Waridi wa BBC: Mwanamke mfugaji wa konokono aliyetengwa akishukiwa kuwa na corona

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC News Swahili

Wangui Waweru anapokumbuka mchana wa tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu hulazimika kujizuia sana kulia kutokana na maisha yake yalivyobadilika siku hiyo.

Kabla ya siku hiyo, maisha yake yalikuwa ya kawaida tu na alikuwa na marafiki wengi. Lakini wapo marafiki wa dhati, na wanaoyeyuka wakati wa shida.

Siku hiyo, gari la kuwabeba wagonjwa lilifika nyumbani kwake kumchukua. Hii ni baada yake kujihisi kana kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vya corona.

Gari hilo lilipoingia kwenye boma lao kumsafirisha hadi hospitalini, marafiki zake na baadhi ya majirani walianza kuzungumzia tukio hilo. Taarifa za kuchukuliwa kwake na maafisa wa afya zikaenea kama moto wa nyikani.

Taarifa zilibuniwa , zikapikwa na kutiwa chumvi chumvi.

"Ni vigumu kusahau yaliyonitokea baada ya kubebwa na gari la wagonjwa mahututi hadi hospitalini. Kumbe niliacha minong'ono ya kila aina kule kijijini mwangu. Watu walieneza uvumi jinsi nilivyodhoofishwa na ugonjwa wa corona," anasema.

"Cha ajabu ni kuwa rafiki yangu wa karibu, niliyekuwa namueleza kuhusu dalili zangu ndiye aliyenisaliti zaidi kwa kunisemasema hapa na pale," Wangui anakumbuka .

Hali hii ilianzaje?

Kwa kipindi cha siku 7 hivi kabla ya kisa hicho, mwanadada huyu alikuwa karantini akiwa nyumbani kwake, mtaa wa Lanet katika Kaunti ya Nakuru. Alipoamka siku hiyo, kipimo cha joto mwilini kilikuwa kimepanda sana kuliko kawaida na kuwa nyuzi 41.2.

Kawaida binadamu huwa na kipimo cha 37. Vile vile alijihisi kuishiwa na nguvu na pia alikuwa na homa kali.

Kutokana na dalili hizo, alikuwa na wasiwasi sana kwamba alikuwa ameambukizwa virusi hiyo.

Ni yeye mwenyewe aliyewaita wahudumu wa hospitali moja mjini Nakuru na kuwaeleza kuhusu dalili zake.

Kulingana na Wangui, wahudumu wa afya walimshauri dhidi ya kusafiri na magari ya umma, bodaboda au teksi.

Njia pekee ilikuwa gari la kuwabebea wagonjwa. Gari hilo hakujua kwamba lingekuwa chanzo cha unyanyapaa.

Wanakijiji walipoliona gari hilo, huku wahudumu wakiwa wamevalia vifaa kinga, basi uvumi ukaenea mno kuhusiana na jirani yao kuwa muathirika wa corona.

Kulingana na mwanadada huyu, wengi ni wale waliohisi kuwa angekuwa chanzo cha kueneza ugonjwa huo maeneo yao, kama hakuwa ameshafanya hivyo tayari.

"Wakati huu ambapo dunia inapigana na corona, sijui ni kutokana na uelewa duni wa corona au ni vipi. Nimepitia hali ngumu mno. Unapodhaniwa una corona unaonekana kana kwamba hufai kukaa karibu na watu, " alisimulia Wangui

Je alikuwa na Corona ?

Wangui huwa mkulima wa konokono, kazi ambayo si wengi wanaojihusisha nayo. Mwanadada huyu anasema kuwa kutoka zamani kutokana na yeye kujitosa kwenye kazi ya konokono baadhi ya watu walijitenga naye.

Wangui amekuwa akiwafuga konokono katika kipande cha ardhi alichopewa na ndugu yake na sio bali na nyumbani kwake.

Mwanadada huyu anasema kuwa biashara hii ilimuwezesha kukidhi mahitaji yake ya kila siku, pamoja na ya watoto wake watatu.

"Ukulima na uuzaji wa konokono ulinipelekea kusafiri kutoka kijiji changu hadi mji mkuu wa Nairobi katika juhudi za kukutana na wateja wangu. Wateja wangu wengi sio raia wa Kenya, kuna wale kutoka Uchina Nigeria na kadhalika," anasema.

Kutokana na hayo mwanamke huyu amekuwa akitangamana na raia wa nchi za kigeni.

Alipoteza konokono wake

Majirani zake kwalidai angekuwa chanzo cha kusambaza corona.

"Kabla ya tukio la kubebwa na gari la wagonjwa, nilikuwa Nairobi kwa warsha na mikutano mbalimbali na washikadau wa konokono. Wawili kati ya hao baadaye walilazwa katika hospitali moja kwa kupatikana na virusi vya korona. Kwa hivyo niliporejea Nakuru na mwili wangu ukaanza kuwa na joto moja kwa moja nilidhani kuwa nilikuwa muathiriwa."

Alipofanyiwa vipimo baada ya kukimbizwa hospitalini, hakugunduliwa kuwa na corona.

Kisa kimoja kati ya matukio yaliyomtia hofu kilifanyika alipokuwa akipata matibabu.

Baadhi ya jamaa zake wa karibu walivamia kituo chake cha kuwahifadhi konokono na kuwaua kwa kuwamwagilia chumvi.

Wangui anasema kuwa mtaji wake na jasho lake vyote viliangamia siku hiyo kutokana na uelewa finyu kuhusu ufugaji wa konokono .

"Kuna wale waliosema kuwa konokono hao walikuwa na corona na hawafai kuishi karibu na binadamu. Nilipata hasara kubwa," anasema.

Alipotoka hospitalini Wangui alipigwa na butwaa asijue la kufanya.

Kwanza alikuwa anapitia unyanyapaa mwingi mno kutoka kwa majirani, watu wa jamii yake na marafiki zake.

Mwanadada huyu anasema kuwa hakuna aliyekuwa anataka kumuona, na muda mwingi alijifungia nyumbani kwake kutokana na hofu ya kutengwa.

Pia alipogundua kuwa konokono wake waliuliwa alihisi kana kwamba amepoteza kitu cha muhimu maishani mwake kwani ilikuwa njia yake ya kujipatia riziki.

"Kipindi kile nilikumbwa na msongo wa mawazo. Nilianza kuhisi huzuni isiyoeleweka na ikabidi nianze kusaka matibabu ya kiakili. Mwanasaikolojia ambaye amekuwa akinishauri alinipa dawa za kunisaidia kutulia. Ni kupindi ambacho hakijakuwa rahisi kwangu," Wangui anasema

Ni miezi miwili sasa tangu kisa hicho. Amesonga mbele licha ya yaliyompata , ila angali ana wasiwasi wa kuendelea kufuga konokono katika eneo hilo hilo ambalo alinyanyapaliwa.

Biashara ya konokono ikoje?

Wangui anasema kuwa ufugaji wa konokono una tija sana. Nyama ya konokono ni biashara kubwa mno katika nchi za nje na ndiposa wanaoila wanatumia dola nyingi kuinunua.

Kila kilo moja ya konokono inagharimu kama dola 400 hivi, na kwa hivyo wenye kufurahia kitoweo hicho ni watu wenye hela.

Wangui anasema kuwa hata yeye amekuwa shabiki wa kula nyama ya konokono.

"Kitoweo cha konokono siwezi kukisaza. Mimi hufurahia kuwala na mchuzi, nikiandamanisha na sima au wali. Watu hunishangaa mno kwa mtindo huu. Pengine huenda ndio sababu baadhi yao walinibagua hivyo."

Wangui anasema siri ya kumpika konokono ni kumchemsha kwa muda mrefu sana, ili kuhakikisha kuwa yale makamasi yake yamekauka kabisa.

Kwasasa Wangui ameibuka kama mmoja wa watoa ushauri nasaha kipindi hiki cha Covid-19, kwani anaelewa fika jinsi fikra za baadhi ya watu zinavyoweza kuchangia unyanyapaa na hatari zake.

Pia anashiriki pakubwa katika hutoa mafunzo maalum kuhusu ufugaji wa konokono