Virusi vya corona: Kwanini chanjo ya corona iliotolewa na Urusi inatiliwa shaka?

Urusi imeidhinisha chanjo ya kwanza ya virusi vya corona duniani. Hatahivyo chanjo hiyo imezua wasiwasi na hofu miongoni mwa washikadau wengi wa afya duniani ikiwemo wataalamu.

Lakini kwanini inatiliwa shaka?

Afisi ya BBC nchini Urusi imesema kwamba nje na ndani ya taifa hilo watalaamu kadhaa na wachambuzi wameonesha hofu kwamba majaribio yake huenda hayakufikia viwango vinavyohitajika duniani - ikiwa ni juhudi za serikali kupata chanjo mbele ya mataifa mengine.

Rais wa Urusi aliagiza serikali mwezi Aprili kufanya maamuzi baada ya kubainika kwamba wanasayansi kutoka taasisi ya Gamaleya walijidunga dawa hiyo wakati walipokuwa katika awamu ya kuifanyia majaribio miongoni mwa wanyama.

Hatahivyo, mkurugenzi wa Taasisi hiyo Alexander Gintsburg, alielezea kwamba wafanyakazi wa taasisi hiyo walijidunga dawa ya majaribio ili kuweza kuiendeleza bila ya hatari ya maambukizi wakati wa mlipuko, akidai kwamba wanayansi hao hawakupatwa na madhara yoyote.

Idhaa hiyo ya BBC nchini Urusi inasema kwamba kuna ripoti za hivi karibuni kuwa baadhi ya wanachama wa jeshi la Urusi waliingilia chanjo hiyo mwezi Aprili suala ambalo limepuuzwa na wizara ya Afya.

Lakini siku ya Jumanne, rais Putin alithibitisha kwamba mmoja ya watoto wake amepatiwa chanjo hiyo na kwamba anahisi vyema.

Watalaamu kadhaa wa kimataifa akiwemo Anthony fauci, pia wametilia shaka kasi hiyo ya Urusi, uwezo wa chanjo hiyo na hatua yake ya kutangaza kampeni kubwa kama hiyo bila kukamilisha majaribio yake.

Mtu yeyote anaweza kusema kwamba kuna chanjo na kuitengeneza lakini ni lazima uoneshe kwamba ni salama na ina uwezo, kitu ambacho nina hakika hawajaweza kuthibitisha, fauci alisema mwisho wa mwezi Julai katika mahojiano na BlackPressUSA TV.

''Lazima tuwe makini na watu wanaodai kwamba wanamiliki chanjo'', aliongezea.

Mwandishi wa masuala ya sayansi nchini Urusi, Irina Yakutenko pia alihoji ratiba iliochukuliwa, ''kwa kuwa watawadunga watu na kusubiri kuona kitakachotokea ,uchambuzi wa kawaida unaofanywa na ulinganishaji wake hautarajiwi'', alisema katika Telegramu.

Kulingana na idhaa hiyo ya Urusi, suali jingine ambalo linasalia kutatuliwa ni uwezo wake iwapo taifa hili litaanzisha uzalishaji wake kwa kiwango kikubwa kabla ya tarehe ilioahidiwa, hususan wakati ambapo miundo mbinu inakabiliwa na changamoto kubwa.