Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Kwa nini rais wa Marekani ameagiza majasusi wake kuchunguza chanzo cha Corona?
Rais wa Marekani Joe Biden ameagiza mashirika ya ujasusi ya nchi hiyo kuongeza nguvu katika kuchunguza chanzo cha Covid-19, ikiwemo nadharia ya kuwa virusi hivyo vilitengenezwa maabara.
Bw Biden ameyataka mashirika yake ya kijasusi kukamilisha uchunguzi na kuripoti kwake ndani ya kipindi cha siku 90.
Covid-19 kwa mara ya kwanza iligundulika katika mji wa Uchina wa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019. Utata kuhusu asili ya virusi hivyo pado unaendelea kuongezeka.
Zaidi ya watu milioni 168 wamethibitishwa kupata maambukizi ya virusi hivyo kote duniani na takriban watu milioni 3.5 wameripotiwa kufa.
Maafisa walihusisha maambukizi ya kwanza ya virusi vya Covid na soko la vyakula vya baharini lililopo katika mji wa Wuhan, na wanasayansi waliamini kuwa virusi hivyo vilisambazwa mara ya kwanza kwa binadamu kutoka kwa wanyama.
Lakini taarifa za hivi karibuni za vyombo vya habari vya Marekani zinaonesha kuongezeka kwa ushahidi kwamba virusi hivyo huenda viliibuka kutoka katika maabara nchini Uchina.
Beijing imelaani ripoti hizo na badala yake imesema kuwa huenda vilitokea katika maabara ya Marekani.
Kwanini Biden anaitisha ripoti ya uchunguzi sasa?
Katika taarifa ya Ikulu ya White House ya siku ya Jumatano, Rais Bisen alisema alikuwa ameitaka ripoti juu ya chanzo cha Covid-19 baada ya kuingia mamlakani, "ikiwa ni pamoja iwapo viliibuka kutoka kwa binadamu aliyekutana na mnyama aliyeambukizwa au viliibuka kutoka kwenye maabara kwa bahati mbaya."
Alipoipokea mwezi huu, alitaka apewe ripoti ya "ufuatiliaji wa ziada."
"Hadi kufikia leo, mashirika ya ujasusi ya Marekani yameungana katika nadharia hizo mbili lakini hayajafikia hitimisho dhahiri la swali," Bw Biden alisema.
Rais sasa anayataka mashirika ya ujasusi ku"ongeza mara dufu juhudi zao kukusanya na kuchambua taarifa ambazo zinaweza kutuleta karibu na hitimisho dhahiri ", na kuripoti kwake katika kipindi cha siku 90.
Ametaka pia baraza la Congress "kufahamishwa kikamilifu" kuhusu kazi hiyo.
Alihitimisha kwa kusema kuwa Marekani itaendelea " kufanya kazi na washirika wenye mtazamo huo kote duniani kuishinikiza Uchina kushiriki kikamilifu , kwa uwazi , katika uchunguzi wa kimataifa na kuwezesha upatikanaji wa data zote muhimu na ushahidi."
Lakini makala ya gazeti la Washington Post siku ya Jumatano iliushutumu utawala wa Biden kwa kuzuia uchunguzi wa Congress kuhusu chanzo cha Covid-19, huku akiunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO).
Je Covid imetoka maabara ?
Mwezi Machi mwaka huu, WHO ilitoa ripoti iliyoandikwa kwa ushirikiano na wanasayansi wa Uchina juu ya asili ya Covid-19, ikisema uwezekano kwamba ilianzia katika maabara ''ni jambo lisilowezekana kabisa''. WHO ilikubali uchunguzi zaidi unahitajika.
Lakini maswali yameendelea kuwepo na ripoti za hivi karibuni kutoka vyanzo vya mashirika ya ujasusi ya Marekani zinasema wajumbe watatu wa taasisi ya masuala ya virusi ya Wuhan walilazwa hospitalini mwezi Novemba mwaka 2019, wiki kadhaa kabla ya Uchina kukubali kisa cha kwanza cha ugonjwa mpya katika jamii.
Anthony Fauci, mshauri mkuu wa tiba wa Rais Biden, anaamini kuwa virusi vya corona vilisambazwa kwa binadamu kutoka kwa wanyama, licha ya kwamba alikiri mwezi huu kwamba haamini tena kwamba covid-19 iliibuka kawaida.
Taarifa ya Bw Biden inakuja siku moja baa ya Waziri wa Afya wa Marekani Xavier Becerra, kuitaka WHO kuhakikisha uchunguzi wa "uwazi" juu ya chanzo cha virusi vya corona.
Taarifa ya Bw Biden inakuja siku moja baa ya Waziri wa Marekani wa afya na huduma za kibinadamu , Xavier Becerra, kuitaka WHO kuhakikisha uchunguzi wa "uwazi" juu ya chanzo cha virusi vya corona.
"Janga la Covid-19 halikuiba mwaka wa maisha yetu tu, limeiba maisha ya mamilioni ya watu," Bw Becerra alisema katika hotuba yake kwa kikao cha afya cha dunia kilichoandaliwa na WHO.
"Awamu ya pili ya uchunguzi wa asili ya Covid izinduliwe kwa masharti ya uwazi, kwa misingi ya kisayansi, na kuwapatia wataalamu wa kimataifa uwezo wa kufikia chanzo cha virusi na siku za kwanza za mlipuko."
Madai ya uvujaji wa virusi kutoka kwa maabara yalipuuziliwa mbali kwa kiasi kikubwa mwaka jana na kutajwa kama dhana potofu ya njama, baada ya rais wa wakati huo Donald Trump kusema kuwa asili ya Covid-19 ilikuwa ni katika taasisi ya virusi ya Wuhan. Vyombo vingi vya habari vya Marekani vilielezea madai ya aina hiyo kama uongo au upotoshaji.
Jumanne, Bw Trump alitaka kutambuliwa na kusifiwa, na katika taarifa iliyotumwa barua pepe kwa gazeti la New York Post alisema ''Kwangu mimi ilikuwa ni wazi kuanzia mwanzo lakini nilikosolewa vibaya : ''Sasa wote wanasema: ''Alikuwa sahihi.''