Waliokuwa wakitafuta wapenzi mtandaoni walaghaiwa karibu dola miliojni 7

Wanaume wanane wa Nigeria wanaotuhumiwa kwa kashfa ya ulaghai wa uchumba kupitia mtandao wameshtakiwa katika korti ya Afrika Kusini baada ya operesheni kubwa ya kimataifa iliyohusisha FBI na Interpol.

Mamlaka nchini Marekani ambapo uchunguzi ulianzia na kuna wahanga zaidi zimeomba wasafirishwe hadi nchini humo .

Wanadaiwa kulaghai zaidi ya wahasiriwa 100 karibu $ 7m (£ 5m) kwa jumla katika muongo mmoja uliopita.

Hawajatoa maoni juu ya mashtaka.

Ni ugunduzi mkubwa zaidi wa uhalifu huo wa ulaghai wa mapenzi kuwahi kupatikana nchini Afrika Kusini, kulingana na msemaji wa polisi Kanali Katlego Mogale.

Washukiwa hao, wenye umri kati ya miaka 33 na 52, walikamatwa Cape Town Jumanne kufuatia ombi la msaada wa kupambana nao kutoka Marekani

Inaaminika FBI na Secret service waliongoza uchunguzi na walifanya kazi na mamlaka ya Afrika Kusini, pamoja na kitengo maalum cha polisi, Hawks.

Wanaume hao wanatafutwa Texas na New Jersey kwa makosa mbali mbali pamoja na kula njama ya kufanya udanganyifu wa barua pepe, utakatishaji fedha na wizi wa utambulisho wa watu .

Akipinga kuachuliwa kwao kwa dhamana, mwendesha mashtaka Robin Lewis alidai wanaume hao wanachama wa genge la uhalifu kwa jina Black Axe , shirika la kimataifa la uhalifu uliopangwa kutoka Nigeria, ambalo hutekeleza uhalifu kama utakatishaji fedha kupitia akaunti ya za uwongo

Serikali ilisema wanaume hao wanaweza kukimbia kwa sababu bado wanazifikia akaunti wanazodaiwa kutumia.

Washukiwa wapo katika hatari ya kupewa kifungo cha miaka 20 jela ikiwa watahukumiwa.

Washukiwa walitunga 'visa vya kuhurumisha'

Inadaiwa walikutana na wahasiriwa wao kupitia tovuti za kuchumbiana kwa kutumia vitambulisho vya uwongo. Waathiriwa, mara nyingi wajane walio katika mazingira magumu au watu waliotalakiana ulimwenguni kote, walidhani walikuwa katika uhusiano wa kweli wa kimapenzi.

Kanali Mogale alisema mara tu watuhumiwa "walipokuwa wamejishughulisha na wahasiriwa wao, inasemekana walitunga hadithi za kilio juu ya kwanini wanahitaji pesa - yaani ushuru ili kutolewa urithi, safari muhimu ya nje ya nchi, deni linalodhoofisha, nk - na kisha wakachukua pesa kutoka kwa wahanga".

"Matapeli hao waliwatisha na kuwasingizia wahasiriwa wao, waliharibu maisha yao na kisha kutoweka," alisema.

Jirani wa washukiwa wawili, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, aliiambia BBC alishtuka kusikia ndugu hao wawili wanadaiwa kuwa wanachama wa genge la uhalifu la Nigeria.

"[Walikuwa] wenye urafiki na hawajawahi kuleta uhalifu wowote katika eneo hilo. Ndugu mmoja alikuwa ameomuoa raia wa Afrika Kusini," alisema.

"Mara moja kwa wiki takriban magari 10 ya kifahari yangewasili na kuondoka tena baada ya masaa machache. Haya yalikuwa magari ya kifahari zaidi kama Mercedes Benz ya 2021, Jeep na Ferrari. Jinsi walivyovaa unaweza kusema walikuwa matajiri."

Jirani huyo aliamshwa na sauti ya mbwa wakibweka wakati nyumba za ndugu hao zilipovamiwa Jumanne. Karibu wanaume 60 kutoka vitengo mbali mbali vya polisi walitumia karibu masaa sita kukusanya ushahidi katika nyumba zao . majumba mengine saba pia yalivamiwa katika mtaa huo.

Bwana Lewis alisema baadhi ya wanaume hao hawakuwa nchini Afrika Kusini kwa njia halali kwa kuwa hati zao za kusafiria zimekwisha muda. Pia alisema kuwa ikiwa wanaume hao wangeachiliwa kwa dhamana, wanaweza kudhoofisha ushahidi kwa njia ya kidigitali.

Ombi kamili la dhamana lilipangwa kusikizwa Jumanne na Alhamisi ijayo ili kusubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo.

TimeLive ya Afrika Kusini iliripoti Hawks walikuwa wakitafuta mtu wa tisa aliyehusishwa na kesi hiyo.