Telegram: Mtandao ambapo picha za utupu za wanawake husambazwa bila idhini

.

Chanzo cha picha, KLAWE RZECZY

Uchunguzi wa BBC umegundua kuwa picha za siri za wanawake zinasambazwa ili kuwanyanyasa, kuwaaibisha na kuwachafua kwa kiwango kikubwa, kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram.

ONYO:Makala haya yana maudhui ya vitendo vya ngono

Katika muda wa sekunde moja, Sara aligundua kuwa picha yake ya utupu ilikuwa imevuja na kusambazwa kwenye mtandao wa Telegram, maisha yake yalibadilika. Akaunti zake za Instagram na Facebook zilikuwa zimeongezwa, na nambari yake ya simu. Ghafla akawa anatafutwa na wanaume wasiojulikana wakiomba picha zaidi.

"Walinifanya nijisikie kama kahaba kwa sababu waliamini ni mimi mwenyewe nilisambaza picha zangu za utupu. Ilimaanisha sikuwa na thamani kama mwanamke," anasema.

Sara aliwacha kwenda katika burudani picha zake za utupu ziliposambazwa katika mtandaoni
Maelezo ya picha, Sara aliwacha kwenda katika burudani picha zake za utupu ziliposambazwa katika mtandaoni

Sara, sio jina lake halisi, alikuwa ametuma picha hiyo kwa mtu mmoja, lakini ilikuwa imeishia kwenye kikundi cha Telegram chenye wafuasi 18,000, wengi kutoka kijiji chake huko Havana, Cuba. Sasa anahofia kuwa huenda watu asiowajua mtaani wamemwona akiwa uchi. "Sikutaka kutoka, sikutaka kuwasiliana na marafiki zangu. Ukweli ni kwamba niliteseka sana."

Hayuko peke yake. Baada ya miezi kadhaa ya kuichunguza Telegram, tuligundua vikundi vinavyosambaza maelfu ya picha za wanawake zilizorekodiwa kisiri, zilizoibwa au kuvuja katika angalau nchi 20. Na kuna ushahidi mdogo kwamba Telegram inashughulikia tatizo hili.

Nigar amelazimika kwenda mafichoni
Maelezo ya picha, Nigar amelazimika kwenda mafichoni

Anatoka Azerbaijan, lakini amelazimika kuondoka katika nchi yake. Mnamo 2021, video yake akifanya mapenzi na mumewe ilitumwa kwa familia yake, na kisha kutumwa kwenye kikundi cha Telegraph.

"Mama yangu alianza kulia na kuniambia: 'Kuna video, ilitumwa kwangu'," anasema. "Nilivunjika moyo kabisa."

Video hiyo ilisambazwa katika kikundi chenye wanachama 40,000. Katika picha hiyo, uso wa mume wa zamani wa Nigar umefunikwa lakini sura yake inaonekana wazi.

Anaamini kuwa mpenzi wake wa zamani alimpiga picha za siri ili kumchafulia jina kakake, mkosoaji maarufu wa rais wa Azerbaijan. Anasema mamake aliambiwa kuwa video hiyo ingetumwa kwenye Telegram iwapo kaka yake hatakomesha harakati zake.

"Wanakuona kama wewe ni fedheha. Nani anajali kama umeolewa?" Anasema Nigar.

Maelezo ya video, Telegram: Mtandao ambapo picha za utupu za wanawake husambazwa bila idhini

Nigar anasema alimkabili mume wake wa zamani kuhusu video hiyo na akakana kuitengeneza. Tulijaribu kupata maoni kutoka kwake, lakini hakujibu.

Nigar bado anajitahidi kuendelea na maisha yake: " Ninaona madaktari mara mbili kwa wiki," anasema. "Wanasema hakuna maendeleo hadi sasa. Wanauliza ikiwa naweza kusahau, na mimi ninasema hapana."

Picha za Nigar na Sara zote ziliripotiwa kwa Telegraph, lakini mtandao huo haukujibu.

BBC imekuwa ikifuatilia chaneli 18 za Telegram na vikundi 24 katika nchi kuanzia Urusi hadi Brazil, na Kenya hadi Malaysia. Jumla ya watu waliojisajili ni karibu milioni mbili.

.

Maelezo ya kibinafsi kama vile anwani za nyumbani na nambari za simu za wazazi zilichapishwa pamoja na picha za utupu.

Tuliona wasimamizi wa kikundi wakiwauliza washiriki kutuma picha chafu za wapenzi wa zamani, wafanyakazi wenzao au wanafunzi wengine kwenye akaunti ya kiotomatiki, ili ziweze kuchapishwa bila kufichua utambulisho wa mtumaji.

Telegram sasa inasema ina watumiaji zaidi ya nusu bilioni duniani kote - hiyo ni zaidi ya Twitter - huku wengi wakivutiwa na usiri wake.

Mamilioni ya watu walihamia Telegraph mnamo Januari 2021 kutoka WhatsApp, ambayo ilibadilisha masharti yake ya siri.

Telegramu kwa muda mrefu imekuwa maarufu kwa waandamanaji wanaounga mkono demokrasia katika nchi zilizo na udhibiti wa vyombo vya habari. Watumiaji wanaweza kuchapisha bila kushirikisha jina au nambari yao ya simu, na kuunda vikundi vya umma au vya siri vilivyo na hadi wanachama 200,000, au chaneli zinazoweza kutangaza kwa idadi isiyo na kikomo ya watu.

Telegram ilitumika kuandaa mikutano ya maandamano dhidi ya serikali ya Belarus
Maelezo ya picha, Telegram ilitumika kuandaa mikutano ya maandamano dhidi ya serikali ya Belarus

Mtandao huu pia huvutia watumiaji wanaotafuta nafasi isiyodhibitiwa, pamoja na wale ambao wamepigwa marufuku kutoka kwa mitandao mingine.

"Kulingana na Telegram na mmiliki wake, hawataki kuwazuia watumiaji," anasema Natalia Krapiva, mwanasheria wa masuala ya teknolojia katika kikundi cha haki za kidijitali Access Now.

Telegramu haina sera maalum ya kushughulikia usambazaji wa picha za utupu, lakini sheria na masharti yake huwafanya watumiaji wakubali "kutochapisha maudhui haramu ya picha za ngono kwenye vikundi vya Telegraph vinavyoonekana hadharani.

Pia ina sehemu ya kuripoti ndani ya mtandao katika makundi ya umma na ya faragha, na vituo ambapo watumiaji wanaweza kuripoti picha za ngono.

.

Ili kujaribu jinsi Telegram ilivyotekeleza sera zake, tulipata na kuripoti picha 100 kama za ngono kupitia sehemu ya kuripoti ndani ya mtandao. Mwezi mmoja baadaye picha 96 bado zilipatikana. Hatukuweza kupata zingine nne, kwa kuwa zilikuwa katika vikundi ambavyo hatukuweza tena kufikia.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, tulipokuwa tukichunguza vikundi hivi, akaunti kutoka Urusi pia ilijaribu kutuuzia folda iliyo na video za unyanyasaji wa watoto kwa bei ya chini.

Tuliripoti kwa Telegram na Polisi wa Metropolitan, lakini miezi miwili baadaye chapisho na chaneli vilikuwa bado. Akaunti iliondolewa tu baada ya kuwasiliana na timu ya masuala ya habari ya Telegram.

Licha ya udhibiti wake usio mkali, Telegramu huchukua hatua dhidi ya maudhui fulani.

Magenge ya mrengo wa kulia yaliojiunga na Instagram

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Magenge ya mrengo wa kulia yaliojiunga na Instagram

Lakini kuondolewa kwa picha za utupu inaonekana sio kipaumbele.

Tulizungumza na wasimamizi watano wa maudhui ya Telegram kwa sharti la kutokujulikana. Walituambia wanapokea ripoti kutoka kwa watumiaji kupitia mfumo otomatiki.

Walisema huwa hawatafuti picha za ngono sana na kama wanavyojua, Telegramu haitumii teknolojia kufanya hivyo pia. Ukosefu huu wa hatua umesababisha baadhi ya wanawake kuchukua hatua wenyewe.

Joana aliripoti kuhusu picha zilizosambazwa katika mtandao wa telegram
Maelezo ya picha, Joana aliripoti kuhusu picha zilizosambazwa katika mtandao wa telegram

Joanna alipata picha yake akiwa uchi tangu alipokuwa na umri wa miaka 13 katika kikundi cha Telegram cha Malaysia.

Aliunda wasifu ghushi wa Telegraph ili ajiunge na kikundi, ambapo alitafuta bila kujulikana picha za uchi na kuziripoti. Pia alishiriki matokeo yake na marafiki zake.

Kufuatia shinikizo kubwa la vyombo vya habari, kikundi hicho hatimaye kilifungwa. Lakini wakati wa uchunguzi wetu, tuligundua angalau vikundi viwili vinasambaza picha za aina moja.

"Wakati mwingine unajiona mnyonge sana, kwa sababu tulijaribu kufanya mengi kuondoa vikundi hivi. Lakini bado vinaibuka, kwa hivyo sijui kama kuna mwisho wake," anasema Joanna.

Telegramu haikuthibitisha ikiwa kuchapisha picha za watu wa karibu bila kibali kunaruhusiwa kwenye mtandao, au kama zimeondolewa.

Kuwekwa matangazo kwenye baadhi ya chaneli za umma kwenye Telegram - pamoja na uwekezaji - kumeashiria kwamba mwanzilishi Pavel Durov ananuia kuchuma mapato kwenye mtandao.

Hili huenda likaongeza shinikizo kwa Telegram na mwanzilishi wake kufuata nyayo za wapinzani kama vile WhatsApp, ambayo imeanzisha sera dhidi ya usambazaji wa picha za ngono.