Wahamiaji Rwanda: Uingereza inaweza kutuma watu wa kwanza 'ndani ya wiki kadhaa'

Chanzo cha picha, Reuters
Waomba hifadhi wa kwanza wanaweza kusafirishwa hadi Rwanda kutoka Uingereza ndani ya wiki chache, serikali imesema.
Hii inafuatia tangazo la rubani ambaye atashughulika kuwapeleka waomba hifadhi katika nchi hiyo ya Afrika mashariki.
Mpango huo, awali utalenga wanaume wasio na familia wanaotaka kuvuka kivuko kwa boti au kwa kutumia lori kutoka Ufaransa.
Waziri Mkuu alisema "itaokoa maisha ya watu mengi" na kuvunja mtindo wa biashara ya wasafirishaji haramu", lakini wanaharakati wameutaja mpango huo kama "usio wa kibinadamu".
Vivuko viwili zaidi vya wahamiaji vilirekodiwa Ijumaa asubuhi licha ya ukungu mwingi, mwandishi wa BBC Simon Jones alisema.
Andrew Griffith Mbunge na mkurugenzi wa kitengo cha sera katika ofisi ya waziri mkuu, alisema mpango huo mpya hautahitaji sheria mpya na unaweza kutekelezwa chini ya "mikataba iliyopo".
Aliiambia BBC Newsnight kuwa mpango huo unaweza kuzinduliwa "katika wiki au miezi michache ijayo".
Aliongeza kuwa, ikiwa mtiririko wa uhamiaji haramu unaweza kusimamishwa, "idadi kubwa ya watu watakuwa wanatumia njia salama na za kisheria" kuingia Uingereza.
Mpango wa Rwanda ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa kupunguza idadi ya watu wanaoingia Uingereza kwa kuvuka bahari kwa boti ndogo.
Jeshi la Wanamaji la Kifalme limechukua uongozi wa vivuko kadhaa kutoka kwa mpaka wa kikosi cha Uingereza katika juhudi za kugundua kila mashua inayoelekea Uingereza.
Mwaka jana, watu 28,526 walivuka bahari, ikiwa ni ongezeko la 8,404 la mwaka 2020.
Tony Smith, mkurugenzi mkuu wa zamani wa kikosi cha Mipaka cha Uingereza, alisema inaweza kuchukua wiki kabla ya kuwa wazi kama mpango huo mpya utatimizwa".
Aliiambia BBC Breakfast kuwa huenda serikali ikakabiliwa na changamoto ya kisheria wakati watu watawekwa kwenye ndege kuelekea Rwanda.
"Lakini basi sina uhakika ikiwa jibu ni kusimamisha boti… kwa sababu ikiwa hatutafanya kitu, basi watu wengi zaidi watazama na kufa maji," alisema, akiongeza kwamba Uingereza ilikuwa ikikabiliwa na idadi kubwa zaidi ya wanaotaka hifadhi kuwahi kutokea.
Katika hotuba yake siku ya Alhamisi, Boris Johnson alisema makubaliano na Rwanda yatatoa "njia salama na za kisheria kwa wanaotaka hifadhi".
"Wahamiaji wa kiuchumi wanaotumia fursa ya mfumo wa hifadhi hawataweza kukaa Uingereza, wakati wale walio na mahitaji ya kweli watalindwa ipasavyo," alisema.
Alisema mpango huo utashughulikia mtu yeyote ambaye amefika Uingereza kinyume cha sheria tangu kuanza kwa mwaka huu.

'Hatari nyingine tu ya kuzingatia, '
Na Jessica Parker, katika kambi moja huko Dunkirk, kaskazini mwa Ufaransa

Hakuna mtu ambaye tulizungumza naye hapo awali alionekana kujua kuhusu tangazo la Rwanda - lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya habari kuenea.
Hivi karibuni kundi la wanaume lilikuwa likituuliza maswali mengi: "Hili litatokea lini? Kwa nini? Ikiwa nitatoka Afghanistan bado nitaruhusiwa? "
Shafi, ambaye aliniambia alikimbia Afghanistan, alisema: "[Rwanda] ni mahali pabaya zaidi kuliko Afghanistan, hakuna mustakabali wetu nchini Rwanda."
Lakini sikukutana na mtu aliyesema mipango ya serikali itawazuia wasijaribu kuvuka Bahari akiwemo Shafi ambaye alisema hana jinsi.
Wengi wa wanaume hawa tayari wamekabiliwa na hatari kubwa kufika hapa na wako tayari kuhatarisha maisha yao kuvuka Bahari kwa kutumia mashua ndogo.
Hatari ya kutumwa Rwanda, katika hatua hii, ilionekana kama kitu kingine cha kuzingatia.
Zaidi ya mashirika 160 ya kutoa misaada na makundi ya wanaharakati yameitaka serikali kuutupilia mbali mpango huo, wakiuelezea katika barua ya wazi kuwa "ukatili".
Afisa mkuu mtendaji wa Baraza la Wakimbizi Enver Solomon alisema litafanya kidogo kuwakatisha tamaa watu waliokata tamaa na "kusababisha mateso zaidi ya wanadamu".
Kiongozi wa chama cha Labour Sir Keir Starmer alisema Bw Johnson alikuwa akijaribu kuvuruga nchi kutoka kwa kashfa ya Partygate kwa mpango "usioweza kutekelezeka, usio wa kimaadili na wa ulafi".

Maswali pia yanaibuliwa kuhusu gharama ya mpango huo, huku gazeti la The Times likiripoti gharama yake ni pauni 20,000 hadi 30,000 kwa kila mhamiaji aliyetumwa Rwanda.
Lakini waziri wa haki na uhamiaji Tom Pursglove alikataa kutoa takwimu kama hiyo, akiambia BBC Breakfast itategemea mambo kadhaa.
Alisema Uingereza ilikuwa ikitumia karibu £5m kwa siku katika hoteli, wakati mpango huo mpya ungegharimu £120m, na pesa zaidi kutolewa baadaye.
Mpango kama huo nchini Australia uligharimu wastani wa £460m mwaka wa 2021 lakini ulifanikiwa kuwapa makazi 239 pekee - kwa gharama ya karibu £1.9m kwa kila mtu.
Wasiwasi unaongezeka kuhusu rekodi ya haki za binadamu ya Rwanda na rais wake, Paul Kagame.
Bw Pursglove alisema Rwanda ni nchi yenye maendeleo ambayo inataka kutoa hifadhi na imepata "mafanikio makubwa " katika miongo mitatu iliyopita.
Waziri huyo alisema kwa sasa ni mojawapo ya nchi mbili pekee duniani zenye bunge la wanawake wengi na ina sheria ya kupinga ubaguzi inayoendeshwa "kupitia katiba yake".
Hata hivyo, mwaka jana tu serikali ya Uingereza ilionyesha wasiwasi wake katika Umoja wa Mataifa kuhusu "kuendeleza vikwazo vya Rwanda kwa haki za kiraia na kisiasa na uhuru wa vyombo vya habari."
Steve Valdez-Symonds, kutoka Amnesty International Uingereza, alisema kuwatuma watu katika taifa hilo la Afrika mashariki ni "kilele cha kutowajibika".
Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, aliiambia BBC kuwa ni "nchi salama, inaendelea kwa kasi, tunajali kama kila nchi kuhusu haki za binadamu ".
Kulingana na makubaliano kati ya serikali hizo mbili, watu waliotumwa Rwanda watapata malazi na msaada.
Watakuwa huru kuja na kuondoka kutoka kwa makao yao wakati wote..

















