Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gul Agha Sherjoy: Mfahamu mshirika mkubwa wa Marekani aliyepigana dhidi ya Taliban
Bulldozer kwa tafsiri ya kawaida ya Kiswahili ni tingatinga lenye nguvu na linalotumika katika shughuli nzito kama kuchimba, kuangusha miti kusawazisha eneo na mara nyingi yanatumika kwenye shughuli za ukandarasi ikiwemo ujenzi wa barabara. Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, aliwahi kupbatizwa jina hili.
Sasa wananchi wa Afghanistan au wote wanaofahamu siasa za Afghanistan na hali ya mambo yalivyo katika kipindi cha miaka 20 iliyopita watakuwa wanamjua vyema 'Bulldozer' ama tingatinga wa Afghanistan ni nani.
Alikuwa upande wa serikali iliyoangushwa na kundi la Taliban lakini sasa 'bulldozer' hayuko tena upande wa afghanistan, amejiunga na Kundi hilo ambalo sasa bulldozer' ni Taliban na Taliban ni bulldozer.
Gul Agha Sherzai, ni afisa wa zamani wa shirika la kijasusi la Marekani, CIA na mbabe wa kivita anayejulikana kama 'bulldozer na watu wengi wa Afghanistan. Aliwahi pia kuhudumu kama gavana wa Kandahar na Nangarhar.
Ameapa Jumapili hii kuweka imani yake kwa kundi la Taliban huku kundi hilo likitangaza kwamba Gul Agha Sherzai amekuwa sehemu ya serikali yao.
Mwaka 2001, Marekani iliongoza vikosi vya NATO. Gul Agha Sherzai akawa mbabe wa vita wa kwanza kuiunga mkono Marekani alipoishambulia Afghanistan ili kuwafurusha Taliban.
Huko Kusini mwa jimbo la Kandahar, alipambana na Taliban akiwa na CIA.
Alikuwa gavana wa jimbo la Kandahar kabla ya Taliban kuingia madarakani kwa mara ya kwanza Afghanistan. Sherzai akatimka mpaka Taliban walipofurushwa madarakani na Marekani mwaka 2001.
Baada ya Taliban kuondolewa mamlakani nchini Afghanistan, Sherzai akarudi Kandahar na kuendelea na wadhifa wake wa ugavana.
Sherzai amekuwa mtu wa karibu na CIA na rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai. Ndio maana alikuwa gavana wa Kandahar mpaka 2003 baada ya kuondoshwa madarakani kwa serikali ya Taliban nchini Afghanistan. Baadae akawa gavana wa Nangarhar.
Jina la bulldozer lilitoka wapi?
Rafiki yake wa karibu aliwahi kusema Sherzai alilipata jina la Bulldozer huko Nangarhar, alipokuwa gavana kati ya mwaka 2005 mpaka 2013.
Wakati wa uongozi wake kama gavana, Gul Agha Sherzai alikuwa akipenda sana kutembelea maeneo ya ndani kabisa ya vijijini kwenye jimbo hilo Nangarhar.
Wananchi wa maeneo hayo walimtaka atengeneze barabara, kwa sababu ya mazingira magumu yaliyokuwepo ya uhaba wa barabara, au zilizokuwepo duni kufungwa.
Sherzai hakuahidi tu kushughulikia matatizo yao, lakini ujenzi wa barabara ukaanza mara moja katika maeneo hayo ya vijijini.
Akiwa anatembelea vijijini Gavana Sherzai mara kadhaa akawa anagawa pesa na mashine. Akiulizwa wakati wa ziara yake kuhusu ubovu au kutokuwepo kwa barabara , mara moja alileta bulldozer na baadhi ya mashine bila kuchelewa na barabara zikaanza kuchezwa.
Gul Agha Sherzai alikua anamiliki pia kampuni ya ujenzi wa barabara na bulldozer la kampuni yake lilikuwa linatumika mara kwa mara. Kuanzia kila mtu nchini humo akaanza kumuita 'bulldozer'.
Pamoja na kuitwa hivyo, Gul Agha Sherzai alikuwa hatakiwi kujiita jina hilo.
Gul Agha Sherzai ni mmoja wa waliokuwa maadui wakubwa wa Taliban. Alikuwa anajulikana kama 'Taliban Butcher'. Wakati Taliban walivyofurushwa nchini humo na Mrekani mwaka 2001, aliwaua wataliban na wapiganaji wengi wa al-Qaeda.
Sherzai ni mpenda muziki
Agha Sherzai, maarufu kama bulldozer wa afghanistan, pia amekuwa akipenda muziki na kuimba baadhi ya nyimbo mara kadhaa , rafiki yake wa karibu anasema.
Miaka michache iliyopita wimbo wake wa "Raka Jam Raka Jam" ulisambaa na kushika vichwa vya habari.
Wimbo huu wa lugha ya 'pashto' unapendwa na wengi. Hata hivyo, rafiki yake anasema wakati Sherzai alipokuwa gavana wa Nangarhar, alikuwa anapenda kwenda mahali mbali kabisa ya mji akitumia gari ambalo haliingii risasi huku akiimba nyimbo mbalimbali na alikuwa akiuliza kama anaimba vizuri ama la.
Taliban sasa imekuwa 'bulldozer'
Katika video iliyowekwa kwenye mtandao mmoja wa wafuasi wa Taliban , ikimuonyesha Gul Agha Sherzai akiapa kuwa mwaminifu na kujenga Imani kwa kiongozi wa Taliban Khalilir Rahman Haqqani.
Kabla ya tukio hilo, Gul Agha Sherzai, alionekana awali akiwasalimu wataliban kupitia video walipokusanyika Kabul, kumpokea.
Katika video iliyotolewa na Taliban, Mufti Zakir, mmoja wa wanazi wa kundi hilo alisikika kwa sauti akisema Sherzai anaitwa bulldozer wa Afghanistan. Akijibu hilo, Sherzai alisema ndio.
"Yuko vile vile. Atakuwa bulldozer wetu, kama Islamic Emirate, ambaye ataijenga nchi yote ya Afghanistan kwa niaba ya Amir-ul-Mominin," mufti Zakir alisikika akisema.
Baada ya hapo Gul Agha Sherzai, Khalilir Rahman Hakkani, viongozi wa Taliban na watu wengine walisikika wakisema 'Insha Allah, kwa maana isiyo rasmi ya 'kwa mapenzi yake Mola'.
Viongozi wa Taliban walitangaza awali kwamba kwa sasa hawana uadui na kiongozi yeyote wa kisiasa na wamewasamehe wanasiasa wote wa Afghanistan.
Hata hivyo, kuna tuhuma kwamba kundi hilo la Taliban limewaua viongozi wengi wa kisiasa ambao walijisalimisha kwao. Taliban wamepinga tuhuma hizo.