Amazon: Mambo matano kumhusu Andy Jassy

Andy Jassy

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Andy Jassy amekuwa Amazon tangu mwaka 1997

Jeff Bezos anajiondoa katika wadhifa wa mkuu wa Amazon baadaye mwaka huu lakini utendakazi wake utaendelea kusalia katika kumbukumbu za wengi hasa baada ya kusonga mbele hadi kuwa tajiri wa kwanza duniani.

Lakini je anayechukua nafasi yake, ni mtu wa aina gani?

Andy Jassy, 53, inasemekana kwamba ni mtu wa karibu sana wa Bezos, na amekuwa kiungo muhimu katika mafanikio ya kampuni hiyo miaka ya hivi karibuni.

Fahamu mambo matano kumhusu Bwana Jassy:

1. Amekuwa Amazon kwa kipindi cha muda mrefu

Bwana Jassy, alikulia Scarsdale, jimbo la New York, alijiunga na Amazon mwaka 1997, miaka mitatu baada ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo.

"Nilifanya mtihani wangu wa mwisho wa chuo kikuu cha Harvard Business School, Ijumaa ya kwanza ya Mei mwaka 1997 na nikaanza kufanyakazi katika kampuni ya Amazon," Jassy alisema.

"Hakuna, sikujua kazi yangu itakuwa gani, au ningepewa nafasi gani ya uongozi. Lakini muhimu zaidi ilikuwa ni kuwa pamoja na jamii ya Amazon siku ile Jumatatu."

Baada ya kufanyakazi kama msaidizi wa kiufundi wa Bwana Bezos akaanzisha kitengo cha uhifadhi wa data, katika mtandao wa Amazon mwaka 2006 ambao umekuwa na mafanikio makubwa chini ya uongozi wake.

Inasemekana kuwa Bwana Jassy, ndio mwenye uwezekano mkubwa wa kuwa mrithi wa Bwana Bezos kwa muda lakini pia alitangazwa mkuu wa gazeti la Washington Post mnamo mwezi Septemba baada ya Jeff Wilke, kiongozi biashara za watumiaji wa Amazon, kutangaza kuwa atastaafu.

2. Amekuwa akiunga mkono masuala ya kijamii

Tofauti na Bwana Bezos, Bwana Jassy mara kwa mara huzungumzia masuala ya jamii. Mnamo mwezi Septemba aliandika ujumbe kwenye Twitter juu ya umuhimu wa polisi kuwajibika baada ya Breonna Taylor, mwanamke mweusi kupigwa risasi hadi kufa akiwa nyumbani kwake na polisi mzungu wakati wa uvamizi uliofanywa na polisi ambao ulifeli.

"Ikiwa idara za polisi hazitaanza kuwajibika kwa mauaji ya watu weusi, haki haitawahi kutendeka na hakutawahi kuwa na mabadiliko," alisema.

Pia anaunga mkono mapenzi ya jinsia moja na mabadiliko ya uhamiaji lakini akaangaziwa na umma alipotetea programu ya utambuzi wa sura ya Amazon kwa polisi na serikali za kigeni.

Akizungumzia wasiwasi wa kimaadili mwaka jana, alisema watu wanaotumia teknolojia wanastahili pia kuwajibika, "na ikiwa wataitumia kwa kutowajibika, ni lazima wawajibishwe".

A protest against Amazon

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kumekuwa na maandamano dhidi ya kampuni ya Amazon kuwezesha programu ya utambulizi kwa polisi lakini Bwana Jassy akatetea uamuzi huo

3. Alifanikiwa kubadilisha timu ya uhifadhi wa data kuwa na mafanikio makubwa

Sio siri kuwa huduma za tovuti ya Amazon, kitengo cha uhifadhi wa data ndio chenye mapato makubwa sana kwa Amazon na Bwana Jassy alikuwa muhimu katika kufikiwa kwa hatua hiyo.

Sasa hivi kitengo hicho kinamiliki asilimia 30 ya hisa ya soko hilo kwa utoaji wa huduma ya uhifadhi wa data kwa makampuni makubwa kama MCDonald na Netflix.

Lakini pia inakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa kampuni kubwa kubwa za mawasiliano kama vile Google na Microsoft.

4. Anapenda muziki na michezo

Bwana Jassy, ambaye ameoa na kujaaliwa watoto wawili, ni shabiki mkubwa wa muziki. Anapenda kuwa matukio yenye muziki unaochezwa moja kwa moja na pia hupenda kuchagua nyimbo za kuchezwa.

Pia aliwahi kuwa msimamizi wa bendi moja ya muziki kabla ya kujiunga na Amazon na anasema ana shauku ya kipekee ya kutambua wasanii wapya wenye vipaji.

"Tangu nikiwa kijana, Nilikuwa nikihudhuria matasha mengi sana hata nikiwa shule ya sekondari," alizungumza na CRN mwaka 2019.

Pia anapenda michezo kiasi kwamba ana miliki kwa kiasi fulani timu ya mpira wa magongo katika eneo lake la nyumbani pamoja na mtayarishaji wa filamu Jerry Bruckheimer na mwekezaji bilionea David Bonderman.

5. Inasemekana kuwa thamani yake ni dola milioni 394

Juhudi za Bwana Jassy katika kampuni ya Amazon na inasemekana kwamba thamani yake ni takriban dola milioni 394 ni Novemba 2020.

Bado haijulikani mshahara wake utakuwa ni pesa ngapi lakini kuna uwezekani mkubwa ukaongezeka.

Kulingana na wasifu wa gazeti la Business Insider mwaka jana, Bwana Jassy anapendwa sana na wafanyakazi wake na anaelezwa kama mtu ambaye anawasiliana na kuzungumza na wafanyakazi wenzake kwa uhuru.