Abubakar Shekau: Mambo 5 yanayothibitisha kifo cha kiongozi wa Boko Haram aliyeogopwa

Kiongozi wa Boko Haram aliuawa yapata wiki mbili zilizopita
Maelezo ya picha, Kiongozi wa Boko Haram aliuawa yapata wiki mbili zilizopita

Kuna sababu zinazojitokeza wiki hii zaidi na zaidi za kuthibitisha taarifa zilizodai kuwa kiongozi wa Boko Haramu Abubakar Shekau aliuawa .

Hatahivyo, Boko Haram na serikali ya Nigeria hawajathibitisha kifo cha Shekau, ambaye anasakwa na jeshi la Nigeria pamoja na lile la Marekani .

BBC imezungumza na Barrister Bulama Bukarti, mtaalamu wa usalama na afisa katika kituo cha utafiti cha Tony Blair nchini Uingereza, kuhusu sababu kuu tano zinaonesha kuwa kiongozi wa Boko Haram amefariki.

Kuingiliwa kwa mawasiliano ya simu ya makamanda wa ISWAP

Mtaalamu anasema sababu ya kwanza ilikuwa ni jinsi taarifa ya kifo cha Shekau ilivyotangzwa kwa mara ya kwanza.

Na taarifa ilitoka kwanza katika baadhi ya magazeti ya Nigeria ambayo yalikuwa na uhusiano na wanamgambo nchini pamoja na vikosi vya usalama vya Nigeria.

Katika waraka uliotangaza taarifa ya kifo chake, magazeti yalionesha jinshi vikosi vya usalama vilivyoweza kuingilia mawasiliano ya simu ya makamanda wa ISWAP na kuwaambia jinsi walivyokwenda na kumuua Shekau.

Magazeti yenye uhusiano wa karibu na Boko Haram na ISWAP

Mtaalamu wa usalama anasema sababu ya pili ilikuwa ni kuthibitishwa kwa taarifa hiyo kwa baadhi ya magazeti yenye uhusiano wa karibu na vuguvugu la Boko Haram la Shekau na ISWAP.

Anasema walikuwa wameripoti kuhusu jinsi walivyojadili na vyanzo vyao vya habari vya makundi hayo mawili.

Na magazeti yalisema vyanzo hivyo viliwathibitishia kwamba Shekau amekufa.

Vyanzo vinavyohusiana na Boko Haram katika jimbo la Borno

Sababu ya tatu, kulingana na mtaalam ,ilikuwa ni kutoka kwa watu kaskazini mashariki mwa Nigeria ambao walithibitisha kifo cha kiongozi huyo wa Boko Haram. .

Anasema taarifa kadhaa kutoka maeneo ya Borno na Ziwa Chad za watu ambao walikuwa na vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikundi cha Boko Haram zilithibitisha kuwa Shekau amekufa.

Shekau hakujitokeza kukanusha taarifa za kifo chake

Barrister Bukarti amesema mojawapo ya sababu ilikuwa ni kwamba hapakuwa na video mpya kutoka kwa kiongozi wa Boko Haram.

Anasema Shekau bado hajajitokeza kukanusha madai ya kifio chake na kwa kawaida siku za nyuma amekuwa akijitokeza na kukana kosa lolote lililofanyika.

Kama kulikuwa na tetesi kuhusu kiongozi huyo wa Boko Haram au kikundi chenyewe wangekuja na kupinga tetesi hizo, lakini hilo halijafanyika.

Mtaalamu huyo amesema wakati mmoja video ilitolewa ikionesha Shekau akilia, lakini alijitokeza mara moja na na kupinga madai hayo, akisema video hiyo ilikuwa ya zamani.

Ni wiki mbili sasa kufikia leo tangu kifo chake kitangazwe, lakini hakuna taarifa kutoka kwa Shekau wala kuhusu ni wapi alipo , "na kama amekuwa hai basi atakuwa amekwenda mafichoni," Bukarti said.

ISWAP ilithibitisha

Mtaalamu anasema sababu kuu ya tano inayothibitisha kifo chake ni ni kujitokeza kwa ISWAP na kuthibitisha kifo cha Shekau.

Alisema Ijumaa ISWAP ilitoa taarifa ambayo ilithibitisha kwamba Shekau ameuawa na kuelezea jinsi ilivyomuua.

Kulingana na taarifa hiyo, Shekau alijiua kwa kulipua bomu alilokuwa ameliweka kwenye mwili wake.

Barrister Bukarti, ambaye amekuwa akifanya uchunguzi kuhusu harakati za Boko Haramamesema: " Ukweli huu unaweza kuthibitisha kwamba Shekau amefariki.

Aliongeza kuwa wapiganaji wa ISWAP walisema kuwa wanaendelea kupambana na makamanda wa Shekau baada ya kumuua kiongozi wao.