Kaburi la mtoto la miaka 78,000 iliyopita lafichua mazishi yaliyofanyika wakati huo

Taswira ya huzuni ya kibinadamu, ya kupoteza mtoto yapata miaka 78,000 iliyopita, ilifichuliwa kufuatia ugunduzi wa kaburi la zamani zaidi barani Afrika .

Kaburi hilo la zamani zaidi la mtoto wa miaka mitatu lilipatikana ndani ya pango moja nchini Kenya.

Katika jarida la asilia , watafiti waliosomea mabaki hayo ya kale walielezea jinsi kichwa chake kilivyolazwa katika mto.

Kundi hilo la wanaakiolojia kwa makini waliliziba kaburi lote kwa lengo la kuhifadhi vipande vya mifupa vilivyosalia.

Hatua hiyo iliwawezesha kuusafirisha mwili wake hadi katika maabara kwa kwa utafiti zaidi.

''Ilikuwa sawa na kufukua kivuli'', alisema Profesa Maria Martinon Torres, Mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha utafiti wa binadamu nchini Uhispania .

''Tulipobeba mwili huo hatukujua kwamba tumebeba mtoto mikononi mwetu'', aliiambia BBC katika kipindi cha sayansi

Watafiti hao walifanikiwa kufanyia utafiti meno yake ili kuthibitisha kwamba huo ndio uliokuwa mwili mdogo wa mtoto aliye kati ya miaka miwili hadi mitatu.

Uchunguzi ulibaini kwamba mwili wake ulikuwa umelazwa kama mjusi.

Na mifupa hiyo ilikuwa katika hali ambayo ilikuwa imefungwa pamoja kwa nguvu na kuzikwa huku mwili wake ukilalia kitu kama mto ambao ulikuwa nao umeoza.

"Tunadhani kwamba mwili wake ulifungwa kwa pamoja katika sanda ya majani au ngozi ya Wanyama , kama alivyowekwa katika usingizi wake wa mwisho'' , alielezea Profesa Martinon Torr

Uchunguzi zaidi wa ukubwa na umbo la vipande vya mifupa uliwafanya watafiti hao kusema kwamba mtoto huyo alikuwa mvulana.

"Alizikwa katika pango ambalo watu walikuwa wakiishi , Profesa Martino - Torres alisema.

''Tabia zote hizi zilikuwa na maana - pengine huzuni ama pengine hawakutaka kumtupa."

Afrika inajulikana kama chanzo cha binadamu , lakini mbali na ushahidi wote kuhusu vifaa vilivyotumika zamani na jamii iliyoishi, wanasayansi wanasema kwamba mazishi yalikuwa kitu muhimu kilichokosekana katika historia ya mabadiliko ya binadamu wakati huo.

''Kaburi jingine la zamani zaidi barani Afrika lina miaka 74,000'', alielezea Dkt. Louise Humphrey kutoka kwa makavazi ya London.

Cha kushangaza ni kwamba hata huyo alikuwa mtoto lakini mifupa yake ilichimbwa vibaya takriban miaka 50 iliopita , hivyobasi hatuna habari zaidi kuuhusu."