Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mlipuko wa Volkano Goma: ' Mume wangu alikuwa mgonjwa,sikuweza kumuokoa akaochomwa na lava'
Ernestine Kabuo alirudi nyumbani baada ya kukimbia mtiririko wa lava huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kugundua kuwa mumewe alikuwa amefariki dunia.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 alishindwa kumbeba mumewe mgonjwa kutoka nyumbani kwao na akakuta ameungua hadi kufa, aliliambia shirika la habari la Reuters.
Takriban vifo 15 vimethibitishwa kufuatia mlipuko wa Jumamosi wa volkano katika Mlima Nyiragongo.
Lakini lava haikufika katika eneo la jiji la Goma.
Hii iliepusha kiwango kikubwa cha vifo kutokea pamoja na uharibifu mkubwa kama ulioshuhudiwa mnamo 2002. Hata hivyo, iligonga wilaya ya Buhene, ambapo nyumba ya Bi Kabuo ilikuwa.
"Nilijiambia: Siwezi kwenda peke yangu, tumeoana kwa nyakati za furaha na huzuni," aliiambia Reuters akitafakari juu ya kile kilichotokea Jumamosi.
"Nilirudi angalau kujaribu kumtoa lakini sikuweza. Nilikimbia na akaungua ndani. Sijui cha kufanya. Ninailaani siku hii."
Wakazi wengine wa Goma, mji wa watu 670,000 kulingana na makadirio ya UN, wanatafuta wapendwa wao waliopotea wakati jiji hilo, na eneo hilo, linaendelea kushuhudia mitetemeko ya ardhi.
Zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kutoweka na wengine 150 wametengwa na familia zao, shirika la Umoja wa Mataifa la watoto, Unicef limesema, na kuongeza kuwa vituo vitaanzishwa kusaidia watoto walioachwa na wazazi wao.
Tisa kati ya watu 15 waliouawa ni wale waliofariki katika ajali za barabarani wakati watu walipokuwa wakimbia kunusuru maisha yao.
Wengine wanne walifariki wakati walipojaribu kutoroka gerezani huku wawili wakichomwa moto hadi kufa, msemaji wa serikali Patrick Muyaya alithibitisha siku ya Jumapili.
Lava ilikomea katika wilaya ya Buhene, nje kidogo ya Goma, ikizika mamia ya nyumba na hata majengo makubwa. Jitihada za ujenzi zinaweza kuchukua miezi.
"Nyumba zote katika mtaa wa Buhene ziliteketezwa," Innocent Bahala Shamavu aliliambia shirika la habari la Associated Press.
Mahali pengine, lava ilivuka barabara ya N2 inayounganisha Goma na jiji la Beni, ikikata msaada muhimu na njia ya usambazaji. Walakini, uwanja wa ndege wa jiji hilo haukuguswa, licha ya ripoti za mapema kwamba ulikuwa umeathiriwa.
Volkano hiyo, iliyoko 10km (maili sita) kutoka Goma, ililipuka mara ya mwisho mnamo 2002, na kuua watu 250 na kuwafanya 120,000 kukosa makazi.
Wakazi walianza kuondoka katika nyumba zao hata kabla serikali haijatangaza mpango wa uokoaji. Usiku, umati wa watu ulionekana ukikimbia kwa miguu na magodoro na vitu vingine.
Mamlaka ya Rwanda ilisema zaidi ya watu 3,000 walikuwa wamevuka rasmi kutoka Goma. Wengine walianza kurudi Jumapili. Wengine walikwenda kwenye maeneo ya juu magharibi mwa jiji.
Mkazi mmoja wa Goma, Richard Bahati, alisema alikuwa nyumbani kwake aliposikia mayowe na alikuwa na wasiwasi mkubwa alipoona mbingu ikiwa nyekundu nje.
"Niliishi kupitia shida na volkano hii mnamo 2002. Volkano hiyo iliharibu nyumba zetu zote na mali," alisema.
Mfanyabiashara kwa jina , Kambere Ombeni, alikuwa miongoni mwa wale waliorudi katika eneo la tukio huku vifusi vikitapakaa.
''Tulitazama nyumba zote katika eneo la Nyarigongo likichomeka moto. Moto ulifika hadi hapa, hata sasa tunaweza kuona uji wa mlipuko wa volcano hiyo'', alisema.
Mkaazi mwengine , Irene Baula , alisema kwamba watu watahitaji usaidizi kutoka kwa serikali ili kujenga upya maisha yao.
''Kuna ardhi , watu, idadi ya watu ambayo imepoteza kila kitu, pengine pia kuna vifo, ni nani anayejua''?.
''Tunaiomba serikali kuwasaidia manusura wa mlipuko huu''.
Tom Peyra Costa, kutoka baraza la wakimbizi la Norway mjini Goma aliambia BBC kile kilichotokea.
"Uji uliokuwa ukitiririka ulikuwa polepole sana kama kilomita kwa saa, lakini haukusita… ulianza kuchoma nyumba'' , akiongezea kwamba mashirika ya kibinadamu yalikuwa tayari yameanza kuangazia mahitaji ya wakazi.
Mlima Nyiragongo ni moja ya milima inayolipuka Volkano lakini kulikuwa na wasiwasi kwamba vitendo vyake havikuchunguzwa vizuri na shirika la kuchunguza milipuko ya volcano mjini Goma tangu Benki ya dunia ilipositisha ufadhili kufuatia madai ya ufisadi.
Profesa Mike Burton, mtaalamu wa milipuko ya Volcano katika chuo kikuu cha Manchester nchini England , aliambia BBC kwamba uji wa volcano katika mlima Nyiragongo umekuwa na uwezo wa kutiririka kwa kasi .
Katika ripoti yake shirika hilo lilionya kwamba vitendo vya ardhini vya mlima huo vimeongezeka.
Mwaka uliopita , Mkurugenzi wa shirika hilo la Goma aliambia BBC kwamba ziwa la mlima huo wa Volkano limekuwa likijaa kwa haraka hatua ilioongezea uwezekano wa mlipuko katika miaka michache ijayo.
Lakini pia alionya kwamba tetemeko la ardhi linaweza kusababisha janga mapema.
Mlipuko mbaya zaidi wa volakano katika mlima huo ulitokea 1977 ambapo zaidi ya watu 600 walifariki.