Uchaguzi wa Zambia 2021: Fahamu kwa nini wapiga kura wa Zambia wamemng’oa rais wao madarakani

    • Author, Mohammed Abdulrahman
    • Nafasi, Mchambuzi

Wapiga kura nchini Zambia wameamua kuchagua mabadiliko na kumpa ushindi mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa rais dhidi ya rais aliyeko madarakani Edgar Lungu.

Ni uchaguzi wa 7 tangu nchi hiyo iliporudi katika siasa za vyama vingi 1991. Akigombea kwa mara ya 6 ni ushindi mnono kwa Hichilema,kiongozi wa United Party for National Development (UPND) aliyenyakua kura 2,810,75 dhidi ya 1,814,201 za Lungu wa chama tawala Patriotic Front (PF). Hichilema aliungwa mkono na vyama 10 vya upinzani.

Zambia imeshuhudia mabadiliko mara tatu ambapo viongozi walioko madarakani wanaondolewa na wapinzani. Alimtangulia rais wa kwanza na baba wa uhuru wa taifa hilo Kenneth Kaunda aliyeshindwa na Frederick Chiluba katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1991.

Kaunda aliitawala Zambia miaka 27, chini ya mfumo wa chama kimoja, chama chake cha United National Independent Party (UNIP). Waliofuata baada ya Chiluba walikuwa Levy Mwanawasa, Rupiah Banda, Michael Sata, Guy Scott na Edgar Lungu.

Scott mzaliwa wa Zambia mwenye asili ya kizungu aliyekuwa makamu wa rais, alitawala kama rais wa mpito 2014 hadi Januari 2015 baada ya kifo cha Michael Sata.

Taifa hilo la kusini mwa Afrika limekuwa na misukosuko katika zoezi la kujenga demokrasia, lakini misukosuko hiyo haikuhujumu azma yake ya kufuata njia hiyo.

Hata hivyo kitisho cha kulirudisha nyuma gurudumu hilo, kilijitokeza alipoingia madarakani Edgar Lungu, baada ya kuchukua uongozi wa chama chake Patriotic Front (PF) na kushinda uchaguziwa rais 2016 , miaka miwili baada ya kifo cha rais Michael Sata.

Lungu alianza hatua za kuikandamiza demokrasia akiwaandama wapinzani na kuziwekea vizuizi shughuli zao.

Msukosuko wa kidemokrasia

Katika ripoti yake kuhusu hali ya kisiasa nchini Zambia ilioitoa Juni 2021, Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu-Amnesty International, lilisema uhuru wa kutoa maoni na mkusanyiko wa amani wa raia ni mambo ambayo yalizidi kukandamizwa na utawala wa Lungu katika kipindi cha miaka mitano iliopita.

Vile Vile viongozi wa upinzani na wanaharakati kukamatwa na kuwekwa ndani na vyombo huru vya Habari kufungwa.

Hatua kali dhidi ya wapinzani hazikumwacha kando kiongozi wa UPND Hichilema aliyebughudhiwa mara kwa mara na polisi, akikamtwa na kuhojiwa.

Hachilema alishashindana na Lungu mara mbili na kushindwa kwa idadi ndogo tu ya kura.

Wazambia wakihofia kundelea kwa Lungu kusalia madarakani kungeweza sio tu kuidhoofisha zaidi demokrasia katika taifa hilo, bali pia kujenga mazingira ya kuwa na kiongozi mwenye mwelekeo wa kidikteta na hali ya uchumi kuwa mbaya zaidi, ikiandamana na ukosefu mkubwa wa ajira hasa kwa vijana.

Kuchaguliwa Hachilema, mfanya biashara tajiri mwenye umri wa miaka 59, kunatokana na wapiga kura kuamua wakati wa mabadiliko umewadia, mabadiliko ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura, wengi wakiwa vijana.

Katika mazingira hayo ya uchaguzi, kulikuweko pia na wasiwasi kwamba huenda Tume ya Uchaguzi ingetumbukia kwenye ushawishi wa serikali na kutowajibika.

Kuna waliofikiria kingejitokeza kile kinachoshuhudiwa katika nchi nyengine jirani za kanda hiyo na hasa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Miongoni mwa matukio katika nchi ambako Tume zinaelekea zimeelemea utawala ni katika chaguzi nchini Zimbabwe na Tanzania, ambako zoezi baya zaidi katika historia ya taifa hilo tangu kurejea kwa siasa za vyama vingi 1992, ilikuwa katika uchaguzi wa Oktoba 2020.

Wasiwasi mwengine wakati Wazambia walipokuwa wakipiga kura ulikuwa ni kujiingiza kwa jeshi. Lungu alivitumia vyombo vya dola, polisi na jeshi kukandamiza kile alichokiita ghasia za wapinzani. Kinyume na wasiwasi huo, Polisi na Jeshi walijikita katika kusimamia utulivu na usalama na kuhakikisha Wazambia wanapiga kura bila vitisho.

Katika baadhi ya matukio, polisi waliwakamata wasimamizi wadogo wa tume ya uchaguzi waliokuwa wakijaribu kubadilisha matokeo katika vituo vya kupigia kura kwa niaba ya chama tawala PF.

Hatua ya Lungu kutuma wanajeshi katika mikoa miwili hazikufua dafu. Katika kile kinachoonekana ni kufedheheshwa na matokeo ambayo hakuyatarajia, Lungu mwenye umri wa miaka 64, alidai uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Zambia yaendelea kuonesha njia

Kwa mara nyengine tena Zambia imeonesha njia panapohusika na utekelezaji wa demokrasia hasa katika nchi jirani kusini mwa Afrika. Inajiunga na jirani yake wa karibu Malawi ambayo wakati wa ukoloni zilikuwa chini ya kile kilichojulikana kama Shirikisho la Nyasaland, lililovunjika muda mfupi kabla ya nchi hizo kuwa huru.

Zambia ikijulikana kama Rhodesia ya Kaskazini na Malawi, ikiitwa Nyasaland. Zote zilibadili majina baada ya uhuru.

Demokrasia nchini Malawi ilianza kushamiri baada ya rais wake wa kwanza Dr Hastings Kamuzu Banda, aliyetawala kwa mkono wa chuma kushindwa na mgombea wa upinzani Bakili Muluzi. Muluzi alifuatiwa na Bingu wa Mutharika, Joyce Banda, Peter Mudharika na Lazarus Chakwera aliyemshinda Peter Mutharika katika uchaguzi wa 2020.

Joyce Banda alikuwa Rais wa pili mwanamke barani Afrika alipochukua uongozi wa taifa hilo 2012-2014, kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.

Mtihani atakaokabiliana nao Rais mteule Hachilema baada ya kuapishwa na kuanza kazi, ni kuwatatulia Wazambia hali ngumu ya kiuchumi, sababu moja wapo iliomuangusha Lungu.

Kipindi cha miaka mitano iliopita, kilishuhudia serikali ikijiingiza katika ujenzi wa miradi fahari ikiwemo miundombinu mikubwa ambapo fedha nyingi zilitumika na kusahau umuhimu pia wa kuwaondoa raia katika hali ngumu ya maisha.

Hichilema marufu kama "HH", ametoa wito wa amani akisema," Tumechagua mabaduiliko ili tuwe na Zambia ilio bora." Aliwataka wananchi wenzake kuendeleza moyo wa Ubuntu (Utu), upendo na kuishi pamoja kwa furaha.

Pamoja na mabadiliko ya uongozi nchini Zambia yanaashiria kwamba njia bado ni ndefu katika utekelezaji wa demokrasia na utawala bora barani Afrika, licha ya kuweko mabadiliko ya kutia moyo katika nchi nyengine kama Kenya, Senegal, Nigeria, Ghana na visiwa vya Cape Verde.

Yaliotokea Zambia bila shaka sio tu ni ushindi kwa wananchi wa nchi hiyo, bali kwa wote wanaopigania demokrasia barani Afrika kwa jumla. Pia ni ujumbe uliowazi kwa wanaoikandamiza demokrasia hiyo kwamba hakuna kinachodumu milele. Vyama na viongozi wapo na wataondoka, lakini taifa linabaki na taifa ni watu.

Watu hao wanahaki ya kuona maamuzi yao ambayo ni haki yao ya kuzaliwa yanaheshimiwa kwa ajili ya mustakbali wao na wa taifa lao. Upepo wa mabadiliko barani Afrika ulioanza mapema miaka ya 1990, unaendelea kupiga, licha ya wengine kujaribu kurudisha nyuma