Miaka 20 ya Shambulio la Septemba 11: Siku Marekani ilipoanza kuishambulia Afghanistan

Agosti 30 vikosi vya mwisho mwa Marekani viliondoka katika ardhi ya Afghanistan na kuhitimisha vita virefu zaidi vya takribani miongo miwili nchini humo na vita virefu kuwahi kuendeshwa na taifa la Marekani.

Kuondoka pia kwa vikosi hivyo kumekamilisha ahadi ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyeaihidi kumaliza vita hivyo kwa kuondoa vikosi vya jeshi kutoka Kabul mpaka kufikia Agosti 30 2021, akisimamia pia makubaliano yaliyopita kuhusu hatua hiyo.

Kuondoka kwa Vikosi vya Marekani na washirika wake nchini Afghanistan, kumewarejesha madarakani kundi la Taliban ambalo mwaka 2001 takribani miaka 20 iliyopita lilifurushwa kwa Marekani walioanzisha vita kwenye ardhi ya Afghanistan na Iraq.

Ni vita iliyogharimu maisha ya watu wanaokadiriwa kufikia 160,000 na kwa mujibu wa Idara ya Ulinzi ya Marekani, kutoka Oktoba 2001 hadi Septemba 2019, taifa hilo lilikuwa limetumia wastani wa $ 800bilioni kwa ajili ya shughuli za kijeshi na zinazosaidia jeshi kwenye vita hiyo.. Lakini unaijua siku ya kwanza taifa hilo linaivamia hilo?

Oktoba 7, 2001

Siku hii ni ya kukumbukwa kwa raia wengi wa Afghanistan. Ni siku iliyoanza kutikisa maisha yao na usalama wao kwa miaka 20 mbele.

Uhakika wa kesho yao uligubikwa na mashaka makubwa kuanzia siku hii kutokana na mashambulizi yaliyoanzishwa na Marekani pamoja na washirika wake.

Ingawa kabla ya hapo paliwahi kuwa na vita, ghasia, vurugu, mapigano lakini hayakuwa ya muda mrefu na yaliyoathiri maisha ya raia wengi wala kutikisa sana maisha na usalama wa raia wa Afghanistan kwa muda mrefu.

Oktoba 7, 2001 ndio siku Marekani ilipoivamia Afghanistan iliyokuwa chini ya Taliban na kuanza mashambulizi kwa lengo la kuwaangamiza wanamgambo wa Taliban na Kundi la Al-Qaeda.

Kuanzia Oktoba 7, 2001 mpaka Agosti 30 2021, ni miaka 20, iliyojaaa damu, hofu, mashaka. Hakuna aliyetarajia ukumbwa wa mashambulizi yaliyoanza siku hii, ingawa hofu kiasi ya kuvamiwa ilionekana tangu Septemba 11, 2001 baada ya majengo mawili makubwa Marekani kushambuliwa.

Siku ya 'Vita dhidi ya Ugaidi'

Rais wa wakati huo George Bush wa Marekani alijitokeza hadharani na kutangaza kwamba Marekani imeanza vita dhidi ya ugaidi. Ilikuwa Oktoba 7, 2001 siku ambayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kurusha makombora na mabomu kulenga makazi na makambi ya Taliban na Al-qaeda.

Kwa mujibu wa Reuters, Rais Bush alizungumza kwa hisia na kuipa uzito siku hii kuelekea safari ya kupambana na ugaidi. Katika Hotuba yake kwenye Televisheni, Rais Bush alisema 'tunaungwa mkono na wengi duniani' na kuongeza 'leo tunajieekeza zaidi Afghanistan, lakini vita hii ni pana.

Kila nchi inapaswa kuchagua. Katika vita hii hakuna uwanja huru. Kama kuna serikali inadhamini watu wanaoua watu wasio na hatia, na wao wanakua wauaji, na watakuwa peke yao na kujiweka kwenye hatari', alisema Bush kwenye hotuba hiyo.

Siku hiyo hiyo Rais Bush akizungumza, Osama bin Laden, anayetajwa kuwa kiongozi wa Al qaedaaliyepanga na kuongoza mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani alitoa mkanda wa video fupi akianza kwa kusema

'Marekani imeshambuliwa na Mwenyezi Mungu kwa hyo ni jambo zuri, majengo yake muhimu yameporomoshwa. Neema na shukrani kwa mwenyejz Mungu', alisema Osama na kuongeza 'wanachojaribu kukifanya leo Marekani (kushambuli) wanaiga kile tulichofanya'.

Ilikuwa hotuba iliyochochea hasira zaidi kwa wamarekani. Rais Bush akatangaza dhamira ya Marekani ni kumpata Osama akiwa hai ama amekufa.

Jeshi la Marekani likaipachika vita hii kuanzia siku hiyo kwa jina la 'Operation Enduring Freedom', wakitaka iwe endelevu na ya muda mrefu, ili kupata dunia huru dhisi ys vitendo vya ugaidi.

Na kweli leo ni miaka 20 tangu uvamizi na mashambulizi ya Marekani yaanze nchini Afghanistan.

Nini kilitokea kabla ya siku hii?

Uvamizi wa Oktoba 7, 2001, usingekuwepo kama kusingetokea mashambulizi ya Septemba 11, 2001 yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 wengi wao ni wa Marekani wakiwemo wanajeshi na maafisa wa jeshi.

Ndege nne zilizotekwa na wanamgambo 19 wanaodaiwa kuwa sehemu ya kundi la Al-Qaeda walizitumia kuzibamiza kwenye majengo marefu nchini humo.

Ndege mbili zililenga majengo pacha ya kituo cha biashara Marekani, ndege moja ikalenga makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon na nyingine ilianguka huko Pennsylvania baada ya abiria kupambana na watekaji. Ndege hii ililenga kushambulia jengo la bunge la Capitol, huko Washington.

Baada ya shambulio hili, Marekani na baraza la usalama wla Umoja wa mataifa uliitaka Taliban waliokuwa wanashikilia sehemu kubwa ya Afghanistan tangu mwaka 1996 kumsalimisha Osama bin Laden kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka ya uhalifu.

Kundi hilo, likasema litamfikisha Osama kwenye mahakama zake za kijeshi mjini Kabul, na hakukuwa na haja ya kumpeleka Marekani ama kumtoa nchi ya taufa hilo kwenda kushitakiwa.

Majibu hayo hayakuiridhisha Marekani wala Umoja wa mataifa. Marekani ikafanya uamuzi na kuivamia ghafla Afghanistan Oktoba 7, 2001 kwa kushambulia kwa makombora makao ya Taliban na Al-Qaeda kwenye miji ya Kabul, Kandahar, Jalalabad, Kunduz na Mazar-e-Sharif.

Kwa sababu ni vita na vita haina taarifa, ughafla wa uvamizi wa Marekani ulileta taharuki kwa raia wa Afghanistan walioanza kuhamaki kuhusu maisha yao.

Hivyo zingine za washirika wa Marekani zilitumika kudondosha misaada ya kibinadamu ikiwemo vyakula kwa ajili ya raia hao waliokuwa wameanza kukimbia huku na kule kuokoa maisha yao.