Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bwana Rusesabagina ni miongoni mwa majina yaliyopo kwenye waranti ya kimataifa
Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kwamba mpinzani wake mkuu Paul Rusesabagina alidanganywa akajileta mwenyewe nchini Rwanda.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu Rusesabagina kuoneshwa kwa vyombo vya habari wiki iliyopita,Rais Kagame amesema kwamba lazima Rusesabagina awajibishwe kuhusu mauaji dhidi ya raia wa Rwanda kufuatia mashambulio ya makundi ya waasi anayoongoza yaliyofanywa dhidi ya maeneo ya Rwanda miaka miwili iliyopita.
Rusesabagina alifahamika kufuatia filamu ya Hotel Rwanda ikielezea jinsi alivyookoa maisha ya watutsi waliokuwa wamekimbilia katika hoteli moja mjini Kigali aliyokuwa meneja wake mwaka 1994.
Akizungumza kupitia runinga ya taifa,Rais Paul Kagame amesema kikubwa siyo ushujaa wa Bwana Rusesabagina au vitendo vyake wakati wa mauaji ya kimbari akisema kinachoangaliwa kwa sasa ni yeye
kuwajibishwa kuhusu kwa vitendo alivyotaja kuwa vya mauaji dhidi ya raia wa Rwanda
Katika matangazo ya moja kwa moja kwa televisheni ya taifa Jumapili jioni, Bwana Kagame amesema kwamba hajali kuhusu hadithi ya Bwana Rusesabagina kwamba yeye ni shujaa wa mauaji ya kimbari na kwamba ''hilo si jambo ambalo litakalomkabili mahakamani''.
"Kuna maswali ambayo lazima atayajibu.kuna wanaomsaidia wakiwa Ulaya,Marekani na kwIngineko na ambao walimpandisha cheo na kumpa majina ya ushujaa.awe shujaa au la ,mimi sina wasi wasi na hilo.
''Kikubwa tunachoangalia hapa ni kuhusika kwake na mauaji dhidi ya wa raia wa Rwanda, damu ya wananchi wa Rwanda iliyoko mikononi mwake kutokana na yeye kuongoza makundi ya kigaidi, lazima atawajibishwa kwa hayo'' Alisema Rais Kagame.
Bwana Kagame amesema kuwa Paul Rusesabagina alikuwa kiongozi wa makundi ya watu wenye silaha, FNL miongoni mwao, na ambapo hivi karibuni lilianzisha mshambulizi dhidi ya Rwanda na ''kuua watu Kusini Magharibi''.
'' Rusesabagina ametoa maelezo kabla hajafika hapa, mwenyewe akisifia jambo hilo.'' Rais Kagame alisema.
Paul Rusesabagina, ni kiongozi wa muungano wa kisasa MRCD-Ubumwe ambacho Rwanda inauhusisha na mashambulio ya ugaidi yaliyowaua Wanyarwanda katika kituo cha polisi cha mjini Kigali.
Hajazungumza chochote kuhusu madai dhidi yake.
Rusesabagina ambaye alikuwa anaishi ukimbizini Marekani na Ubelgiji,kwa tukio la kushtukiza alioneshwa kwa vyombo vya habari jumatatu iliyopita katika ofisi za shirika la upelelezi la Rwanda.
Familia yake ilidai alitekwa nyara akiwa mjini Dubai,taarifa ambazo viongozi wa Dubai walikanusha.Hili ndilo limekuwa Jibu la Rais Kagame kuhusu jinsi Rusesabagina alivyofika Rwanda:
Akizungumza na BBC mtoto wa kike wa Bwana Rusesabagina -Anaïse Kanimba alisema :''alitekwa nyara alipokuwa safarini Dubai ", katika Muungano wa nchi za kiarabu (UAE).''
"Alifika Jumanne, ndio mara ya mwisho tulipozungumza nae akituambia kuwa amefika salama, hatukumsikia tena hadi tulipoona kuwa amekamatwa na utawala wa Rwanda.
"Hatujui alifikaje huko na kilichotokea, ndio maana tunafikiria kuwa alitekwa kwasababu asingeenda Rwanda kwa hiari yake."
kuhusu kufika kwake Kigali Rais Kagame alisema;
''Jibu ni rahisi sana,itakuwaje nikisema kwamba alijileta hapa mwenyewe? nani atalalamika? unaweza kujileta mwenyewe au ukadanganywa na kujileta.labda tatizo litakuwa kuwa alidanganywa.kilichotokea ni kama kupiga namba ya simu ukajikuta umejidanganya namba.Waliohusika na operesheni hiyo waliniambia kwamba hawakufanya kosa lolote''.
Magazeti ya Rwanda yamesema kwamba tayari Rusesabagina ameishapewa wakili wa kusimamia kesi yake ,anayefahamika kwa jina la David Rugaza .