Afghanistan: Fahamu maisha yalivyo nchini humo tangu Taliban ichukue madaraka?

Je! maisha yamekuaje kwa waliobaki nyuma wakati wanajeshi wa mwisho wa kigeni walioondoka nchini Afghanistan?

Watu wanne kutoka miji na majimbo kote nchini waliiambia BBC wamepoteza uhuru wao wa kimsingi na wanapitia kipindi kigumu wakijitahidi kusukuma gurudumu la maisha.

Baadhi ya majina yamebadilishwa kulinda usalama wa wachangiaji wa taarifa hii.

Mazar-i-Sharif

Mazar-i-Sharif ni jiji kubwa na kitovu cha uchumi kaskazini mwa Afghanistan, karibu na Tajikistan na Uzbekistan.

Na pia kuna wakati ulikuwa ngome ya serikali lakini uliangukia mikononi mwa Taliban mnamo 14 mwezi Agosti.

Majib alikuwa akifanya kazi mkahawani.

Sasa anapitia kipindi kigumu kupata chakula.

Katika mahojiano ya simu kwa njia ya video kutoka Mazar-i-Sharif, ameonyesha sakafu chafu ya jengo lililotelekezwa ambapo mablanketi machache yamerundikwa - kwa sasa ndio nyumba yake mpya.

Majib aliwasili jijini wiki chache tu zilizopita, mmoja kati ya zaidi ya watu nusu milioni ya Waafghan waliotoroka makazi yao mwaka huu kutokana na mzozo kati ya Taliban na vikosi vya serikali iliyoangushwa hivi karibuni.

Baba yake aliuawa na Taliban zaidi ya miaka 10 iliyopita, alisema.

Miaka kumi na baadaye, "anaogopa kutoka nje" kwasababu "wanapiga watu kila siku."

Picha kutoka kwa Mazar-i-Sharif wiki iliyopita zilionyesha Waafghan kadhaa waliokuwa wamebeba masanduku yao na kushikilia mifuko ya plastiki walipokuwa wakipanda mabasi kuelekea mji mkuu, Kabul, kwa matumaini ya kujaribu kuondoka.

Lakini katika siku chache zilizopita, tangu majeshi ya Marekani yalipoondoka, watu wengi wamekuwa wakiwasili kutoka Mazar-i-Sharif kutoka Kabul, Majib anasema - wakijaribu kuelekea mpakani na Uzbekistan kama njia ya kuondoka nchini humo.

Majib pia ana hamu sana ya kutoroka, lakini hajui ikiwa atafanikiwa.

"Taliban wako hapa na hawataki watu waondoke nchini" amesema.

Lashkar Gah, jimbo la Helmand

Mkoa wa Helmand kusini, ambapo wanajeshi wa Uingereza walikuwepo wakati wa vita, ulitwaliwa na Taliban Agosti 13.

Mji mkuu wa mkoa Lashkar Gah ulishuhudia mapigano makali katika wiki zilizotangulia.

Zilizobandikwa kwenye ubao wa matangazo wa ofisi ya Dkt. Viktor Urosevic ni mifuko midogo ya plastiki yenye risasi.

"Tunauita ukuta wenye aibu zetu" alisema, huku akiondoa mmoja kushikilia kamera kwenye mahojiano haya ya njia ya video.

Anasema nyingi zilikuwa risasi ambao zimetolewa kutoka kwa wagonjwa wenye umri mdogo.

Dkt. Urosevic anafanya kazi katika hospitali inayishughulikia wagonjwa wenye wasiwasi huko Lashkar Gah.

Sasa kwa kuwa mapigano yameisha, wadi hazijajaa tena kama ilivyokuwa wiki chache zilizopita.

Mabomu na risasi hayasikiki tena na mitaa imetulia.

"Ni ajabu sana, nimekuwa hapa kwa miaka michache, lakini hakujawahi kuwa kimya sana kiasi hiki," amesema.

"Ninauona ukimya kabla ya dhoruba, natumai nimekosea, lakini wacha tuone itakavyokuwa."

Majengo mengi yaliharibiwa kwa mabomu huko Lashkar Gah na familia zilizokimbia wakati wa mapigano zimerudi na kupata nyumba zao zikiwa magofu, Dkt. Urosevic alisema.

"Wanalala mbele ya msikiti, wanalala mitaani," alisema.

Hawana pesa za kujenga tena nyumba zao kwa hiyo, wengi wao wameishia kukosa makazi au kulazimishwa kukaa na jamaa zao."

Alisema familia nyingi katika eneo hilo wanaishi katika umaskini, wakihangaika kupata chakula wakati wa mchana.

Pamoja na benki zikiwa zimefungwa kwa siku nyingi, wanashindwa kufikia pesa na hayo yamezidisha matatizo.

Wafanyakazi wengi wa mashirika ya kigeni ya kutoa misaada ambao wangesambaza misaada ya aina hii waliondoka nchini wakati Taliban ilichukua madaraka.

Dkt. Urosevic, kutoka Serbia, ni miongoni mwa wale ambao waliamua kubaki nyuma.

"Tuna jukumu, sisi tu ndio kituo pekee kinachohangaikia mifadhaiko wanaopitia watu," amesema.

"Watu wanahitaji chakula, wanahitaji pesa, wanahitaji dawa.

Badakhshan

Moja ya mkoa masikini kabisa wa Afghanistan, Badakhshan, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, unaopakana na Tajikistan.

Taliban ilichukua udhibiti wa mji mkuu wake wa mkoa mnamo Agosti 11.

Abdul ni daktari huko Badakhshan.

Alikuwa mwanafunzi mara ya mwisho Taliban inaendesha nchi.

"Hali wakati huo ilikuwa mbaya sana na tabia zao ni sawa na ilivyokuwa zamani, " amesema.

"Sioni mabadiliko yoyote."

Abdul alitumia BBC picha kadhaa kutoka hospitali katika eneo ambalo sasa linalindwa na Taliban.

Katika moja ya picha, mvulana wa miezi 18 ambaye amekonda, amelala juu ya kitanda huku mama yake akiwa anaomba wafanyikazi wamuokoa.

Kulingana na Abdul, hakuwa na uwezo wa kumlisha.

"Siku hadi siku, watoto zaidi wanaendelea kupata utapiamlo,"alisema.

Kulingana na UN, zaidi ya nusu ya watoto chini ya miaka mitano nchini Afghanistan wanatarajiwa kuwa na utapiamlo mkali katika kipindi cha mwaka ujao.

Umaskini ulikuwa tayari ukweli kwa uhalisia wa mambo kwa wengi katika jimbo hili, lakini bei ya chakula na mafuta imepanda tangu Taliban walipoingia madarakani na wafanyikazi wa serikali wamepoteza ajira zao.

Wengine bado wanasubiri kulipwa kwa miezi michache iliyopita.

Abdul pia anahofia haki za wanawake katika jimbo hilo.

Wakati wafanyikazi wa tiba wa kike wameruhusiwa kufanya kazi, alisema wanawake wengine wengi hawajaruhusiwa kuendelea na kazi zao na wamebaki wakishangaa ni nini kitakachotokea mbeleni.

Wasichana walio juu ya darasa la 6 - zaidi ya umri wa shule ya upili Uingereza - hawaruhusiwi kwenda shuleni tena, Abdul alisema.

"Watu hawana matumaini yoyote kwa maisha yao ya baadaye," alisema.

"Hakuna fursa kwa watu huko Badakhshan."

Herat

Herat, mji wa Barabara ya biashara ya hariri karibu na mpaka na Iran, ulionekana kama moja wapo ya miji yenye uhuru zaidi na siku moja baada ya wanajeshi wa Merekani kuondoka, mamia ya wafuasi wa Taliban walijazaana mitaani. Wengine walibaki nyumbani kwa hofu.

Gul alikuwa amerudi kutoka sokoni alipozungumza na BBC.

"Kote kwenye soko kuu, Wataliban wamesimama na bunduki zao,", alisema.

"Huoni matajiri wengi au wanawake na wasichana mitaani sasa hivi kwasababu wote wanaogopa Taliban."

Mke wa Gul Afsoon sasa hawezi kutoka nje ya nyumbani kwao bila kuwa na mlinzi wa kiume na lazima avae burqua inayofunika uso wake.

"Hatma ya baadaye ya binti yangu haijulikani wazi," alisema.

Siku chache baadaye aliweza kurudi kazini pamoja na wanawake wengine, Gul amesema.

Lakini wanawake wengine wengi walikuwa bado nyumbani, alisema, bila uhakika kama wanaweza kuendelea na kazi za taaluma zao.

Gul na familia yake bado wanatarajia kuondoka Afghanistan.

"Tutakwenda popote pale," alisema. "Marekani, Ujerumani, Ufaransa. Popote."