Moto wa Cox Bazar: ‘Nilitaka kuwanusuru hata kama ningefariki dunia nikifanya hivyo’

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Moto mkubwa umesambaa katika kambi ya Rohingya katika eneo la Cox Bazar, Bangladesh. Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa watu 45,000 wamepoteza makazi yao huku wengine 15 wakifariki duniani na wengine 400 wakiwa hawajulikani walipo.
Wakati maelfu ya watu wakiwa wametatizika kwasababu ya moto huo, Saiful Arakani, 25, ambaye ni mkimbizi, alikimbilia moja kwa moja kwenye moto huo uliokuwa unafuka pasipo kifani kusaidia kutafuta manusura.
"Watu walikuwa wamegeuka na kuwa majivu mbele ya macho yangu," Saiful amesema.

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Akiwa pamoja na wengine waliojitolea, Saiful alitumia jaketi na blanketi kusaidia wale waliochomeka vibaya kwa moto.
Saiful, mtaalamu katika upigaji picha, alikuwa tu amebeba simu yake na akafanikiwa kupiga picha zinazoonesha uharibifu uliotokea.
"Nilianza kupiga picha huku nikiwa ninabubujikwa na machozi," alisema.
Picha zote alizopiga, zile mbaya zaidi zilikuwa zinaonesha vile watoto wadogo walivyochomeka vibaya, moja wao ikiwa ya mvulana aliyekuwa bado amelala kando ya mwanasesere wake aliyemshika vizuri kwenye tumbo.

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Makazi kwa karibu watu milioni moja wa kabila la Rohingya, eneo la Cox Bazar, kusini mashariki mwa Bangladesh, lina kambi 34. Makumi ya maelfu ya Warohingya walitoroka makazi yao katika eneo la Myanmar baada ya msako ulioshuhudia matukio ya kinyama uliotokea mwaka 2017.
Lakini kwasababu makazi yao yameshikana kwa karibu sana katika eneo la mlimani, moto ulipoanza katika kambi ya Kutalapalong Balukhali, ulisambaa kwa haraka sana.
Kwa Saiful, ilikuwa ni mchana wakati mama yake alipotoka nje na kuona moshi mkubwa wa rangi nyeusi na njano unafuka zaidi ya kilomita 2.
"Moto huo ulikuwa umepaa zaidi ya mita 30 kwenye anga," amesema. "Muda huo huo nikapanda teksi na kukimbia hadi eneo la tukio."

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Wakati anafika eneo la tukio, watu walikuwa wamekusanyika. Wengi walikuwa wanajaribu kutabiri moto huo unaelekea pande gani ya kambi.
"Niliona watu wanatoroka makazi yao huku wakiwa wanapaza sauti zao, 'Mnusuru mama yangu, mnusuru dada yangu.' Ilikuwa ni mtafaruku kila upande. Hakuna aliyejua cha kufanya," Saiful alisema.
Akiwa pamoja na waokozi ambao wamefika, mpigaji picha huyo alielekea eneo la tukio na kuona moshi mkubwa ukifuka na moja kwa moja akaanza kutafuta manusura.

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Na kile ambacho angekiona baada ya hapo, hawezi kukisahau milele, Saiful amesema.
"Niliona watu kama mimi wakibadilika na kuwa majivu. Nilitaka kuwasaidia. Nilitaka kuwanusuru, hata kama ingemaanisha nitakufa nikiwa ninafanya hivyo. Nilibeba watoto, wanawake na wanaume wazee, wote kupitia mikono yangi na mabegani. Wengi wao walikuwa wamejeruhiwa sana."
Wakati wa ghasia hizo, alimsikia mwanaume mmoja akipiga uyowe huku akiwa anasema, nisaidie.
"Jina lake lilikuwa Saleem. Umri wake ulikuwa karibu miaka 40. Alikuwa akilia, "Tafadhali, mnusuru binti yangu na mke yangu. Mimi niko hai lakini tafadhali muokoe binti yangu."
Baada ya kuishi katika kambi hizo kwa zaidi ya miaka minne, Saiful anasema anajua mtu anavyohisi akiwa ametengwa.

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Wakati magari kadhaa ya kubeba wagonjwa yalikuwa yamewasili, Saiful alianza kusaidia kuwaingiza walionusurika kwenye magari hayo. Anasema anachojua ni kwamba mmoja miongoni mwa aliowanusuru, alifariki dunia baadaye akiwa hospitali kwasababu ya majeraha mabaya aliokuwa amepata.
"Watu 10 walifariki dunia nikiwashuhudia kwa mcho yangu. Wanne walikuwa watoto wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na sita."

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Kufikia jioni, kiasi kikubwa cha moto ulikuwa umedhibitiwa na mashirika mengi ya kutoa msaada yakawa yameanza kushughulikia wale waliopoteza kila kitu.
Lakini kwa Saiful, alikuwa na mawazo mengi akilini.
"Sina uhakika kama nitalala usiku huu," alisema. "Vilio vya watoto wadogo na kina mama waliokuwa wamekata tamaa bado ninazisikia masikioni mwangu. Natamani kama ningeweza nikanusuru watu wengi zaidi."

Chanzo cha picha, Team Saiful Arakani
Pia unaweza kutazama:













