Waridi wa BBC: Nikiwa Binti wa miaka 9 nilikua mraibu wa ngono

Chanzo cha picha, Eulene Murhando
Eulene Murhando anajionea fahari ufanisi alioupata lakini rohoni mwake ana kumbukumbu za madhila aliyoyapitia utotoni ambayo karibu yasambaratishe maisha yake.
Tangu akiwa mdogo, anasema alikuwa ananyanyaswa kingono na watu alio na ukaribu nao katika jamii kiasi cha yeye kufikiria kuwa lilikuwa jambo la kawaida.
"Wakati vitendo hivi vinafanyika mimi nilikuwa mdogo sana, nikiwa na miaka mitano hivi," anasema.
"Hawa watu walikuwa na tabia ya kunitomasa tomasa sehemu zangu za siri, ila wakati huo nilikuwa sina ufahamu wa vitendo hivyo. Kila mara walinieleza kuwa nisiseme lolote kwa yeyote ."
Ni vitendo ambavyo viliendelea hadi binti huyu alipotimiza miaka 9 hivi.
Anasema wanaume fulani wa jamii yake walimvizia maeneo tofauti nyumbani kwao walipoachwa peke yao na kumnyanyasa kingono.
Anasema kuwa alijihisi mnyonge asijue wa kumueleza.
Kushawishiwa kukaa kimya
Mwanadada huyu anasema watu waliomnyanyasa kingono walikuwa wanampa peremende na chokoleti kama njia ya kumnyamazisha.
Eulene anasema kuwa njia rahisi ya kuhakikisha kuwa hangesema chochote pia ilikuwa kumueleza kuwa vitendo walivyokuwa wanavifanya vilikuwa vya kawaida, na kwamba walikuwa wanamtendea hivyo kwa kumpenda kama mtoto mdogo.
Alivyoanza uraibu wa ngono
Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga alianza kupeleka zile tabia shuleni.
Bila kufahamu ubaya wake, alijaribu kurudia vitendo vile na kuwaonesha wanafunzi waliokuwa wanasoma naye darasani.
Wakati huo wote hadi alipohitimu miaka 9 hivi wazazi wake hawakuwa na ufahamu wa matendo maovu yaliyokuwa yanatendeka katika makazi yao.

Chanzo cha picha, Eulene Murhando
Isipokuwa baada ya kuambukizwa ugonjwa na maambukizi yanayoathiri sehemu za siri za wanawake.
Kwa mfano alianza kuhisi maumivu alipokuwa anakwenda haja ndogo na pia kujikuna sehemu za siri.
Alipopelekwa hospitalini ndipo daktari alipomueleza mama yake kuwa binti alikuwa anadhulumiwa au alikuwa anachezea sehemu zake za siri.
"Mama alielezwa na daktari kuwa sehemu zangu za siri ziliashiria kuguswa , ila mama aliponiuliza sikuwa na ujasiri wa kuwashtaki walionidhulumu," anasema.
"Nilielekeza kidole cha lawama kwa kijana mmoja aliyekuwa jirani wangu."
Hakutaka kuwatia taabuni watu wa jamii yake .
Mama yake alikuwa na wasiwasi kuhusu tabia zake ambazo zilikuwa zinabadilika kila uchao ila hakuelewa chimbuko lake.
Uraibu wa kujichua
Akiwa darasa la nane, alihamishwa kutoka shule mmoja hadi nyingine katika kipindi kifupi.
Alipoingia shule ya msingi mpya pale pale urafiki usiokuwa wa kawaida ulianza kati yake na mwalimu.
Eulene anasema alipokuwa na miaka 13 alihisi kana kwamba alikuwa na hisia za kimapenzi kwa mwalimu yule.
Muda si muda, naye mwalimu alianza tabia sawia na ile iliyokuwa hapo nyumbani wakati akiwa mtoto.
Mwalimu alimdhulumu kwa kumtomasa na kumpapasa .

Chanzo cha picha, Eulene Murhando
"Mimi na mwalimu tulikuwa katika uhusiano ambao haukuwa wa kawaida. Mwalimu alikuwa ananiongoza hadi eneo faraghani shuleni na kumnyanyasa kimapenzi. Ni urafiki uliodumu kipindi cha miaka miwili nilipokuwa nasoma shuleni humo," anakumbuka Eulene.
Mwanamke huyu anasema kuwa maneno ya mwalimu , yaliyoashiria mapenzi na mawazo mema Juu yake , yalimsukuma katika uhusiano wa Chanda na Pete kwa mwalimu wake .
"Pale shuleni kulikuwa na karakana mmoja ambayo ilikuwa sehemu murua kwangu kukutana na mwalimu kipenzi changu , karakana ya shule ilikuwa mbali kidogo na madarasa kwa hiyo hakuna mtu aliyetuhisi''.
Kwangu niliona kama jambo la kipekee kupendwa na mwalimu " anakumbuka Eulene.
Kulingana na mwanamke huyu mwalimu aliyekuwa na uhusiano naye alikuwa na mazoea ya kumdekeza kwa kumpa peremende, biskuti , kila wakati alimkumbatia na kumfanya Eulene kuhisi kupendwa na kukubalika.
Anakiri kuwa manyanyaso ya kingono nyumbani kwao yalimsukuma yeye kutamani kutenda uasherati akiwa msichana mdogo.
"Akilini mwangu nikiwa mtoto nilihisi kila wakati haja ya ngono na kutomaswa- ni uraibu ulionisakama mno , sikujua kuwa nilikuwa na matatizo ya kisaikolojia "anakumbuka Eulene -ni kana kwamba mwili wake ulianza kuzoea vitendo hivyo.
Kwa hivyo, alianza kujichua kila mara akiwa pekee yake, na likawa ni jambo la desturi kati ya miaka yake 9 hadi 14.
Alipoingia shule ya sekondari, Mwalimu kipenzi chake hakuwepo alitokomea asijue atamtoa wapi.
Kwa hiyo Eulene anasema alibadilisha tabia na pia desturi aliyokuwa nayo ya kujichua. Alikuwa kwenye shule ya bweni.
"Nilipoingia kidato cha kwanza, nilitulia na kuamua kujenga jina upya kwa hivyo nilijitenga na tabia za kujichua kwa miaka minne nikiwa shule ya sekondari," anasema Eulene.
"Sikukumbwa na kisa chochote kibaya - cha mno ni kuwa nilijitosa kwenye kilabu cha dini na kuwa mmoja wa waimbaji wa nyimbo za sifa shuleni."
Baada ya shule Eulene alikutana na kijana mmoja na kwa muda walikuwa kwenye mahaba makubwa kabla ya yeye kushika mimba.
Uhusiano ambao uligeuka na kuwa kama maji na mafuta. Kijana aliyekuwa amempenda na kumpa ahadi za kuwa pamoja hadi milele aligeuka na kukataa majukumu ya malezi.
Eulene alipitia kipindi kizito cha kubeba ujauzito bila mwenza wake na pia kuanza majukumu ya kumlea mwanawe wa kiume pekee yake akiwa bado nyumbani kwao.
Baba na mama walipokea mtoto wake na kuendelea kutumaini kuwa Eulene angetimiza ndoto zake.
Kuuzwa kwenye Danguro
Baada ya mtoto kutimiza miezi tisa kama kawaida ya wanawake wengi, Eulene alikuwa na tamaa ya kuanza kazi au kutafuta biashara ambayo ingemuwezesha kumlea mtoto wake.
Katika pilikapilika watu wa karibu naye pia waliokuwa na tabia ya kumdhulumu utotoni mwake walipanga njama ambayo waliiwasilisha kama mpango wa kumtafutia kazi.
Walipotembea nyumbani kwa wazazi wa Eulene walimueleza baba yake kuwa walikuwa wamemtafutia kazi katika mgahawa mmoja na walihitaji kumpeleka kule kumtambulisha kwa mwajiri wake.
Bila kusita baba aliridhia hayo na kufurahia kuwa hatimaye Eulene alijaaliwa kupata ajira.
Kilichoibuka baadaye ni kuwa dada zake Eulene walikuwa wakimuuza shilingi elfu 50 kwenye danguro moja.
"Nakumbuka walinielekeza hadi hoteli moja viungani mwa mji wa Nairobi, pale waliniwasilisha kwa wanaume wawili- kuanzia wakati huo nilifungiwa kwenye chumba kimoja, katika kipindi cha wiki mbili nilitumika kama mtumwa wa ngono na watu tofauti. Waliutumia mwili wangu," anasema.
"Siwezi kuyakumbuka mengi yaliyojiri kwani ni kana kwamba nilikuwa napewa kinywaji ambacho kilinifanya nipoteze ufahamu wa mazingira niliyokuwepo,"anakumbuka Eulene.
Kufanikiwa kutoroka
Siku moja Eulene alipata fursa ya kutoroka alipogundua kuwa mlango wa chumba alichokuwa amefichwa ulikuwa wazi.
Kumbe kipindi hicho chote Eulene alikuwa anatafutwa na wazazi wake wasijue alikokwenda.
Upande mwingine waliomuuza kwa madanguro walijitia hamnazo kuhusiana na alipotokomea.
"Kwa kuwa nilikuwa na desturi ya kupotea potea nyumbani wakati mwingine kwa siku tata au wiki, ilikuwa rahisi kuwaza kuwa huenda nilikuwa kwenye anasa zangu za kawaida, kila mara baba alipouliza nilipopelekwa kazini," Eulene anasema.
Anasema kuwa kabla ya kisa hicho alikuwa na desturi ya kutorudi nyumbani kwa siku mbili au tatu na pia alikuwa ameanza uraibu wa kunywa vileo na kuvuta sigara.
Kwa hivyo haikuwa ajabu kwamba hakuonekana kwa siku nyingi nyingi ila kwa baba yake mzazi alikuwa na wasiwasi ila hakuna aliyefahamu alikopotelea.
Wazazi wake walimpokea kwa mshtuko waliposikia kilichojiri.
Alifanikiwa kubadilika?
Eulene anasema kuwa kwa miaka mingi ya utu uzima wake hadi alipotimiza miaka 40 , aliishi na machungu na kero za dhuluma za kingono alizofanyiwa na watu mbali mbali akiwemo mwalimu wake wa shule ya msingi.
Eulene anasema kuwa ilichukua juhudi za kila siku kuondosha mawazo ya kale hasa kwa kukumbatia dini na maombi kama njia ya uponyaji.
Baada ya kujitokeza hadharani kuzungumzia madhila yake hasa alipoanza kuzungumza kwenye vyombo vya habari nchini Kenya, amegundua kuwa kuna watoto ambao hudhulumiwa kingono pale pale katika jamii zao na wala hawana sauti katika kuzungumzia dhuluma hizo.
Yeye amejitokeza kama mhanga na kuzungumzia hali hiyo na kuwasaidia wale ambao wameathirika wanapotafuta msaada.
Kwa Sasa Eulene Murhando ni Rais wa huduma ya , Wellspring of life international ambayo huwapa ushauri walio na matatizo ya ngono na changamoto za mahusiano












