USSR: Sababu tano kwa nini Muungano wa Sovieti ulianguka

Miaka thelathini iliyopita, nchi kubwa zaidi ulimwenguni na taifa la kwanza la kikomunisti lilianguka rasmi. Tunaangazia sababu kuu tano za kuanguka kwa Muungano wa Jamhuri za Kijamaa za Kisovieti.

Bendera nyekundu yenye nyundo na mundu, ambayo hapo awali ilikuwa ishara mojawapo ya nchi zenye nguvu zaidi duniani, ilishushwa Kremlin.

Gorbachev aliingia madarakani mwaka 1985, akiwa na umri wa miaka 54 pekee. Alianza mfululizo wa mageuzi ili kuleta maisha mapya katika nchi hiyo ambayo ilikuwa imedumaa.

Wengi wanahoji kwamba mageuzi hayo, yanayojulikana kama Perestroika (kujenga upya na kurekebisha) na Glasnost (uwazi na uhuru wa kujieleza), yalisababisha kufa kwa nchi. Wengine wanasema kwamba Umoja wa Kisovieti ilikuwa ni zaidi ya kuokolewa, kutokana na ugumu wa muundo wake.

Hapa tunaangalia sababu za msingi za kuanguka ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa Urusi ya sasa kwa namna inavyojiona na kujingiluinganisha na ulimwengu wote.

1. Uchumi

Kuanguka kwa uchumi ilikuwa ndio tatizo kubwa zaidi kati ya matatizo yote ya Umoja wa Kisovieti. Nchi ilikuwa na uchumi uliopangwa serikali kuu, tofauti na uchumi wa soko wa nchi zingine nyingi.

Taifa la USSR liliamua kiasi gani cha kila kitu cha kuzalisha (magari mangapi au jozi ngapi za viatu au vipande vya mkate)

Pia iliamua ni vitu vingapi kati ya hivyo ambavyo kila raia mmoja mmoja alihitaji, ni kiasi gani kila kitu kinapaswa kugharimu na ni kiasi gani watu wanapaswa kulipwa.

Nadharia ilikuwa kwamba mfumo huu ungekuwa mzuri na wa haki, ingawa ulijitahidi kufanya kazi.

Usambaji wa vitu daima ulikuwa nyuma ya mahitaji na pesa mara nyingi haikuwa na maana.

Watu wengi katika Muungano wa Sovieti hawakuwa maskini kabisa, lakini hawakuweza kupata bidhaa za msingi kwa sababu zilikuwa hazitoshelezi.

Ili kununua gari, ulipaswa kuwa kwenye orodha ya kusubiri kwa miaka. Ili kununua koti au jozi ya buti za msimu wa baridi, mara nyingi ulilazimika kupanga foleni kwa masaa na unaweza ukagundua kuwa saizi yako tayari zimeisha.

Watu hawakuzungumza kuhusu kununua kitu, bali ilikuwa kuhusu kukipata.

Kilichofanya mambo kuwa mabaya zaidi ni gharama ya uchunguzi wa anga na mmashindano ya silaha kati ya Umoja wa Kisovieti na Marekani, zilizoanza mwishoni mwa miaka ya 1950.

USSR ilikuwa nchi ya kwanza ulimwenguni kupeleka chombo angani na ilikuwa na safu ya silaha za nyuklia na makombora ya hali ya juu ya balestiki, lakini yote haya yalikuwa ghali sana.

Umoja wa Kisovieti ulitegemea rasilimaili zake, kama vile mafuta na gesi, kulipia mashindano hayo lakini mwanzoni mwa miaka ya 1980, bei ya mafuta iliporomoka na hii iliathiri sana uchumi ambao tayari ulikuwa unayumba.

Sera ya Rais Gorbachev ya kujenga na kufufua uchumi ilianzisha baadhi ya kanuni za soko, lakini uchumi wa Kisovieti ulikuwa mgumu sana kurekebishika kwa haraka.

Bidhaa zilibaki chache na mfumuko wa bei uliongezeka sana.

Kwa nini ni muhimu leo?

Upungufu wa bidhaa ilikuwa na athari ya kudumu katika mawazo ya watu wa baada ya Soviet.

Hata sasa na kizazi cha baadaye hofu ya kwenda bila mahitaji ya msingi inaendelea.

Ni hisia kali ambayo inaweza kubadilishwa kwa urahisi wakati wa kampeni za uchaguzi.

2. Itikadi

Sera ya rais Gorbachev ya kuongeza uwazi katika taasisi za kiserikali ilikuwa na lengo la kuleta uhuru wa kujieleza katika nchi ambayo kwa miongo kadhaa ilikuwa chini ya utawala wa mabavu ambapo watu waliogopa kusema mawazo yao, kuu;liza maswali au kulalamika.

Alianza kwa kufungua makumbusha ya kihistoria yakionesha kiwango halisi cha ukandamizaji chini ya Joseph Stalin (kiongozi wa Soviet kati ya 1924 na 1953), ambayo yalisababisha vifo vya mamilioni ya watu.

Alihimiza mjadala kuhusu mustakabali wa Umoja wa Kisovieti na miundo yake ya nguvu juu namna inavyopaswa kufanyiwa mageuzi ili kusonga mbele.

Pia aligusia wazo la mfumo wa vyama vingi , akipinga utawala wa chama cha Kikomunisti.

Serikali ya Gorbachev ilijaribu kwa haraka kuingiza baadhi ya vipengele vya uhuru na haki katika mchakato wa uchaguzi, lakini ilikuwa imechelewa sana.

Kwa nini ni muhimu leo?

Rais wa Urusi Vladimir Putin alitambua mapema juu ya umuhimu wa wazo dhabiti la kitaifa, haswa kwa serikali ambayo sio ya uwazi na ya kidemokrasia.

Ametumia muundo kutoka enzi mbalimbali za zamani za Urusi na Soviet ili kukuza hali bora ya kitaifa katika urais wake,.

Enzi ya Usovieti imechanganyika kikamilifu ili kuhamasisha uzalendo (na kuangalia nyuma ya shida nyingi za maisha ya kila siku nchini Urusi leo).

3.Utaifa

Umoja wa Kisovieti ilikuwa serikali ya mataifa mbalimbali, mrithi wake ndio Milki ya Urusi.

Ilikuwa na jamhuri 15, ambazo kila moja linalingana kinadharia katika haki kama mataifa ya ndugu.

Kiuhalisia, Urusi ilikuwa kubwa zaidi na yenye nguvu na lugha ya Urusi na utamaduni wa Kirusi ulitawala maeneo mengi.

Sera ya uwazi ilifanya watu wengi katika jamhuri nyingine kufahamu kuhusu ukandamizaji wa kikabila wa siku za nyuma, ikiwemo njaa ya Ukreini miaka ya 1930, utekaji nyara wa Mataifa ya Baltic na Ukreini magharibi chini ya mapatano ya kirafiki na Unazi, na kulazimishwa kufukuzwa kwa makabila mengi wakati wa vita vya pili vya dunia.

Matukio haya na mengine mengi yalileta kuongezeka kwa utaifa na matakwa ya kujitawala.

Wazo la Muungano wa Sovieti kuwa familia ya mataifa yenye furaha lilidhoofishwa sana na majaribio ya haraka ya kuurekebisha kwa kutoa uhuru zaidi kwa jamhuri ilionekana kuwa imechelewa sana.

Kwa nini ni muhimu leo?

Mvutano kati ya Urusi, ikipambana kudumisha lengo l lake kuu na nyanja ya ushawishi, na nchi nyingi za baada ya Soviet bado lipo pale pale.

Uhusiano mkali kati ya Moscow na majimbo ya Baltic, Georgia hivi karibuni na madhara yake kwa Ukraine uinaendelea kuunda mazingira ya kijiografia ya Ulaya na kwingineko.

4. Kuvunjika moyo na matumaini

Kwa miaka mingi, watu wa Kisovieti waliambiwa kwamba nchi za Magharibi "zimeoza" na watu wake walikuwa wakiteseka katika umaskini na uharibifu chini ya serikali za kibepari.

Wazo hili lilizidi kutiliwa shaka kutoka mwishoni mwa miaka ya 1980 wakati wa ukuaji wa usafiri na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya watu wa kawaida.

Wananchi wa Soviet waliweza kuona kwamba katika nchi nyingine nyingi kiwango cha maisha, uhuru wa kibinafsi na hali ya ustawi ulizidi sana waliokuwa nao wao

Pia waliweza kuona yale ambayo mamlaka yao ilikuwa inajaribu kuwaficha kwa miaka mingi kwa kuwakataza kusafiri nje ya nchi, kufungia vituo vya redio vya kigeni (kama vile BBC World Service) na kukagua chapa za filamu zozote za kigeni zinazoruhusiwa kuingia katika Muungano wa Sovieti.

Gorbachev anasifiwa kwa kumaliza vita baridi na kusimamisha tishio la mapigano ya nyuklia kwa kuboresha uhusiano na nchi za Magharibi, lakini matokeo yasiyotarajiwa ya uhusiano huu ulioboreshwa ni kwamba watu wa Soviet waligundua jinsi maisha yao yalikuwa duni ikilinganishwa na wale wa nchi zingine.

Gorbachev alizidi kuwa maarufu nje ya nchi huku akikabiliwa na ukosoaji zaidi na zaidi nyumbani.

Kwa nini ni muhimu leo?

Serikali ya Urusi imekuwa hodari katika kudhibiti taarifa za vyombo vya habari kwa manufaa yake.

Mafanikio ya kisayansi, ushindi katika vita ya dunia vya pili na urithi wa kitamaduni hutumiwa mara kwa mara katika masimulizi ya vyombo vya habari ili kupeleka ujumbe wa upekee wa kitaifa, kugeuza umakini wa Urusi kutoka katika shida za kila siku.

5. Uongozi

Gorbachev alijua kwamba mabadiliko makubwa yanahitajika ili kukomesha kuzorota zaidi kwa uchumi wa Soviet na maadili ya umma, lakini maono yake ya namna ya kufikia hii labda hayakuwa na uwazi.

Kwa kumaliza Vita Baridi, alikua shujaa kwa ulimwengu wa nje, lakini nyumbani alikosolewa na wanamageuzi ambao walihisi kuwa hachukui hatua sahihi na kwa wahafidhina walihisi anaenda mbali sana.

Matokeo yake, alizitenga kambi zote mbili.

Wahafidhina walianzisha mapinduzi mabaya mnamo Agosti 1991 ili kumwondoa Gorbachev mamlakani.

Badala ya kuiokoa USSR, jaribio lililoshindwa lilisababisha kifo cha muungano huo. Chini ya siku tatu baadaye, viongozi wa mapinduzi walijaribu kuikimbia nchi na rais Gorbachev akarudishwa mamlakani, lakini kwa muda mfupi tu.

Boris Yeltsin wa Urusi na viongozi wa mitaa katika maeneo mengine ya USSR walijitokeza.

Katika miezi iliyofuata jamhuri nyingi walipiga kura huru zao za maoni na kufikia Desemba hatima ya serikali kuu ilitiwa muhuri.

Kwa nini ni muhimu leo?

Vladimir Putin ni mmoja wa watawala wa muda mrefu zaidi wa Urusi.

Siri moja ya maisha yake marefu ni kuiweka Urusi kwanza, au angalau hata kuonekana kufanya hivyo.

Wakati rais Mikhail Gorbachev alipokosolewa kwa kuwaondoa haraka wanajeshi wa Soviet kutoka Ujerumani Mashariki, Vladimir Putin anapambana kwa jino na ukucha kwa kile anachoamini kuwa ni kwa maslahi ya Urusi.

Putin alikuwa afisa katika kikosi cha KGB huko Ujerumani Mashariki wakati Ukuta wa Berlin ulipoanguka na kushuhudiwa kwa machafuko ya kujiondoa kwa Soviet.

Miaka thelathini kuendelea, anapinga kabisa NATO kukaribia mipaka ya Urusi na yuko tayari kuunga mkono hili kwa nguvu, kama ambavyo tukio la hivi karibuni la wanajeshi wa Urusi kuisogolea Ukraine inavyoonyesha.