Mzozo wa Ukraine: Mfanyabiashara tajiri mwenye ushawishi wa kisiasa ni nani?

Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) akimsalimia bilionea na mfanyabiashawa Arkady Rotenberg (Kulia) huku ndugu yake, Boris Rotenberg (katikati) akifuatilia mazungumzoyao wakati wa hafla ya kuzawadia washindi wa mwaka 2017 Formuila 1 x wa Russia Grand Prix mjini Sochi , Russia, Aprili, 30, 2017

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Putin alipigwa picha mnamo 2017 akisalimiana na Boris na Arkady Rotenberg, walioitwa "marafiki wa Putin" kwenye vyombo vya habari vya Magharibi.

Wafanyabiashara maarufu wa Urusi kwa mara nyingine tena wamejipata katikati ya mgogoro wa kimataifa huku mzozo kati ya Urusi, Ukraine na nchi za Magharibi ukiendelea.

Baada ya Urusi kuvamia Ukraine, nchi za Magharibi zimeimarisha vikwazo dhidi ya benki za Urusi na watu kadhaa, ambao wamekuwa wakitajwa na vyombo vya habari vya Magharibi kuwa "washirika" wa Putin.

Tunawaangazia wafanyabiashara hawa tajiri na wenye ushawishi (oligarchs) ni kina nani na kwa nini wafanyabiashara kadhaa mashuhuri wa Urusi wanakabiliwa na vikwazo.

Neno oligarch linamaanisha nini?

Chelsea Football Club owner Roman Abramovich walks past the High Court in London November 16, 2011.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mmiliki wa klabu ya soka ya Chelsea Roman Abramovich ni mmoja wa wafanyabiashara tajiri na maaruru zaidi duniani kutoka Urusi

Neno "oligarch" lina historia ndefu lakini katika nyakati zetu, limepata maana maalum zaidi.

Oligarch kwa maana ya jadi ni mwanachama au mfuasi wa kundi la watu wenye ushawishi walio kwenye - mfumo wa kisiasa ambao hutawalaliwa na watu wachache.

Lakini sasa, linatumika zaidi kuelezea kundi la Warusi tajiri ambao walipata umaarufu baada ya kuanguka kwa Muungano wa Sovieti mnamo 1991.

Neno hilo kwa Kigiriki bi oligoi, ambalo linamaanisha"wachache", na arkhein, linalomaanisha "kuongoza".

Ni tofauti na ufalme (utawala wa mtu mmoja, monos) au demokrasia (utawala wa watu, demos).

Nini hufafanua oligarch?

Kwa hivyo oligarch anaweza kuwa mshiriki wa tabaka tawala lililotofautiana na jamii kwa misingi ya dini zao, ukoo, ufahari, hali ya kiuchumi na hata lugha.

Watu kama hao huwa na tabia ya kutawala kwa masilahi yao wenyewe, mara nyingi kwa njia za kutilia shaka.

Oligarchs ni kina nani?

Siku hizi, oligarch anatambuliwa zaidi kama mtu tajiri zaidi ambaye amepata utajiri wake kwa kufanya biashara na serikali.

Pengine oligarch anayejulikana zaidi nchini Uingereza ni mfanyabiashara wa Urusi Roman Abramovich, mmiliki wa Klabu ya Soka ya Chelsea. Thamani yake ya utajiri ni wastani wa dola bilioni 14.3 na alijitajirisha kwa kuuza mali ya awali ya serikali ya Urusi ambayo alipata kufuatia kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti.

Mwingine ni Alexander Lebedev, afisa wa zamani wa KGB na benki, ambaye mtoto wake Evgeny ndiye mmiliki wa gazeti la London Evening Standard. Evgeny ni raia wa Uingereza na amefanywa kuwa mwanachama wa House of Lords- sehemu ya Bunge la Uingereza ambalo wajumbe wake hawakuchaguliwa na wapiga kura..

Nchi zingine pia zina oligarchs.

Rais wa zamani wa Ukraine Leonid Kuchma akizungumza na vyombo vya habari mjini Kyiv, mnamo Juni 6, 2019.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Ukraine, Leonid Kuchma, alisimamia ubinafsishaji na kuleta mageuzi ya kiuchumi huria.

Wafanyabishara hao walipata vipi utajiri wao ?

Mkurugenzi Mtendaji wa UIF, Victor Andrusiv, alisema katika hafla ya 2019 kwamba oligarchs ni "tabaka maalum" la watu, wenye "mfumo maalum ya kufanya biashara" na wana "njia maalum ya maisha na ushawishi".

"Sio wafanyabiashara hasa. Ni watu tajiri,lakini jinsi walivyopata utajiri wao ni tofauti kabisa na jinsi watu wanavyochuma mali katika serikali za kibepari," Andrusiv alisema wakati wa hafla katika Kituo cha Wilson mjini Washington.

"Hawakuanzisha bishara: walinyakua biashara kutoka kwa serikali."

Kwanini wafanyabiashara wengi wa Urusi ni oligarchs?

Kinachofanya wafanyabiashara tajiri wa Urusi wenye ushawishi mkubwa wa kisisa kuangaziwa zaidi ni kile kilichotokea baada ya kumalizika kwa Muungano wa Soviet mnamo 1991.

Siku ya Krisimasi, 1991, Mikhail Gorbashev alijiuzulu kutoka kwa urais wa Sovieti na kukabidhi madaraka kwa Boris Yeltsin, ambaye alikua rais wa Urusi mpya iliyojitegemea.

Mikhail Gorbachev (kushoto) alijiuzulu Disemba 1991 na kumkabidhi Boris Yeltsin (Kulia) madaraka yake ya urais

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mikhail Gorbachev (kushoto) alijiuzulu Disemba 1991 na kumkabidhi Boris Yeltsin (Kulia) madaraka yake ya urais

Ijapokuwa chini ya utawala wa Kikomunisti hapakuwa na mali binafsi, Urusi ya kibepari ilishuhudia ubinafsishaji kwa kiwango kikubwa - hasa katika sekta ya viwanda, nishati na fedha.

Kutokana na ubinafsishaji huo, watu wengi walitajirika sana mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Wale waliokuwa na uhusiano wa karibu na viogozi wa ngazi ya juu walijipatia sehemu kubwa ya viwanda vya Urusi - hasa vile vilivyokuwa vikijishughulisha na malighafi kama vile madini au mafuta na gesi, ambayo ilikuwa inahitajika kote duniani.

Kisha walilipa maofisa waliofanikisha hilo au kuwapa kazi kama wakurugenzi.

Wafanyabiashara hao walimiliki vyombo vya habari, maeneo ya mafuta, viwanda vya chuma, makampuni ya uhandisi, na mara nyingi walilipa kodi ndogo sana kwa faida zao.

Walimuunga mkono Yeltsin na kufadhili kampeni yake ya urais ya mwaka 1996.

Putin na wafanyabiashara tajiri

Putin alipomrithi Yeltsin, alianza kuwakingia kifua wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, wale walioshirikiana naye kisiasa walipata faida zaidi.

Baadhi ya wafanyabiashara tajiri wa awali ambao walitofautiana naye kama vile Boris Berezovsky, walilazimika kutoroka nchi.

Mikhail Khodorkovsky, ambaye wakati mmoja aliaminiwa kuwa Mwanaume wa Urusi tajiri zaidi, sasa anaishi London.

Alipoulizwa kuhusu wafanyabiashara tajiri wenye ushawishi wa kisiasa mwaka 2019, Putin aliliambia gazeti la Financial Times: "Hatuna tena wafanyabiashara tajiri wenye ushawishi wa kisiasa."

Lakini watu ambao walikuwa na uhusiano wa karibu sana na Putin wameweza kujenga himaya za biashara kutokana na ufadhili wake.

Putin akiwa kwenye picha baada ya mafunzo ya judo mjini Sochi yakiongozwa na mabilionea Arkady Rotenberg (katikati) na Vasily Anisimov (kushoto)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Putin akiwa kwenye picha baada ya mafunzo ya judo mjini Sochi yakiongozwa na mabilionea Arkady Rotenberg (katikati) na Vasily Anisimov (kushoto)

Boris Rotenberg, ambaye alikuwa katika klabu moja ya judo na Putin walipokuwa watoto, ametajwa na serikali ya Uingereza kuwa "mfanyabiashara mashuhuri wa Urusi na mwenye uhusiano wa karibu" na Bw Putin.

Kulingana na Jarida la Forbes, thamani ya mali ya Bw Rotenberg ni dola bilioni 1.2.

Rotenberg na kaka yake Arkady walilengwa na vikwazo vya Uingereza baada ya Putin kutambua maeneo mawili yanayojitenga ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine kama "jamhuri za watu".

Sawa na Uingereza, Ukraine, Marekani, Muungano wa Ulaya (EU), Australia na Japan pia zimewawekea vikwazo wafanyabishara tajiri wa Urusi kufuatia hatua hatua ya Urusi kuvamia Ukraine - Baadhi ya vikwazo hivyo huenda vikaimarishwa zaidi.