serikali ya Iran Irna liliripoti kwamba Bw Pezeshkian alimwambia Sir Kier kwamba uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Israel umeifanya "kuendeleza ukatili" na kutishia amani na usalama.

  3. Habari za hivi punde, Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka Afrika ipewe kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutierrez

    Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa Afrika kupewa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama sehemu ya mageuzi ya kurekebisha dhuluma za kihistoria.

    Baraza la Usalama lenye - wanachama watano wa kudumu ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani – kwa muda mrefu limekuwa likikosolewa kwa kuwakilisha hali halisi iliyokuwepo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia wakati sehemu kubwa ya Afrika ilikuwa bado chini ya ukoloni.

    "Ulimwengu umebadilika tangu 1945. Lakini muundo wa Baraza, licha ya mabadiliko machache, haujabadilika," Bw Guterres alisema.

    Wajumbe 10 wasio wa kudumu wa baraza hilo wanawakilishwa kikanda, lakini tofauti na wajumbe watano wa kudumu, hawana uwezo wa kura ya turufu.

    Umoja wa Afrika kwa muda mrefu umekuwa ukishinikiza bara la Afrika kuwa na wawakilishi wawili wa kudumu katika baraza hilo na viti vingine viwili kama wawakilishi wasio wa kudumu.

    Mjadala wa Jumatatu uliitishwa na Sierra Leone - na Rais wake Julius Maada Bio aliwakilisha hoja ya bara hilo."

    ''Wakati wa hatua nusu za maendeleo ya ziada umekwisha. Afrika lazima isikizwe, na matakwa yake ya haki na usawa lazima yatimizwe,” alisema.

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina majukumu makubwa, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha operesheni za ulinzi wa amani, kuweka vikwazo vya kimataifa na kuamua jinsi UN inapaswa kukabiliana na migogoro kote duniani.

    Maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa waliunga mkono maoni ya mageuzi, akiwemo Dennis Francis - rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, pamoja na Bw Guterres.

    "Hatuwezi kukubali kwamba chombo kikuu cha amani na usalama duniani hakina sauti ya kudumu kwa bara lenye zaidi ya watu bilioni moja –Lenye idadi ya vijana na inayokua kwa kasi - ambayo ni asilimia 28 ya wanachama wa Umoja wa Mataifa," mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema.

    .Afrika ilikuwa na uwakilishi mdogo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taasisi za fedha za kimataifa lakini "iliwakilishwa kupita kiasi katika changamoto ambazo miundo hii imeundwa kushughulikia", aliongeza.

  4. Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachojua kufikia sasa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iwapo unajiunga nasi tu, au unahitaji mshikamano, hebu tuangalie baadhi ya matukio ya hivi punde katika vita vya Urusi na Ukraine, wiki moja baada ya uvamizi wa Ukraine ndani ya eneo la Urusi.

    • Takriban watu 200 ambao wamekimbia eneo la Kursk waliwasili Moscow siku ya Jumanne, kulingana na wizara ya dharura ya Urusi.
    • Ukraine imesema sasa inadhibiti karibu kilomita za mraba 1,000 (maili za mraba 386) za eneo la Urusi katika eneo la Kursk.
    • Lakini Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) inasema Kyiv inaweza kudhibiti karibu kilomita za mraba 800
    • Mapema siku ya Jumanne, mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine ulidungua ndege 30 zisizo na rubani zilizorushwa na Urusi na asubuhi ya leo ulizuia harakati za raia wa Ukraine ndani ya eneo la kilomita 20 (maili 12) linalopakana na Urusi.
    • Katika kukabiliana na uvamizi wa kushtukiza wa Kursk, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema jana usiku kwamba "Urusi imeleta vita kwa wengine, na sasa vinakuja nyumbani"
    • Wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema Kyiv itapokea kile alichokiita "jibu linalofaa"Kama ukumbusho, Urusi ilizindua uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022. Ingawa Ukraine ilianzisha uvamizi hapo awali, ndio mara ya kwanza vikosi vya kawaida vya Ukraine vimetumiwa kwa njia hii.
  5. Urusi lazima ilazimishwe kuleta amani - Zelensky

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky jana usiku alisema "Urusi ilileta vita kwa wengine, sasa vinawarudia,".

    Katika hotuba yake ya jioni, Zelensky aliongeza "ni haki tu kuwaangamiza magaidi wa Urusi mahali walipo, pale wanapotekeleza mashambulizi yao".

    "Tunaona jinsi hii inaweza kuwa na manufaa kwa kuleta amani karibu. Urusi lazima ilazimishwe kuleta amani ikiwa Putin anataka kuendelea na vita," aliongeza.

    Zelensky alisema alikuwa amepewa taarifa na Kamanda Mkuu Oleksandr Syrskyy juu ya "operesheni katika Mkoa wa Kursk", na kwamba kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi sasa ziko chini ya udhibiti wa Ukraine.

    Matamshi ya Syrskyy na Zelensky ilikuwa mara ya kwanza kwa afisa yeyote mkuu wa Ukraine kutaja wazi uvamizi wa Kursk kwa jina.

    Soma zaidi:

  6. Mahojiano ya Trump na Musk yakumbwa na changamoto za kiufundi

    .

    Chanzo cha picha, X/Reuters

    Mjadala uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kati ya Elon Musk na mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump kwenye jukwaa la bilionea la X, ulighubikwa na changamoto za kiufundi.

    Mazungumzo hayo, ambayo Bw Musk aliuliza maswali ya kirafiki kuhusu mada kama vile uhamiaji na mfumuko wa bei, dakika 40 baadaye tangu muda uliokuwa umepangwa kuanza, huku watumiaji wengi wakihangaika kuyafikia.

    Ilichukuliwa kama mahojiano lakini Trump alitoa mfululizo wa madai ambayo hayajathibitishwa na hayakupingwa na yeyote.

    Bw Musk alirudia kumuunga mkono Trump, ambaye atakabiliana na mgombea mpya wa chama cha Democratic, Makamu wa Rais Kamala Harris, katika uchaguzi wa Novemba.

    Alilaumu changamoto hizo za kiufundi kutokana na uvamizi wa mtandao lakini mtaalamu mmoja aliambia BBC kwamba hilo haliwezekani.

  7. Nigeria: Mwanamke ahojiwa kwa kuchana pasipoti ya mumewe

    xx

    Idara ya Uhamiaji nchini Nigeria inamhoji mwanamke aliyerekodiwa akichana pasipoti ya mume wake katika uwanja wa ndege wa Lagos katika video ambayo imesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

    Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Favour Igiebor, alionekana akimfokea mume wake kwenye video hiyo huku vipande vya pasipoti ya Nigeria vikiwa chini.

    Wanandoa hao na watoto walitua katika uwanja wa ndege wa Murtala Mohammed ambapo kisa hicho kilitokea mbele ya makumi ya wasafiri wengine. "Niliichana," alisikika akisema.

    Mamlaka ilisema katika taarifa kwamba inachunguza kisa tukio hilo.

    "Huduma ya Uhamiaji ya Nigeria (NIS) imeanzisha uchunguzi rasmi, video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonyesha msafiri wa kike akiharibu Pasi ya usafiri ya Nigeria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Mohammed (MMIA), Lagos. "Mtu aliyehusika ametambuliwa kama Bi. Favour Igiebor," taarifa hiyo ilisema. Ilibainisha kuwa kuharibu pasipoti ya nchi ni kosa la jinai, ambalo adhabu yake ni kifungo cha hadi mwaka mmoja gerezani.

    Pasipoti iliyochanwa

    Baada ya video hiyo kuibua gumzo mitandaoni, Bi Igiebor aliachia video yake mwenyewe. Hakuelezea kwa undani lakini alisema alikuwa akiteseka.

    "Angalia macho yangu - mimi hulia sana. Watu wananisimanga kwenye mitandao ya kijamii na hawajui ninachopitia. "Lazima uhoji chanzo cha ugomvi - usiangalie tu kitendo kilichotokea . Nina sababu zangu. Nimepitia changamoto nyingi za kifamilia.

    Siwezi kuendelea kuteseka.” Akiongeza kuwa alifikiria kuicha pasipoti hiyo wakiwa ulala huko lakini akaona kwamba ingemsababishia mume wake matatizo mengi sana.

  8. Viongozi wa upinzani Tanzania waachiliwa kwa dhamana,

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Freeman Mbowe

    Viongozi wakuu wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe na makamu wake Tundu Lissu wameachiwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa kabla ya kufanyika kwa mkutano wa vijana.

    Takriban watu 520 walikamatwa katika msako mkali uliofanyika nchi nzima ili kuzuia Chadema kufanya maandamano katika mji wa kusini-magharibi mwa Mbeya siku ya Jumatatu.

    Polisi wamesema baadhi yao walisalia rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

    Kukamatwa kwa watu hao kuliibua hofu kuwa Tanzania inarejea katika utawala dhalimu wa hayati Rais John Magufuli, licha ya mrithi wake Samia Hassan kuondoa zuio la mikutano ya upinzani na kuahidi kurejesha siasa za ushindani.

    Polisi walipiga marufuku mkutano wa Chadema wakisema ulikuwa na nia ya kusababisha vurugu.

    Walitoa mfano wa mwito wa watu kukusanyika pamoja kama ilivyofanyikana "vijana nchini Kenya" - wakimaanisha wiki za maandamano mabaya dhidi ya serikali kama ilivyofanyika katika nchi jirani ya Afrika Mashariki.

    Umoja wa vijana wa Chadema umesema ulitarajia watu 10,000 kuhudhuria mkutano huo, chini ya kauli mbiu ya "chukua jukumu la maisha yako ya baadaye".

    Siku ya Jumanne, chama kilichapisha kwenye X kwamba ofisi zake Mbeya "zimezingirwa na polisi na hawaruhusu watu kuingia".

    Msemaji wa Chadema John Mrema alithibitisha kuachiliwa kwa viongozi kadhaa wa chama - ikiwa ni pamoja na Bw Mbowe na Bw Lissu - lakini akasema kwamba wengine kadhaa walisalia kizuizini.

    Hata hivyo, polisi walisema “viongozi wote wakuu wa Chadema waliokamatwa baada ya kuhojiwa na taratibu nyingine wamerudishwa walikotoka”.

    Chidema alisema Lissu alikamatwa Jumapili, na Mbowe Jumatatu alipofika uwanja wa ndege wa Mbeya kwa ajili ya kumuokoa mwenyekiti wa chama na viongozi wengine wawili akiwemo kiongozi wa tawi la vijana wa chama hicho John Pambalu.

    Lissu, ambaye alinusurika katika jaribio la kuuawa mwaka 2017 baada ya kupigwa risasi 16, alirejea Tanzania mwaka 2023 baada ya kukaa uhamishoni kwa miaka miwili nchini Ubelgiji.

    Rais Samia, aliyeingia madarakani kufuatia kifo cha ghafla cha Bw Magufuli mnamo 2021, alisifiwa kwa kuachana na sera nyingi za mtangulizi wake.

    Lakini kutokana na kukamatwa kwake, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamemkosoa, wakitilia shaka dhamira yake ya kuleta maridhiano ya kisiasa.Tanzania inatarajiwa kufanya kura za urais na wabunge mwishoni mwa mwaka ujao

    Soma zaidi:

  9. FBI yachunguza madai kuwa Iran ilidukua kambi ya kampeni ya Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la Ujasusi la Marekani(FBI) limeanzisha uchunguzi kuhusu madai kuwa kambi ya kampeni ya Trump ililengwa na wadukuzi wanaofanya kazi kwa ajili ya serikali ya Iran.

    "Tunaweza kuthibitisha kuwa FBI inachunguza suala hilo," shirika hilo lilisema katika taarifa fupi siku ya Jumatatu bila kumtaja rais wa zamani au Iran.

    Msemaji wa kambi ya kampeni ya Trump aliiambia BBC kuwa hati hizo zilipatikana kinyume cha sheria na "vyanzo vya kigeni vinavyoichukia Marekani".

    Maafisa wa Iran wamekanusha kuhusika na udukuzi huo na serikali ya Marekani haijaishutumu rasmi Iran.

    FBI pia inachunguza ikiwa wadukuzi wa Iran walilenga kambi ya Joe Biden-Kamala Harris, kulingana na CBS News, mshirika wa habari wa BBC, akinukuu watu wanaofahamu uchunguzi huo.

    Taarifa ya kambi ya kampeni ya Trump imetolewa siku moja baada ya Microsoft kutoa ripoti inayoonyesha kwamba wadukuzi wa Iran walilenga kampeni ya mgombea urais wa Marekani ambaye hakutajwa jina mnamo mwezi Juni.

    Siku ya Jumamosi, Trump alisema wadukuzi "waliweza tu kupata habari zilizokusudiwa kutolewa kwa umma".

    Kulingana na gazeti la Washington Post, wafanyikazi watatu wa kambi ya kampeni ya Biden-Harris pia walilengwa na barua pepe za ulaghai siku chache kabla ya Rais Joe Biden kutangaza kwamba anajiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuingia ikulu.

    Msemaji wa kambi ya kampeni ya Harris alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba "wanafuatilia kwa uangalifu na kuhakikisha ulinzi dhidi ya vitisho vya mtandao, na hatufahamu ukiukaji wowote wa usalama wa mifumo yetu".

    BBC imeomba kambi ya kampeni ya Harris kutoa maoni.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Uingereza yaitaka Iran kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israeli

    .

    Chanzo cha picha, 10 Downing Street

    Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ameitaka Iran "kujizuia" kuishambulia Israeli wakati wa mazungumzo ya simu na rais mpya wa Iran.

    Sir Keir alimwambia Masoud Pezeshkian kulikuwa na "hatari kubwa ya kufanya makosa na sasa ulikuwa wakati wa kutulia na kuzingatia kwa makini".

    Ni mazungumzo ya kwanza kati ya waziri mkuu wa Uingereza na rais wa Iran tangu Machi 2021 wakati kiongozi wa zamani wa Uingereza Boris Johnson alipozungumza na Hassan Rouhani.

    Mazungumzo yao ya dakika 30 yanafanyika wakati Uingereza ikitoa taarifa ya pamoja na Marekani, Ufaransa, Italia na Ujerumani - kuitaka Iran kukomesha vitisho vyake vya kuishambulia Israeli.

    Waliitaka Iran "kuacha vitisho vyake vinavyoendelea vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Israeli na kujadili madhara makubwa kwa usalama wa kikanda iwapo shambulio kama hilo litatokea".

    Viongozi hao pia walizungumzia suala la kuunga mkono "ulinzi wa Israeli dhidi ya uvamizi wa Iran na mashambulizi ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Iran".

    Hofu ya kutokea kwa mzozo mkubwa huko Mashariki ya Kati imekuwa ikiongezeka kufuatia mauaji ya hivi karibuni ya viongozi wakuu wa Hezbollah na Hamas.

    Siku ya Jumapili, Marekani ilithibitisha kuwa imetuma nyambizi inayoongozwa na kombora katika eneo hilo kujiandaa kutokana na wasiwasi huu.

    Nyambizi hiyo inaweza kubeba hadi makombora 154 ya Tomahawk, ambayo hutumiwa kulenga nchi kavu.

    Soma zaidi:

  11. Ukraine yadai kudhibiti kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kamanda mkuu wa Ukraine amesema vikosi vya Kyiv vinadhibiti kilomita za mraba 1,000 za ardhi ya Urusi huku wakiendeleza uvamizi wao mkubwa wa kuvuka mpaka katika miaka miwili na nusu ya vita.

    Kamanda Oleksandr Syrskyi alisema Ukraine iliendelea "kuendesha operesheni ya kimkakati katika eneo la Kursk" siku saba baada ya kuanza.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeleta vita kwa wengine na sasa vinarejea kwao.

    Lakini kiongozi wa Urusi Vladimir Putin alielezea shambulio hilo kama "uchokozi mkubwa" na akaamuru vikosi vya Urusi "kumfukuza adui nje ya eneo letu".

    Idadi inayoongezeka ya watu wamehamishwa kutoka eneo la magharibi mwa Urusi kwa usalama wao, huku wengine 59,000 wakiamriwa kuondoka.

    Gavana wa eneo hilo alisema baadhi ya vijiji 28 vimetekwa na vikosi vya Ukraine, na kwamba raia 12 wameuawa na "hali bado ni ngumu".

    Wanajeshi wa Ukraine walifanya shambulizi lao la kushtukiza Jumanne iliyopita, na kusonga hadi maili 18 (km 30) kuingia Urusi.

    Mashambulizi hayo yanasemekana kuongeza ari kwa upande wa Ukraine, lakini wachambuzi wanasema mkakati huo unaleta hatari mpya kwa Ukraine.

    Chanzo kikuu cha kijeshi cha Uingereza, ambacho hakikutaka jina lake litajwe, kiliiambia BBC kwamba kuna hatari Moscow itaghadhabishwa na uvamizi huo kiasi kwamba inaweza kuongeza mashambulizi yake yenyewe dhidi ya raia na miundombinu ya Ukraine.

    Soma zaidi:

  12. Habari ya asubuhi msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 13/08/2024.