Kirusi Kipya cha Covid-19: Abiria13 kutoka Afrika Kusini wakutwa na maambukizi Uholanzi

Abiria kutoka Johannesburg wakisubiri majibu ya kipimo cha Covid-19

Chanzo cha picha, Reuters

Aina mpya ya virusi vya corona Omicron imegunduliwa kwa watu 13 waliofika katika mji mkuu wa Uholanzi Amsterdam kwa ndege mbili kutoka Afrika Kusini.

Ni miongoni mwa abiria 61 waliopimwa na kukutwa na virusi vya corona.

Hilo Iinakuja wakati vizuizi vikali vinapoanza kutumika nchini Uholanzi, huku kukiwa na rekodi za maambukizi ya Covid na wasiwasi juu ya aina mpya.

Hii ni pamoja na nyakati za kufunga mapema za kumbi za kitamaduni, na kudhibiti mikusanyiko ya watu wengi nyumbani.

Omicron iliripotiwa kwa mara ya kwanza na Afrika Kusini kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) siku ya Jumatano, na ushahidi wa mapema unaonesha kuwa kuna hatari kubwa ya maambukizi

Taasisi ya Kitaifa ya Uholanzi ya Afya ya Umma imetangaza Jumapili kuwa watu 13 wameambukizwa virusi aina ya Omicron , lakini ilibaini kuwa uchunguzi wake "bado haujakamilika", ikimaanisha kuwa aina mpya bado inaweza kupatikana katika sampuli zaidi za vipimo.

Waziri wa Afya wa Uholanzi Hugo de Jonge alitoa "ombi la dharura" kwa watu ambao wamerejea kutoka kusini mwa Afrika kupima Covid "haraka iwezekanavyo".

"Si jambo lisilofikirika kuwa kuna kesi zaidi nchini Uholanzi," aliwaambia waandishi wa habari.

Abiria ndani ya uwanja wa ndege wa Schiphol

Chanzo cha picha, Reuters

Maambukizi ya aina mpya ya virusi sasa yameripotiwa katika nchi kadhaa ulimwenguni, zikiwemo kadhaa za Ulaya, kama vile Uingereza, Ujerumani na Italia.

Ndege za shirika la kitaifa la Uholanzi KLM kutoka Johannesburg ziliwasili Ijumaa asubuhi. Abiria 600 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walizuiliwa kwa saa kadhaa baada ya kuwasili huku wakipimwa virusi hivyo.

Mwandishi wa New York Times Stephanie Nolen, ambaye alikuwa kwenye mojawapo ya ndege hizo, alitweet kwamba abiria hao hawakuletewa hata maji huku wakisalia ndani ya ndege.

Abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Afrika Kusini kuelekea Uingereza kupitia Amsterdam waliIambia BBC kwamba walizuiliwa kwenye lami katika uwanja wa ndege wa Schiphol kwa saa nne, kabla ya kushuka.

Abiria ambao walithibitishwa kuwa na Covid-19 tangu wakati huo wametengwa katika hoteli karibu na uwanja wa ndege wa Schiphol.

Wale waliopimwa na kukutwa hawana maambukizi wametakiwa kujitenga nyumbani kwa siku tano na kuchukua vipimo zaidi. Maafisa walisema wanaoendelea na safari wataruhusiwa kuendelea na safari zao, ingawa kulikuwa na ripoti Jumamosi kwamba baadhi ya abiria hawakupokea uthibitisho wa maandishi kuwa hawana maambukizi kwa hivyo hawakuweza kupanda ndege za kuendelea na safari.

Mamlaka ya afya ya Uholanzi pia ilikuwa ikijaribu kuwasiliana na maelfu ya abiria wengine ambao walikuwa wamesafiri kutoka nchi saba za kusini mwa Afrika - Afrika Kusini, Botswana, Eswatini, Lesotho, Msumbiji, Namibia au Zimbabwe - tangu Jumatatu.

Uholanzi ni mojawapo ya nchi nyingi duniani ambazo sasa zimeweka vikwazo vya usafiri kwa nchi za kusini mwa Afrika ili kukabiliana na kirusi hicho kipya.