Glen Snyman: Mwanaume ashutumiwa kudanganya asili yake ili kupata ajira

Chanzo cha picha, PEOPLE AGAINST RACE CLASSIFICATION
Mwalimu mmoja nchini Afrika Kusini ameitwa kwenye kamati ya maadili, akishutumiwa kwa udanganyifu, kwa kujitambulisha kuwa yeye ni 'Mwafrika' katika maombi ya kazi
Glen Snyman ni mtu mwenye asili ya mchanganyiko- kama wanavyotambuliwa na watu tangu nchi hiyo ilipokuwa chini ya utawala wa watu weupe.
Ni mwanzilishi wa kundi la harakati la Watu dhidi ya mgawanyo wa matabaka.
Anapinga matumizi ya matabaka ya rangi: ''weusi'', ''rangi mchanganyiko'' ''asili ya India'' na ''weupe'' katika nyaraka mbalimbali , ikiwemo fomu za kuomba kazi.
Taarifa hizi hutumika kwa ajili ya kufuatilia majaribio ya kuwapa nafasi zaidi wale waliokabiliwa na ubaguzi wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi .
Tangu mwaka 2010 Snyman amekuwa akifanya kampeni dhidi ya matumizi ya kipengele cha rangi , akisema kuwa anajitambua kuwa ''kwanza '' kama raia wa Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Times Live mwalimu wa shule ya msingi alijitambulisha kuwa yeye ni ''Mwafrika'' alipokuwa akiomba nafasi ya kazi ya kuwa mwalimu mkuu mwaka 2017. Taarifa inasema hakupata kazi.
Tovuti hiyo inaripoti kuwa imeona hati ya mashtaka kwa mamlaka za kielimu huko Western Cape ikimshutumu Bwana Snyman kwa udanganyifu.
''Umevunja sheria kwa kufanya udanganyifu kwa kutoa maelezo yako ukiomba kazi ya ualimu mkuu katika Shule ya Sekondari ya Fezekile ukisema kuwa wewe ni mwanaume Mwafrika, wakati ukweli wewe ni mwenye asili ya mchanganyiko na kuwa ulifanya kitendo hicho ili upate faida ya kuchaguliwa,'' hati ya mashtaka ilieleza.
Bwana Snyman hajasema chochote kuhusu suala hilo.
Uchambuzi wa Pumza Fihlani, mwandishi wa habari Kusini mwa Afrika
Bwana Snyman anatuhumiwa kujaribu kunufaika na mfumo huo bila haki. Kwa nini? Kweli, uainishaji wa rangi bado ni muhimu nchini Afrika Kusini miaka 26 baada ya kumalizika kwa utawala wa wazungu.
Sera mpya zilizoanzishwa na kuzaliwa kwa demokrasia zililenga kugeuza baadhi ya dhuluma nyingi za utawala wa ubaguzi wa rangi - dhuluma ambazo ukali wake ulitokana na rangi ya watu.
Kwa urahisi, kadiri unavyokuwa ukifanana na asili nyeupe ilikuwa mbaya zaidi.
Ikiwa unafikiria tabaka, watu weusi au wale walioitwa Waafrika walikuwa kwenye tabaka la ngazi ya chini. Watu wa rangi (au wenye mchanganyiko wa jamii) na watu wa Kihindi waliwekwa juu kwenye tabaka chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Hii haimaanishi kuwa hawakubaguliwa - bali walipendelewa kuliko Waafrika.
Katika Afrika Kusini ya leo, wengine wamesema mabadiliko yamekuwa polepole na hata kushiriki fursa imekuwa hatua ya polepole.
Na taasisi nyingi zinazotaka kushughulikia usawa zinalipa kipaumbele zaidi kwa kufikiria zinamuajiri nani - ikimaanisha rangi ya ngozi zao.
Wanasema hatua hii hailengi kupuuza sifa bali ni kuhakikisha tu kwamba watu hao hawaachwi kama ilivyokuwa mazoea hapo zamani.
Wakati wa kuomba kazi hii inaweza kumaanisha kuelezea rangi yako na hata jinsia kwa machapisho fulani, haswa kazi za serikali.
Lakini sera za rangi zimesababisha utata- watu wachache nchini Afrika Kusini wamezielezea kama "ubaguzi wa rangi".
Kesi ya Bwana Snyman hata hivyo imeibua maswali kuhusu namna watu wanavyochagua utambulisho wao, namna gani wanavyojitambulisha katika nchi ambayo suala la rangi limekuwa kama silaha ya ukandamizaji kwa karne. Ni swali kubwa.












