Tundu Lissu: Mambo sita anayotaka ahakikishiwe utekelezaji wake kabla ya kurejea nyumbani kutoka uhamishoni

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu mwenyekiti wa chama cha Chadema (Bara) Tundu Lissu amedai hakikisho la usalama wake kutoka kwa serikali,msamaha kwa wafungwa wa kisiasa na kukabidhiwa kwa gari alilopanda katika siku ambayo alinusurika baada ya kupigwa risasi 16 mjini Dodoma.
Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki pia anataka hakikisho la serikali kuwa itamlipa gharama za matibabu aliyotumia, mafao yake kama mbunge wa zamani na kutathminiwa upya kwa kesi dhidi yake.
Bw Lissu alikuwa akizungumza na gazeti la Mwananchi kutoka nchini Ubelgiji ambako alikwenda kwanza kwa ajili ya matibabu mwezi wa Januari 2018 baada ya kushambuliwa na 'watu wasiojulikana' mjini Dodoma.

Chanzo cha picha, TWITTER/@SULUHUSAMIA
Kauli za Bw Tundu Lissu zinajiri wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu akiahidi kukutana kwa mazungumzo na viongozi wa upinzani nchini humo, jambo lililopokelewa vyema na viongozi wa upinzani.
Mara baada ya shambulio dhidi yake tarehe 7 Septemba, 2017, Bw Lissu alisafirishwa kwa ndege hadi katika Hospitali ya Nairobi Kenya ambako alipokea matibabu kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu maalumu.
Hatahivyo akizungumza mwaka jana Spika wa bunge la taifa Job Ndugai alisema Bw Lissu alipokea takriban shilingi milioni 500 za kitanzania kufikia mwezi Juni 2019 zikiwemo shilingi milioni 200 za mishahara yake na shilingi milioni 360 za posho akiwa Ubelgiji .

Akizungumza jana, Bw Lissu alisema anahofia sana uamuzi wa kumuondolea walinzi wa usalama wake ambao alipewa mwaka 2020 alipogombea kiti cha urais mwaka kupitia chama cha Chadema kwani uamuzi huo unatishia maisha yake.
"Baadaye nilikamatwa na kuachiliwa, kabla ya kukamilisha mchakato ambao uliniwezesha kutoroka nchi. Kwahiyo, ningependa kuwa na hakikisho katika suala hili kwasababu Rais Samia Suluhu Hassan anafahamu hili vyema baada ya kunitembelea katika Nairobi Hospital," alisema , na kuongeza kuwa ."Ninataka kujua watu waliojaribu kuniua, na usalama wangu nitakaporudi nyumbani. Je hizo kesi za…zitaendelea ? Na, ikiwa nitaruhusiwa kushiriki katika siasa."
Alisema angependa kujua hatma ya mafao yake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 wakati alipofahamishwa kuhusu kutostahili kwake kuwa mbunge wa Singida Mashariki.
"Pia sijapokea malipo ya gharama za matibabu( kutoka kwa serikali). Hili Rais Hassan ambaye alinitembelea katika hospitali ya Nairobi Hospital analifahamu . Ninahitaji kujua ni kwanini sijalipwa ,"alisisitiza.
Taarifa ya polisi.
Hatahivyo jana, Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania David Misime alisema uchunguzi juu kesi ya Bwana Lissu ulisimamishwa baada ya kukataa kujibu ombi la polisi la ushirikiano katika uchunguzi huo . "Hawezi kukamatwa … lakini anapaswa kueripoti na kutoa maelezo ."

Aidha Bw Misime alisema polisi wana wajibu wa kisheria wa kuwalinda watu na mali zao bila kujali utaifa wao, kutambua, kuzuia na kutekeleza sheria ili kuimarisha Amani, na usalama na mwingiliano.
"Amani endelevu na usalama huwawezesha wananchi wakiemo wageni kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, kwahiyo kama mtu , awe mkazi au mgeni anapanga kuja anakaribishwa ."
Alisema polisi wanatoa usalama kwa raia wote bila ubaguzi na upendeleo, akisema changamoto za kiuslama zinapaswa kuripotiwa kulingana na taratibu ili mamlaka husika zichukue hatua.












