Siku 100 za Rais Samia Suluhu: Jinsi serikali ya Muungano inaathiri utendaji wa serikali ya Zanzibar

Samia na Mwinyi

Chanzo cha picha, CCM

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Kwa sababu ya Muungano wa miaka 57 ulioundwa na nchi mbili za Zanzibar na Tanganyika. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), hushirikiana katika mambo kadhaa.

Pia, kuna yale ambayo hayahesabiwi kama mambo ya Muungano, serikali ya Zanzibar kwa upande wake huyasimamia yenyewe. Ingawa kwa kuwa serikali hiyo imekosa meno kamili ya kiutawala. Hujikuta inafuata nyuma ya sera za serikali ya Muungano hata kwa mambo ambayo hayahusu Muungano.

Lakini si kila wakati Zanzibar inaathirika katika namna hasi kwa kuwa mfuataji. Zipo nyakati ambazo kuathirika kwake ni kwa namna nzuri. Hivyo huathirika vibaya au vizuri kutegemeana na hali ya mambo.

Vita dhidi ya Corona

Wakati janga la Corona linaikumba dunia. Serikali ya Rais Magufuli ilikuwa mstari wa mbele kuipa dunia takwimu za mwenendo wa ugonjwa huo nchini. Idadi ya walioambukizwa, waliopona na idadi ya vifo.

Kwa upande wa Zanzibar takwimu kama hizo zilikuwa zinatolewa vilevile. Hii ni kwa sababu swala la afya haliko katika orodha ya mambo ya Muungano. Zanzibar inasimamia yenyewe sekta ya afya.

Mwezi Aprili 2020, ndio ulikuwa mwezi wa mwisho kwa Tanzania kuweka wazi takwimu zake za corona. Takwimu za mwisho zilionesha ina wagonjwa 480, vifo 16 na watu 167 wamepona.

Rais Magufuli alipobadili sera na kuzuia takwimu za corona, sanjari na kupuuza hatua za kujikinga zilizokuwa zikishauriwa na wataalamu afya. Na Zanzibar sera zikabadilika vilevile. Takwimu za corona hazikutolewa tena.

Rais

Chanzo cha picha, EPA

Baada ya mabadiliko hayo Zanzibar iligeuka na kuwa pepo ya watalii kutoka mataifa ya Ulaya. Walijazana na kuzajana kwa sababu hakukuwa na vikwazo vyovyote wakati wa kuingia.

Baada ya Rais Magufuli kufariki. Ndani ya siku mia za utawala wa Rais Samia Suluhu amekuja na sera tofauti kuhusu corona, kwa sasa anahimiza kujilinda kwa kuvaa barakao.

Aliunda tume ambayo ilitoa mapendekezo. Na serikali yake imekubali kuyafuata. Moja ya mapendekezo hayo ni kukubali kupokea chanjo ya corona.

Rais Samia anaamini ukitaka kufika mbali uende na wenzako. Serikali yake imekubali kwenda na dunia katika mapambano dhidi ya corona.

Serikali ya Zanzibar nayo imefuata mkia. Rais Mwinyi ameonekana mara kadhaa akiwa na barakoa, na amekiri uwepo wa janga hilo visiwani. Fauka ya hayo, Zanzibar iko tayari kupokea chanjo ya corona.

Kesi ya Uamsho

Baada ya takribani miaka nane kizuizini, washitakiwa maarufu kwa jina la Masheikh Wa Uamsho wameachiwa huru wiki hii baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwafutia mashitaka ya ugaidi.

Miaka nane bila ya kesi hiyo kupata ushahidi, imeongeza uzito yale maadai ya baadhi ya Watanzania kwamba watu hao walishikiliwa kwa sababu za kisiasa.

Mara tu baada ya kuingia madarakani Rais Samia alikemea hadharani kesi za kubambika na kutaka mamlaka zilizo chini yake kufuta mashtaka yote ya aina hiyo.

Masheikh

Chanzo cha picha, THE CITIZEN/TWITTER

Harakati za mashekhe hao dhidi ya Muungano zilipata umaarufu visiwani Zanzibar katika ya mwaka 2011 na 2012. Waliendesha kampeni ya kudai mamlaka kamili ya visiwa hivyo.

Zanzibar ina mahakama yake ambayo ina uwezo wa kuendesha kesi ambayo ilikuwa inawakabili. Swali la msingi, kwanini walihamishiwa Tanzania bara? Je, Mahakama ya Zanzibar iliporwa haki na Tanzania bara kuendesha kesi hiyo?

Wakati huu ambao Masheikh hao wapo nje, mjadala muhimu pia ni kuhusu nguvu ya Zanzibar kuendesha kesi za watuhumiwa wake bila kuhamishiwa bara.

Uwazi na Uwajibishwaji

Kwa miaka mingi utendaji wa watumishi wa umma Zanzibar ulikuwa ni wa kimazoea. Hakukuwa na uwajibishwaji wala uwazi. Hakukuwa na ripoti kutoka Ikulu za kusimamishwa kazi au kuenguliwa nafasi zao watumishi ambao hufanya ufisadi.

Kwa sasa mambo yamebadilika, watumishi wanawajibishwa, kuenguliwa ama kusimamishwa ili kuchunguzwa. Hata watumishi katika nyadhifa nyeti wamejikuta wakipigwa panga.

Mwezi Aprili mwaka huu, Rais Hussein Mwinyi alitengua uteuzi wa makamanda wakuu wa vikosi vitatu vya SMZ, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Chuo cha Mafunzo.

Utumbuaji huo ulikuja baada ya Rais kupokea ripoti kutoka kamati ya uchunguzi, iliyobaini uwepo wa wafanyakazi hewa, ubadhirifu na ufisadi katika idara hizo za SMZ.

Hussein Mwinyi

Chanzo cha picha, Getty Images

Pia kumekuwa na uwazi mkubwa katika mambo mengi. Mwezi Mei, Rais Mwinyi alipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali mbele ya kamera. Katika tawala zilizopita ripoti hii mara nyingi ilikuwa siri, haikuwa inatolewa hadharani na kumfanya kila mtu asikie mazuri na maovu yaliyomo katika taasisi mbali mbali.

Utendaji wa aina hii uliasisiwa na mwendazake John Pombe Magufuli kwa upande wa Tanzania bara. Rais Mwinyi anaonekana kufuata nyayo hizo hizo kwa upande wa Zanzibar.

Rais Samia Suluhu Hassan nae anaendeleza utendaji wa aina hiyo. Siku mia za utawala wake, zimekuja na kuwaondoa na kusimamisha kazi watendaji kadhaa wa serikali yake.

Uhusiano wa vyombo vya habari na utawala

Hayati Magufuli hakuwa na uhusiano rafiki na vyombo vya habari. Hofu ilishamiri, vyombo vilifungiwa, vilipigwa faini. Na uhuru wa kukosoa utawala ukakosekana.

Siku mia za utawala wa sasa zimepunguza makali. Vyombo vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa. Na bado hakujaripotiwa kauli yenye kuashiria vitisho kwa vyombo vya habari, kutoka Rais Samia au watumishi wa serikali.

Vyombo vya habari vimepata nafuu kwa upande wa Zanzibar pia. Serikali inahimiza ofisi za umma kutoa ushirikiano kwa kuwapa taarifa waandishi wanapofika katika ofisi hizo.

Kuna tukio la mwandishi wa gazeti la Mwananchi kupigwa na maafisa wa vikosi vya SMZ, Serikali ya Zanzibar iliomba radhi kupitia Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ na Wizara ya Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo.

Pia, waliohusika na shambulio hilo, Wizara inayohusika na vikosi vya SMZ ilieleza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa wanaoelewa utendaji wa SMZ, kuomba radhi mwandishi na kuchukua hatua dhidi ya maafisa wake, ni hatua ambayo haikuzoeleka. Iliashiria mabadiliko makubwa katika utawala wa sasa na vyombo vya habari.

Kauli ya Rais Samia alipokuwa akihutubia vijana mkoani Mwanza wiki hii, inaashiria uwepo wa ahueni si tu katika vyombo vya habari bali pia mitandao ya kijamii.

Rais Samia alisema, "tumieni mitandao vizuri, kama una jambo la kulaumu, laumu na toa ushauri. Kama unakosoa, kosoa na toa mapendekezo nini kifanyike."

Hapa ni kusema kuwa kila mambo yakiharibika upande wa Serikali ya Muungano, yanaharibika vilevile upande wa Zanzibar. Na yakitengemaa upande wa Muungano hutengemaa pia katika utawala wa Zanzibar.