Kuanzia kunusa makwapa hadi kusukuma wasafiri, hizi ni baadhi ya ajira za zinazotajwa kuwa za 'ajabu' duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati tatizo la ajira likiendelea kuongezeka duniani, baadhi ya watu wamekuwa wakifikiria na kubuni ajira mbalimbali. Hata hivyo kuna ajira ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu ambazo huwapatia watu kipato cha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Kwa baadhi ajira hizi zimeonekana kuwa sio za kawaida. Lakini kama Waswahili wasemavyo, kazi ni kazi ilimradi mkono uingie kinywani. Je unaweza kufayanya kazi hizi?
Kunusa kwapa ili kutambua ufanisi wa manukato
Kama una kipaji cha kunusa nusa na kutambua harufu, basi huenda kazi hii inakufaa. Katika kazi hii wenye uwezo wa kunusa makwapa ya watu kubaini nguvu za manukato ya deodorant au aina nyingine za manukato kwa kukabiliana na harufu ya jasho la kwapani basi kazi hii inakufaa. Ukifanya kazi hii itakubidi kunusa aina mbali mbali za manukato na kutoa ushauri kwa wenye viwanda endapo kuna marekebisho yanayohitajika ili kukidhi viwango hitajika vya manukato
Kazi ya msukumaji wa watu ndani ya treni

Chanzo cha picha, Getty Images
Kazi hii inapatikana nchini Japan kutokana umati unaokwenda kazini nyakati za asubuhi kwa kutumia usafiri wa treni. Japan ni taifa linalochapa kazi, na huhakikisha kila mtu anafika kazini kwa wakati unaotakiwa. Kutokana na wingi wa watu, Japan imewaajiri watu wenye taaluma ya kuwasukuma watu ndani ya treni wakati kuna msongamano ili pasiwe na mtu hata mmoja wa kuchelewa kazini.
Wasukumaji hawa wakati mwingine hulazimika kuwasukuma ndani ya treni wasafiri ambao huchelewa kupanda treni au wakati wanapositasita kupanda kwa madai kwamba treni imejaa. Wanaotaka kazi hii wanatakiwa kuvaa sare nyeupe na glovu nyeupe na watatakiwa kufanya kazi hiyo kati ya saa moja na saa tatu asubuhi, kisha saa moja jioni hadi saa tatu usiku .
Kazi hiyo huchukuliwa kama kama kazi ya ziada na mara nyingi hufanywa na wanafunzi na mshahara haufahamiki.
Rafiki wa kiume (Boyfriend) wa kukodisha
Mjini Tokyo, kama una pesa, kumpata rafiki wa kiume ni rahisi sana. Ni jambo linalowashangaza wengi, lakini hii ni kazi na inafanyika.
3. Kazi ya kusimama kwenye mstari wa kungojea huduma

Chanzo cha picha, Getty Images
Kila mahali penye misururu mirefu ya kupata huduma basi wapo wanaopata ajira. Nchini Japan wapo watu ambao wanakuwa tayari kusubiri kwenye mstari mreefu kwa ajili yao ili mradi utawalipa pesa kidogo. Malipo yao hutegemewa maelewano kati ya msimamaji na aliyepewa huduma ya kusimamiwa kwenye msururu.
Kazi ya kunusa karatasi za usafi za choo

Chanzo cha picha, Getty Images
Watengenezaji wa karatasi za choo huwa makini sana kuhakikisha karatasi hizo hazina harufu mbaya kabla na baada ya kutumiwa. Katika viwanda vya kutengeneza karatasi hizi watu mahsusi huajiriwa kwa ajili ya kunusa harufu ya karatasi hizi mara baada ya kutengenezwa na baada ya kutumiwa kabla ya kuziweka sokoni au madukani. Mwenye kazi hii hutoa ushauri wa maboresho iwapo unahitajika hususan pale anapogundua kuwa karatasi hizi zinatoa harufu mbaya kabla ya kutumiwa au hata baada ya kutumiwa.
Kazi ya mtaalamu wa kusinzia
Huenda ukajiuliza , ala! Kusinzia nayo ni kazi ya kulipwa?. Ndio ni kweli unaweza kulipwa kwa kusinzia ... Kulala fofofo, baada ya kupewa dozi ya dawa huku wanasayansi wakifanya utafiti juu ya matatizo ya kulala. Bila shaka kazi hii huenda ikawa kazi rahisi zaidi duniani
Kazi ya kusafisha matapishi (Vomit Cleaner)
Katika mataifa mengi ya magharibi kazi hii ni ajira na mara nyingi hufanyika katika maeneo ya umma. Sio kila mtu anayeifanya bali ni yule mwenye taaluma hii. Unapotaka kazi hii basi itabidi uende kwenye maeneo ya umma hususan katika bustani ambapo watu huenda kujipumzisha na wakiwa na familia zao na watoto, ukisubiri ''ajali'' ya kutapika itokee. Wamilikiwa maeneo ya burudani huwatafuta wenye uwezo wa kufanya kazi hii. Swali ni je unaweza kuifanya?
Kazi ya utambuzi wa jinsia ya kuku -Chicken Sexer

Chanzo cha picha, Getty Images
Kazi ya utambuzi wa jinsia ya kuku inahusisha kubaini kifaranga cha kuku ni jinsia ya kike au ya kiume. Baraza la kuku la Uingereza mwaka jana lilitangaza kuwa na upungufu wa Watambuzi wa jinsia za kuku, licha ya kwamba likuwa tayari kutoa malipo ya pauni 40,000 kwa mwaka kwa mtu anayefanya kazi hii. Hii inamaanisha ajira hii ipo nchini uingereza.
Kwa wale wanaoomba kazi hii hutakiwa kuwa wamemaliza mafunzo maalumu ya miaka mitatu, ili kuweza kufanya kazi yao ipasavyo.
Kazi ya kukumbatia
Nchini Japan iwapo utamkosa rafiki yako wa kike wa kumkumbatia basi unaweza kumpata rafiki mbadala. Unaweza kutoa pesa kiasi na kumpata mwanamke wa kulala kando yako. Na mwanamke huyu ni wa kukukumbatia pekee.
Kazi ya kuzuia namba za magari zisionekane

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika juhudi za kuzuia msongamano wa magari barabarani, Iran imeweka sera ya ajabu ambapo magari yenye namba za magari zinazoishia na Uwitiri na shufwa zinaruhusiwa kuingia barabarani kwa kupishana siku tofauti. Kutokana na hilo Wairan huwakodisha wanaume wanaotembea nyuma ya magari yao ili kamera za barabarani CCTV zisinase namba zao wanapokiuka sheria hiyo.
Kazi ya kuomboleza misibani

Chanzo cha picha, Getty Images
Kazi hii imeshika kasi katika maeneo mbali mbali ya dunia. Kama unaweza kulia bila hata kumfahamu marehemu, wala ndugu zake kwa huzuni na kwikwi, basi kazi hii inakuhusu. Japokuwa inaonekana kama kazi ya ajabu kwa baadhi ya watu ni kazi kama kazi nyingine. Vijana wengi wamejipatia ajira hii hata katika mataifa ya Afrika kama vile Kenya na Nigeria.
Wasemao husema mchagua jembe si mkulima…Japo kazi hizi zinaonekana kwa baadhi kuwa sio za kawaida, kwa wanaozifanya ni kazi tu na zina walisha na kuwawezesha kuzitunza familia zao na kukidhi mahitaji yao hasa ya kimsingi.












