Mzozo wa Ukraine: Putin asema Marekani inajaribu kuingiza urusi kwenye vita

Rais Putin

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Urusi Vladimir Putin amelaumu Marekani kwa kujaribu kuingiza nchi yake katika vita dhidi ya Ukraine.

Katika tamko lake la kwanza kuhusu mzozo huo wa wiki kadhaa, alisema lengo la Marekani ni kutumia makabiliano kama kisingizio cha kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

Pia alisema Marekani inapuuza wasiwasi wa Urusi kuhusu vikosi vya muungano wa Nato huko Ulaya.

Hali ya taharuki inaendelea kupanda kufuatia kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi karibu na mipaka ya Ukraine.

Urusi katika wiki za hivi karibuni imepeleka karibu wanajeshi 100,000 - waliojihami kwa kila kitu kuanzia magari ya kivita na silaha nzito nzito ardhini na angani- katika mpaka wa Ukraine.

Lakini Urusi inapinga madai ya nchi za Magharibi kuwa inapanga uvamizi, karibu miaka manane baada ya kuchukua jimbo Ukraine la kusini katika rasi ya Crimea na kuunga mkono uasi hatari wa umagaji damu katika eneo la Donbasma mashariki.

Moscow kwa upande wake ililaumu serikali ya Ukraine kwa kushindwa kutekeleza mkataba wa kimataifa wa kuleta amani mashariki, ambako karibu watu 14,000 waliuawa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanaodhibiti maeneo kadhaa.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumanne alionya kuwa uvamizi wa Urusi "hautakuwa vita kati ya Ukraine na Urusi - hii itakuwa vita vya Ulaya, vita kamili ".

Akizungumza baada ya kusema na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban mjini Moscow, Bw. Putin alisema: "Nionavyo mimi Marekani haina haja sana na usalama wa Ukraine... lakini kazi yake kuu ni kudhibiti maendeleo ya Urusi. Kwa maana hii Ukraine yenyewe ni chombo cha kufikia lengo hili."

Uhasama kati ya Urusi na Marekani, ambayo bado inamiliki silaha kubwa za nyuklia duniani, ulianza tangu zama za Vita Baridi (1947-89). Ukraine wakati huo ilikuwa sehemu muhimu ya Muungano wa Sovieti, ya pili baada ya Urusi.

Bw. Putin alisema Marekani ilipuuza wasiwasi wa Moscow katika jibu lake kwa Urusi ya kutaka kuhakikishiwa usalama kisheria, ikiwa ni pamoja na kuzuia upanuzi wa Nato kuelekea mashariki.

Aliashiria kuwa Ukraine ikipewa nafasi ya kujiunga na Nato,inaweza kuwaingiza washirika wengine katika vita dhidi ya Urusi.

"Tafakari kuwa Ukraine ni mwanachama wa Nato na oparesheni ya kijeshi [ya kukomboa Crimea] inaanza," kiongozi huyo wa Urusi alisema. "Tutakuwa - tunapigana na Nato kwa nini? Je mtu yeyote amefikiria kuhusu hili? Inaonekana hawajafanya hivyo."

.

Nchini Ukraine kwenyewe, Waziri Mkuu wa Ungereza Boris Johnson alipokuwa ziarani alimlaumu Bw. Putin kwa "kwa kuelekeza mtutu wa bunduki... kwenye kichwa cha Ukraine" na kutoa wito kwa Kremlin kurudi nyuma kwenye "janga la kijeshi ".

Baada ya kufanya na mazungumzo na Bw. Zelensky katika mji mkuu wa Kyiv, Bw. Johnson aliwaambia waandishi wa habari kwamba jeshi la Ukraine litajibu mashambulizi endapo watavamiwa.

"Kuna watu 200,000 wanaume na wanawake waliyo na silaha nchi Ukraine," alisema.

"Watakabiliana vikali kijilinda , nadhani kwamba wazazi na akina mama nchini Urusi wanapaswa kutafakari juu ya hatua hiyo. Na ninatumai sana kwamba Putin atarudi nyuma kutoka kwenye njia ya mgogoro na kwamba tutashiriki katika mazungumzo."

Bw. Johnson alionya kuwa Uingereza itajibu uchokozi wa Urusi kwa "furushi la vikwazo na hatua zingine zitakazotekelezwa wakati vikosi vya Urusi vitavuka na kuingia himaya ya Ukraine".

Uingereza imetangaza kuwa itatoa £88m ($119) kwa Ukraine kukuza utawala thabiti na uhuru wa nishati kutoka kwa Urusi.

Bw. Zelensky ametoa wito wa vikwazo kabla chochote hakijafanyika, akisema ataunga mkono hatua yoyote ya Uingereza ya kukabiliana na "fedha chafu " zinazodaiwa kuhusishwa na Kremlin kuibiwa kupitia jiji la London.