Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona : Kulikuwa na mapungufu makubwa katika WHO na jinsi ulimwengu ulivyojibu janga hilo
Janga la Covid-19 lilikuwa linazuilika, jopo huru la ukaguzi limesema.Jopo, lililoundwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, limesema maandalizi ya pamoja ya WHO na serikali za ulimwengu kujibu janga hilo yalikuwa "mseto wenye sumu ".
WHO ilipaswa kutangaza hali ya dharura ulimwenguni mapema kuliko ilivyofanya, ripoti yake ilisema, na kuongeza kuwa bila mabadiliko ya dharura ulimwengu ulikuwa hatarini kwa mlipuko mwingine mkubwa wa magonjwa.
Zaidi ya watu milioni 3.3 kote ulimwenguni sasa wamekufa kutokana na virusi vya Corona.
Wakati Marekani na Ulaya zikianza kupunguza vizuizi na kuanza tena kurejelea maisha ya kabla ya janga, virusi hivyo bado vinaangamiza sehemu za Asia.
India haswa imeshuhudia idadi kubwa ya visa na vifo vinavyovunja rekodi, na upungufu mkubwa wa oksijeni katika hospitali kote nchini humo.
Ripoti hiyo imesema nini?
Ripoti hiyo -Covid-19: Liwe ndilo janga la mwisho , iliandaliwa na Jopo Huru la Kujitayarisha kwa Janga na jinsi ya Kukabiliana nalo.
Lengo lake lilikuwa kupata majibu ya jinsi virusi hivyo viliua zaidi ya watu milioni 3.3 na kuambukiza zaidi ya milioni 159.
"Hali tunayojikuta leo ingeweza kuzuiwa," mwenyekiti mwenza Ellen Johnson Sirleaf, rais wa zamani wa Liberia, aliwaambia waandishi wa habari.
"Ni kwa sababu ya kutofaulu, mapungufu na ucheleweshaji wa utayari na majibu."
Jopo hilo lilisema kwamba Kamati ya Dharura ya WHO ilipaswa kutangaza kuzuka huko China kuwa dharura ya kimataifa wiki moja mapema kuliko ilivyofanya.
Ilipaswa kufanya hivyo katika mkutano wake wa kwanza tarehe 22 Januari mwaka jana, ripoti ilisema, badala ya kungojea hadi 30 Januari.
Mwezi uliofuatia tamko la WHO kuhusu hatari ya Corona "ulipotea" wakati nchi ziliposhindwa kuchukua hatua zinazofaa ili kukomesha kuenea kwa virusi.
Wakati huo WHO ilibanwa na kanuni zake kwamba vizuizi vya kusafiri vinapaswa kuwa suluhisho la mwisho, jopo lilisema, na kuongeza kuwa Ulaya na Marekani zilipoteza mwezi mzima wa Februari na zilichukua hatua tu wakati hospitali zao zilipoanza kujaa.
Wakati nchi zilipopaswa kuwa zinaandaa mifumo yao ya afya kuwashughulikia wagonjwa wa Covid, sehemu kubwa ya ulimwengu ilikuwa iking'ang'ania vifaa vya kujikinga na dawa, ilisema ripoti hiyo.
Ili kuzuia janga jingine, ripoti hiyo inashauri mageuzi muhimu:
- WHO inapaswa kuwa na baraza la kushughulikia tishio la afya duniani lenye uwezo wa kuziwajibisha nchi wanachama
- Kuwe na mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ili kuchapisha habari bila idhini ya nchi zinazohusika
- Chanjo lazima zichukuliwe kama bidhaa za umma na kuwe na kituo cha kufadhili shughuli za kukabiliana na majanga
- Mwenyekiti mwenza wa jopo na Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand Helen Clark alisema ni "muhimu kuwa na WHO yenye mamlaka'. "Ikiwa vizuizi vya kusafiri vingewekwa haraka zaidi, kwa upana zaidi, hilo lingezuia kusambaa kwa ugonjwa huo na hilo limesalia kuwa hivyo hadi leo'
Maradhi mengine yanayosababishwa na Corona
Wakati wimbi kali la pili la maambukizi ya Covid-19 linaloua watu likiikumba India, madaktari sasa wanaripoti ongezeko la haraka la visa vya maambukizi ya nadra ya kuvu -ambao pia huitwa "black fungus" - miongoni mwa wagonjwa waliopona Covid-19.
Mucormycosis ni nini?
Mucormycosis ni maambukizi ya nadra sana. Hutokea pale mtu anapokaa katika mazingira ya ukungu unaofanana na kamasi ambao kwa kawaida hupatikana katika udongo, mimea, mbolea na matunda yaliyooza, na makamasi ya watu wenye afya," anasema Dkt Nair.
Huathiri pua, ubongo na mapafu na unaweza kutishia maisha kwa watu wenye maradhi ya kisukari au wenye tatizo kubwa la ukosefu wa kinga mwilini kama vile, watu wenye magonjwa ya saratani au HIV/UKIMWI
Madaktari wanaamini mucormycosis, ambayo kwa ujumla ina uwezekano wa kuua kwa kiwango cha 50%, huenda husababishwa na matumizi ya homoni zinazotengenezwa na binadamu (steroids), tiba ambayo hutumiwa kwa mtu mgonjwa wa Covid-19 ambaye maisha yake yamo hatarini.
Steroids hupunguza hali ya kuungua katika mapafu kutokana na Covid-19 na inaonekana kusaidia kuzuia baadhi ya uharibifu ambao unaweza kutokea wakati mfumo wa kinga ya mwili unapohangaika kupambana na virusi vya corona.
Lakini pia zinazuia upungufu wa kinga ya mwili na kusukuma juu viwango vya sukari ya mwili miongoni mwa wagonjwa wenye kisukari na wasio na kisukari wanapopata maambukizi ya Covid-19.
Inadhaniwa kwamba kushuka huku kwa kinga ya mwili kunaweza kusababishwa na visa hivi vya kuvu aina ya mucormycosis.
"Kisukari hushusha kinga ya mwili, virusi vya corona vinaizidisha , na halafu steroids ambayo husaidia kupambana na Covid-19 huwa kama mafuta kwenye moto kwa kuzidisha hali hiyo ," anasema Dkt Nair.
Dkt Nair - anayefanya kazi katika hospitali tatu mjini Mumbai, mojawapo ya miji iliyoathiriwa sana na wimbi la pili -anasema amekwisha shuhudia wagonjwa wapatao 40 wakiwa wanaugua kuvu hiyo mwezi Aprili.
Wengi wao walikuwa na ugonjwa wa kisukari na walikuwa wamepona Covid-19 wakiwa nyumbani. Kumi na mmoja kati yao ilibidi wafanyiwe upasuaji wa kuondoa macho yao.
Kati ya Disemba na Februari, madaktari wenzake katika hospitali za miji mitano - Mumbai, Bangalore, Hyderabad, Delhi na Pune -waliripoti visa 58 vya maambukizi hayo.
Wengi wa wagonjwa waliyapata maambukizi katika kipindi cha sku 12 na 15 baada ya kupona Covid-19.
Hospitali yenye shughuli nyingi ya mjini Mumbai Sion, imeripoti wagonjwa 24 wa maambukizi ya kuvu, katika kipindi cha miezi miwili,kulingana na Dkt Renuka Bradoo, kuu wa kitengo cha magonjwa ya masikio, macho na koo.
Kumi na mmoja kati yao ilibidi apoteze jicho , na sita kati yao walikufa. Wengi miongoni mwa wagonjwa hao walikuwa na umri wa kati wa utu uzima waliokuwa na ugonjwa wa kisukari na walipata kuvu(fungus) baada ya kupona . "Tunashuhudia tayari visa viwili hadi vitatu kwa wiki. Ni tatizo katika kipindi hiki cha janga ," alisema.
Dkt Nair anasema amekutana na visa visivyopungua 10 mjini Mumbai katika kipindi cha miaka mwili iliyopita. "Mwaka huu ni kitu tofauti," anasema
Katika Bengaluru, Dkt Hegde hajawahi kushuhudia zaidi ya kisa kimoja au viwili kwa mwaka katika kipindi cha muongo mzima alichofanya kazi ya udaktari , lakini anasema pia mwaka huu visa vimeongezeka.
Wagonjwa wanaougua maambukizi ya kuvu ( fungal infection) wana dalili za kuvimba na kutokwa damu puani, uvimbe wa jicho, kushindwa kuona vyema na hatimaye, kupoteza kabisa uwezo wa kuona.
Kunaweza kuwa na ngozi yenye vipele vyeusi kando ya pua.
Madaktari wanasema wengi miongoni mwa wagonjwa wao hufika wakiwa wamechelewa hospitalini, wakati tayari wanapoteza uwezo wa kuona, na hivyo kuwabidi madaktari kuwafanyia upasuaji wa kuyaondoa macho yao ili kuzuia maambukizi kuufikia ubongo.
Katika baadhi ya wagonjwa,madaktari nchini India wanasema, wagonjwa wamepoteza uwezo wao wa kuona katika macho yao yote mawili. Na katika visa vya nadra, madaktari wamelazimika kuondoa kabisa mifupa ya taya ili kuzuia ugonjwa kusambaa katika maeneo mengine ya mwili.
Njia mojawapo ya kuzuia uwezekano wa maambukizi ya kuvu ni kuhakikisha kwamba wagonjwa wa Covid-19 - wanapopokea matibabu na baada ya kupona wanapewa dozi sahihi na kupewa homoni za steroids ipasavyo , anasema dokta Rahul Baxi,daktari bingwa wa maradhi ya kisukari mwenye makao yake Mumbai.
Anasema aliwatibu wangonjwa wapatao 800 wenye kisukari waliokuwa na Covid-19 mwaka uliopita, na hakuna hata mmoja wao aliyepata maambukizi ya kuvu. "Madaktari wanapaswa kujali viwango vya sukari ya mwili baada ya wagonjwa kuruhusiwa kwenda nyumbani ," anasema dokta Baxi.
Mgonjwa wake mwenye umri mdogo kwa wote alikuwa na miaka 27 mwanaume, ambaye hata hakuwa na maradhi ya kisukari . "Ilitubidi tumfanyie upasuaji wakati wa wiki yake ya pili ya Covid-19 na kuondoa jicho lake. Ni pigo kwa kweli."