Mzozo wa Israeli na Palestina: Kundi la Hamas lilipata wapi roketi 4,000?

Mapigano kati ya Israeli na kundi la Palestina la Hamas yalisitishwa baada ya siku 11.

Hata hivyo, juhudi zinaendelea kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa kwa muda mrefu zaidi.

Timu ya Misri ilikuwa Israeli Mei 22. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken huenda pia akahudhuria eneo hilo wiki ijayo.

Kundi la Palestina la Hamas, ambalo linazozana na Israeli limedai kuibuka na ushindi. Na vita hivyo vya Gaza vimesababisha vifo vya watu 250.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema Ijumaa (Mei 21) kwamba uharibifu uliotekelezwa dhidi ya kundi la Hamas ulikuwa "mafanikio makubwa."

Alisema, "Ikiwa Hamas ilifikiria tunaweza kuhangaishwa na viroketi kidogo tu, wamekosea."

Upande mwingine, kundi la Hamas pia limedai ushindi na kusema kuwa mapigano hayo yamefungua ukurasa mpya.

Roketi zilizotengenezwa kwa nyenzo kidogo tu

Pande zote mbili zinadai kuwa zimepata ushindi lakini ukanda wa Gaza umeathirika zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya waliojeruhiwa na pia imepata hasara kubwa kifedha.

Katika mapigano haya, mfumo wa Israeli wa kujikinga dhidi ya makombora ulidhihirika kuwa muhimu kwao kama silaha ya kujikinga.

Mfumo huo ulizuia maelfu ya roketi za upande wa Hamas kulipuka.

Lakini je, Hamas ilifanikiwa vipi kushambulia Israeli kwa zaidi ya roketi 4,000? Kundi la Hamas lilipata wapi silaha zote hizo wakati Israeli na Misri zilikuwa zinalinda mpaka?

Ripoti iliyotolewa na shirika la habari la Reuters, imenukuu wachambuzi na maafisa wakidai kwamba raia wa Palestina huko Gaza wamejenga kituo cha kutengeneza maroketi kwa usaidizi wa Iran.

Kinachohitajika ni mabomba na zege kutengeneza roketi. Nyenzo hizi zitahitajika kuanza ujenzi tena katika eneo la Gaza na pia masharti yanaweza kuwekwa kuhakikisha upatikanaji wake. Na hii ndio changamoto kwa Israeli na jamii ya kimataifa.

Kulingana na Reuters, Hamas na washirika wake wenye msimamo mkali wa Palestinian Islamic Jihad, wameongeza thamani na idadi ya maroketi tangu kutokea kwa vita vya mwaka 2014 kati ya Israeli na Gaza.

Madai dhidi ya Iran

Afisa mwandamizi wa Ulaya ambaye hakutaka kutajwa, amesema: "Safari hii, uwezo wa kundi la Hamas ulikuwa wa kipekee.

Hamas, kundi la Kiislamu la Jihad na makundi mengine yenye msimamo mkali yalirusha roketi 4,360 kuelekea upande wa Israeli wakati wa mapigano hayo. Kati ya hayo, roketi 680 zilitua katika ukanda wa Gaza.

Kulingana na wachambuzi, nyingi ya roketi hizo zilitengenezwa kwa mfumo duni yaani yalifanikiwa kufika umbali wa masafa mafupi tu.

Daniel Benjamin, aliyekuwa afisa katika wizara ya mambo ya nje, amesema kuwa maroketi huwa ni rahisi kutengeneza na hutumia bomba la chuma. "Unaweza usiamini lakini mara nyingi kulitumika vipande vya makombora vilivyorushwa na Israel."

Akizungumza katika jarida la Wall Street, Ephraim Sneh, brigedia jenerali aliyestaafu alisema kuwa muundo wa roketi hizo ulikuwa unafanana na silaha za Iran lakini zilitengenezwa ndani ya Palestina.

Kulingana na gazeti moja, Iran inasaidia kundi la Hamas kwa namna mbalimbali. Roketi hizo zimetengenezwa kwa muundo wa Iran na kufanywa kuwa roketi kwa kutumia mabomba yanayotumika kila siku, mbarika na vipande vya makobowa yaliyorushwa na Israeli.

Alhamisi (Mei 20), Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu iliishtumu Iran kwa kuunga mkono makundi yenye msimamo mkali huko Gaza, akisema "Ikiwa Iran haitaungwa mkono, mashirika yote hayo yatasambaratika katika kipindi cha wiki mbili tu."

Katika taarifa zilizopeperushwa na kituo cha Al Jazeera, Hussein Salami, mkuu wa kikosi maalum jeshi la Iranian Revolutionary Guards, alisema, "Iran inaunga mkono Palestina katika vita vyake dhidi ya Israeli, na ni kwasababu ya wao, Palestina ina makombora."

Uhusiano kati ya Iran na Hamas

Uhusiano kati ya Iran na kundi la Hamas huko Plaestina, pamoja na lile la Palestinian Islamic Jihad, sio wa kufichika.

Wiki jana, Jenerali Ismail Kani wa kikosi cha Kikurdi alisema kupitia taarifa zilizopeperushwa na shirika la taifa la Iran, alisema kuwa ana muunga mkono kiongozi wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh.

Palestina ilitumia nyenzo za ndani ya eneo hilo kukabiliana na mahasimu wao.

Jarida la Wall Street lilimnukuu afisa wa Israeli akisema kwamba makundi yaliyopo Gaza yalikuwa yanatengeneza ndege zisizokuwa na rubani kwa kutumia kioo nyuzi, roketi zilizotengenezwa kwa mabomba ya chuma na mafuta ya mbarika ya chumvi.

Hamas sasa hivi inajenga roketi za kawaida tu. Bado hawajatengeneza silaha za kushambulia kwasababu kwa hili kufanyika, wanahitaji teknolojia ya kisasa, usaidizi wa mtaalamu na mafunzo.

Hivi karibuni, kundi la Hamas lilidai kutengeneza ndege isiyo na rubani kwa jina Shehab na wakatoa video yake. Pia injini ilikuwa ya China ikiwa pamoja na mfumo wa kupokea habari kutoka kwa setilaiti (GPS).

Hata hivyo, ndege isiyokuwa na rubani ya Hamas haikuhimili mfumo wa kujikinga na makombora wa Israeli.

Kulingana na ripoti za jarida la Forbes, ndege hiyo isiyokuwa na rubani iliundwa kufanana na ndege isiyo na rubani iliyotumika na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran huko Yemen.

Pia Iran International hivi karibuni ilitoa ripoti iliyosema kuwa ndege zisizokuwa na rubani za Palestina ziliiga muundo wa kitambo wa Iran.

Roketi ndio silaha pekee ya Hamas

Kwa miaka mingi, makundi ya Palestina yenye msimamo mkali yamekuwa yakitumia roketi kushambulia Israeli. Kabla ya Israeli kujiondoa Gaza mwaka 2005, makazi ya Israeli yalivamiwa kwa kutumia mota na roketi zilizorushwa kutoka upande wa makazi ya eneo la kiarabu la Palestina.

Na baada ya Israeli kujiondoa Gaza na kuchukua eneo la Ukanda wa Gaza 2003, kundi la Hamas lilisalia na roketi kama silaha yake ya pekee.

Rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia alikuwa Mohamed Morsi, aliyeng'atuliwa madarakani mwaka 2013. Na hadi wakati huo, kundi la Hamas na lile la Kiislam la wapiganaji wa Jihad yamekuwa yakipata silaha kutoka kwa mtambo mmoja uliopo Rasi ya Sinai huko Misri.