WARIDI WA BBC : Nilijaribu kujadiliana na mbakaji ambaye sikufahamiana naye

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Karen Lina kwa jina maarufu kama Princess ni mwanamke mwenye umri wa miaka 44 , ambapo miaka miwili iliyopita alipitia kipindi ambacho kamwe hawezi kukisahau maishani mwake .

Kulingana naye ni kitendo ambacho hakudhania kwamba kingeweza kumtokea.

Alibakwa na mtu ambaye hakuwahi kumuona wala kumfahamu katika maisha yake yote .Anaposimulia kisa hiki bado makovu yaliompata humjia kwa hisia za uchungu na kero ila ameamua kukubali hali na kusonga mbele .

"Wakati ambao nilipitia kitendo cha ubakaji , nilikuwa nimeishi kwa miezi mitatu tu baada ya kuondoka katika ndoa yangu.

Kwa kifupi aliyekuwa mume wangu alikuwa amenipatia talaka na alikuwa amenifukuza katika makao tulioishi kama mke na mume jijini Nairobi'',anakumbuka Princess

Masaibu yake yalianza punde tu baada ya kutoka kwenye ndoa yake ya miaka mitatu .

Alipoanza maisha ya kuishi peke yake ilibidi achukue hatua ya kutembea kwa muda mrefu akielekea eneo la ibada za asubuhi kama njia ya kufanya mazoezi.

"Nilikuwa nimeishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi mitatu hivi , kila siku kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili na nusu nilikuwa nafanya mazoezi yangu .Sikuwahi kuogopa,eneo lile lilikuwa salama kwa hivyo sikuwa na wasiwasi wa kutembea muda huo" anakumbuka mwanadada huyo .

Hivyobasi anasema kwamba anakumbuka siku ya Jumannena kujiandaa ili kuelekea upande wa barabara kuu .

"Nilikuwa nimeanza kutembea tu niliposikia mtu ambaye alikuwa anatembea kwa kasi nyuma yangu akielekea katika eneo nililokuwa nikienda. Niligeuka na kuona alikuwa mwanamme na nikamtaka apite mbele yangu. Lakini alisisitiza kwamba niendelee tu. Na ghafla kabla nifahamu ni kipi kilikuwa kinatendeka niliona upanga kwenye shingo langu na akasema kwamba nisijaribu kusonga "Princes anasimulia

Mwanadada huyo anasema mambo yalifanyika kwa haraka sana. Kwanza anasimulia kwamba mkoba aliokuwa ameubeba ulianguka.

Anakumbuka kumwambia mtu huyo kwamba alikuwa anaelekea katika ibada na kwamba alikuwa radhi achukue chochote alichokitaka ndani ya mkoba wake.

Anasema kutokana na mafunzo yake ya hapo awali yaliohusu kujilinda wakati wa mashambulizi, alikuwa amefahamu kwanza sio vizuri kujibizana na mshambuliaji na kwamba wakati huo wote utulivu ulihitajika.

"Mtu aliyekuwa ananishambulia alinieleza kuwa nisijaribu kushindana naye na kuwa ikiwa nitakubali yote atakayo kuwa akisema basi hakutakuwa na mabaya yatakayonisibu'

Iwapo ningekaidi alikuwa radhi atumie upanga aliokuwa nao.

''Muda mchache baadaye alinitaka nielekee barabara tofauti ambayo haikuwa na watu na hapo nikaanza kuingiwa na hofu"Princess alisema

Mwanadada huyo anasema kwamba wakati huo wote mtu huyo alimshika mkono na hakutaka kuzungumza naye .

Baadaye alimwelekeza katika nyumba moja iliokuwa na mlango mwekundu.

Wasiwasi ulizidi kwani eneo alilokuwa akipelekwa lilikuwa na giza totoro na mara moja akatakiwa asimame mbele ya mlango huo.

Anasema kwamba tayari mtu aliyemshika mateka alikuwa amechukua mkoba wake na kuanza kupekua ili kubaini kilichokuwa ndani.

"Muda mfupi baadaye alinitaka kuvua nguo zangu na hapo ndiposa nilihisi wasiwasi zaidi, si kwamba sikusikia amri yake ila nilimuuliza eti umesema nini? Akarudia tena . Nilijipata nikimweleza ikiwa anawezakunipa fursa ya kuomba kwanza . Nilitaka kumshawishi asinibake .Nakumbuka nikimweleza kwamba mimi bado sina mume na tunaweza kuwa wapenzi'.

Hizi zote zilikuwa mbinu za kuanza mazungumzo ambayo yangemshawishi kuchukua hatua tofauti .Princess anasema kwamba alikuwa amekubali kumpa namba yake ya simu ili waanze mawasiliano.

Mwanadada huyo anasema kwamba mtu huyo alikuwa na nia moja tu kumbaka kwa hiyo hakuwa na wakati wa kumsikiliza

Hatahivyo cha ajabu ni kwamba alimpatia fursa ya kuomba kwa dakika chache .

"Kwa maisha yangu yote tangu nikiwa binti nilikuwa naomba Mungu na kumkumbusha kwamba , nisiwahi kujipata katika mikono ya mbakaji , nilidhani kwamba fursa niliyopewa ya kuomba pengine Mwenyezi Mungu angenihurumia na kupigana na mbakaji aliyekuwa tayari kunidhulumu, ila baada ya kumaliza dua yangu alinifanyia kitendo hicho cha kinyama bila kujali '', anasema mwandada huyo .

Anakumbuka mtu huyo akimtolea maneno makali na kumfokea kwamba sasa ilikuwa wakati wa kuvua nguo alizokuwa amevalia .

Hakuamini kwamba kitendo cha dhuluma ya kingono kingefanyika chini ya dakika chache tu .

"Uchungu huu ni mwingi hata sasa ninapoongea bado nahisi uchungu wa dhuluma hiyo' Anasema

Baada ya kitendo hicho kutoka kwa mtu ambaye hakuwa anamfahamu Princess hakuwa na ujasiri wa kumpigia yeyote simu .

Mwanadada huyu anasema kwamba anakumbuka tu akirudia maneo haya "Princess hujabakwa , wewe hujabakwa wewe ni mgonjwa tu'

Anasema kwamba ni hali ambayo wanawake wengi wanaobakwa hupitia i ya kukataa hali halisi kwamba wamedhulumiwa , ila huwa hawana nguvu au ujasiri wa kujitokeza wazi.

Princess anakumbuka akisimama na kububujikwa na machozi akimuomba Mungu "Nimebakwa nikielekea kwa ibada na wala sio kwa kilabu, sasa naomba unipe nguvu ya kuelekea kwenye ibada na kuendelea na maisha yangu"

Licha ya mbakaji huyo kumwibia fedha zake mwanamke huyu alipata ujasiri wa kumsogelea mhudumu mmoja wa boda boda ambaye alimsaidia. Wakati huu wote alikuwa anaficha sana kitu ambacho kilikuwa kimefanyika

Mwanadada huyu anasema kwamba halikuwa jambo rahisi kulieleza kwa wakuu wa kanisa lake hali kadhalika kwa kina dada ambao walikuwa swahiba zake wa karibu .

Kulingana naye hatua za haraka zilichukuliwa katika maandalizi ya kuwasilisha ripoti kwa kituo cha polisi na vilevile mchakato mzima wa kutafuta matibabu kutokana na maumivu aliyokuwa nayo.

Hatua zakusonga mbele baada ya Ubakaji

Hatua za kusonga mbele baada ya ubakaji , hazikuwa rahisi kulingana na jinsi mwanadada huyu anavyoelezea .

Princess anasema kwamba kwanza kukubali kwamba alikuwa amedhulumiwa kingono na mtu ambaye hakuwa anamfahamu lilikuwa tatizo kubwa na pili ni ndoto za kila siku kujiona akiwa kwenye mazingira ya mashambulizi hayo ya ubakaji yalijirudia kila mara kwa muda mrefu.

Hadi leo anasema kwamba yule aliyemtendea ukatili huo hajawahi kukamatwa ikiwa sasa ni miaka miwili baada ya kisa hicho.

Princess anasema kuwa imekuwa ni safari ya kila siku ya kutafuta kujisamamia , kujipenda na kujikubali .

Tangu tukio la kubakwa kwake Princess anasema kwamba kuna harufu na aina ya mavazi na mitindo ya nywele kwa wanaume ambayo hapendi kuiona na watu wengine.

Anasema kwamba yote hayo humkumbusha siku aliyobakwa .

Licha ya yote Princess anasema kwamba alipata ujasiri wa kujitokeza wazi kuzungumzia ulimwengu wa wanawake wanaobakwa ili simulizi yake iwe somo kwa watu wote hasa wanawake ambao wanaishi na makovu ya kubakwa.

Anasema waathiriwa wa ubakjaji wasiweke siri kitendo cha kubakwa kwani kina athari ya kuwapa karaha na machungu ya kila siku ambayo yamepelekea wengine kupata magonjwa na msongo wa mawazo