Iceland: Taifa ambalo limerekodi zaidi ya mitetemeko 40,000 ya ardhi chini ya mwezi mmoja

Grindavik ni eneo lenye milipuko mingi ya volakano

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Grindavik ni eneo lenye milipuko mingi ya volakano

Wakazi wa Grindavik, kijiji cha wavuvi chenye idadi ya watu 3,500 kusini mashariki mwa Iceland, wamekuwa wakilalamika kutoweza kulala.

Sio kwa sababu ya usumbufu wowote wa mwili au akili, lakini kwa sababu ya idadi ya mitetemeko ambayo imesajiliwa hivi karibuni na ambayo imekuwa ikiwaamsha wakati wa usiku; zaidi ya 40,000 ikisajiliwa katika wiki tatu zilizopita

Grindavik iko kwenye peninsula ya Reykjanes, karibu kilomita 60 kutoka mji mkuu Reykjavik. Ni mkoa unaojulikana kwa mitetemeko , kwa sababu ni sehemu ya mfumo wa volkano.

Hatahivyo, masafa ya mitetemeko ya ardhi imeongezeka sana tangu mwaka jana na kwa kushangaza mwezi uliopita.

"Yote ilianza Februari 24 baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.7," Njala Gudmundsdottir, mratibu wa habari wa Ofisi ya Hali ya Hewa ya Iceland (IMO), aliiambia BBC Mundo Bergthora.

Kristin Vogfjord, mkurugenzi wa sayansi katika kituo cha hali Hewa cha Iceland , amesema kuna ongezeko la matetemeko ya ardhi katika mkoa huo.

Mwaka 2019, takriban mitetemeko 3,400 ilirekodiwa ,mwaka 2020 ikarekodi mitetemeko 34,000, lakini tangu mwezi Februari tarehe 24 mwaka huu, mitetemeko miwili ilio na ukubwa Zaidi wa 5 katika vipimo vya Richa ilifuatiliwa na msururu wa mitetemeko 40,000 kufikia sasa.

Sio mitetemeko yote imekuwa ya kiwango sawa, lakini kumekuwa na angalau 60 ya ukubwa zaidi ya 4, Gudmundsdottir alisema.

Wanasayansi wa IMO wanakadiria kuwa kutakuwa na mlipuko hivi karibuni, lakini hawatarajii kutokea kwa janga.

''Mfumo huu umekuwa kile tunachokiita vitendo vya wastani kwa takriban miaka 8000 iliopita, anaelezea Gudmundsdottir. Milipuko ya mwisho ambayo tunaifahamu ilifanyika karne ya 12 wakati ambapo kulikuwa na milipuko mikubwa''.

Wakati wa milipuko ya volcano , hawatarajii itoe jivu jingi kama lile la volcano ya Eyjafjallajökull mwaka 2010.

Wakati huo jivu jingi lilirushwa angani ambapo takriban safari za ndege 900,000 zilisitishwa huku mamia ya raia wa Iceland wakilazimika kutafuta hifadhi.

Kile wanachoona sasa, kama ilivyoelezewa na afisa wa IMO, ni "milipuko ya basaltic ambayo hutoa mtiririko wa lava polepole kwa kilomita kadhaa''.

Kristin Vogfjord, mkurugenzi wa sayansi ya ardhi katika kituo cha hali ya hewa cha Iceland

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kristin Vogfjord, mkurugenzi wa sayansi ya ardhi katika kituo cha hali ya hewa cha Iceland

Wamechoka Zaidi ya kuogopa

Hatahivyo , wataalamu wanatambua kwamba athari hizo zinaweza kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine na sio kila mtu anafurahia kiwango cha mitetemeko hiyo.

"Tuna ripoti za watu ambao wamechoka na hawaogopi tena kwasababu wanaamka usiku," Gudmundsdottir alisema.

" Ni kama kutembea kwenye daraja dhaifu , "mkazi wa Grindavik alielezea hali hiyo kwa shirika la habari la Reuters.

Mlipuko wa volkano kama ule wa Eyjafjallajökull 2010 hautarajiwi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mlipuko wa volkano kama ule wa Eyjafjallajökull 2010 hautarajiwi

Rannveig Gudmundsdottir, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, alielezea Reuters kuwa kila mtu katika kijiji amechoka.

"Wakati naenda kulala usiku, kitu pekee ninachoweza kufikiria ni: je! Nitaweza kulala usiku wa leo?"

Wakazi kadhaa wameenda kutembelea jamaa, wamehamia kwenye nyumba zao za majira ya joto, au vyumba vya kukodisha katika hoteli za Reykjavik ili kupumzika kidogo.

Kwengineko, watu wanaamini mipango ya mamlaka na wanaendelea na maisha yao ya kila siku.

Ni nini hufanyika katika maeneo mengine yenye mitetemeko ya ardhi?

Sababu ya mitetemeko iliyopatikana katika wiki za hivi karibuni huko Iceland inatokana na mtiririko wa mwamba ulioyeyushwa, unaojulikana kama magma

Magma inasonga kilomita moja chini ya peninsula, ikijaribu kutafuta njia ya kujitoa sakafuni.

''Kwa jumla ni kwamba mitetemeko hiyo inahusishwa na milipuko ya volcano katika eneo hilo'', alisema afisa wa idara ya habari katika chuo cha utafiti wa ardhini nchini Marekani (USGS).

Msichana mdogo akitazama ziwa lililotengezwa na mlipuko wa volakano

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Msichana mdogo akitazama ziwa lililotengezwa na mlipuko wa volakano

Ni kitu tofauti ya kinachotokea katika maeneo mengine ambayo ni maarufu kwa mkitetemeko mikubwa kama vile Mexico na Chile.

Mitetemeko ya maeneo hayo hutokea kutokana na sahani mbili ardhini kugongana na moja kuisukuma nyengine.