Wakimbizi wa Rohingya: 'Miili ilikuwa inarushwa baharini usiku'

Illustration of Khadiza Begum’s portrait
Maelezo ya picha, Khadiza alikimbia Myanmar baada ya mume wake na kijana wa kiume kuuawa
    • Author, Swaminathan Natarajan and Moazzem Hossain
    • Nafasi, BBC World Service

"Hakuna anayejua ni watu wangapi wamekufa. Inaweza kuwa 50 au hata zaidi," anakumbuka Khadiza Begum.

Mwanamke huyo, 50, alikuwa miongoni mwa waislamu wa Rohingya 396 waliojaribu kuingia Malaysia lakini hatimaye wakarejea pwani ya Bangladeshi baada ya boti iliokuwa imewabeba kushindwa kufika ufuoni na kuzunguka baharini kwa miezi miwili.

Idadi anayokadiria yeye ya waliokufa ni kutokana na mazishi ambapo kijana wake alikuwa imam, mhubiri wa Kiislamu katika boti hiyohiyo.

Wasafirishaji haramu wa watu hawakuwafikisha katika maeneo ambayo walikuwa tayari kuhatarisha maisha yao na waliokuwa wameyatama sana kufika.

Khadiza alilazimika kutoroka kwao nchini Myanmar kwasababu ya vurugu ambazo wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanazielezea kama mfano wa kitabu cha kiada chenye simulizi ya ''utakaso wa kikabila.''

Nchi jirani ya Bangladesh ilimpa makazi na kukubali Waislamu raia wa Rohigya eneo ambalo sasa hivi linafahamika kama kambi kubwa zaidi duniani ya wakimbizi.

Karibia raia milioni moja wa Rohingya wamehifadhiwa katika eneo la Cox Bazar nchini Bangladesh, na baadhi yao kama vile Khadiza, bado wana ndoto ya kuwa na maisha mazuri nchini Malaysia, iliopo katika ghuba ya Bengal.

Illustration of a boat full of people
Maelezo ya picha, Boti la wakimbizi lilikuwa limebeba watu kuwapeleka Malaysia

Lakini kwa Khadiza, ndoto yake ilibadilika na kuwa jinamizi.

Anakumbuka vile timu nzima - ya wasafirishaji binadamu kwa njia haramu - walivyojaribu kuficha ukweli wa idadi ya waliokuwa wamekufa ndani ya boti lililowasafirisha ambalo lao lilikuwa na watu kupita kiasi.

"Walikuwa wanaendesha injini zote mbili ili wasafiri wasisikie sauti ya maji wakati miili ya watu inaporushwa baharini."

Anasema, miili hiyo ilikuwa inarushwa usiku: "Ninachojua kwa uhakika ni kwamba wanawake 14 hadi 15 walikufa."

Kifo cha mwanamke ambaye alikuwa ameketi karibu na Khadiza bado kinampa mfadhaiko wa akili. Akiwa amechanganyikiwa, mwanamke huyo alianza kuonesha tabia za ajabu ajabu. Wamiliki wa boti walimpeleka eneo la juu ambapo Khadiza anasema alikufa.

"Bado kifo chake kinanisumbua akili. Alikufa mbele ya macho yetu."

The woman had four children with her. "My son informed the eldest daughter, just 16 years old, that her mother had died."

Mwanamke huyo alikuwa amebeba watoto wake wanne. "Mtoto wangu wa kiume akamfahamisha msichana wake mkubwa mwenye umri wa miaka 16 pekee, kwamba mama yake amekufa."

Illustration of a boat alone in the open sea
Maelezo ya picha, Boti llililokuwa limebeba Khadiza lilikuwa majini kwa miezi miwili

Mwanamke huyo alikuwa amebeba watoto wake wanne. "Mtoto wangu wa kiume akamfahamisha msichana wake mkubwa mwenye umri wa miaka 16 pekee, kwamba mama yake amekufa."

"Watoto wengine watatu wa mama huyo hawakujua kilichokuwa kimemtokea mama yao." anasema. "Walikuwa wanalia tu. Lilikuwa tukio la kuhuzunisha sana.

"Mara moja mwili wake ukarushwa baharini."

Khadiza ni mama wa watoto wanne pia yeye. Aliachwa bila makazi 2017 baada ya mume wake na mmoja kati ya vijana zake kuuawa katika oparesheni iliyokuwa inatekelezwa jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Kijiji chake kilichomwa, na akalazimika kwenda Bangladesh na kuanza maisha mapya katika kambi ya wakimbizi ya Cox Bazar pamoja na watoto wake.

Baada ya kumuoza msichana wake mkubwa, alitamani sana vijana wake waliosalia kuwa na maisha mazuri. "Maisha yetu yalikuwa magumu. Sikuona namna yoyote ile ya kuwa na maisha mazuri tukiwa kwenye kambi ya wakimbizi."

Maelezo ya video, Watch: Rohingya ni kina nani?

Simulizi alizozisikia kuhusu raia wa Rohingya waliovuka bahari na kuingia Malaysia kutafuta maisha ni jambo lililompa hamasa sana. Khadiza aliuza vito vyake vyote vya thamani ya $750 (£610) ili kulipa wasafirishaji haramu ambao waliwatafuta boti la usafiri.

Kisha usiku mmoja Februari, akapokea simu ambayo amekuwa akiisubiri kwa hamu.

Aliamua kuficha nia yake na kuweka vito vyake vya thamani na nguo kwenye begi dogo. "Niliwaambia rafiki zangu na jirani zangu kwamba ninakwenda kupata matibabu," ameiambia BBC.

Akiwa na kijana wake wa kike na kiume tayari kuondoka, Khadiza alifunga nyumba yao na kuondoka usiku ule.

Mwanamme mmoja aliwapokea katika stendi ya basi, na kuwaongoza hadi kwenye shamba moja ambapo walikuwa na mamia ya watu wengine.

Kundi hilo lilipelekwa kwenye boti ambayo ilianza kuondoka taratibu katika ghuba ya Bengal kati ya visiwa vya Saint Marin huko Bangladesh na Akiab upande wa Myanmar.

"Ni jambo ambalo nilikuwa nimelipanga kwa miezi kadhaa. Nilitamani sana kuwa na maisha mazuri. Nilikuwa na ndoto ya kuanza maisha mapya katika nchi mpya," anasema.

Illustration of Khadiza Begum in the foreground and her son in prayer with children next to him
Maelezo ya picha, Kijana wa Khadiza aliongoza ibada ya waliokufa ndani ya boti

Baada ya siku mbili walihamishwa katika boti jingine: kubwa kuliko la awali ambalo lilikuwa limejaa watu.

Khadiza anasema hakuwa hata na nafasi ya kunyoosha miguu yake: "Kulikuwa na familia zilizokuwa na wanawake na watoto. Nafikiri kulikuwa na watu zaidi ya 500."

Boti lilikuwa kubwa kuliko lile linalotumika Kusini mwa Asia lakini halikuwa kubwa kutosha watu wote waliokuwepo.

Wenye boti walikuwa sehemu ya juu, wanawake walikuwa katikati huku wanaume wakawa sehemu ya chini. Cha kushangaza ni kwamba wenye boti walikuwa raia wa Kiburma kutoka Mynmar - nchi ambayo Warohingya walikuwa wamefukuzwa.

"Awali nilikuwa ninaogopa," Khadiza anakumbuka. "Sikujua hatma yetu itakuwaje, lakini kadiri siku zilivyosonga na mambo kuanza kusonga nikaanza tena kuwa na ndoto zangu.

"Nilifikiri kwamba tutakuwa na maisha bora. Na changamoto yoyote ile ambayo tulikuwa tunaipitia kwangu hilo lilikuwa la muda tu."

Boti hiyo haikuwa na vifaa vya msingi kama vile maji na usafi ulikuwa duni. Khadiza anakumbuka fika kwamba katika safari yake hiyo, alioga mara mbili tu katika kipindi cha miezi miwili kwa kuchota maji kutoka baharini mbele ya wengine.

Vyoo vilikuwa vimejengwa kwa mbao mbili na shimo katikati.

"Siku chache baada ya kuanza safari yetu kwenda Malaysia, mvulana mmoja alianguka kwenye shimo hilo na kutumbukia baharini," Khadiza anakumbuka.

Huo ulikuwa mwanzo wa vifo vingu tu alivyoshuhudia.

Illustration of a boat on a shore
Maelezo ya picha, Khadiza anaamini kwamba karibia watu 50 walikufa wakiwa safarini

Baada ya kuwa safarini baharini kwa siku saba, wakati mwengine hali ya hewa ikiwa ni mbaya, hatimaye wakafika pwani ya Malaysia. Hapa walikuwa wanatarajia boti ndogo zitakazowapeleka hadi nchi kavu.

Lakini hakuna boti hsts moja iliyowasili.

Mlipuko wa virusi vya corona ulikuwa umesababisha usalama mipakani kuimarishwa huku walinzi wa Pwani wakishika doria kila wakati, na kufanya iwe vigumu kuingia nchini humo kisiri.

Nahodha aliwaambia wakimbizi hao kwamba hawataweza kufika nchi kavu upande wa Malaysia. Matumaini ya Khadiza yakawa yamedidimizwa na janga la corona.

Wenyeji wao wakaamua kusalimu amri lakini wakakumbwa na ukosefu wa chakula na maji.

Wakiwa njiani kuelekea Malaysia, wakimbizi hao walikuwa wakipewa wali mara mbili kwa siku, wakati mwengine na dengu na kikombe cha maji ya kunywa.

"Mara ya kwanza walikuwa wanapata mlo mmoja kwa siku. Kisha ikawa ni mlo mmoja baada ya siku mbili - wali mkavu bila chengine chochote," Khadiza anakumbuka.

Ukosefu wa maji ya kunywa ikawa ni jambo sasa ambalo haliwezi tena kuzuilika.

Khadiza anasema kwamba wakiwa wamekataa tamaa, baadhi ya wakimbizi walikunywa maji ya baharini : "Watu walijaribu kukata kiu kwa kutia nguo zao ndani ya maji, na kuzikamua ili wapate matone tu ya maji hayo mdomoni."

Maelezo ya video, Serikali ya Malaysia iliwafukuza wakimbizi wa WaRohingya kwa hofu ya virusi vya corona

Siku kadhaa baadae, kando ya pwani ya Thailand, boti dogo lililokuwa limetafutwa na wasafirishaji haramu wa binadamu likaleta bidhaa za msingi.

Lakini wakati wanasubiri fursa nyengine kuingia Malaysia, jeshi la Burma likawakamata.

"Walimshika nahodha na timu yake ya watu watatu lakini baadae wakaachiliwa huru," Khadiza anasema. "Naona pengine waliafikiana makubaliano fulani."

Jaribio lao la pili na la mwisho kuingia Malaysia pia nalo likafikia ukomo wake. Kila mmoja aliyekuwa kwenye boti akajua kwamba sasa hakuna mahali wanakokwenda zaidi ya walipofika.

"Tulikuwa tunazunguka tu baharini bila matumaini hata ya kufika ufuoni. Watu sasa walianza kukata tamaa. Tulikuwa tu tunajiuliza tutaendelea na maisha haya hadi lini."

Kwahiyo, kundi moja la wahamiaji likaenda juu kwa wamiliki wa boti na kuwaomba wawashukishe popote ama kuwe Myanmar au Bangladesh popote pale.

Lakini wengine walikataa, na kuamini kwamba hatua hiyo ilikuwa hatari mnoo. Wangeweza kukamatwa na boti lao kuchukuliwa.

Wakati boti lilikuwa linatembea tu katika ghuba ya Bengal bila ya kuwa na pakwenda, kukaaanza kusambaa taarifa za wenye boti kutekelezaji ubakaji na mateso.

"Mambo yakanza kuwa mabaya na kushindwa kudhibitiwa," Khadiza anasema. "Nasikia kwamba mmoja wa wamiliki alishambuliwa na kuuawa - na mwili wake ukatupwa baharini."

Kulikuwa na watu kumi kutoka Burma wamiliki wa boti ambao walikuwa wanatunza wakimbizi karibia 400. "Wakagundua kwamba itakuwa vigumu kwao kupigana vita na kushinda," anasema.

Wamiliki walitaka pesa zaidi ili kukomboa boti dogo ambalo lingewapeleka hadi eneo la nchi kavu. Wakimbizi hao wakachanga na kufikisha $1,200.

Baada ya siku kadhaa, boti dogo likafika. Na mara moja, nahodha na wamiliki wengine wakawa wa kwanza kuingia kwenye boti hilo.

Wale waliosalia kwa usaidizi wa wamiliki wawili walipanda boti na kuanza kurejea Bangladesh.

Khadiza Begum, a Rohingya Muslim refugee
Maelezo ya picha, Khadiza Begum kwa sasa hivi amerejea katika kambi ya wakimbizi huko Bangladesh akiwa ni mwenye kufadhaishwa na kile alichopitia

"Nilikuwa na furaha sana baada ya kuona eneo la pwani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi miwili." Khadiza anakumbuka.

Wakarejea tena Bangladesh. Baada ya kuona watu walivyokuwa na hali zao zikiwa mbaya, wenyeji waliwafahamisha walinzi wa Pwani wa Bangladesh.

Baada ya kuwa kwenye karantini kwa wiki mbili, Khadiza alirejea kwenye kambi ya wakimbizi, lakini eneo alilokuwa anaishi akapata tayari kuna familia nyengine inayoishi eneo hilo.

Kwa hiyo ana matumaini ya kurejea Myanmar na kuanza tena maisha katika nchi ambayo wakati fulani alikuwa hata analima.

Kwa sasa hivi, ile sehemu ndogo aliyonayo, analazimika kuishi pamoja na msichana wake na kijana wake.

"Nilipoteza kila kitu kwasababu tu ya ndoto yangu," anasema, akitafakari yaliyomkuta. "Usiwahi kufanya makosa kama yangu."

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video, Wakimbizi wa Rohingya 'walazimika kunywa maji ya bahari kuokoa maisha' baada ya kufurushwa