Wanawake ambao wameamua kuwalea watoto wao bila waume

Chanzo cha picha, Mam Issabre
Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wanaotumia wafadhili wa mbegu za kiume ni wanawake wasio na waume wanaonuia kulea mtoto wao pekee, kulingana na data ya hivi punde kutoka kwa benki kubwa zaidi ya mbegu duniani, Cryos International.
Cryos hutoa mbegu za wafadhili na mayai yaliyogandishwa kwa zaidi ya nchi 100 ulimwenguni.
Kulingana na shirika la UN Women, kuna zaidi ya akina mama wasio na waume milioni 100 duniani kote.
Ingawa hakuna data ya kutosha kuhusu idadi ya akina mama wasio na waume kwa hiari yao, wanawake wanaochagua kulea watoto wao peke yao mara nyingi hukabiliana na changamoto za kijamii, kitamaduni na hata kisheria wanapoanzisha familia.
Tulizungumza na wanawake wanne kuhusu safari yao ya kibinafsi ya kuwa mama na jinsi wanavyohisi kulea watoto wao bila baba.
"Uamuzi bora katika maisha yangu"

Chanzo cha picha, Mam Issabre
Mam Issabre, kutoka Ufaransa, ametamani kuwa mama sikuzote. Baada ya kuifikiria kwa miaka mingi, hatimaye aliamua kufanya hivyo peke yake miaka miwili iliyopita.
"Niliamua kuzungumza na mama yangu kuhusu hilo, na aliniambia unaweza kuwa wakati mzuri wa kujaribu, kwa sababu nilikuwa na umri wa miaka 38 wakati huo," anakumbuka.
"Nilifanya uamuzi wangu mnamo Desemba na Februari nilikuwa mjamzito," mtangazaji huyo wa redio anasema.
Miezi tisa baadaye, Mam alijifungua mtoto wa kike mwenye afya njema aitwaye Imany.
Kila kitu kinaonekana kuwa rahisi, lakini kwanza alipaswa kushinda kikwazo kikubwa: wakati huo, matibabu ya uzazi hayakuwepo kwa wanawake wasio na waume nchini Ufaransa.
Daktari wake alikuwa amependekeza kwamba asafiri nje ya nchi kwa ajili ya upandikizi, lakini Mam alifanikiwa kumpata daktari mwingine aliyekuwa tayari kumhudumia.
Anasema hakujua kuwa ni kinyume cha sheria, alifikiria tu kwamba haikuwezekana kutekeleza utaratibu huo nchini Ufaransa.
Mwezi Juni mwaka jana, Ufaransa ilipitisha sheria inayowaruhusu wanawake wasio na waume na wapenzi wa jinsia moja kufaidika na matibabu ya uzazi, ambayo hapo awali yalitengwa kwa wapenzi wa jinsia tofauti, baada ya miaka miwili ya mjadala bungeni na maandamano makubwa.
"Zawadi kutoka kwa Mungu"

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka mmoja baadaye, Mam anatafakari kuhusu ukweli kwamba amekuwa mama.
"Mara ya kwanza nilipomshika binti yangu ndipo nilipogundua kuwa mimi ni mama," anasema. "Nililia sana siku hiyo."
"ulikuwa wakati wa hisia sana - ulikuwa uamuzi bora zaidi katika maisha yangu,"
Mama alichagua mtoaji mbegu asiyejulikana kwa sababu alitaka kumlinda binti yake dhidi ya kukataliwa.
"Nilihisi kama alikuwa kila kitu kwangu na nilikuwa kila kitu kwake"

Chanzo cha picha, Anne Marie Vasconcelos
Kwa Anne Marie Vasconcelos, mwanamke mwenye umri wa miaka 44 kutoka New Jersey, Marekani, safari ya kuwa mama imekuwa ndefu na ngumu.
Miaka kumi iliyopita, Anne Marie aligunduliwa kuwa na ugonjwa unaojulikana kama ovary polycystic (PCOS), hali ambayo huathiri utendaji wa ovari ya mwanamke na inaweza kusababisha matatizo ya uzazi.
Ugunduzi huu, pamoja na kufiwa na babake hivi majuzi, ulimchochea kufanya uamuzi wa kubadili maisha.

Chanzo cha picha, Anne Marie Vasconcelos
"Mtaalamu aliniambia, kulingana na vipimo vyangu vya maabara, kwamba ningekuwa na matatizo ya kuwa na watoto na kwamba ikiwa ningetaka watoto, nilipaswa kuanza," anaeleza mfanyakazi huyu wa serikali ya shirikisho.
Lakini kama mwanamke mseja mwenye umri wa miaka 34, kuwa mama lilionekana kuwa jambo lisilowezekana.
"Nilimwambia kuwa sijaolewa, na aliniambia kuwa haukuhitaji kuolewa ili kupata watoto. Sijawahi kufikiria hivyo," anakumbuka Anne Marrie.
"Sikuweza kuamini"

Chanzo cha picha, Anne Marie Vasconcelos
Mnamo 2016, mwana wa kwanza wa Anne Marie, William alizaliwa, akifuatiwa na mtoto wake wa pili Wyatt miaka michache baadaye.
Watoto hao wawili walitungwa mimba kwa njia ya IVF kwa kutumia manii ya mtoaji huyo huyo, na mimba hizo mbili zilikuwa zikikumbwa na matatizo, kila mtoto wa kiume akiletwa ulimwenguni mapema kwa njia ya upasuaji.
"Nilijua tu"

Chanzo cha picha, Sarah
Sarah [sio jina lake halisi] sikuzote alitaka kuwa mama.
"Sidhani kama nilikuwa na wakati mmoja maishani mwangu ambapo nilikuwa na mashaka yoyote kuhusu kama ningefanya au la - nilijua tu," Sarah mwenye miaka 36 anasema.
Kwake, coronavirus ilionyesha wazi kwamba hakuwa na sababu ya kungoja tena.
"Janga hili liliniruhusu kuungana tena na hamu hii ya kuwa mama, kwa hivyo nilimuuliza rafiki, na akakubali ombi langu la kubeba mtoto wake," anasema.
Mnamo Agosti, Sarah aligundua kuwa alikuwa mjamzito baada ya jaribio lao la kwanza.
"Nilikuwa nje, kulikuwa na joto, na nilihisi na nilijua," anasema.
Sasa akiwa na ujauzito wa miezi sita, anatafakari jinsi utoto wake ulivyoathiri uamuzi wake.
"Nilikulia Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Nilizaliwa mwaka wa 1985 katikati ya kipindi kigumu zaidi cha vita," anasema. "Nilikuwa na maisha ya utotoni yenye furaha lakini pia yalikuwa yamejawa na kiwewe."
"Hakuna kitu cha ushujaa kwa kile nilichofanya"

Chanzo cha picha, Sarah
Sarah anasema hali ya nchi yake na vifo vya wapendwa vilikuwa na athari kubwa katika uamuzi wake.
"Nadhani kulikuwa na mwito wa maisha baada ya mfululizo wa matukio ya kutisha ambayo yaliathiri watu wangu, nchi yangu, jamii yangu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na janga hilo lilikuwa kichocheo," anasema.
Kwa Sarah, kuwa mama asiye na mwenzi si uamuzi wa ujasiri.
"Sidhani kama kuna kitu maalum au cha kishujaa juu ya nilichoKIfanya, kwa sababu wanawake walioolewa mara nyingi huwalea watoto wao peke yao," anasema.
"Nahitaji mtu wa kumpenda"

Chanzo cha picha, Nyakno Okokon
Kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaochagua kuwa mama wasio na waume kunaweza kuashiria mabadiliko ya mtazamo kuelekea muundo wa familia ya wazazi wawili, lakini mlinzi, Nyakno Okokon mwenye umri wa miaka 37 anasema hakuwa na chaguo.
"Haikuwa chaguo," anasema. "Ilikuwa hatima yangu na ilibidi nijifunze kuikubali."
Nyakno alikulia katika familia ya watoto 20 na baba mwenye wake wengi - mama yake alikuwa mke wake wa nne.
"Ilitubidi kupambana ili kujikimu sisi wenyewe, kwa hivyo hatukupata elimu bora, tulipata elimu ya shule za msingi na sekondari tu.
"Lakini siwezi kuwalaumu kwa sababu hayo yalikuwa ni mawazo yao," aliiambia BBC.
Nyakno aliondoka Nigeria kuelekea Dubai miaka sita iliyopita kwa matumaini ya maisha bora.
Yeye hufanya kazi saa 12 kwa siku na anasema hana wakati wa kukutana na watu wapya.
Lakini ameamua kwamba mwaka huu atafanya "chochote kinachohitajika" kupata mtoto.
"Niligundua hakuna kinachonizuia kuwa mama ikiwa nitaweza kuwahudumia, kuwapa upendo na malezi bora," anasema.
"Ninahitaji mtu wa kumpenda," anaongeza, "na ikiwa sina watoto, nadhani nitapata uchungu sana."
Mipango isiyo ya kawaida

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyakno anapanga kupata mimba kwa njia ya kawaida, lakini ikiwa hiyo haitafanya kazi, atajaribu IVF au njia mbadala.
Hata hivyo, hana mpango wa kufichua mipango yake kwa baba mzazi hadi atakapokuwa mjamzito.
"Ni kwa sababu sitampa jukumu, hilo ndilo jambo pekee litakalomtia hofu kwa sababu ana maisha yake na mipango yake," anasema.
Nyakno anasema familia yake imekubali mipango hiyo yake isiyo ya kawaida na itamsaidia kama mzazi asiye na mwenzi.
"Familia yangu inaniunga mkono kwa sababu wanajua umri wangu unazidi kuwa mkubwa na hiyo itaniletea furaha."












