G20: Tabia nchi, Covid ni ajenda kuu ya mkutano wa viongozi wa dunia

Mabadiliko ya tabia nchi na Covid ni ajenda kuu kwani viongozi kutoka nchi zenye uchumi mkubwa duniani wanakutana nchini Italia.

Ni mara ya kwanza kwa viongozi wa G20 kukutana ana kwa ana tangu kuanza kwa janga hili.

Hata hivyo, Xi Jinping wa China na Vladimir Putin wa Urusi hawatakuwa mjini Roma kwa ajili ya mkutano huo, badala yake watashiriki kwa njia ya video.

Mkutano huo unakuja huku kukiwa na onyo kali kwa siku zijazo ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Kundi hilo - linaloundwa na nchi 19 na Umoja wa Ulaya - linakadiriwa kuchangia 80% ya uzalishaji wa hewa ya ukaa duniani.

Akizungumza kabla ya mkutano wa kilele wa siku mbili, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kushindwa kuchukua hatua kungesababisha "ustaarabu wetu" kurudi nyuma, na kukabidhi "vizazi vijavyo maisha ambayo hayakubaliki sana kuliko yetu".

Hata hivyo, alikiri kwamba si mkutano wa G20, wala mkutano ujao wa COP26 mjini Glasgow, ambao unaanza Jumatatu, utakaosimamisha ongezeko la joto duniani, akisema "kitu kikubwa tunachoweza kutumaini kufanya ni kupunguza ongezeko hilo".

Kwamujibu wa shirika la habari la Reuters, taarifa ya pamoja inaelezea ahadi kutoka kwa G20 kufanya kazi katika kupunguza ongezeko la joto hadi 1.5C (2.7F) - lakini hakuna makubaliano ya kisheria yatafanywa.

Rasimu hiyo pia inaahidi kuchukua "hatua madhubuti" kukomesha ukataji haramu wa miti, uchimbaji haramu wa madini na biashara ya wanyamapori, inaripoti Reuters.

Bwana Johnson pia anatarajiwa kugusia ukosefu wa usawa wa chanjo ya virusi vya corona wakati wa mkutano huo, akiwaambia viongozi wenzake "kasi ya kupona itategemea jinsi tunavyoweza kushinda Covid", kipaumbele cha kwanza kikiwa "usambazaji wa haraka, na usawa wa usambazaji chanjo kimataifa".

Zaidi ya dozi bilioni sita za chanjo ya Covid zimetolewa duniani kote. Hata hivyo, barua iliyotumwa kwa Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi, ambaye ni mwenyeji wa G20, kutoka kwa zaidi ya viongozi 160 wa zamani wa dunia na takwimu za kimataifa ilibainisha ni 2% tu ya watu katika nchi za kipato cha chini wamepata chanjo.

Siku ya Jumamosi, Bw Draghi aliita tofauti hiyo "kutokubalika kimaadili". Alitoa wito kwa viongozi wenzake "kufanya kila tuwezalo" kuchanja asilimia 70 ya watu wote duniani kufikia katikati ya mwaka ujao.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Joe Biden atashinikiza nchi kuongeza uzalishaji wa nishati, wakati bei zikiwa juu, na pia kujadili mpango wa kuzuia milipuko ya siku zijazo. Pia anatazamiwa kukutana na Bw Johnson, pamoja na Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela anayeondoka wa Ujerumani Angela Merkel, kujadili kufufua mapatano ya nyuklia ya Iran.

Kundi hilo pia linatarajiwa kuidhinisha kiwango cha chini cha ushuru wa shirika duniani cha angalau 15%, ambacho kinaungwa mkono na nchi 140 kote ulimwenguni. Rasimu ya tamko hilo inataka iwepo kwa muda fulani mnamo 2023.