Mzozo wa Ukraine: Je Urusi itatumia silaha zake za nyuklia za kimkakati?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda mfupi baada ya Urusi kuivamia Ukraine, Rais Vladimir Putin alisema anaviandaa "vikosi vyake vya silaha" - ikimaanisha silaha za nyuklia - "kuwa tayari" kutekeleza majukumu.

Hii imezua hofu kwamba Moscow inaweza kutumia silaha za nyuklia "tactical" - sio vita vya nyuklia kabisa, lakini bado ni hatua kubwa.

Silaha za nyuklia za 'kimbinu' ni nini?

Silaha za nyuklia za kimbinu 'Tactical nuclear' ni zile ambazo zinaweza kutumika kwa umbali mfupi.

Hii inatofautisha na silaha za nyuklia za "kimkakati". Katika Vita Baridi, haya yalikuwa mabomu ambayo mataifa mawili yenye nguvu, Marekani na Umoja wa Kisovyeti, yalikuwa yakirushiana kwa umbali mrefu kwenda katika ardhi baina ya mataifa hayo.

Silaha za "kimbinu" hata hivyo zinajumuisha aina nyingi za silaha, ikiwa ni pamoja na mabomu madogo na makombora yanayotumika katika uwanja wa kivita.

Ni silaha gani za kimbinu za nyuklia ilizo nazo Urusi?

Urusi inakadiriwa kuwa na silaha 2,000 za nyuklia. Hizi zinaweza kuwekwa kwenye makundi ya aina mbalimbali za makombora ambayo kwa kawaida hutumika kutoa milipuko ya kawaida.

Pia yametengenezwa kwa ajili ya kutumiwa kwenye ndege na meli - kwa mfano torpedoes yanayotumika kulenga manowari.

.

Silaha za nyukilia za Urusi za masafa mafupi

Vichwa hivi vya kivita vinaaminika kuwa katika vituo vya kuhifadhi, havijapelekwa kwenye uwanja wa mapambano tayari kutumika.

Lakini upo wasiwasi mmoja kwamba Urusi inaweza kuwa tayari kutumia silaha ndogo ndogo za kimbinu kuliko makombora makubwa ya kimkakati.

"Wanaweza wasilione hilo kama kuvuka kizingiti hiki kikubwa cha nyuklia. Wanaweza kuiona kama sehemu ya silaha zao na vikosi vyao vya kawaida, "anasema Dk Patricia Lewis, mkuu wa mpango wa usalama wa kimataifa katika kituo cha Chatham House.

Zina nguvu kiasi gani?

Silaha za nyuklia za kimbinu hutofautiana sana kwa ukubwa na nguvu.

Ndogo zaidi inaweza kuwa kiloton moja au chini ya hapo (sawa na tani elfu ya TNT ya kulipuka) - kubwa labda inaweza kufikia kilotons 100.

Madhara yangetegemea ukubwa wa kichwa husika cha silaha hizi za vita, umbali gani juu ya ardhi inalipua na mazingira ya ndani.

Lakini kwa kulinganisha, lile bomu lililoua watu 146,000 huko Hiroshima, Japan, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lilikuwa la kilotons 15.

Silaha kubwa zaidi za kimkakati za Urusi zinadhaniwa kuwa angalau kilotons 800.

Je, mazungumzo ya Putin kuhusu silaha za nyuklia ni kuleta wasiwasi?

Rais Putin ametaja silaha zaidi ya moja za nyuklia za Urusi - inaonekana ni kujaribu kuleta hofu.

Wapelelezi wa Marekani wanaona hii ni kama taarifa kwa nchi za Magharibi zisiingilie sana mgogoro wa Ukraine, sio kama ishara kwamba anapanga vita vya nyuklia.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Urusi inaweza kutumia silaha za kinyuklia

Lakini wengine wana wasiwasi kwamba ingawa uwezekano ni mdogo, inawezekana Urusi, katika hali fulani, inaweza kujaribiwa kutumia silaha ndogo za kimbinu za nyuklia nchini Ukraine.

Shirika la kijasusi la Marekani linasema Urusi ina nadharia inayoitwa "escalate to de-escalate" ikiwa iko katika mgogoro na Nato.

Hii inahusisha kufanya jambo kubwa - kama vile kutumia silaha ya kimbinu kwenye uwanja wa vita, au kufanya maonyesho ya silaha hizo mahali fulani - au kutishia kufanya hivyo.

Lengo hapa ni kuogopesha upande mwingine wasiunge mkono.

James Acton, mtaalam wa nyuklia huko Washington DC, anasema: "Nina wasiwasi kwamba katika hali hiyo Putin anaweza kutumia silaha za nyuklia, uwezekano mkubwa ni kwenye uwanja wa mapambano nchini Ukraine kumtisha kila mtu. Kwa sasa bado hatujafikia hatua hiyo."

Dr Heather Williams, mtaalamu wa nyuklia katika Chuo cha Kings College London, anasema tatizo moja ni kwamba haijulikani "ushindi" nchini Ukraine unafananaje kwa Putin - hivyo hicho ndicho kinachoweza kuisukumua Urusi kutumia silaha za nyuklia.

Je, Urusi kutumia silaha hizi ni kulamba matapishi yake?

Putin anadai Ukraine ni sehemu ya Urusi, hivyo kutumia silaha za nyuklia katika eneo lake itakuwa ni kitu cha ajabu.

Wakati pekee silaha za nyuklia zilitumika katika vita ilikuwa ni Marekani iliyoumia mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia dhidi ya Japan. Je, Putin angetaka kuwa kiongozi wa kwanza kuvunja mwiko na kuutumia silaha hizi?

.

Baadhi wana wasiwasi kwamba ameshaonyesha nia ya kufanya mambo ambayo wengine walidhani hatafanya, mfano kuivamia Ukraine au kutumia wakala wa neva huko Salisbury.

Dkt Williams anasema kuna sababu zaidi kwa nini Urusi haiwezi kutumia silaha za nyuklia - China.

"Urusi inategemea sana msaada wa China, lakini China ina simamia misingi ya kisera ya 'kutokuwa wa kwanza kutumia silaha za nyuklia. Kwa hivyo ikiwa Putin anataka kuzitumia, itakuwa vigumu sana kwa China kusimama naye. Kama atazitumia, huenda akaipoteza China."

Je, hatua ya Putin inaweza kusababisha vita vya nyuklia?

Hakuna mtu anayejua kwa hakika kabisa matumizi ya silaha za nyuklia za kimbinu zitatupeleka wapi. Inaweza kuchochea hilo na Putin asingetaka kuwepo kwa vita vya nyuklia. Lakini kucheza kete vibaya katika mazingira haya daima ni hatari.

Marekani inasema inafuatilia hali hiyo kwa karibu.

Ina mashine kubwa ya kijasusi ya kukusanya taarifa za shughuli za nyuklia za Uru - kwa mfano ikiwa silaha hizo zinatolewa zilikohifadhiwa, au ikiwa kuna lolote linaendelea katika vituo vya kurushia silaha hizo.

Hadi sasa Marekani inasema hawajaona mabadiliko yoyote makubwa.

Ni vigumu kubashiri namna gani Marekani na Nato watajibu mapigo dhidi ya matumizi yoyote ya nyuklia ya Urusi. Wanaweza wasitake kuchochea hali ya mambo zaidi, na kusababisha hatari ya vita vya nyuklia lakini pia wangetaka kuweka mipaka kudhibiti nyuklia. Lakini Urusi itafanya nini?

"Mara baada ya kuvuka kizingiti cha nyuklia, hakuna hatua ya kawaida kuzuia hilo," anasema James Acton.

"Sidhani kama mtu yeyote anaweza kuwa na imani na kile ambacho dunia na vita hiyo itakavyokuwa."