Brexit: Boris Johnson apongeza mkataba uliyofikiwa kati ya Uingereza na EU

Chanzo cha picha, Downing Street
Uingereza na Muungano wa Ulaya zimefikia makataba wa baada ya -Brexit kumaliza mvutano wa miezi kadhaa kuhusu kanuni za biashara na haki ya uvuvi.
Katika mzungumzo na wanahabari Downing Street, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema: "Tumechukua tena udhibiti wa sheria zetu na hatima yetu."
Bw. Johnson ameongeza kuwa japo mashauriano yalikuwa "makali" ulikuwa "mkataba mzuri kwa Ulaya nzima", utakaobuni nafasi za kazi na ustawi.
Mkuu wa Muungano wa Ulaya (EU) Ursula von der Leyen amesema ulikuwa mkataba wa "haki na usawa".
Katika mkutano na waadishi wa habari mjini Brussels, Rais wa Tume ya Ulaya amesema: "Huu ulikuwa mchakato mrefu lakini hatimaye tumefikia mkataba.
"Ni mkataba mzuri, uliyo na usawa, na jimbo zuri kwa pande zote."
Aliongeza kuwa sasa "ni wakati wa kuangazia hatua inayofuata" na kuongeza kuwa Uingereza "itasalia kuwa mshirika wa kuaminika".
Kutakuwa na kipindi cha miaka tano na nusu cha mpito kwa sekta ya uvuvi, alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
'Kulinda ajira'
Ushirikiano utaendelea kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, kawi, usalama na usafiri.
Akiashiria kauli mbiu ya uchaguzi mkuu wa Bw Johnson, iliongeza "tumemaliza Brexit".
Bwana Johnson alituma picha yake akitabasamu na vidole gumba vyote vikiwa vimeinuliwa hewani.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, alisema: "Tumekamilisha mpango mkubwa zaidi utakaogharimu pauni bilioni 668 kwa mwaka.
"Mkataba kamili wa mitindo ya Canada umefikiwa kati ya Uingereza na EU. Mkataba ambao utalinda ajira kote nchini, ambayo itawezesha bidhaa za Uingereza kuuzwa bila ushuru, bila upendeleo katika soko la EU.
"Mkataba ambao utaruhusu kampuni zetu kufanya biashara zaidi na marafiki wetu wa Ulaya."
Amesema anatumai Bunge la Uingereza litarejelea vikao vyake mnamo 30 Desemba kupiga kura juu ya mpango huo - pia itahitaji kupitishwa na Bunge la Ulaya.
Chama cha upinzani Labour - ambacho kinatarajiwa sana kuunga mkono makubaliano hayo - kimesema kitatoa kauli yake rasmi "kwa wakati unaofaa"
Mpango huo imewapa afueni kubwa kwa wafanyabiashara wengi wa Uingereza, ambao tayari wanaathirika kutokana na athari za janga la corona, waliyokuw wakihofia kutatizika mipaka wakati Uingereza itakapojiondoa katika sheria za biashara za EU Alhamisi ijayo.












