Fahamu kwanini Korea Kaskazini imerusha makombora mengi kinyume na kawaida yake?

Chanzo cha picha, EPA
Korea Kaskazini imerusha makombora mawili ya masafa mafupi kwenye maji nje ya pwani ya Japan, ikiwa ni majaribio ya hivi punde katika mfululizo usio wa kawaida wa majaribio.
Makombora hayo yaliripotiwa kurushwa kutoka uwanja wa ndege karibu na mji wa Pyongyang mapema Jumatatu kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini. Japan pia ilithibitisha jaribio hilo.
Ni mara ya nne Korea Kaskazini inarusha kombora ndani ya wiki mbili.
Umoja wa Mataifa umeipiga marufuku Korea Kaskazini kutokana na kufanya majaribio ya silaha za makombora na nyuklia, na imeiwekea vikwazo vikali.
Lakini taifa hilo la Asia Mashariki mara kwa mara linakaidi marufuku hiyo, na kiongozi Kim Jong-un ameapa kuimarisha ulinzi wa nchi yake.
Siku ya Ijumaa ilisema kuwa ilirusha makombora ya masafa mafupi ya kutoka kwa mabehewa ya treni, wakati siku zilizopita ilifanya majaribio mawili ya kile inachodai kuwa makombora ya kasi, ambayo ni ngumu kuyatambua
Kwa nini Korea Kaskazini inarusha makombora sasa?
Kasi ya majaribio na wakati yanafanywa mwezi Januari sio jambo la kawaida. Korea Kaskazini kawaida hurusha makombora yake kuashiria matukio muhimu ya kisiasa nchini humo, au kama ishara ya kutofurahishwa kwake na mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini.
Korea Kaskazini kwa kawaida hurusha silaha ili kuendeleza uwezo wa makombora na kudumisha utayari wa kufanya kazi, na majaribio ya hivi punde yanaonekana kuthibitisha hili, alisema Ankit Panda, mtaalam wa Shirika la Carnegie Endowment for International Peace.
Lakini wakati huo huo, "Kim Jong-un pia ana mambo ya ndani: wakati wa matatizo ya kiuchumi, uzinduzi huu unamruhusu kudhihirisha kwamba vipaumbele vya ulinzi wa taifa havitaanguka," Bw Panda aliambia BBC.
Korea Kaskazini imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa chakula na uchumi unaodorora. Hii ni kwa sababu ya kizuizi cha kujiwekea ili kuzuia Covid ambayo imekata biashara na Uchina, mshirika wake mkuu wa kiuchumi na kisiasa - ingawa kumekuwa na ripoti kwamba hii inaweza kuanza tena hivi karibuni.
Bw Kim hivi majuzi alikiri kwamba nchi hiyo ilikuwa inakabiliwa na kipindi kugumu ziaidi, na pia aliapa kuongeza nguvu zake za kijeshi ikiwa ni pamoja na kuunda makombora ya hypersonic.
Mazungumzo na Marekani, ambayo inaitaka Korea Kaskazini kuachana na silaha zake za nyuklia, yamekwama tangu Rais wa Marekani Joe Biden achukue hatamu. Utawala wa Bw Biden uliiwekea vikwazo vyake vya kwanza Korea Kaskazini wiki jana, kujibu baadhi ya majaribio ya mapema mwezi huu.
Urushaji wa leo Jumatatu unaweza kuwa jibu kwa vikwazo, kuonyesha kwamba "Korea Kaskazini inapinga hatua za Marekani, kwa mujibuwa Park Won-gon, profesa wa masomo wa Korea Kaskazini katika Chuo Kikuu cha Ewha Womans.
Je, majaribio ni kwa sababu ya China?
Urushaji huo unafanyika wiki chache kabla ya Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi, tukio lenye heshima kubwa kwa Uchina, ambalo linatarajiwa kuanza Beijing mnamo Februari 4.
"Nafikiri kuwa China haitakubali majaribio ya Korea Kaskazini mashindano ya Olimpiki yanakribia kuanza," mchambuzi wa Korea Kaskazini Chad O'Carroll alisema kwenye Twitter.
"Ikiwa hili litaendelea, hatuwezi kupuuza uwezekano kwamba Korea Kaskazini huenda imekasirishwa na China kuhusu jambo fulani."
Lakini Bw Panda anasema ingawa China inaweza isifurahishwe na majaribio haya, kuna uwezekano yatavumilika vya kutosha" ikizingatiwa kwamba hayahusishi majaribio ya silaha za nyuklia au makombora ya masafa marefu.

Chanzo cha picha, AFP
"Kwa kuzingatia uhusiano wake na China, kuna uwezekano uongozi wa Korea Kaskazini unataka kusitisha mazoezi yake ya kijeshi ya mapema mwaka 2020 na majaribio ya makombora kabla ya mashindano ya Olimpiki ya Beijing.
"Wakati wa majaribio haya pia pia unaonyesha kuwa Korea Kaskazini haitaki kukaa kimya kabla ya uchaguzi wa rais wa Korea Kusini au kuonekana iko hali mbaya wakati China inatuma msaada kwenye mpaka."













