Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ethiopia: Mkurugenzi wa WHO ashutumiwa kuunga mkono viongozi wa Tigray
Mkuu wa majeshi ya Ethiopia amemshutumu Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani kwa kufanya ushawishi kwa maslahi ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), kinachopambana na majeshi ya serikali.
Mamia wameuawa katika mzozo jimboni Tigray tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba.
Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus anatoka katika jamii ya Watigray na alikuwa waziri wa afya katika serikali iliyopita ya Ethiopia,iliyoongozwa na TPLF.
Hajajibu ombi la BBC kujibu shutuma hizo.
Jenerali Berhanu Jula amesema kuwenye mkutano na wanahabari kuwa Dkt Tedros "anafanya kila awezalo" kuunga mkono chama cha TPLF na kuwasaidia kupata silaha lakini hajatoa ushahidi kuhusu tuhuma hizo.
"Hatumtarajii kuunga mkono Waethiopia na kukemea watu hawa. Amekuwa akifanya kila kitu kuwaunga mkono, amefanya kampeni ili nchi jirani zikemee vita," alisema Jenerali Berhanu.
"Amewafanyia kazi ili wapate silaha."
Baada ya kuchaguliwa kuongoza WHO mwaka 2017, Dkt Tedros alifahamika vyema janga la virusi vya corona lilipoanza na kwa sasa anaelezwa kuwa mtu wa jamii ya Tigray anayefahamika sana nje.
Wakati huo huo, msaidizi wa sera ya mambo ya nje wa Rais mteule wa Joe Biden ametoa wito kwa pande zote mbili kumaliza mapigano.
"Nina wasiwasi mkubwa juu ya mgogoro wa kibinadamu nchini Ethiopia, ripoti za vurugu za wenyewe kwa wenyewe , na hatari kwa amani na usalama wa kikanda," Antony Blinken aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter.
Haya yanajiri wakati Ethiopia ikiwa imetoa hati ya kukamatwa kwanza maafisa 76 wa kijeshi wanaotuhumiwa kushirikiana na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Vikosi vitiifu kwa chama hicho vinapigana na serikali katika jimbo la Tigray .
Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema majeshi yake yanaelekea mji mkuu, Mekelle.
Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na maelfu wengine kutoroka eneo hilo baada ya wiki mbili za makabiliano.
Kuthibitisha hali ilivyo katika Jimbo la Tigray ni vigumu kwasababu huduma za mawasiliano zimekatizwa.
Ni yapi yanayojiri kwa sasa?
Siku ya Jumatano mamlaka za polisi katika serikali kuu zilitoa hati ya kukamatwa kwa maafisa 76 wa kijeshi, baadhi yao wanadaiwa kustaafu. Wanatuhumiwa kushirikiana na TPLF "kutekeleza uhaini", kwa mujibu wa shirika la AFP .
Akizungumza na BBC, Billene Seyoum - msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed - alipinga madai kwamba watu kutoka jamii yaTigrinya katika maeneo mengine nchini wanakamatwa kwa misingi ya kikabila.
Lakini amekiri kuwa watu kadhaa wanazuiliwa kwa kuwa wanachama wa kile alichokiita mtandao wa uhalifu.
Taarifa hizo zinakuja baada ya vikosi vya serikali kuteka miji ya Shire na Axum baada ya makataa ya siku tatu iliyotolewa na Waziri Mkuu Abiy kwa vikosi vya Tigray kujisalimisha kuisha siku ya Jumanne.